Mafuriko Msimbazi Dar: Mwarobaini watua Ofisi ya Rais

Deus J. Kahangwa

Verified Member
Jan 7, 2013
184
225
Msimbazi--Picha 00.png


Usuli

Kwa mujibu wa Kanzidata ya Kimataifa kuhusu Majanga Asilia yaliyotokea tangu mwaka 1990, Tanzania inakabiliwa na hatari ya majanga asilia yafuatayo, frikwensi zake zikiwa zimeonyeshwa katika mabano: mafuriko (62.2%), ukame (13.3%), tetemeko la ardhi (11.1%), kimbunga (8.9%), moto wa nyikani na maporomoko ya miamba (4.5%).

Kwa mujibu wa takwimu hizi, janga la mafuriko linayo nafasi kubwa kuliko majanga mengine yote, ambapo kwa miaka 25 iliyopita, kumetokea mafuriko 19ya mitoni, mafuriko 10 ya ufukweni mwa bahari na mafuriko 4 ya maji yanayozagaa katika tambarare isiyo na mto.

Kwa kuwa Dar es Salaam ni Jiji katika mwambao wa Bahari ya Hindi na linayo mito mingi limekuwa likikumbwa na mafuriko zaidi kuliko mikoa mingine, mafuriko mengi yakiwa yanatokea katika Bonde la Mto Msimbazi.

Mafuriko haya husababisha vifo, uharibifu wa mali na majeruhi. Matukio haya yamelibadilisha Jiji kuwa hatari kwa maisha ya wakazi.

Kwa sababu hii, serikali ya Tanzania imeamua kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa salama kwa kubuni na kutekeleza “Mradi wa Fursa ya Msimbazi” kwa ajili ya “Kulibadili Bonde la Msimbazi hadi kuwa Kielelezo cha Miji iliyo salama Katika Afrika.”

Mradi huu unayo maeneo mawili ya kimkakati, maeneo manne ya kimatokeo, mikakati kumi na majukumi 50. Mradi unafadhiliwa kwa nia ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP). Kiasi cha dola za Marekani 114 milioni zinahitajika kuukamilisha.

Utekelezaji wake ulianza mwaka 2019 na unasonga mbele kwa kuanza na utekelezaji wa kazi zenye vipaumbele vikubwa. Utaendelea mpaka mwaka 2050, kupitia mipango kazi ya miaka mitano mitano, ambapo mpango kazi wa kwanza unaanzia 2019 mpaka 2024.

Mmiliki wa mradi huu ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Kitengo cha TAMISEMI, na msimamizi mkuu ni Katibu Mkuu TAMISEMI. Ripoti ifuatayo inajadili changamoto, fursa na wadau wa mradi huu.

Utangulizi


Sasa ni wazi kwamba mafuriko yanayotokana na mvua kubwa zinazonyesha jijini Dar es Salaam tangu miaka ya 1990 yameikumbusha serikali ya Tanzania kuhusu umuhimu, uharaka na ulazima wa kubuni na kutekeleza jawabu la kudumu, dhidi ya mafuriko ya kila mara katika Bonde la Msimbazi.

Tayari serikali imekamilisha andiko linalofahamika kama “Mradi wa Msimbazi” kwa ajili hiyo.

Andiko hili limeandaliwa kwa kuzingatia ukweli kwamba, ndani ya Bonde la Mto Msimbazi, mvua zimekuwa zikisababisha mafuriko makubwa yenye kuhatarisha maisha ya raia, mali zao na miundombinu ya kiuchumi na kijamii kama vile barabara, madaraja, shule, hospitali na makazi ya watu.

Kwa sababu ya mvua hizi, nyumba zilizoko bondeni humo zimekuwa zinajaa maji na hivyo watu kadhaa kukosa makazi. Pia, madaraja mengi yaliyo katika Mto Mzsimbazi na matawi yake yamekuwa yanafunikwa na maji, likiwemo daraja la Jangwani, daraja la Mkwajuni, daraja la Mugabe katika barabara ya Shekilango na daraja la Kigogo.

Kwa sababu hii, shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zimekuwa zinasimama kwa muda. Usafiri wa umma unatatizwa siku nzima. Pia, kuna nyumba zinabomoka, samani kusombwa na maji, na watu kadhaa wasio na hatia kupoteza maisha. Vyombo vya ulinzi na usalama wa raia na mali zao vimekuwa vinafanya doria na kuthibitisha jambo hili.

Lakini sasa, huenda mateso haya kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, na hasa wale wanaokaa katika Bonde la Msimbazi, yakabaki ni historia. Tayari serikali ya Tanzania iko mbioni kutekeleza “Mradi wa Msimbazi” kwa ajili ya kukomesha maafa yanayotokana na mafuriko haya ya kila mwaka.

Kwa kushirikiana na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID), Benki ya Dunia (WB), na wadau wengine wa maendeleo, Serikali ya Tanzania imekamilisha andiko la “Mradi wa Msimbazi.”

Andiko hilo linataja mikakati ya kulifanya Bonde la Mto wa Mzimbazi kuwa mfano rejea wa suluhisho la kudumu dhidi ya majanga ya kibinadamu yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya mijini.

Kihistoria, mvua za El-Nino za mwaka 1997, ndizo zilianzisha mafuriko makubwa na hatarishi katika Bonde la Mto Msimbazi. Tangu wakati huo, yamekuwa yakitokea mafuriko karibu kila mwaka. Mafuriko yaliyotokea katika mwaka 2009, 2010, 2011, 2014, 2015, 2017 na mwaka 2018. Na sasa, mwaka 2019 umeongezea matukio mengine ya mafuriko ya aina hiyo.

Kuandaliwa kwa andiko la “Mradi wa Msimbazi” ni matokeo ya juhudu za pamoja zilizofanywa kwa miezi 9 kati ya Januari na Agosti 2019, kupitia vikao 30, vilivyoshirikisha wawakilishi 150 kutoka taasisi 59, pamoja na wananchi wapatao 1000.

Wadau muhimu ni pamoja na Manispaa ya Ilala, Manispaa ya Kinondoni, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Makamu wa Rais Kitengo cha Mazingira, na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Wengine ni Ofisi ya Rais Kitengo cha TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA), na Mamlaka ya Barabara Tanzania (TANRPADS).

Mchakato huu ulifadhiliwa na serikali ya Uingereza na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kwa ajili ya kuhuisha mchakato huu, hivi karibuni, ulifanyika mkutano maalum Jijini Dar es Salaam, mnamo tarehe 29 Novembea 2019. Katika mkutano huo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, George Simbachawene, aliiwakilisha Serikali ya Tanzania.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DFID) nchini Tanzania, Tim Bushell, aliwawakilisha wadau wa kimataifa waliofanya kazi kama wataalam washauri na wadhamini wa kifedha wakati wa kuandaa andiko la “Mradi wa Msimbazi.

Huu ni mradi mojawapo kati ya miradi mingine mingi inayotekelezwa na serikali ya Tanzania chini ya programu kabambe ya “Kuelekea Tanzania iliyo na Miji yenye Usalama wa Kudumu Dhidi ya Majanga ya Kibinadamu kwa Sababu ya Mabadiliko ya Tabianchi.” Yaani, “the Tanzania Urban Resilience Program” iliyoanza kutekelewa mwaka 1996.

Dira ya
Mradi wa Msimbazi” ni kulibadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni mzigo kwa wakazi wa Dar es Salaam mpaka kuwa bonde ambalo ni mtaji kwao, kwa kufanikisha mabadiliko yafuatayo:

Kukomesha ujenzi holela unaolifanya Bonde la Msimbazi kupotosha mkondo wa maji ya mvua, kuhatarisha mifumo ya kiikolojia na kutishia maisha ya watu, kwa kuzalisha ujenzi uliopangiliwa kwa kuzingatia kanuni za mipango miji utakaoliwezesha Bonde la Msimbazi kuongoza vizuri mkondo wa maji ya mvua, kulinda mifumo ya kiikolojia na kuboresha maisha ya watu.

Dhima yaMradi wa Msimbazi” kwa ajili ya kufukuzia dira iliyotajwa hapo juu inataja maeneo makuu matatu ya kimkakati (Strategic Result Areas-SRAs) yanayogawanyika katika matawi makuu manne ya kiutekelezaji (Key Result Areas-KRAs).

Katika eneo moja la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa mazingira hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa mazingira kwa kuchukua hatua tatu zitakazolifanya bonde hili liwe kama “mapafu katika mwili wa jiji.

Katika eneo la pili la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa maisha ya watu hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa maisha ya watu kwa kuchukua hatua tatu zitakazolifanya liwe kama “moyo katika mwili wa jiji.

Na katika eneo la tatu la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa maisha ya watu na mazingira hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa maisha ya watu na mazingira kwa kuchukua hatua za kiutawala zitakazolifanya liwe kama “moyo na mapafu katika mwili wa jiji.

Hatimaye, dhima yaMradi wa Msimbazi” kwa ajili ya kufukuzia dira iliyotajwa hapo juu inayagawanya maeneo makuu mawili ya kimkakati kwenye makundi makuu manne ya kiutekelezaji (Key Result Areas-KRAs), ambayo ni: kuzuia mafuriko kwa kushambulia chimbuko lake (“mitigation”), kuzuia madhara ya mafuriko kwa kuwalinda watu walio hatarini (“protection”), kubadilisha matumizi ya maeneo ya Bondo la Msimbazi yaliyomo katika hatari ya kushambuliwa na mafuriko mara kwa mara (“transformation”), na kujenga uwezo wa kitaasisi kwa kuunda mfumo wa uongozi shirikishi kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa Bonde la Msimbazi kwa weledi, kasi na ufanisi (“governance”).

Haya maeneo makuu manne ya kiutekelezaji (KRAs) yaliyo katika andiko la “Mradi wa Msimbazi” yamegawanywa katika mikakati kumi.

