MAFUTA BALAA: Treni yasitisha safari kwenda bara; Wachumi watabiri hali mbaya zaidi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Treni yasitisha safari kwenda bara

*Nauli, vyakula mikoani bei zapanda
*Wachumi watabiri hali mbaya zaidi

Na Waandishi Wetu

UPUNGUFU wa mafuta katika maeneo mbalimbali nchi umezidi kukolea na kusababisha athari mbalimbali za kiuchumi, ikiwamo kusitishwa kwa safari za treni ya kati, kupanda kwa nauli na bei za vyakula, huku wachumi wakitabiri hali mbaya zaidi.


Safari za treni kusitishwa

Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imesitisha safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda bara kutokana na kukosa mafuta.

Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Bw. Midladjy Maez alisemsa jana kuwa kutokana na hatua hiyo, treni iliyokuwa imepangwa leo saa 10:00 jioni kwenda bara na iliyopangwa kuondoka Tabora kwenda Mpanda kesho hazitakuwapo.

"Kampuni imeamua kusitisha safari za treni za abiria kwenda bara kutokana na maghala yetu kukosa mafuta ya kutosha, hivyo safari zitarejea endapo zitapata mgawo wa kutosha wa nishati hiyo," alisema Bw. Maez.

Aliwataka watu wote waliokata tiketi za kuondoka kwenda maeneo hayo kuonana na wakuu wa vituo ili kurejeshewa nauli zao, huku akiomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki kutokana na usumbufu wanaoupata.

Mbeya nauli juu

Tatizo hilo la mafuta nchini limechukua sura mpya baada ya wamiliki wa daladala mkoani Mbeya kupandisha nauli kutoka sh. 350 mpaka 500 kutokana na nishati hiyo kupandishwa hadi sh. 3,000 kwa lita moja.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo la Uyole jijini Mbeya walisema kuwa kiwango hicho cha nauli kimepanda bila kuzingatia utaratibu huku magari mengine yakishindwa kufanya kazi.

Mkazi wa Uyole, Bw. Ablahamu Kazubele alisema kuwa nauli ya awali kutoka Uyole kwenda mjini ilikuwa sh. 350 na sasa imekuwa sh. 500 ambayo si ya kawaida.

Dereva wa daladala inayofanya kazi zake kati ya Uyole na Igawilo maarufu kwa jina la Mwagito alisema kuwa wao wamelazimika kupandisha nauli kutokana na mafuta kupanda bei hadi sh. 3,000 kwa wachuuzi mitaani.

Vyakula vyapanda bei Songea

Mkoani Ruvuma, mgomo huo umesababisha kupanda bei kwa kilo ya unga kutoka sh. 600 hadi 1,500 na mchele kutoka sh. 1,000 hadi sh. 1,500 katika manispaa ya Songea.

Bw. Rashidi Hussein mkazi wa eneo la Mpambalioto mjini hapa alisema kuwa tatizo la kutokuwepo kwa dizeli na petroli limeleta athari kubwa, hasa kwa waumini wa dini ya kiislamu ambao kwa sasa wako katika mfungo wa Ramadhani.

Naye Bw. Didas Lyakulwa maarufu kwa jina moja la Mabrandi, alisema:

"Ndugu waandishi leo nimenunua mafuta ya petroli lita moja
sh. 5,000 badala ya sh. 2,135 kwa lita, kwa ajili ya kuweka kwenye jenereta ninalotumia kwenye biashara yangu ya baa na hoteli, hivyo kupata hasara kubwa," alisema Bw. Lyakulwa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Christine Ishengoma alisema tayari ameshawaagiza wamiliki wa vituo vyote vya mafuta mkoani humo wahakikishe kuwa mafuta yanapofika wayauze kwa bei halali, vinginevyo watachukuliwa hatua.

Wachumi watabiri mabaya

Wakati huo huo, wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa wametahadharisha kuwa kama tatizo hilo na mgawo wa umeme havitatatuliwa kwa njia sahihi, uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja utaendelea kuporomoka.

Wachumi hao wamesema kuwa wananchi wajiandae kwa hali ngumu ya maisha, ikiambatana na ukosefu wa ajira kuliko ilivyo sasa.

Profesa Samuel Wangwe alisema kuwa ni wakati mwafaka sasa serikali ijue kwa undani namna biashara ya mafuta inavyoendeshwa, ili siku nyingine isikurupushwe kama inavyoonekana kutokea hivi sasa.

"Kama hali hii itaendelea, kwa kweli kutakuwa na tatizo kubwa, vitu kutofika, gharama za kusafirisha, kupanda kwa bei za vitu...hili la ulanguzi linaloonekana sasa ni matokeo tu ya upungufu huu wa mafuta.

