Maggid Mjengwa: Wazee wa Dar es Salaam ni akina nani na wana sifa zipi?

Linguistic

JF-Expert Member
Mar 16, 2021
3,671
8,237
Wazee Wa Dar Es Salaam Ni Akina Nani? Je, Sifa Za Mzee wa Dar es Salaam Ni Zipi?

Ndugu zangu,

Leo Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan ataongea na Wazee wa Dar es Salaam.

Kwenye juzuu ya kwanza kati ya tatu, kitabu ' The Making Of A Philosopher Ruler, ukurasa 124-125., mwandishi Mtanzania, Prof. Saida Yahya- Othman anawazungumzia Wazee wa Dar es Salaam.

Kati ya anaowataja, amemtaja Marehemu Mangara Tabu Mangara. Mwandishi anaelezea jinsi Julius Nyerere alivyowatumia Wazee wa Dar es Salaam kupata taarifa za hali halisi za watu wa kawaida mitaani.

Tabu Mangara alikuwa mmoja wa ‘ Watoto wa Mjini.’ Alipata pia kuwa bosi wa mama yangu mzazi wakati Mangara akiwa Mkuu wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali- Government Press.

Tabu Mangara Tabu Mangara alikuwa pia Mwenyekiti wa Yanga. Aliishi Kariakoo na alikuwa na nyumba pia pale Mtaa Mwanz Ilala ,jirani na Mtaa wetu tulioishi utotoni mwangi, Iringa Street.

Mwandishi Saida Yahya- Othman anakielezea kisa cha ndani ya Baraza la Mawaziri miaka ya 80.

Kulikuwa na uhaba wa bidhaa madukani na kukawa na bei za kulangua. Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Joseph Mungai akapendekeza Serikali iyafunge maduka binafsi na kuwepo na maduka ya Serikali.

Mawaziri waliunga mkono hoja ya Mungai, lakini, Nyerere akawaambia wasubiri kwanza kabla hajapitisha maamuzi.

Nje kwenye korido za Ikulu, Julius Nyerere akamwambia Balozi Sued aende akamtafute Mangara Tabu Mangara, na amwambie Nyerere anamuhitaji Msasani kwa mazungumzo.

Pale Msasani Nyerere akamwelezea Mangara jambo zima na kumwomba ushauri.

Mangara akamweleza Nyerere hali halisi ya wananchi mitaani, kwamba watu wanaishi kwa madeni. Bajeti zao ni za siku kwa siku. Leo mtu akiwa hana kitu mfukoni, anakwenda dukani kwa Mshihiri kukopa. Mwingine anaweka rehani hereni za mkewe ili apate bidhaa za dukani.

Sasa, Mangara akamwuliza Nyerere;

“Maduka ya Serikali nayo yatafanya hivyo hivyo?”

Nyerere akamwelewa Mangara. Maamuzi yale ya kufunga maduka hayakufanyika.

Nini adili ya jambo hili?

Mwalimu alifahamu udhaifu wa baadhi ya Mawaziri wake wasomi , kwamba baadhi yao kwa vile wanaishi Oysterbay, walipoteza mawasiliano na watu wa kawaida na hali zao za maisha. Mangara ambaye hakuwa hata na digrii ya Chuo Kikuu, aliwazidi hekima baadhi ya Mawaziri wa Nyerere.

Mwalimu pia alijua, kuwa watu wa aina ya Mangara Tabu Mangara, hawakuwa wasaka tonge. Ni watu ambao kwenye kushauri kwao, hawakutarajia Nyerere awape vyeo. Walitoa ushauri kwa mapenzi ya nchi yao na kwa kumtakia mema Nyerere. Ndio hawa walioitwa ‘ Wazee wa Dar es Salaam.’

Wazee wa Dar es Salaam ni kina nani haswa?
Tangu enzi za Mwalimu’, kukiwa na jambo kubwa kitaifa, basi, Mwalimu aliliongea kupitia kwa “ Wazee Wa Dar Es Salaam”. Na mahali haswa wanapokutana ‘Wazee wa Jiji’ kumsikiliza ‘ Mkuu Wa Kaya’ ilikuwa ni pale Upanga kwenye Ukumbi wa Diamond.