Mikakati mitatu ya kwanza ni: kuboresha mifumo ya kiikolojia na kuhuisha bayoanuai kwa kupanda miti; kuongeza uwezo wa bonde kupokea na kutunza maji ya mvua kwa kulinda sehemu za bonde zenye uwezo mkubwa wa kufyonza maji ya mvua; na kudhibiti mmomonyoko wa ardhi katika kuta za mto na kupunguza mchanga unaotuama kwenye kitako cha mto kwa kuzuia shughuli za kibinadamu karibu na mto.

Mikakati mingine mitatu ni: kuongeza uwezo wa mto kusafirisha maji kwenda kwenye mlango bahari wa Msimbazi ulioko Daraja la Salenda kwa kupanua kina chake, kuongeza upana wake na kujenga ngazi za kuongoza maji; kupunguza madhara ya mafuriko kwa wakazi walioko bondeni kwa kuinua kingo za mto; na kuhamisha mkazi na biashara za watu wanaokaa bondeni na kuwapeleka katika maeneo yaliyo salama dhidi ya mafuriko.

Mikakati mingine mitata ni: kuzuia uchafuzi wa mto unaofanyika kwa kutupa takamwili na maji machafu; kuzuia uchafuzi wa mto unaofanyika kwa kutupa taka ngumu kana kwamba mto huu ni dampo; na kujenga Subule ya Jiji kati ya Daraja la Salenda na Barabara ya Kawawa, ikiwa inajumuisha viwanja vya michezo, majengo ya makazi, biashara, mikutano na maofisi.

Na mkakati wa kumi ni kujenga uwezo wa kitaasisi kwa kuunda mfumo wa utawala utakaosimamia uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kwa na weledi, ufanisi, na kasi, katika kipindi cha miaka 50 kuanzia 2020 mpaka 2050, kinachogawanyika katika awamu fupi za miaka mitano mitano.

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” linaonyesha kuwa, angalu jumla ya Dola za Marekani milioni 114, sawa na trililioni za kitanzania 255, zinahitajika ili kuukamilisha.

Mchanganuo wa kibajeti unaonyesha kuwa, Dola za Marekani milioni 55 zinahitajika kwa ajili ya kukarabati nusu ya chini ya Bonde la Msimbazi. Dola za Marekani milioni 49 zinahitajika kukarabati nusu ya juu ya Bonde la Msimbazi. Gharama za kupanda miti, kusafisha taka ngumu zilizolundikana mtoni katika ukanda wa juu ya mto ni dola za Marekani milioni 10.

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” linapendekeza kwamba, katika pingili ya chini ya Bonde la Msimbazi zijengwe nyumba 12,000 za biashara, maofisi, supamaketi, na sebule za kuegesha magari. Pia inapendekezwa kuwa katika eneo hili zijengwe nyumba 2,500 za makazi ya watu.

Makadirio ya mtiririko wa mapato yatakayotokana na uwekezaji huu yanaonyesha kuwa, gharama za uwekezaji katika Bonde la Mto Msimbazi zinaweza kurejea ndani ya miaka 12, kila mwaka zikiwa zinarejea kwa asilimia 18.

Wasemavyo wanachi juu ya mradi

Tayari wakazi wa ukanda wa chini wa Bonde la Msimbazi wameunda jukwaa moja kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili na kutetea maslaji yao ya pamoja, kwa sauti moja. Jukwaa hilo linaitwa “Muungano wa Serikali za Mitaa 18,” au “M18” kwa kifupi.

Jukwa la M18 linajumuisha serikali za mitaa kumi (10) kutoka Manispaa ya Kinondoni na serikali za mitaa nane (8) kutoka Manispaa ya Ilala.

Serikali za mitaa zilizo katika Manispaa ya Kinondoni ni Mkunguni A, Mkunguni B, Hananasif, Kawawa, Sunna, Idrisa, Mwinyi Mkuu, Kigogo Mbuyuni, Kigogo Kati, na Mtaa wa Kigogo Mkwajuni.

Na serikali za mitaa zilizo katika Manspaa ya Ilala ni Charambe, Mtambani A, Mtambani B, Kariakoo Kaskazini, Misheni Kwota, Ilala Kwota, Msimbazi Bondeni na Mtaa wa Amana.

Jukwaa la M18 linaunganisha serikali za mitaa zilizoko katika eneo linalozungukwa na Barabara ya Kawawa, Barabara ya Mandela, Darala la Salenda, Barabara ya Umoja wa Mataifa inayopitia sekondari ya Tambaza, na Barabara ya Kigogo.

Jukwaa la M18 linao uongozi unaojumuisha Mwenyekiti, Katibu na Mratibu. Mwenyekiti ni Zainab Orty, kutoka Mtaa wa Amana, Ilala. Mratibu ni Godwin Cathbert Mapuga (52), kutoka Magomeni Mapipa, Mtaa wa Mwinyi Mkuu, Kata ya Mzimuni. Na Katibu ni Habiba Ally Mondoma (59), kutoka Magomeni Mapipa, Mtaa wa Sunna, Kata ya Magomeni.

Akiongea kuhusu “Mradi wa Msimbazi,” Mratibu wa M18, Godwin Cathbert Mapuga (52), alimwambia mwandishi maneno yafuatayo:

“Tukiwa ni wawakilishi wa wananchi tumeshiriki katika mchakato wa kuandaa mradi huu tangu Januari mpaka Agosti 2018.”

“Tulijumuika pamoja na watu wengi wengi kama 200 katika vikao vya majadiliano yaliyoshirikisha wananchi ili kujua matatizo yetu. Vikao vile vilijulikana kama vikao vya Charrete.”

“Nakumbuka kwamba, hata mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Mama Bella, alikuwa anahudhuria vikao hivyo.”

“Pia, mwakilisho wa Benki ya Dunia alisema kwamba fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu ipo tayari, isipokuwa kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa taratibu za kiserikali.”

“Hata wafadhili wengine walioshiriki vikao cha Charrete walionyesha nia ya kuwezesha mradi na kutwambia kwamba fedha ziko tayari,” alimalizia maelezo yake Mapuga.

Naye Katibu wa M18, Habiba Ally Mondoma (59), alimwambia mwandishi wa makala hii, maneno yafuatayo:

“Katika mradi wa Msimbazi, tunayo imani kubwa Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo; pamoja na Waziri anayeshughulikia Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, George Simbachawene.”

“Nakumbuka, TAMISEMI ndio wasimamizi wa mradi huu, na walikwisha mwaandikia Waziri wa Fedha, kumshauri aanzishe mchakato wa kuomba fedha kutoka Benki ya Dunia.”

“Mwezi Machi 2019 sisi viongozi wa M18 tulikwenda Dodoma kuongea na Katibu Mkuu Hazina, Dotto James, juu ya mradi huu. Tulionana naye na kumkabidhi barua yenye maombi yetu.”

“Tulijibiwa kwa njia ya kupewa nakala ya barua iliyowaandikwa kwenda TAMISEMI.”

“Katika barua hiyo, Katibu Mkuu Hazina, aliwaomba TAMISEMI kutuelimisha kuhusu utaratibu wa kuomba fedha za mikopo kutoka benki ya Dunia. Barua inasema kuwa mchakato ni mrefu na tunapaswa kuwa na subira.”

“Hata hivyo, mpaka sasa hatuna taarifa mpya kutoka serikalini zinazotufahamisha mradi huu umefikia wapi.”

“Hivyo, tumemwandikia tena Katibu Mkuu wa Hazina, Dotto James, kutaka kujua kinachoendelea juu ya mradi huu. Mpaka sasa hatujajibiwa barua ya pili.”

“Hivyo, tumeazimia kwenda Dodoma tena, kwa Katibu Mkuu wa Hazina, kufuatilia suala hili kusudi tujue hatima yake, kwani tunaona kuwa wananchi wetu wanateseka wakati tumekwisha tangaziwa kwamba tayari fedha ya mradi imekwishapatikana.”

Dakta Wilson Babyebonela, ni mkazi wa Kijitonyama Mtaa wa Bukoba na Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kampala International University, Kampasi ya Dar es Salaam. Anaufahamu Mradi wa kukarabati Bonde la Mto Msimbazi kwa sababu kadhaa.

Kwanza ni mkazi wa kata iliyo katika Bonde hilo. Na pili, katika masomo yake ya Uzamivu aliandika shahada ya uzamivu iliyochunguza mfumo wa uzalishaji na uzoaji wa taka ngumu katika Manispaa ya Kinondoni.

“Tatizo la kutupa taka ngumu katika Mto Msimbazi na tawi lake la Kijito cha Sinza ni kubwa. Nimefurahi kuona kwamba Andiko la Mradi wa Kukarabati Bonde la mto huu linaelekeza sehemu ya bajeti yake katika eneo hili pia,” anasema Dk. Babyebonela.

Profesa Anna Tibaijuka aliwahi kuwa Waziri wa Nyumba na Makazi. Kwa mujibu wa Tibaijuka, kabla ya kufika kwenye Daraja la Salenda maji yanapoingia bahari ya Hindi, Bonde la Msimbazi ndiyo njia pekee kwa maji yote yanayotoka Vilima vya Pugu, Ukonga, Uwanja wa Ndege, Tazara, Tabata, Kigogo, Magomeni, Ilala, Manzese, Tandale, Magomeni Kagera, Hananasif, Muhimbili, na viwanja vya Jangwani.

“Hutakiwi kuwa Mtaalam wa Mipango Miji kufahamu kuwa maji hujitafutia njia yake kwa kuzingatia kanuni ya uzito. Pia, hutakiwi kuwa mtaalam sana ili kufahamu kuwa kuna baadhi ya miaka mvua nyingi zitanyesha kwa wingi. Mambo yote haya yanatabirika,” alisema Profesa Tibaijuka.

Kwa hiyo, “tatizo siyo mvua kubwa bali tatizo ni kuzibwa kwa njia asilia ya maji ya mto, hivyo maji ya mvua kushindwa kwenda baharini,” anafafanua Profesa Tibaijuka. Kwa maoni yake, “bila nidhamu ya kuheshimu Mipango miji mafuriko yatakuwa sifa ya kudumu ya jiji la Dar es Salaam.”


Picha Na. 00: Eneo uliko Mradi wa Msimbazi
Msimbazi--Picha 11.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework
(Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.iv).”

