Magufuli ahamishia utumbuaji jipu EAC

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
WAKUU wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia Rais John Magufuli awe Mwenyekiti wa jumuiya, kwa maana kwamba Tanzania iendelee mwaka mwingine kuongoza kipindi ambacho Burundi ndiyo ilipaswa kushika wadhifa.

Dk Magufuli ambaye anaongoza jumuiya hiyo ambayo imepata mwanachama mwingine, Sudan Kusini, ameanza kwa kasi kubwa huku akipenyeza msimamo na falsafa yake ya ‘kutumbua majipu’ kuhakikisha nchi wanachama wanakwenda pamoja na kuleta maendeleo ya wananchi.

Hayo yalifanyika katika mkutano wa kawaida wa 17 wa Jumuiya, ambapo wakuu hao wa nchi pia walikubaliana kwa pamoja Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kushirikiana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kutatua mgogoro wa Burundi.

Magufuli aliahidi atafuatilia Sekretarieti ya EAC, kuhakikisha inafanya kazi kwa maslahi ya wananchi wa nchi wanachama na si kuwanyonya.

Msimamo wa Magufuli

Rais Magufuli alihimiza viongozi wakuu wa umoja huo, kutoa kipaumbele katika ujenzi wa viwanda. Alisisitiza msimamo wake kupitia Sekretarieti ya jumuiya hiyo, kubana matumizi kuhakikisha malengo ya kuleta maendeleo katika nchi wanachama yanatimia.

Akizungumzia gharama za ukumbi waliotumia kwa ajili ya mkutano huo wa 17 kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Magufuli alisema dola 45 kwa kichwa zilizotumika ni nyingi ambazo kama zingebanwa, zingeokoa fedha ambazo zingenunua madawati na kwenda kusaidia mahali pengine.

“Mwito wangu kwa sekretarieti, muwe cost conscious (macho na gharama),” alisema. “Tubane sana matumizi iwezekanavyo, tukahudumie watu masikini na si kuwa na Sekretarieti inayokuwa parasite (nyonyaji),” aliendelea kusema.

Sekretarieti hiyo inaongozwa na Liberal Mfumukeko kutoka Burundi, aliyeteuliwa na wakuu hao wa nchi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano baada ya Dk Richard Ssezibera wa Rwanda, muda wake kumalizika.

Magufuli katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, alisema amepiga hesabu ukumbi huo ni ghali. Alitoa mwito kwa sekretarieti na watumishi wote kwamba ni lazima wafahamu kwamba wako kwa watu masikini na wanahudumia watu masikini katika nchi wanachama.

“Nataka niiambie Sekretarieti, Marais wamefanya kosa sana kunichagua mimi kuwa mwenyekiti. Nitahakikisha nawafuatilia kweli. Kwa hiyo mjipange vizuri na kama patakuwapo mmoja wa wafanyakazi anakwenda sehemu isiyotakiwa, nitaripoti kwa nchi anakotoka ili atumbuliwe jipu,” alisema.

Alisisitiza ifanye kazi kwa niaba ya nchi zao kwa kutengeneza sheria na mambo yatakayozisaidia. Alihimiza sekretarieti isiwe sehemu ya walalamikaji, bali wawe watatuzi wa matatizo ya jumuiya. Alisema nchi wanachama wanapaswa kubadilika, kuwa na mtazamo wa kuhakikisha wananchi wake wananufaika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tunapaswa kutembea pamoja kwa maslahi ya jumuiya,” alisema. Rais Magufuli anaongoza jumuiya hiyo kwa mwaka mmoja, nafasi ambayo ilipaswa sasa ichukuliwe na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. Hali hiyo inatokana na nchi hiyo kuomba kuachia nafasi hiyo ili kuelekeza nguvu zake katika kushughulikia matatizo yake ya ndani, lakini ilipewa nafasi ya kutoa Katibu.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi huku Sudan Kusini ikiwa imekidhi vigezo na kukubaliwa kuwa mwanachama mpya wa jumuiya hiyo katika mkutano huo wa 17.