"Lakini ni vyema serikali ikaijua vyema biashara hii, si kama sasa hivi ambapo inaonekana imekuwa taken by surprise. Waelewe biashara hii inakwendaje, imekaaje, wajue serikali inapaswa ku-play role gani hasa katika biashara ya mafuta, wadhibiti wakiwa na taarifa kamili ya nini kinafanyika. Wajifunze katika hali kama hii, nchi zingine kama Ujerumani, Sweden, Marekani au Uingereza zinafanyaje katika kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisisitiza kauli yake amabyo amekuwa akiitoa mara kwa mara juu ya ombwe la uongozi, ambalo alisema limekuwa likionekana katika serikali iliyoko madarakani, akiongeza kuwa kama ufumbuzi sahihi hautapatikana kwa wakati mwafaka taifa na wananchi kwa ujumla watakuwa katika matatizo makubwa kuliko ilivyo sasa.

Prof. Lipumba ambaye yuko katika mapumziko ya kujenga afya yake baada ya kufanyiwa operesheni nchini India hivi karibuni, aliungana na Prof. Wangwe, akisema kuwa kama hakutakuwa na suluhisho la haraka, kutakuwa na mfumuko mkubwa bei kuliko ilivyo sasa, hivyo kusababisha hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu.

"Tatizo ni hilo hilo ambalo mara kwa mara tumelisema, bahati mbaya na ninyi ujumbe mmekuwa hamuufikishi sawa sawa kama inavyotakiwa. Suala la mafuta limedhihirisha ombwe la uongozi ambalo nimekuwa nikisema. Suala la kupunguza bei lilifanywa kisiasa zaidi kwa ajili ya kujipatia umaarufu. Inavyoonekana serikali haikufanya utafiti kabla, kuwasiliana na wauzaji kabla ya bajeti.

"Serikali ilipaswa kujua mapema kuwa utaratibu mpya hautakuwa na athari yoyote...leo kuna mtu kaniambia bei za bajaj zimepanda, sasa mafuta yanaanza kuuzwa kwa bei ya magendo kwa bei ya kuruka...matatizo yatakuwa makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Hakuna sheria inayowapatia EWURA mamlaka ya kupanga bei, wanaweza kutoa bei elekezi tu, ingawa pia wauzaji hawaruhusiwi kupanga njama za kuuza bei kubwa maana hiyo ni jinai.

"Kwa sababu hakuna price control huwezi kuwashtaki, bali unaweza kuwanyang'anya leseni wasiuze mafuta tena. Lakini serikali ilipaswa kulifanyia suala hili utafiti kabla hata ya bajeti, kujua kama uamuzi huo ungeweza kuongeza matatizo zaidi. Serikali lazima ifanye mambo kwa uhakika. Na katika hali ya sasa ujue hata meli zinaweza kuelekezwa kupeleka mafuta sehemu nyingine badala ya kuleta Tanzania, hivyo tukaendelea kuwa katika matatizo makubwa."

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Heche alidai kuwa anazo nyaraka zinazoonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina mikataba ya kibiashara na baadhi ya makampuni ya mafuta, ndiyo maana hakiwezi kukemea hali inayoendelea nchini, huku pia akisema kuwa baadhi ya wabunge na mawaziri wana mgongano wa maslahi katika tatizo hilo.

"Ninazo nyaraka, nitazitoa wakati mwafaka, CCM wana mikataba ya kibiashara na baadhi ya makampuni ya mafuta, mmoja una kiasia cha sh. bilioni 3. Hiyo ni mbali na kuwa uongozi wa sasa wa serikali ya CCM uliingia kwa ufadhili wa fedha za makampuni hayo, ndiyo maana mpaka sasa hatujasikia kauli 'serious' juu ya suala hili.

Akizungumzia shutuma hizo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Bw. Nape Nnauye alisema "mwambieni Heche azitoe hizo nyaraka, maana sasa hivi ndiyo wakati mwafaka, suala la mafuta linazungumzwa sana, atoe tu. Sisi tunaweza kutoa mikataba yote, ingawa unaweza kumtafuta Mwigulu Nchemba, maana yeye ndiyo hasa anahusika na Idara ya Fedha na Uchumi, anaweza kukwambia mengi.

"Lakini hayo ni maneno ya kihuni, yamekuwa yakitolewa na watu mbalimbali, nimeyaona hata mtandaoni...lakini hata maneno kuwa hatujachukua hatua...ukiuliza sisi ndiyo tulikuwa tunahangaika kuhakikisha mambo yaende. Mpigie Mwichemba atazungumza zaidi."

Majira lilimtafuta Bw. Nchemba kwa simu yake ya mkononi lakini ilikuwa ikiita bila kupokewa, hivyo ikalazimu kumtumia ujumbe mfupi, kumwomba azungumzie shutuma hizo, lakini hatukupata majibu hadi tunakwenda mitamboni.

Imeandikwa na Esther Macha, Mbeya; Cresensia Kapinga, Songea; Tumaini Makene na Grace Ndossa.
 
Back
Top Bottom