Wasemavyo serikali juu ya mradi

Changamoto zilizomo katika “Bonde la Mto Msimbazi” zinayo historia ndefu na hivyo, tayari zimeongelewa na vongozi mbalimbali wa ngazi za juu serikalini.

George Simbachawene ni Waziri Katika Ofisi ya Makamu wa Rais Kitengo cha Mazingira. Anasema kuwa serikali iko mbioni kutekeleza Mradi wa Msimbazi.

“Mradi huu utaleta manufaa makubwa katika Jiji la Dar es Salaam kwa kubadili maeneo yaliyo hatari kwa mafuriko na kuyafanya salama kwa maendeleo ya jiji,” anasema Waziri Simbachawene.

“Ni mradi ambao utapendezesha jiji kwa kuweka maeneo mazuri ya maegesho ya magari, maeneo kwa ajili ya shughuli za umma kama mikutano na matamasha na kubadilisha eneo la Mto Msimbazi kuwa eneo linalofaa kwa ajili ya michezo na lenye manufaa ya kiikolojia kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam,” anafafanua Waziri Simbachawene.

Selemani Jafo ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais kitengo cha TAMISEMI. Jafo ndiye Waziri mwenye dhamana na mradi huu kwa niaba ya serikali.

“Sasa tunalo andiko la Mradi wa Msimbazi, na serikali ya Tanzania iko tayari kuutekeleza mradi huu, kwa kushirikiana na jumuiya ya wadau wa maendeleo,” anasema Jafo.

Kisha Waziri Jafo anasisitiza kwamba, ni muhimu na lazima kwa serikali kuunga mkono Mradi wa Msimbazi kwa sababu, kupitia mradi huu tunaweza kupata faida kuu mbili.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo, faida ya kwanza ni kuwa, kupitia mradi huu “tunaweza kupenyeza pumzi ya uhai mpya katika mapafu ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufufua kazi za mifumo ya kiikolojia iliyoko katika Bonde la Msimbazi.”

Na faida ya pili, kwa mujibu wa Waziri Jafo, ni kwamba, kupitia mradi huu tunaweza “kufungua milango ya fursa za maendeleo kwa kuugeuza ukanda hatari wa Bonde la Msimbazi kuwa eneo salama na lenye majengo ya kisasa katika kitovu cha mkoa wa Dar es Salaam.”

Mhandisi Nyariri Nanai ni Mratibu wa “Mradi wa Msimbazi” kupitia Ofisi ya Rais, Kitengo cha TAMISEMI. Mnamo tarehe 03 Januari 2020, mwandishi wa makala hii alimtembelea ili kujua utekelezaji wa “Mradi wa Msimbazi” umefikia hatua gani. Maongezi yalifanyika kwenye ofisi yake iliyoko katika Ofisi za TAMISEMI, ndani ya jengo la Millenium Tower, Kijitonyama ya Jijini Dar es Salaam.

“Bado serikali inajipanga ili kuona njia bora zaidi ya kutekeleza Mradi wa Msimbazi. Mpaka sasa kilichopo mikononi mwetu ni dhana ya mradi, yaani concept note. Tunaifanyiwa upembuzi yakinifu,” anasema Nanai.

“Hivyo, sisi TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha tunafanya upembuzi yakinifu ili kuona kama kukopa fedha kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Msimbazi ni mtaji au mzigo kwa Taifa, maana uamuzi wa kukopa fedha kutoka nje unamaanisha kuongezeka kwa deni la Taifa,” anafafanua Nanai.

Kisha, Nanai anasisitiza kuwa “kabla ya hatua nyingine yoyote kuchukuliwa na serikali ni lazima kwanza serikali ijiridhishe kama uamuzi wa kukopa fedha kutoka Benki ya Dunia au kwingineko utakuwa na tija kwa Taifa.”

Kwa mujibu wa andiko la “Mradi wa Msimbazi,” sera ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) itatumika katika kuhakikisha fedha yote inayohitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi huu inapatikana.

Mazingira ya kihistoria

Kwa mujibu wa Ramani ya Mipango Miji ya Dar es Salaam (1979), Bonde la Msimbazi limetengwa kama hifadhi maalum isiyopaswa kutumika kwa ajili ya makazi ya watu, ispokuwa kwa ajili ya matumizi kama kituo cha burudani za nje.

Sababu kuu ya uamuzi huu ni ukweli kwamba, tangu miaka ya 1975, Mto Msimbazi ulikuwa ni mto wenye mkondo wa maji kwa mwaka mzima. Hivyo, Bonde la Msimbazi, lilikuwa na manufaa makubwa ya kiikolojia kama vile kudhibiti mafuriko, kuchuja taka ngumu zinazotupwa mtoni, na kufanikisha kilimo cha mazao ya msimu kama vile mboga na maua.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, hali imebadilika kwa sababu mbalimbali zinazalisha mafuriko ya kila mara.

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” linasema kuwa, baada ya mvua za El-Nino za mwaka 1997, kilichozoeleka kuwa ni mto wa kudumu na ulio rafiki wa watu, uligeuka kuwa mto wa msimu ulio adui wa watu.

Tunaelezwa kuwa, wakati wa kiangazi, kitako cha mto huu kilianza kukauka kabisa. Na katika majira ya mvua mto huu ulibadili tabia yake ghafla. Mvua za masa machache ziliufanya mto kufufuka na kusababisha mafuriko makubwa. Katika muda mfupi Bondo la Msimbazi lilianza kufurika, maji yakiwa yamejaa na kuinuka kwa kiasi cha meta mbili au zaidi juu ya kingo za mto.

Kwa sababu ya mafuriko haya, vifo, upotevu, na uhamisho wa watu wasio na hatia ni miongoni mwa madhara yaliyoshuhudiwa. Aidha, uharibifu wa mali za watu, barabara, madaraja, hospitali, shule na miundombinu baki ya kijamii ni miongoni mwa madhara hayo.

Kadhalika, shughuli za kilimo cha mazao ya chakula husimama, sehemu za wazi kwa ajili ya michezo na mapumuziko hufunikwa na maji yenye matope, na ukosefu wa maji yasiyo na matope kwa ajili ya kunywa hutokea.

Wakati mwingine, mafuriko haya huambatana na majanga kama vile ukame, magonjwa ya mazao ya kilimo, vifo vya mifugo, na ujio wa maradhi mapya ya watu.

Kwa ujumla, Bonde la Mto Mzimbazi, liligeuka kuwa kitovu cha mafuriko ya kila mwaka tangu mwaka 1997, wakati wa mvua za El-Nino. Tangu wakatyi huo kuna mafuriko yaliyotokea mwaka 2009, 2010, 2011, 2014, 2015, 2017 na mwaka 2018. Mafuriko yanayotokea mwaka 2019 na 2020 ni mwendelezo wa historia hii.

Mara tu baada ya mafuriko ya mwaka 2011, kaya 680 zilizoathirika zilihamishwa na kupewa viwanja huko Mabwepande, kilometa 25 Kaskazini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Viwanja 1,007 vilipimwa na watu 3,400 kuhamishiwa huko. Mfumo wa maji ya bomba uliwekwa na shule za msingi kujengwa.

Hata hivyo, watu wengi waliohamishiwa huko, walirudi katika Bonde la Msimbazi mara tu baada ya mvua kupungua. Sababu zinazotajwa na watu waliorudi bondeni ni pamoja na uhaba wa shughuli za kiuchumi kwa wanaotaka kujiajiri na ukosefu wa huduma za usafiri wa umma kwa ajili ya kuwapeleka watu katika maeneo yenye fursa za kujiajiri na soko la huuduma ndogo ndogo.

Kwa hiyo, umuzi wa kurudi katika Bonde la Msimbazi ulisukumwa na dhamira ya kusaka shughuli za uchumi wa kujiajiri na kujinufaisha na huduma za kijamii zinazopatikana latika maeneo yaliyo karibu na kitovu cha Jiji la Dar es Salaam. Sababu hizi mbili zikawafanya watu wasahau ukubwa wa hatari zinazoambatana na mafuriko.

Ni katika mazingira haya, mwaka 2015, serikali iliendesha opereshani ya kuvunja nyumba zipatazo 700 za wakazi wa Bonde la Msimbazi katika kata ya Hananasif, Wilaya ya Kinondoni. Lengo lilikuwa ni kuwatimua watu waliokuwa wamevamia eneo la meta 60 kutoka kwenye mto. Baada ya kilio cha umma na amri ya mahakama iliyolitaja zoezi hilo kama haramu kisheria, operesheni ilisitishwa.

Picha Na. 01: Mafuriko katika Bonde la Msimbazi, eneo la Vingunguti, mwaka 2012
Msimbazi--Picha 00.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.16).”

Kwa ujumla, andiko la “Mradi wa Mzimbazi” linaeleza kwamba, mafuriko ya Bonde la Msimbazi yanaambatana na matatizo makuu nane yanayohitaji majibu ya kisera na kisheria.

Kuna ujenzi wa makazi ya watu katika maeneo ya mafuriko; mmomonyoko wa ardhi; ujenzi wa miundombinu kusababisha mikingamo dhidi ya maji ya mvua; utupaji hovyo wa takangumu; uhaba wa mifereji ya kusafirisha maji ya mvua na maji machafu; udhibiti wa chimbuko na madhara ya mabadiliko ya tabianchi; uharibifu wa mazingira; na kuboresha maisha ya watu wanaoishi katika bonde la Msimbazi.

Kwa ujumla, pamoja na kasi kubwa ya ukuaji wa watu, inakadiriwa kwamba kiasi cha makazi ya watu yaliyopimwa na kuendelezwa jijini Dar es Salaam ni asilimia 30 pekee.

Hivyo, andiko la “Mradi wa Msimbazi” linabainisha kwamba, chimbuko la mafuriko katika Bonde la Msimbazi ni mto kutumiwa na wakazi kama dampo la taka ngumu; ukataji wa miti; mmomonyoko wa udongo kutokana na uchimbaji wa mchanga; ujenzi holela wa makazi ya watu; na mvua nyingi zinazonyesha kiholela kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Maji ya mvua hizi hubeba taka ngumu na udongo uliomomonyolewa na kuupeleka katika maeneo ya mianya finyu kama vile madaraja katika Mto Msimbazi, ambayo huziba na kusababisha mafuriko.