Ujenzi wa viwanda

Akizungumzia suala la ujenzi wa viwanda, suala ambalo amekuwa akilipa msisitizo mkubwa tangu wakati wa kampeni na hata baada ya kuingia Ikulu, Rais Magufuli alisema suala hilo ni miongoni mwa kazi kubwa mbili ambazo ni lazima zipewe msisitizo mkubwa na viongozi wakuu wa EAC.

Alisema kwa bahati mbaya, pamoja na kuwa na utajiri wa rasilimali, bado rasilimali hizo zimeshindwa kutumika ipasavyo katika kuchochea ukuaji wa viwanda ndani ya Mtengamano wa Afrika Mashariki na badala yake zimekuwa zikisafirishwa kwenda kutumika kwa viwanda nje ya ukanda huo.

“Imekuwa ni bahati mbaya sana kwamba, tunatumia tusichokizalisha na tunazalisha tusichokitumia. Ni lazima mtindo huo uachwe mara moja,” alisema Rais Magufuli. Kiswahili Mbali ya viwanda, Rais Magufuli alisema kazi kubwa ya pili ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaanza kutumika kama lugha kuu ya mawasiliano ndani ya vikao vya EAC.

Alisema si jambo la kujivunia kuona Kiswahili hakipewi umuhimu katika ukanda ambao ndiko kilipozaliwa, huku watu wa mataifa ya mbali wakiiona kama lugha adhimu na adimu.

Rais Magufuli alihimiza kutumika kwa lugha ya Kiswahili, kama lugha kuu ya mawasiliano ndani ya EAC sanjari na Kiingereza, akisema umoja huo hauwezi kuendelea kukipa Kiswahili nafasi finyu huku asilimia kubwa ya wananchi wa ukanda huo wakiitumia.

Alisema ingawa Mkataba wa Uanzishwaji wa Mtengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unatamka kwamba lugha kuu ya mawasiliano ndani ya jumuiya hiyo ni Kiingereza huku ikitamka kuwa Kiswahili kitaendelea kuendelezwa, haiwezekani kuendelea kutumia Kiingereza katika ukanda wa EAC wakati ni watu milioni mbili tu ndio wanaozungumza lugha hiyo, huku asilimia kubwa iliyobaki ikizungumza Kiswahili.

Rais Magufuli ambaye amekuwa Mwenyekiti kwa miezi minne, huku minane iliyotangulia ikiwa imetekelezwa na Rais Jakaya Kikwete (mstaafu), alisema kazi kubwa imefanyika katika kuijenga jumuiya hiyo.

Kuhusu uimarishaji wa Itifaki ya Ushuru wa Pamoja wa Forodha, Rais Magufuli alisema kazi kubwa imefanywa katika kuimarisha itifaki hiyo, ikiwemo ujenzi wa Vituo vya Forodha vya Pamoja Mipakani ambavyo vimerahisisha upitishaji wa bidhaa na kuokoa muda na fedha.

Alisema pia kazi kubwa imefanywa katika kuimarisha Soko la Pamoja la EAC, ikiwa ni pamoja na kurekebishwa kwa sheria zinazosimamia ushuru wa bidhaa kwa nchi wanachama, kwa kuendelea kuboresha urari wa tozo kwa nchi zote kuondoa migongano isiyo ya lazima.

Alisifu pia kazi kubwa iliyofanyika kuharakisha Itifaki ya Fedha ya Pamoja kupata sarafu moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisema kikosi kazi cha EAC kilikuwa kimemaliza kutengeneza mwongozo kuhusu Itifaki ya Fedha ya Pamoja na wakati wowote utawasilishwa kwa wakuu wa nchi kupata baraka.

Alisema pia kazi kubwa imefanyika kuimarisha uwepo wa amani na utulivu kwa nchi wanachama.