Jambo hilo lililoasisiwa na Mwalimu likaja kuwa ni utamaduni wa kisiasa. Mathalan, ni pale Upanga Diamond Jubilee ndipo Mwalimu alipotangaza vita dhidi ya Idi Amin kupitia Wazee Wa Dar Es Salaam.

Nini chimbuko la Wazee wa Dar es Salaam?
Chimbuko lake ni Wazee wale 120 waliounda Baraza la Wazee wa TANU kwenye harakati za kupigania Uhuru. Waliongozwa na Mzee Suleiman Takadir.

Baada ya Uhuru Nyererw akaja kugombana na Wazee wa Baraza hili. Akalifutilia mbali Baraza mwaka 1963. Nyerere akaendelea kuongea na Wazee wa Dar es Salaam bila Baraza.

Kwanini Nyerere aligombana na akina Takadir?
Hii ni mada nyingine. Nimepata kujadiliana na rafiki yangu mwanazuoni Mohamed Said. Nitakuja siku moja kusimulia.

Nani anastahili kuwa Mzee Wa Dar es Salaam?
Ndio, kuna Mzee mmoja wa Dar es Salaam alipata kuniambia, kuwa sifa ya kwanza ya kuwa ‘Mzee wa Dar Es Salaam’ ni lazima uwe na zaidi ya umri wa miaka 50. Uwe mkazi wa Dar Es Salaam kwa miaka isiyopungua 20 mfululizo!

Hilo halijaandikwa popote, lakini ‘Wazee’ wenyewe wa jiji wanauzingatia utaratibu huo. Aliniambia.

Na kuna “Kijana wa Dar es Salaam” alipata kuninong’oneza, kuwa wako mbioni kuwashawishi wazee wa jiji waongeze sifa za kuwa mzee wa Darisalama.

Kwamba ili uwe Mzee wa Dar Es Salaam ni sharti, ama uwe umezaliwa na kukulia Dar, au umezaliwa nje ya Dar lakini ujana wako wote umeishi Dar. Hivyo basi, unapoteza sifa ya kuwa Mzee wa Dar es Salaam kama umekuja Dar ukubwani!

Na Wazee wa Dar Es Salaam wana Mwenyekiti wao. Kwa kawaida siku ya ‘shughuli’ ya wazee, Mwenyekiti wao huvalia kanzu, kibagharashea na kizibau.

Ndiye huyu ambaye huwa wa kwanza kumpokea ‘Mkuu wa Kaya’ anapoingia ukumbini kuwahutubia wazee.

Ni kwa namna gani basi Mwenyekiti wa Wazee wa Dar Es Salaam anachaguliwa?
Hilo ni swali la kizushi na usithubutu kuliuliza mbele ya ‘Wazee wa Dar es Salaam’- watakutoa mbio kwa bakora!

Lakini , lililo dhahiri ni kuwa, Wazee Wa Dar Es Salaam hawajawahi kuwa na Mwenyekiti mwanamke. Na leo itakuwa ni mara yao ya kwanza kuhutubiwa na Mkuu wa Kaya Mwanamke.

Kwenye uenyekiti, hata Bi. Titi Mohammed hakupata kufikiriwa. Heshima ya kumpa barabara kuitwa kwa jina lake ilitosha, na amshukuru Julius, alipata kuniambia Mzee ' orijino’ wa Dar Es Salaam.

Ndio, Mkuu yeyote wa Kaya katika nchi hii atashauriwa aongee mbele ya Wazee wa Dar Es Salaam kama ana kubwa analotaka liwafikie wananchi.

Katika miaka ya karibuni Rais wa nchi, hayati Magufuli, alipata kulihutubia taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dodoma.

Inasemekana jambo hilo liliwashtua baadhi ya Wazee wa wa Dar Es Salaam. Na kuna siku nilitembea kwa miguu mitaa ya Kariakoo Kusini; Livingstone, Mahiwa, Swahili na mingineyo.

Hatimaye nikafika kwenye kijiwe cha chai na kahawa pale Mtaa wa Lumumba. Nilukuta mjadala juu ya Wazee wa Dar Es Salaam. Na hapo nikayasikia manung’uniko.