Mazingira kijiografia

Mkondo wa maji ya Mto Msimbazi unatiririka kuanzia katika vilima vya Pugu-Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, vilivyoko kilometa 16 Magharibi mwa kitovu cha Jiji la Dar es Salaam.

Mto huu unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi kupitia Daraja la Salanda. Maji haya humwagika baharini baada ya kutembea safari ndefu inayokatiza bonde linalounganisha wilaya za Kinondoni, Ilala na Kisarawe.

Katika bonde hili, lenye eneo la kilometa za mraba 271, Mto Msimbazi hupokea maji ya ziada kutoka matawi yake kama vile Mto Kimanga, Mto Kibangu, Mto China na Mto Ng’ombe.

Kijiografia, andiko la “Mradi wa Msimbazi” limegawanya Bonde la Msimbazi katika pingili kuu nne, kuanzia vilima vya Pugu-Kazimzumbwi hadi kwenye mlango bahari wa Msimbazi unaomwaga maji katika Bahari ya Hindi. Kuna ukanda wa juu (upper basin), ukanda wa kati (middle basin), ukanda wa kati (middle basin), ukanda wa kati chini (lower middle basin), na ukanda wa chini (lower basin).

Picha Na. 02: Kanda nne za Bonde la Msimbazi
Msimbazi--Picha 02.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.20).”

Mafuriko makubwa na hatarishi hutokea katika ukanda wa kati na ukanda wa chini wa Bonde la Msimbazi, na kusababisha uharibifu mkubwa wa makazi na mali za wananchi pamoja na miundombinu ya kijamii inayowazunguka.

Katika ukanda wa juu wa Bonde la Msimbazi, shughuli za kujenga makazi ya watu hufanyika na kubadilisha matumizi ya ardhi, ambapo, mashamba hugeuzwa makazi ya watu au maeneo ya kibiashara. Kwa sababu hii, maji ya mvua hushindwa kuzama ardhini kwa urahisi.

Badala yake maji haya huingia katika Mto Msimbazi kama maporomoko makubwa yanayobeba taka ngumu nyingi kutoka kwenye makazi ya watu.

Ukanda wa juu na ukanda wa kati chini wa Bonde la Mto Msimbazi ni sehemu zilizoendelezwa hadi kupata sura ya mji inayoambatana na idadi kubwa ya wakazi. Kingo za mto katika ukanda huu zinapata misukosuko mingi hadi kumomonyoka kwa kasi.

Na ukanda wa chini wa Bonde la Mto Msimbazi unazo hekta 400 zinazokwenda mpaka kwenye mlango bahari wa Msimbazi unaomwaga maji katika Bahari ya Hindi. Huu ni uwanja wa mafuriko uliofunikwa na msitu wa miti ya mikoko, matope na taka ngumu zinazosombwa na mafuriko ya maji.

Mazingira ya kiutawala na kidemografia

Dar es Salaam ni jiji ambalo liko miongoni mwa majiji 20 duniani, yanayokua kwa kasi kubwa duniani, kiasi kwamba.

Jiji hili unakadiriwa kuwa na wakazi 6,000,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018. Inakadiriwa kuwa, ifikapo mwaka 2030, Dar es Salaam itakuwa na wakazi milioni 10. Kwa upekee, Bonde la Mto Msimbazi linabeba 27% ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, sawa na watu milioni 1,600,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018.

Wakazi hawa wametawanyika katika kata 24. Kwa kuzingatia sensa ya mwaka 2012, kata husika, pamoja na wakazi wake katika mabano, ni kama ifuatavyo: Hananasifu (37,115), Kijiitonyama (58,132), Ubungo Kisiwani (28,008), Tabata (74,742), Upanga (24,643), Mwanyamala (50,560), Kikogo (57,613), Vingunguti (106,946), na Kisutu (8,308).

Pia kuna kata za Makumbusho (68,093), Mabibo (85,735), Segerea (83,315), Kariakoo (13,780), Manzese (70,507), Ukonga (80,034), Magomeni (24,400), Ubungo (28,008), Pugu (49,422), Ilala (31,083), Sinza (40,546), Jangwani (17,647), Tandale (54,781), Buguruni (70,585), na Ngugumbi (36,841).

Inakadiriwa kuwa, ifikapo mwaka 2030, wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi wataongezeka kutoka watu 1,600,000 za sasa mpaka watu 2,500,000.

Kwa ujumla, andiko la “Mradi wa Msimbazi” linaonyesha kwamba, wakazi 50,000 wako katika hatari ya kufunikwa na mafuriko kila mwaka; na kwamba nyumba 9,000 ziko katika hatari ya kufunikwa na mafuriko kila mwaka, na hivyo hazifai kwa maisha ya watu.

Picha Na. 03: Mipaka ya Kiutawala katika Bonde la Msimbazi
Msimbazi--Picha 03.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.43).”

Sababu za mafuriko ya Msimbazi

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” linataja sababu sita za mafuriko. Kuna ujenzi holela wa makazi na viwanda karibu na kingo za mto, mmomonyoko wa ardhi katika kingo za mto, miundombinu inayogeuka vizingiti vya maji, kutumia mto kama dampo la taka ngumu na majitaka, ukosefu wa mifereji ya maji ya mvua na majitaka, na mwinuko wa usawa wa bahari kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu ujenzi holela wa makazi na viwanda karibu na kingo za mto, tayari maeneo yaliyo karibu na kingo za Mto Msimbazi yamejengwa viwanda na makazi holela ya watu. Ujenzi huu unasababisha taka ngumu kutupwa mtoni. Tabia hii ya kutupa hovyo taka ngumu inapunguza kina cha mto; inaongeza upana wa mto; inaharibu uoto wa asili kama vile miti ya mikoko; inapunguza uwezo wa ardhi tifutifu kufyonza maji ya mvua; na inamomonyoa kingo za mto.

Kuhusu ukataji holela wa miti katika Bonde la Msimbazi, na hasa katika hifadhi ya misitu ya Pugu-Kazimzumbwi, miti inakatwa kwa sababu ya kutafuta kuni na nguzo za ujenzi. Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, inakadiriwa kuwa eneo la nchi kavu lililokuwa linafunikwa na majani ya misitu ya Pugu limepungua kwa 25%, wakati eneo la nchi kavu lililokuwa linafunikwa na majani ya misitu ya Kazimzumbwi limepungua kwa 31%.

Picha Na. 04: Ukataji wa miti katika Misitu ya Pugu na Kazimzumbwi
Msimbazi--Picha 04.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.28).”

Kuhusu mmomonyoko wa ardhi katika pingili za juu za mto, jambo hili huzalisha mlundikano wa mchanga katika kitako cha mto kwenye pingili za chini za mto. Shughuli za binadamu katika kingo za mto, hasa tabia ya kuchimba mchanga kutoka mtoni, zinasababisha sana tatizo hili.

Mchanga hupunguza kina cha mto na kuongeza upana wa mto. Katika sehemu zenye madaraja mchanga huu hupunguza kipenyo cha mkondo wa maji. Na karibu na mlango bahari wa Msimbazi, mchanga hufunika mizizi ya miti ya mikoko kwa kiwango ambacho huinyima hewa na hatimaye mikoko kunyauka na kufa. Jambo hili huharibu uhai wa mtandao wa kiikolojia katika Bode la Mto Mzsimbazi.

Picha Na. 05: Mmomonyoko wa ardhi na mlundikano wa mchanga Mto Msimbazi
Msimbazi--Picha 05.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.30).”

Kuhusu miundombinu inayogeuka vizingiti vya maji, kuna madaraja yenye kipenyo kidogo cha mkondo wa maji kwa sababu ya kuminywa na mchanga pamoja na taka ngumu. Jambo hili hupunguza kasi ya mkondo wa maji.

Barabara nyingi zinazokatiza Mto Msimbazi zina madaraja yenye mwanya kidogo kwa ajili ya maji mengi kupita nyakati za mvua kubwa. Madaraja haya hugeuka kuta za maji wakati wa mvua kubwa na hivyo kusababisha madimbwi ya muda na hatimaye mafuriko yanayofunika daraja husika.

Picha Na. 06: Daraja la kina kifupi, taka ngumu zinazoziba njia nyembamba za maji
Msimbazi--Picha 06.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.33).”

Kuhusu utupaji wa takangumu na majitaka katika Mto Msimbazi, na hivyo kuutumia mto kama dampo la taka ngumu na majitaka, chanzo ni ukosefu wa mfumo thabiti kwa ajili ya kusimia uzoaji wa taka ngumu na usafirishaji wa maji taka.

Kwa mujibu wa takwimu za mkoa wa Dar es Salaam katima mwaka 2015, taka ngumu zinazalishwa kwa kasi ya wastani wa kilo moja kwa siku kwa kila mtu, sawa na tani 6,000 kwa siku, au tani 1,800,000 kwa mwaka. Ni sehemu ndogo ya taka hizi, karibu na 37%, ndio huzolewa kupitia mfumo rasmi.

Na sehemu ya taka ngumu iliyobaki hutupwa hovyo katika maeneo ya wazi, barabarani, na mitoni. Hatimaye, mafuriko huzoa taka hizi na kuzipeleka mpaka kwenye madaraja au katika mizizi ya miti ya mikoko zinakonaswa na kupunguza njia ya maji, na hatimaye kudhoofisha kasi ya mkondo wa maji ya mto.

Picha Na. 07: Utupaji holela wa taka ngumu katika Bonde la Msimbazi
Msimbazi--Picha 07.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.34).”

Kuhusu ukosefu wa mifereji ya maji ya mvua na majitaka, hii ni sababu nyingine ya mafuriko katika Bonde la Msimbazi. Kati ya mifereji ya maji ya mvua iliyoko kandoni mwa barabara, zaidi ya 50% imezibwa na taka ngumu, matope na mchanga.