Alisema changamoto kubwa ni kuondoka kwa amani na utulivu nchini Burundi, huku akisema wananchi wa Burundi, viongozi wa EAC na Jumuiya za Kimataifa, wanapaswa kuuunga mkono maazimio ya Mkutano ulioitishwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni Julai 2, mwaka jana, katika jitihada za kurejesha amani Burundi.

Museveni aliteuliwa na EAC kuwa msuluhishi wa umoja huo kwa mgogoro wa Burundi, huku Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa akiteuliwa kuongoza Kamati ya Umoja huo itakayokuwa inaripoti kwa Rais Museveni, hatua mbalimbali za kutatua mgogoro huo.

Alisema katika kipindi hicho, EAC pia imeshuhudia mabadiliko ya Katiba ya Rwanda, huku mchakato huo ukijumuisha sauti ya wananchi wote wa nchi hiyo.

Magufuli alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Paul Kagame kwa kusimamia suala hilo katika hali ya amani na utulivu.

Rais Magufuli alizungumzia pia mikakati mbalimbali inayoendelea kuchukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuboresha uhusiano baina yake na Jumuiya nyingine za Kikanda, ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na nyinginezo katika hatua za kukuza uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii.

Wakati huo huo, wakuu hao wa EAC walizindua hati ya kusafiria ya kielektroniki kwa nchi wanachama kuwezesha wanachama kufanya shughuli zao za uchumi na kupata maendeleo. ‘Tuvumiliane’ Magufuli alitoa mwito kwa nchi wanachama kuvumiliana na kujiona familia moja, itakayosaidia kusonga mbele. Alisema kila nchi zina matatizo yake, hivyo hazina budi kuvumiliana.

“Lakini sisi sote tunapaswa kujiona ni familia moja itakayotusaidia kusonga mbele,” alisema na kueleza furaha yake kuona Sudan Kusini inakuwa miongoni mwa wanachama. Katika hatua nyingine, Mkutano huo wa 17 ulienda sanjari na kutoa tuzo pamoja na motisha kwa wanafunzi wa sekondari wa nchi za jumuiya waliofanya vizuri katika uandishi wa insha.

Mwanafunzi Simon Mollel kutoka Tanzania aliyemaliza Kidato cha Nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya Mzumbe mkoani Morogoro, aliibuka mshindi wa kwanza na kukabidhiwa kitita cha dola za Marekani 1,500 na Mwenyekiti wa kikao hicho.

Mkutano huo wa 17 ulihudhuriwa na Marais Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Kagame wa Rwanda na Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Joseph Butore ambao wote walipopewa nafasi ya kutoa neno, walimpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake na uongozi anaoonesha.

Sudan Kusini

Baada ya Sudan Kusini kukubaliwa kuwa nchi mwanachama wa EAC, mwakilishi wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Igga ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais, aliwashukuru marais wa nchi wanachama.

Alieleza furaha yake kwa marais hao kukubali kuipokea nchi yake, licha ya changamoto zinazowakabili. Aliahidi nchi yake itaonesha ushirikiano kwa nchi za jumuiya hiyo. Rais Kenyatta, Rais Kagame na Rais Museveni waliipongeza Sudan Kusini kwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Nina furaha sana kuona hatimaye Sudan Kusini imejiunga na jumuiya hii. Hatua hii ni moja ya mambo ambayo sisi viongozi tumekuwa tukipigania kwa miaka mingi,” alisema Museveni.

Sudan Kusini ni nchi isiyokuwa na bandari iliyopo Kaskazini Mashariki mwa Afrika. Ilipata uhuru wake kutoka Sudan Kaskazini Julai 9 mwaka 2011. Mji Mkuu wa nchi hiyo ni Juba na Rais wake ni Salva Kiir. Ina watu milioni 11.3. Fedha ya nchi hiyo ni Pauni ya Sudan Kusini na wastani wa kuishi ni miaka 55.
 
Back
Top Bottom