Ndio, baadhi ya Wazee wa Dar Es Salaam wanaamini pia, kuwa Ilala ndio Dar Es Salaam. Na kwamba ni Wazee wa Ilala ndio waliompokea Julius Nyerere alipoingia mjini.

Wanahoji;

Iweje Wazee wa ‘mashambani’ Kinondoni na Temeke nao waitwe Wazee Wa Dar Es Salaam?

Swali linabaki;

Wazee Wa Dar Es Salaam ni akina nani?

Ni Tafakuri Jadidi.

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam.
 
Wazee wanaoitwa wa Dar es Salaam hawa wa sikuhizi ni wale makada kindakindaki wa CCM, na believe me utaona hiyo dress code yao leo kimsingi ni watu ambao wamesghaandaliwa wameambiwa cha kuzungumza hayo ya kina mzee Mangara yalikua zamani sikuhizi wazee hawa wanaokesha kula bata kwa hela za chama hawana lolote wanaloweza kushauri ili mambo yaende believe me, hata Jiwe alijidai kukutana nao baadaye akaona anapoteza muda tu akaachana nao.
 
Makada watiifu wa Ccm . Wale wenye kusifu na kuabudu. Sasa sijui kama mama anaendekeza usanii huo
 
Wazee wanaoitwa wa Dar es Salaam hawa wa sikuhizi ni wale makada kindakindaki wa CCM , na believe me utaona hiyo dress code yao leo kimsingi ni watu ambao wamesghaandaliwa wameambiwa cha kuzungumza hayo ya kina mzee Mangara yalikua zamani sikuhizi wazee hawa wanaokesha kula bata kwa hela za chama hawana lolote wanaloweza kushauri ili mambo yaende believe me, hata Jiwe alijidai kukutana nao baadaye akaona anapoteza muda tu akaachana nao
Sasa ulitaka na wale wa chadema wenye kushangilia ushoga nao wawemo?

Hiyo haikubaliki

Hata wakialikwa wao watawaza kumuangusha raisi na hayo ndio mawazo yao.
 
Nyerere alitambua hekima ya wazee kwani bila wao hata Tanu asingeiongoza na ingewezekana hata Uhuru ungechelewa.

Sifa ya mzee ni kutoa ushauri bila kuogopa, kusema ukweli bila kutegemea kupewa chochote. Kwa sasa sifa hizi kwa wazee wanaoitwa kuongea na rais wengi hawana lakini Nyerere alikuwa hautubii wazee bali alikuwa akiongea nao ili kupata ushauri na mara nyingi walikuwa wanampa taarifa zile ambazo vyombo vingine vilikuwa vinamficha rais kama TISS.

Sasa hivi wazee wanaokuja wengi ni makada wa ccm na wengine hawana hata sifa ya uzee.

Wakifika watahutubiwa kisha watapewa posho hata risala yao itakuwa imeandikwa na watu wengine.

Wangekuwepo wazee wenye sifa mojawapo ya ajenda zao ingekuwa ni madai ya pensheni pamoja na bomoabomoa ya kimara na mengineyo wanayoona yanafaa.

Ila Nyerere hakuwa akiongea na wazee wa Dar es salaam peke yake alikuwa akifanya hivyo kila mkoa na faida yake alikuwa akipata taarifa sahihi za wananchi wa kawaida.
 
Kwa lugha nyepesi isiyo na kificho, kulingana na muandishi, wazee wa Dar lazime wawe ni wawe ni wanaume wa kiislamu, wacheza bao na wasio na elimu ya kutosha
 
Kwani wazee wenyewe wanasemaje?
Kwa kumbukumbu niliyonayo kuhusu maduka ya kaya enzi hizo, si Waziri Mungai aliyetaka kuyafunga maduka ya binafsi bali ni Mhe. Rashid Kawawa aliyetoa amri "fungeni maduka" bila ya kuangalia athari ambayo ingejitokeza kwa kufanya hivyo. Wahenga tulipata shida sana kipindi hicho.
 
Back
Top Bottom