Aidha ni 13% ya wakazi wa jiji wenye kunufaika na huduma za mfumo wa majitaka. Wwatu wengine 87% ama hutumia vyoo vya shimo au hutumia mfumo wa maji ya mvua kama mfumo wa majitaka. Hivyo, uhaba wa mifereji ya maji ya mvua na mfumo wa majitaka huchangia katika ukubwa wa mafuriko ambapo maji ya mafuriko huwa na kiasi kikubwa cha kinyesi na mkojo.

Na kuhusu kuinuka kwa usawa wa bahari kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, hiki nacho ni chanzo cha mafuriko katika Bonde la Msimbazi. Ongezeko la gesi ya kaboni angani ni sababu muhimu ya mabadiliko ya tabianchi. Gesi ya kaboni huongeza joto katika uso wa sayari. Kwa mfano, kati ya 1901 and 2012, gesi hii imesababisha joto katika uso wa dunia kuongezeka kwa kiasi cha nyuzi sentigredi 0.89. Ongezeko la halijoto husababisha mvua kubwa ambazo husababisha maji mengi baharini, na hivyo mwinuko wa usawa wa bahari. Ndani ya karne iliyopita, usawa wa bahari umeinuka kwa wastani wa sentimeta 19. Mwinuko wa usawa wa bahari husababisha mabadiliko katika mipaka ya eneo la nchi kavu linalohusiana na kujaa na kupwa kwa maji ya bahari. Katika milango bahari, kama vile mlango bahari wa Msimbazi, jambo hili husababisha mafuriko katika ukanda wa chini wa mto.

Hatimaye, sababu hizi saba huzalisha mafuriko pale mvua zinaponyesha, vifo vya watu wasio na hatia, uharibifu wa nyumba, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii.

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” linaonyesha kuwa miundombinu ya kiuchumi ifuatayo iko hatarini: Daraja la Salenda katika Mto Msimbazi River, daraja katika Barabara ya Mkwajuni katika mto Sinza, daraja la Jangwani katika Mto Msimbazi, na daraja katika Barabara ya Kawawa katika Mto Msimbazi.

Pia kuna daraja katika Barabara ya Nelson Mandela katika Mto Msimbazi, daraja katika Reli ya TAZARA, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bohari ya Kampuni ya Mabasi ya Mwendokasi (DART), Bohari ya kiwanda cha simenti, na eneo la viwanda lililoko karibu na barabara ya Mandela. Aidha, kuna kituo cha Mabasi ya Mwendokasi katika eneo hili, karibu na daraja la Jangwani lililoko kwenye Barabara ya Morogoro.

Sababu zinazozalisha tabia hatarishi miongoni mwa wananchi ni pamoja na unafuu wa gharama za ujenzi katika eneo hili, upatikanaji wa ardhi ya kilimo kwa urahisi, ukaribu wa huduma na fursa zilizo katikati ya jiji, na ujinga wa watu juu ya madhara hasi ya mafuriko.

Picha Na. 08: Dafina zinazoshambuliwa na mafuriko katika Bonde la Msimbazi

Msimbazi--Picha 08.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.22).”

Changamoto zinazotokana na mafuriko ya Msimbazi

Kwa mujibu wa andiko la “Mradi wa Msimbazi” kuna changamoto kumi zinazohusiana na mafuriko katika Bonde la Msimbazi.

Changamoto ya kwanza ni uharibifu wa maeneo ya misitu inayofyonza gesi ya kaboni kutoka angani. Uharibifu huu unachangia katika kukuza tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuchukua hatua za kuzuia mabadiliko ya tabianchi na kupunguza makali yake kwa kukarabati mtandao wa kiikolojia katika Bonde la Msimbazi kupitia upandaji na ulinzi wa miti.

Changamoto ya pili ni uharibifu wa ardhi tifutifu ambako maji ya mvua hupokelewa na kufyonzwa, na hivyo, uwezo mdogo wa Bonde la Msimbazi katika kupokea na kuhifadhi maji ya mvua. Jambo hili linayaachia maji yatiririke kuelekea kwenye mlango bahari wa Msimbazi, na hivyo kuzalisha mafuriko.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuchukua hatua za kujenga na kukarabati mfumo wa kuhifadhi maji ya mvua kwa kujenga mabwawa, madimbwi, kujenga visima vya kuvuna maji ya mvua na kulinda maeneo yenye ardhi tifutifu katika Bonde la Msimbazi

Changamoto ya tatu ni mlundikano mkubwa wa mchanga na taka ngumu katika mkondo wa maji ya mto kwa sababu ya mmomontoko wa ardhi na shughuli za kibinadamu zinazohusiana na uchimbaji wa mchanga. Kwa hiyo, kitako cha mto kimeinuka; upana wa mto kuongezeka, na hasa wakati wa mafuriko; na mwanya wa mkondo wa maji chini ya madaraja umepungua. Hatimaye, kasi ya mkondo wa maji imepungua.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuondoa taka ngumo katika mto, kuuchonga mto ili kuongea kina chake, na hivyo kuyaongoza maji kuelekea kwenye mlango bahari wa Msimbazi kwa kasi kubwa zaidi.

Changamoto ya nne ni tofauti kati ya kasi ya maji yanayoingia katika Mto Msimbazi kutoka vilima vya Pugu na Kazimumbwi na kasi ya maji yanayoingia Bahari ya Hindi kupitia mlango bahari wa Msimbazi. Kasi ya maji yanayoingia ni meta za ujazo 80 kwa sekunde, wakati kasi ya maji yanayotoka ni kati ya meta za ujazo 400 kwa sekunde na meta za ujazo 600 kwa sekunde. Tofauti huu ni chanzo cha mafuriko.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuongeza ujazo wa mto na kuongeza mwinuko wa mkondo wa maji kwa kutengeneza ngazi zitakazoongoza maji kwenda Baharini.

Changamoto ya tano ni mafuriko makubwa wakati wa mvua kubwa sana, yenye uwezo wa kuvuka mipaka ya ngazi zitakazojengwa kwa ajili ya kuongoza maji.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuwepo na mpango mkakati wa kulinda watu, mali na biashara zao dhidi ya mafuriko yenye ukubwa ulipindukia.

Changamoto ya sita ni ulazima wa kuwahamisha wakazi wa Bonde la Msimbazi ili waweze kupisha ujenzi na ukarabati unaokusudiwa. Kuna nyumba 8,500 zilizo katika aneo linalohitaji kujengwa upya, na nyumba 10,000 zilizo katika hatari ya kumezwa na mafuriko.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuweka na kutekeleza mpango wa kuhamisha watu walioko Bonde la Msimbazi.

Changamoto ya saba ni uchafuzi wa Mto Msimbazi kutokana na taka za kibayolojia na taka za kikemia, jambo linaloufanya mto usifae kwa matumizi ya kilimo au kwa matumizi ya nyumbani.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kusafisha Mto Msimbazi kwa lemgo la kuhakikisha kuwa maji yake yanaweza kutumika mashambani na majumbani.

Changamoto ya nane ni uchafuzi wa Mto Msimbazi kutokana na taka ngumu zinazotokana na ujenzi na shughuli za viwandani. Inakadiriwa kuwa tani 180,000 kwa mwaka zinatupwa katika Bonde la Msimbazi.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kubuni mfumo wa menejiementi ya taka ngumu katika Bonde la Msimbazi.

Changamoto ya tisa ni ukosefu wa maeneo ya wazi yaliyo na uoto wa kijani yanayotosheleza mahitaji ya wakazi milioni sita wa Jiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya mapumziko, burudani, makazi na biashara. Pia inaonekana kuwa upungufu wa maeneo ya wazi yaliyo na uoto wa kijani unawaathiri zaidi watu wanyonge katika jamii, kama vile wazee, wanawake na watoto, kwani matajiri wanao uwezo wa kujenga na kumiliki bustani za miti na maua nyumbani kwao.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuwajali watu wanyonge katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwajengea sebule za mapumziko na burudani zenye uoto wa kijani na hewa safi.

Na changamoto ya kumi ni ukosefu wa uwezo wa kitaasisi katika Jiji la Dar es Salaam unaohitajika kukabiliana na changamoto zilizo katika Bonde la Msimbazi. Wizara, Idara na Wakala wa serikali ni vyombo vilivyo na majukumu yanayokomea katika sekta husika. Lakini, changamoto zilizo katika Bonde la Msimbazi zinahitaji chombo chenye majukumu mtambuka, kwa kiwango kinachovuka mipaka ya Wizara, Idara na Wakala wa serikali.

Hivyo, andiko la mradi linapendekeza kuwa, kuna haja ya kuunda chombo cha kusimamia utekelezaji wa “Mradi wa Msimbazi” chenye madaraka mtambuka.

Kwa sababu ya changamoto hizi, andiko la “Mradi wa Msimbazi” linawaalika wahandisi, wanaikolojia, maafisa mipango miji, watunga sera, wanasheria na watawala kuunganisha nguvu kwa ajili ya kukabili changamoto zilizomo katika “Bonde la Msimbazi” kwa kufukuzia dira ya pamoja inayowataka kutekeleza mikakati minne, iliyogawanyika kwenye mbinu 10 na majukumu 48, kama inavyosimuliwa hapa chini.

Dira ya mradi

Muundo wa “Mradi wa Msimbazi” ulio katika andiko la “Mradi wa Msimbazi” unajumuisha dira, dhima, mikakati, mbinu, majukumu na matokeo. Aya zifuatazo zinafafanua mambo haya hatua kwa hatua.

Dira yaMradi wa Msimbazi” ni kulibadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni mzigo kwa wakazi wa Dar es Salaam mpaka kuwa bonde ambalo ni mtaji kwao, kwa kufanikisha mabadiliko yafuatayo:

Kukomesha ujenzi holela unaolifanya Bonde la Msimbazi kupotosha mkondo wa maji ya mvua, kuhatarisha mifumo ya kiikolojia na kutishia maisha ya watu, kwa kuzalisha ujenzi uliopangiliwa kwa kuzingatia kanuni za mipango miji utakaoliwezesha Bonde la Msimbazi kuongoza vizuri mkondo wa maji ya mvua, kulinda mifumo ya kiikolojia na kuboresha maisha ya watu.

Kwa maneno mengine, dira ya “Mradi wa Msimbazi” ni kulibadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa maisha ya watu kwa sababu ya mafuriko hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa maisha ya watu kwa sababu ya kufanya kazi kama “moyo na mapafu ya jiji” la Dar es Salaam.

Yaani, kuna shabaha ya kulibadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni mzigo kwa wakazi wa Dar es Salaam mpaka kuwa bonde ambalo ni mtaji kwao.

Ndio kusema kwamba, kuna dhamira ya kulibadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde la mafuriko hadi kuwa sebule ya jiji ambayo ni mfano rejea duniani kwa sababu ya kuwa na ngazi za kuongoza maji ya mafuriko, viwanja vya burudani vilivyopambwa na uoto wa kijani, na majumba makubwa ya kisasa yanayofaa kwa kwa ajili ya matumizi ya makazi, biashara na burudani.

Dhima ya mradi

Dhima ya
Mradi wa Msimbazi” kwa ajili ya kufukuzia dira iliyotajwa hapo juu inataja maeneo makuu matatu ya kimkakati (Strategic Result Areas-SRAs) yanayogawanyika katika matawi makuu manne ya kiutekelezaji (Key Result Areas-KRAs).

Katika eneo moja la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa mazingira hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa mazingira kwa kuchukua hatua tatu zitakazolifanya bonde hili liwe kama “mapafu katika mwili wa jiji.

Hatua ya kwanza, ni kupanua ukubwa wa eneo la kijani katika ukanda wa misitu asilia ya hifadhi ya Pugu-Kazimzumbwi. Hatua ya pili, ni kwa kupanua ukubwa wa eneo la kijani linalofunikwa na vichaka katika kingo za Mto Msimbazi. Na hatua ya tatu, ni kwa kupanua ukubwa wa eneo linalofunikwa na miti ya mikoko lililopo kati ya Hananasif na Upanga.

Hatua hizi tatu zinakusudiwa kuzalisha matokeo matatu muhimu. Tokeo la kwanza ni kuongezeka kwa uwezo wa Bonde la Msimbazi kutunza kiasi kikubwa cha maji yake katika maeneo mvua zinakonyesha badala ya maji hayo kutiririka na kwenda maeneo mengine kwa njia ya mfuriko.

Tokeo la pili ni kuongezeka kwa uwezo wa Bonde la Msimbazi kutumika kama bohari kubwa ya kutunza kiasi kikubwa cha hewa ya kaboni, baada ya kuifyonza kutoka angani, na hivyo kuchangia katika kuzuia mabadiliko ya tabianchi.

Na tokeo la tatu ni kuongezeka kwa uwezo wa kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kujenga sebule ya mapumziko yenye uvuli na ubaridi wa kutosha katika Jiji la Dar es Salaam.

Katika eneo la pili la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa maisha ya watu hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa maisha ya watu kwa kuchukua hatua tatu zitakazolifanya liwe kama “moyo katika mwili wa jiji.

Hatua ya kwanza, ni kuongeza kasi ya mkondo wa maji ya mto kwa kurefusha kina, kuongeza upana na kuzibua njia ya maji ya Mto Msimbazi kati ya Barabara ya Kawawa na Daraja la Salenda. Katika hatua hii, taka ngumu zilizotupwa mtoni zitaondolewa na miti ya mikoko inayoziba mkondo wa maji kukatwa.

Hatua ya pili ni kurefusha kingo za Mto Msimbazi kwa kujenga ngazi pana tatu, zitakazotengenezwa kwa kutumia kifusi kitakachozopatikana wakati wa kuchonga kitako cha mto, kila ngazi ikiwa ni ukanda wenye matumizi mahsusi. Kwa pamoja, ngazi hizi tatu, zitakuwa ni kanda yenye ukubwa wa eneo la hekta za mraba 400, kati ya Barabara ya Kawawa, Daraja la Salenda na Barabara ya Mandela.

Ngazi ya nchini kabisa utakuwa ni ukanda kwa ajili ya kuongoza maji ya mto. Hii ni ngazi ya kuongoza maji ya mafuriko wakati wa mvua kubwa, na hivyo kuondoa hatari ya mafuriko kwa wakazi wa eneo lote. Aidha, ngazi hii itakuwa maalum kwa ajili ya kutunza ardhi yenye unyevu na uoto asilia ulioko kandoni mwa mto Msimbazi, kama vile miti ya mikoko.

Ngazi ya pili utakuwa ni ukanda kwa ajili ya kujenga vituo vya michezo ambavyo vitatumika kama Sebule ya Burudani za Jiji. Ngazi hii itajengwa katika namna ambayo inaruhusu itumike kwa ajili ya michezo na burudani na wakati huo huo kupokea na kusafirisha maji wakati wa mafuriko. Ngazi hii itakuwa na eneo la kilometa za mraba nne.

Na ngazi ya tatu ni ukanda kwa ajili ya kujenga majumba yenye matumizi anuai yatakayolifanya Bonde la Msimbazi kugeuka kituo cha biashara. Ngazi hii, yenye ukubwa wa hekta 57, itakuwa salama dhidi ya mafuriko, na hivyo kufaa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa miundombinu inayoweza kutumika muda wote. Utengenezaji wa ngazi ya pili utatanguliwa na kazi ya kuhamishiwa kwa wakazi waliopo kwa sasa katika maeneo husika.

Na hivyo, hatua ya tatu ni kazi ya kujenga safu za majumba makubwa ya kisasa kwa ajili ya makazi, biashara na burudani kuzunguka eneo lililo kati ya Barabara ya Kawawa na Daraja la Salenda.

Na katika eneo la tatu la kimkakati, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” inaongelea kubadilisha “Bonde la Msimbazi” kutoka katika hali ya kuwa bonde ambalo ni adui wa maisha ya watu na mazingira hadi kuwa bonde ambalo ni rafiki wa maisha ya watu na mazingira kwa kuchukua hatua za kiutawala zitakazolifanya liwe kama “moyo na mapafu katika mwili wa jiji.

Kwa ujumla, dhima ya “Mradi wa Msimbazi” kwa ajili ya kufukuzia dira iliyotajwa hapo juu imeyagwanya maeneo makuu mawili ya kimkakati (Strategic Result Areas-KRAs) katika makundi makuu manne ya kiutekelezaji (Key Result Areas-KRAs), ambayo ni: kuzuia mafuriko kwa kushambulia chimbuko lake (“mitigation”), kuzuia madhara ya mafuriko kwa kuwalinda watu walio hatarini (“protection”), kubadilisha matumizi ya maeneo ya Bondo la Msimbazi yaliyomo katika hatari ya kushambuliwa na mafuriko mara kwa mara (“transformation”), na kujenga uwezo wa kitaasisi kwa kuunda mfumo wa uongozi shirikishi kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa Bonde la Msimbazi kwa weledi, kasi na ufanisi (“governance”).

Mikakati, mbinu na majukumu ya mradi

Andiko la “Mradi wa Msimbazi” limefafanua kwa kina dhima ya mradi iliyotajwa hapo juu, kwa kuweka bayana mchanganuo wa mikakati, mbinu na majukumu kadhaa. Kuna mikakati minne (4), iliyogawanyika kwenye mbinu kumi (10) na majukumu arobaini na nane (48).

Mkakati wa kwanza ni kuzuia mafuriko kwa kushambulia chimbuko lake (“mitigate strategy”) kupitia mbinu tano. Yaani, kukarabati mtandao wa kiikolojia katika Bonde la Msimbazi kwa kupanda miti; kuongeza uwezo wa Bonde la Msimbazi kutunza maji ya mvua; kuongeza uwezo wa Mto Msimbazi kupokea na kutunza maji ya mvua; kupanua eneo la bonde linalofunikwa na miti ya mikoko iliyoko kati ya Daraja la Salenda na Daraja la Jangwani kwa kupanda miti hiyo kuelekea baharini; kuongeza uwezo wa mto kusafirisha maji yake kwa kasi kubwa kuelekea baharini.

Ndio kusema, mbinu ya kwanza, chini ya mkakati wa kwanza, ni kukarabati mtandao wa kiikolojia katika Bonde la Msimbazi kwa kupanda miti katika milima ya Pugu Kazimzumbwi na kupanua eneo la bonde linalofunikwa na vichaka.

Mbinu ya pili, chini ya mkakati wa kwanza, ni kuongeza uwezo wa Bonde la Msimbazi kutunza maji ya mvua kupitia majukumu manne. Jukumu la kwanza ni kutumia kanuni za mipango miji kukomesha ujenzi holela katika maeneo yenye uwezo mkubwa wa kutunza maji ya mvua. Jukumu la pili ni kujenga mabwawa katika mto kwa ajili ya kutunza maji ya mvua. Jukumu la tatu ni kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kupitia mapaa ya nyumba na kuyahifadhi kwenye visima. Na jukumu la nne ni kujenga madimbwi kandoni mwa mto kwa ajili ya kutunza maji ya mvua, ambapo maji haya yanaweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji.

Mbinu ya tatu, chini ya mkakati wa kwanza, ni kuongeza uwezo wa Mto Msimbazi kupokea na kutunza maji ya mvua kupitia majukumu matatu. Jukumu la kwanza ni kujenga mfumo wa kufuatilia kasi na kiasi cha mchanga unaotuama katika kitako cha mto kutokana na mmomonyoko wa ardhi ili kufahami lini kazi ya kuvuna mchanga huo ifanyike. Jukumu la pili ni kujenga kuta maalum katika mto kwa ajili ya kuzitumia kama machujio ya mchanga. Jukumu la tatu ni kuweka program ya kudumu ya kusafisha mto kila mwaka ili kuondoa mchanga na taka ngumu zinazotupwa mtoni. Jukumu la nne ni kutumia mchanga unaochimbwa mtoni kujenga ngazi zinazoinua kingo za mto. Jukumu la tano ni kupanda mimea inayoweza kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika kingo za mto. Jukumu la sita ni kutambua maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kushambuliwa na mafuriko na kuyafuatilia kwa karibu.

Mbinu ya nne, chini ya mkakati wa kwanza, ni kupanua eneo la bonde linalofunikwa na miti ya mikoko iliyoko kati ya Daraja la Salenda na Daraja la Jangwani kwa kupanda miti hiyo kuelekea baharini. Misitu ya mikoko inazo faida kadhaa. Inafanya kazi ya kuzuia mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza gesi ya kaboni kutoka angani na kuihifadhi; inafanya kazi ya kufubaza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuzalisha kivuli kinachowakinga viumbe walioko ardhini dhidi ya jua kali; ni mazalia na kantini ya viumbe wa baharini kama vile kaa, pronzi, na samaki; na inazuia mmomonyoko wa ardhi katika pwani ya bahari.

Na mbinu ya tano, chini ya mkakati wa kwanza, ni kuongeza uwezo wa mto kusafirisha maji yake kwa kasi kubwa kuelekea baharini, kupitia majukumu sita. Jukumu la kwanza ni kuongeza upana na kina cha mto kati ya Daraja la Salenda na Daraja la Jangwani. Jukumu la pili ni kuongeza upana na kina cha mto kati ya Daraja la Jangwani na Daraja la Kawawa. Jukumu la tatu ni kuongeza upana na kimo cha madaraja ya Mkwajuni, Kawawa, Nelson Mandela na Relini. Jukumu la nne ni kuongeza upana na kimo cha daraja la Jangwani. Jukumu la tano ni kubomoa majengo yote yanayokwamisha mkondo wa maji. Na Jukumu la sita ni kuhamisha na kuhifadhi mali za kituo cha Mabasi ya Mwendokasi kilichoko Jangwani.

Mkakati wa pili ni kuzuia madhara ya mafuriko kwa kuwalinda watu walio hatarini (“protect strategy”) kupitia mbinu mbili. Yaani, kulinda watu, mali na mifumo yao ya kujipatia mkate wa kila siku; na kuwahamisha wakazi wa Bonde na Msimbazi na kuwapeleka katika makazi na maeneo mapya ya shughuli za kibishara.

Ndio kusema, mbinu ya kwanza, chini ya mkakati wa pili, ni kulinda watu, mali na mifumo yao ya kujipatia mkate wa kila siku, inayotekelezwa kupitia majukumu matano. Jukumu la kwanza ni kukarabati kuta za mto katika maeneo yenye rasilimali nyeti. Jukumu la pili ni kujenga ngazi za kuongoza maji ya mafuriko. Jukumu la tatu ni kubuni mifumo ya upashanaji habari kuhusu hali ya hewa. Jukumu la nne ni kujenga mfumo wa maafa na uokoaji wa waathirika. Jukumu la tano ni kubadilisha eneo kiwanda cha kutibu maji machafu kilichopangwa kujengwa nyuma ya Hospitali ya Muhimbili.

Na mbinu ya pili, chini ya mkakati wa pili, ni kuwahamisha wakazi wa Bonde na Msimbazi na kuwapeleka katika makazi na maeneo mapya ya shughuli za kibishara, inayotekelezwa kupitia majukumu matano. Jukumu la kwanza ni kuandaa makadirio ya gharama za kuwahamisha watu wanaoishi kati ya Daraja la Salenda na Barabara ya Kawawa. Jukumu la pili ni kuanda mpango wa kuwahamisha wakazi wa Bonde la Msimbazi wanaokaa kati ya Daraja la Msimbazi na Barabara ya Kawawa. Jukumu la tatu ni kuandaa na kutangaza mpango wa kutoa huduma za mpito za mpito kwa watu walio katika makazi mapya. Jukumu la nne ni kutekeleza mpango wa kutoa huduma za mpito za mpito kwa watu walio katika makazi mapya. Na jukumu la tano ni kuanda mpango wa kuwahamisha wakazi wa Bonde la Msimbazi wanaokaa kati ya kati ya Barabara ya Kawawa na Barabara ya Nelson Mandela.

Mkakati wa tatu ni kugeuza matumizi ya maeneo ya Bondo la Msimbazi yaliyomo katika hatari ya kushambuliwa na mafuriko mara kwa mara (“transform strategy”) kupitia mbinu tatu. Yaani, kutakatisha maji ya mto Msimbazi kwa kujenga mfumo wa kusafirisha maji machafu kutoka majumbani na viwandani na kiwanda cha kuyatibu; kuondoa taka ngumu toka mtoni’ na kujenga sebule za biashara na mapumziko kwa ajili ya wakazi wa jiji.

Ndio kusema, mbinu ya kwanza, chini ya mkakati wa tatu, ni kutakatisha maji ya mto Msimbazi kupitia majukumu manne. Jukumu la kwanza ni kuandaa orodha ya tabia ambazo ni vyanzo vya uchafuzi wa mto. Jukumu la pili ni kuandaa programu ya kuzuia uchafuzi wa mto. Jukumu la tatu ni kuandaa mifereji na mabomba kwa ajili ya kuondoa maji ya mafuriko katika maeneo yaliyo jirani na eneo rasmi la mradi. Na jukumu la nne ni kuandaa mifumo ya majitaka kwa ajili ya kusafirisha majitaka kutoka majumbani na viwandani kwa maeneo yaliyo jirani na mto.

Mbinu ya pili, chini ya mkakati wa tatu, ni kuondoa taka ngumu toka mtoni, kupitia majukumu sita.

Jukumu la kwanza ni kuandaa mpango kazi wa kusimamia uondoaji wa taka ngumu mtoni. Jukumu la pili ni kujenga uwezo wa Halmashauri zinazohusika na mradi kwa kuandaa sheria, rasilimali watu na vifaa kwa ajili ya kufanya menejimenti ya taka ngumu. Jukumu la tatu ni kuzibua madaraja na makalavati. Jukumu la nne ni kusafisha madampo yaliyopo kwa sasa. Jukumu la tano ni kutumia asasi za kiraia kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kutupa taka ngumu katika mito. Na jukumu la sita ni kushirikisha sekta binafsi katika kubuni na kuchangamkia fursa za biashara zinazohusiana na menejimenti ya taka ngumu.

Na mbinu ya tatu, chini ya mkakati wa tatu, ni kujenga sebule za biashara na mapumziko kwa ajili ya wakazi wa jiji, mbinu inayotekelezwa kupitia majukumu matano.

Jukumu la kwanza ni kujenga korido ya sebule za kibiashara yenye eneo la kilometa za mraba 27, kuanzia Daraja la Salenda mpaka Vingunguti.

Jukumu la pili ni kujenga Sebule Burudani yenye ukubwa wa hekta 400, ikijumuisha bustani za miti na viwanja kwa ajili ya maofisi, biashara, burudani, ikiwa inaanzia Daraja la Salenda mpaka Barabara ya Kawawa.

Jukumu la tatu ni kujenga Sebule ya Biashara inayojumuisha majengo kwa ajili ya ya maofisi, biashara, burudani, ikiwa inaanzia Daraja la Salenda mpaka Barabara ya Kawawa, sawa na eneo la hekta 57.

Jukumu la nne ni kuunganisha miundombinu ya eneo rasmi la mradi na miundombinu iliyo katika maeno jirani yanayolizunguka eneo hili.

Na jukumu la tano ni kuhamasisha uwekezaji wa mitaji binafsi katika Bonde la Msimbazi ili kupata mtaji unaohitaji kwa ajili ya mradi huu unaokaribia dola milioni 200.

Na mkakati wa nne ni kuweka mfumo wa uongozi shirikishi kwa ajili ya kusimamia ikolojia ya Mto Msimbazi ili kuhakikisha kwamba unabaki kuwa mto salama kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam (“govern strategy”) kupitia mbinu moja tu.

Mbinu hiyo ni kujenga uwezo wa kitaasisi, kwa maana ya kuunda mfumo wa utawala kwa ajili ya kuratibu, kushirikisha, kupashana habari na kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati iliyowekwa.

Mbinu hii inapaswa kutekelezwa kupitia majukumu matatu. Yaani, kushauriana na wadau juu kazi ya kuunda mfumo wa utawala kwa ajili ya kuendesha mradi, kwa kuonyesha nani anafanya nini, na yupi anawajibika kwa nani; kuweka mfumo wa utawala wa muda mfupi (2019-2020) wa kusimamia “Mradi wa Msimbazi”; kuunda mfumo wa utawala wa muda mrefu (2020-2050) kwa ajili ya kusimamia “Mradi wa Msimbazi”; na kutekeleza mpango kazi wa mradi kama ulivyoandikwa katika sura ya nne ya andiko la “Mradi wa Msimbazi.

Katika jukumu la kwanza, chini ya mkakati wa nne, yaani, kushauriana na wadau juu kazi ya kuunda mfumo wa utawala kwa ajili ya kuendesha mradi, kwa kuonyesha nani anafanya nini, na yupi anawajibika kwa nani, wadau wafuatao wanahusika.

Jukumu la pili, chini ya mkakati wa nne, ni kuweka mfumo wa utawala wa muda mfupi wa kusimamia “Mradi wa Msimbazi” kwa kuunda MSC and PIU.

Mfumo wa kuendesha mradi kwa muda mfupi (2019-2020), kama unavyoonekama pichani hapa chini, unajumuisha vyombo vitatu vipya. Kuna “Kamati ya Kusimamia Mradi wa Msimbazi,” yaani “Msimbazi Steering Committee (MSC)”; “Kikosi cha Kusimamia Utekelezaji wa Mradi,” yaani “Project Implementation Unit (PIU)”; na “Kamati ya Ushauri wa Kitaalam,” yaani “Technical Advisory Committee (TAC).”

Picha Na. 09: Muundo wa utawala kwa ajili ya Mradi kwa kipindi kifupi (2019-2020)
Msimbazi--Picha 09.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.98).”

Majukumu ya MSC ni kuratibu utekelezaji wa mikakati kumi iliyomo katika “Mradi wa Msimbazi,” na inaripoti kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI. Majukumu ya PIU ni kuanzisha, kuandaa, kutekeleza na kufuatilia matokeo ya mikakati yote iliyomo katika “Mradi wa Msimbazi,” na inaripoti kwa TAC. Tayari PIU imeundwa tangu mwezi Agosti 2018, kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Na majukumu ya TAC ni kutoa ushauri wa kitaalam kwa MSC kadiri hali inavyolazimu.

Jukumu la tatu, chini ya mkakati wa nne, ni kuunda mfumo wa utawala wa muda mrefu kwa ajili ya kusimamia “Mradi wa Msimbazi” kwa kutunga sheria ya Bunge itakayounda MPA na MADC.

Mfumo wa kuendesha mradi kwa muda mrefu (2020-2030), kama unavyoonekama pichani hapa chini, unajumuisha vyombo vinne vipya. Kuna “Kamati ya Kusimamia Mradi wa Msimbazi,” yaani “Msimbazi Steering Committee (MSC)”; “Kamati ya Ushauri wa Kitaalam,” yaani “Technical Advisory Committee (TAC)”; “Shirika la Kuendeleza Eneo la Msimbazi,” yaani “Msimbazi Area Development Corporation (MADC).” Na “Mamlaka ya Mradi wa Msimbazi,” yaani “Msimbazi Planning Authority (MPA).”

Picha Na. 10: Muundo wa utawala kwa ajili ya Mradi kwa kipindi kirefu (2020-2050)
Msimbazi--Picha 10.png

Chanzo: PORALG & WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group; 2019, pg.98).”

Majukumu ya MSPA ni kushughulikia masuala yote yanayohusu utekelezaji ya “Mradi wa Msimbazi,” kwa kuhakikisha kuwa kuna ufanisi, kasi na uendelevu katika utoaji huduma. MSPA inaripoti kwa MSC.

Na majukumu ya MADC ni kuunadi “Mradi wa Msimbazi” kwa wawekezaji binafsi na hivyo kuhamaisisha upatikanaji wa mtaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. Pia MADC inalo jukumu la kusimamia uwekezaji katika mradi huu katika kipengele cha wawekezaji binafsi, ikiwa inafanya hivyo kwa niaba ya serikali ya Tanzania na inaripoti kwa MSPA.

Na jukumu la nne, chini ya mkakati wa nne, ni kutekeleza mpango kazi wa PIU kama ulivyoandikwa katika andiko la “Mradi wa Msimbazi” sura ya nne.

Hitimisho

Kwa ujumla, “Mradi wa Msimbazi” ni mradi unaoonyesha ubunifu wa hali ya juu katika kutatua tatizo la miji iliyo adui wa maisha ya watu kwa kuifanya kuwa miji iliyo rafiki wa maisha ya watu. Kadiri mradi huu unavyohusika, kuna mambo matatu muhimu yanayoweza kuigwa na mataifa ya nje kutoka Tanzania.

Kwanza, utaratibu wa ushirikishwaji wa wananchi wapatao 1000 na taasisi zipatazo 60 ni jambo la kuigwa na nchi baki.

Pili, mkakati wake wa kutafuta fedha kutoka ndani na nje ya serikali ni wazo linalopaswa kuigwa na mataifa mengine. Ni mkakati muhimu kwa kuwa trililioni 255 zinazotakiwa ni sawa na bajeti ya Taifa la Tanzania kwa miaka tisa. Bila kutumia mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi mradi huu hauwezi kutekelezeka.

Na tatu, ni ubunifu katika kuweka muundo wa utawala kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa mradi. Ni muundo unaotumia vyombo vya serikali vilivyopo kwa zaidi ya 50%. Lakini pia, kuna vyombo vipya vinapendekezwa kuundwa kwa ajili ya kuziba mapengo yanayojitokeza katika muundo wa sasa wa kiserikali. Kwa njia hii kasi na ufanisi vinawezekana sana.

Bibliografia

1. PORALG and WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Executive Summary (Washinton DC: World Bank Group, 29 January 2019).

2. PORALG and WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume A, Strategy and Management Framework (Washinton DC: World Bank Group, 29 January 2019).

3. PORALG and WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume B, Detailed Plan for the Lower Basin (Washinton DC: World Bank Group, 29 January 2019).

4. PORALG and WBG, The Msimbazi Opportunity, Transforming the Msimbazi Basin into a Beacon of Urban Resilience: Volume C, Appendices (Washinton DC: World Bank Group, 29 January 2019).

5. Viktoriia Pavlova, Strategies for city resilience to riverine floods: Case of Mzimbazi River, Dar es Salaam (2016). Master Of Science Degree In Urban Planning And Policy Design. Politecnico Di Milano School Of Architecture Urban Planning Construction Engineering.

Hisani:
Utafiti uliowezesha makala hii kuandikwa umedhaminiwa na taasisi ya “The National Geography Society for the Info Nile.”
 

Deus J. Kahangwa

Verified Member
Jan 7, 2013
184
225
Atakaye soma hili bandiko lako mpaka mwisho lazima aende peponi
Hadhira yangu ni watu wenye uwezo mkubwa wa kusoma kurasa 22 za A4 zenye font size ya pointi 12 kwa saa moja.

Wasomaji wenye uwezo mdogo tumeshawaandikia zao via MwanaHalisi Online na Raia Mwema.

Vinginevyo, ukisoma Usuli mwanzoni kabisa inatosha.
 

VAPS

JF-Expert Member
Jul 10, 2012
4,024
2,000
Hii ni habari njema, utekelezaji ufanyike Japo mipango imeanza zama hizo,tutapongeza awamu ya tano endapo utekelezaji utaanza.
Japo kwa design mradi sio economy Tzs 255 Trillion!? Utekelezaji wake hauwezekani sioni mbia serious kuungana na awamu hii ya tano.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Wo shi niubi

JF-Expert Member
Aug 14, 2015
907
1,000
Wanajenga lini? mradi utagharimu tril 250 au BIL 250 USD? jengeni bhana imekuwa muda mrefu, hata ni aibu kwa mji mkubwa kama DAR mvua zikinyesha inakumbwa na mafuriko, yaani haiingiii akilini kabisa, miji zote hata za hapa tu EAC hazifuriki kama sisi DAR yetu inavyofurika.
 

Osaba

JF-Expert Member
Apr 10, 2011
1,805
1,500
Ndefu sana utafikiri kitabu cha historia

Sent using Iphone 7s
 

Deus J. Kahangwa

Verified Member
Jan 7, 2013
184
225
aliyesoma yote anipe summary.
Usuli

Kwa mujibu wa Kanzidata ya Kimataifa kuhusu Majanga Asilia yaliyotokea tangu mwaka 1990, Tanzania inakabiliwa na hatari ya majanga asilia yafuatayo, frikwensi zake zikiwa zimeonyeshwa katika mabano: mafuriko (62.2%), ukame (13.3%), tetemeko la ardhi (11.1%), kimbunga (8.9%), moto wa nyikani na maporomoko ya miamba (4.5%).

Kwa mujibu wa takwimu hizi, janga ma mafuriko linayo nafasi kubwa kuliko majanga mengine, ambapo kwa miaka 25 iliyopita, kumetokea mafuriko 19ya mitoni, mafuriko 10 ya ufukweni mwa bahari na mafuriko 4 ya maji yanayozagaa katika tambarare isiyo na mto.

Kwa kuwa Dar es Salaam ni jiji la mwambao wa Bahari ya Hindi na linayo mito mingi limekuwa likikumbwa na mafuriko zaidi kuliko mikoa mingine, mafuriko mengi yakiwa yanatokea katika Bonde la Mto Msimbazi, na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na majeruhi. Matukio haya yamelibadilisha Jiji kuwa hatari kwa maisha ya wakazi.

Kwa sababu hii, serikali ya Tanzania imeamua kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa salama kwa kubuni na kutekeleza “Mradi wa Fursa ya Msimbazi” kwa ajili ya “Kulibadili Bonde la Msimbazi hadi kuwa Kielelezo cha Miji iliyo salama Katika Afrika.”

Mradi huu unayo maeneo mawili ya kimkakati, maeneo manne ya kimatokeo, mikakati kumi na majukumi 50. Mradi unafadhiliwa kwa nia ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP). Kiasi cha dola za Marekani 114 milioni zinahitajika kuukamilisha.

Utekelezaji wake ulianza mwaka 2019 na unasonga mbele kwa kuanza na utekelezaji wa kazi zenye vipaumbele vikubwa. Utaendelea mpaka mwaka 2050, kupitia mipango kazi ya miaka mitano mitano, ambapo mpango kazi wa kwanza unaanzia 2019 mpaka 2024.

Mmiliki wa mradi huu ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Kitengo cha TAMISEMI, na msimamizi mkuu ni Katibu Mkuu TAMISEMI. Ripoti ifuatayo inajadili changamoto, fursa na wadau wa mradi huu.
 

Deus J. Kahangwa

Verified Member
Jan 7, 2013
184
225
Mkuu huu mradi hautekezeki 255 T,tzs!? kwa uchumi wetu!?.Option B kuhamisha wakazi na kujenga kingo pekee kulinda mto. Pia kuweka madaraja ya juu. Below 1 Trilion Tzs.
Mpango uliopo ni kutumia utaratibu wa PPP, yaani ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Sekta binafsi itachangia kama mwekezaji.

Wawekezaji wa ndani na nje watakaribishwa.

Serikali itachangia kama mmiliki wa mradi.
 

Kalamu1

JF-Expert Member
Jul 7, 2018
6,940
2,000
Mimi itanibidi nitafute muda mzuri niisome hii kwa utulivu.

Sababu moja kuu ya kufanya hivyo ni kiswahili chake.

Nataka kuona jinsi kiswahili kilivyokomaa kama lugha inayoweza kutumika kwenye tafiti kama hizi. Najua si kamilifu, lakini ni ngazi nzuri iliyofikiwa. Natambua pia kwamba andiko hili ni 'tafsiri' tu toka kwenye lugha iliyotumika mwanzo.

Kama kuna kitu cha kujivunia Tanzania, ni hiki. Kazi ya BAKITA (sijui kama ni sahihi braza hili la kiswahili) na wengine inaonekana wazi.

Matokeo yanayoonekana ya mafanikio yetu tokea tupate uhuru wetu, mwaka 1961. Ni kipi kingine tunachoweza kukiweka hapa kama mfano wa mafanikio yetu kama hii ya kukuza lugha yetu ya taifa.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom