Mafisadi watashinda, lakini…

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,048
Mafisadi watashinda, lakini…

Padri Privatus Karugendo Julai 30, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

VITA ya kupambana na mafisadi wa nchi ilianzia mbali, watu wengi wameshiriki vita hii, tumeandika mengi, tumeonya, tumetoa maoni na kutabiri mambo mbali mbali ambayo leo hii yanaonekana.

Nakumbuka kuandika makala juu ya wapambe wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, nikisisitiza kwamba matatizo mengi yanaletwa na wapambe wake, ukweli ambao umejionyesha wazi mbele ya macho yetu. Leo nisingependa kwenda nyuma sana, bali nianze na hatua ya bunge kumsimamisha Zitto Kabwe katika sakata la Buzwagi. Maana hapo ndipo dalili za ufisadi mkubwa zilianza kujionyesha.

Yaliyofuata kwa mfululizo wote mnayakumbuka, mara Mwembeyanga na orodha ya mafisadi, mara EPA na kufukuzwa kazi kwa Gavana wa Benki Kuu, mara Richmond na Dowans, mara kuvunjwa kwa baraza la Mawaziri, mara “kifo” cha Gavana Ballali, mara Chenge na Vijisenti, mara ushirikina bungeni, mara TAKUKURU na mafaili ya vigogo kwenda mahakamani huku hawaendi, mara Kubenea na Ndimara Tegambwage kuvamiwa na vibaka, Juzi Kubenea huyo huyo kuvamiwa na kupekuliwa na makachero na vituko vingi zaidi. Kinachoonekana wazi ni kama gari lililokwama katika tope, likisukumwa hatua kumi mbele halafu linarudi nyuma kumi na tano. Swali linabaki ni nani wa kulitoa gari hili kwenye tope?

Watu wengi wamekuwa wanajiuliza nafasi ya Rais katika mvutano huu. Amekaa kimya labda kwa vile pande zote zina watu wake wa karibu. Pande zote zina umuhimu kwake na kwa chama chake cha CCM. Pamoja na yote ni wazi kwamba ufisadi hauwezi kuwa na umuhimu wowote ule kwa taifa! Rais ni mtu lakini pia ni asasi wakati huo huo. Kwa hiyo ni vema watu wakaelewa toka mapema kuwa vita ya kupambana na ufisadi nchini Rais wao anasimama wapi.

Kwa vyovyote vile upande atakaokuwa Rais wa nchi ndio utakaoshinda. Najua haya si maneno mazuri kuyasema, lakini Tanzania yetu wote tunaijua, kuwa kiongozi wa nchi anategemewa sana kutoa mwelekeo wa vita yoyote. Ndiyo maana sasa tunaona, wanaoitwa mafisadi wakiwemo kundi lote la mtandao maslahi wanamg’ang’ania Rais kuwa yuko upande wao, na kwa sehemu kuwa Rais naye hakuwaacha sana anatoa dalili za kuonyesha kuwaunga mkono.

Hakuna hatua zinazochukuliwa. Bunge liliagiza na kupitisha azimio kwamba mapendekezo yote ya Tume ya Mwakyembe yafanyiwe kazi. Kuna watu waliotajwa kwa majina na kuomba wachukuliwe hatua. Watu hao ni wateule wa Rais, hivyo yeye ndiye mwenye wajibu wa kuwaondoa. Hadi leo bado wako kwenye kazi zao. Kwanini watu wasifikiri kwamba Rais yuko upande wa hao mafisadi. Na je si lazima mafisadi watambe na kujivuna kwa kufikiri kwamba Rais,yuko upande wao maana hawachukulii hatua?

Rais mwenyewe alitoa ahadi kwa Watanzania, kulichunguza swala la EPA na kulichukulia hatua. Aliteuwa tume ambayo ilipewa miezi sita kufanya kazi. Muda huo umemalizika bila wananchi kusikia chochote juu ya EPA na wale walioshiriki kuchota mafedha ndani ya Benki Kuu. Kwa nini Rais wetu anasita kuchukua hatua? Je, hatua hii si inawapatia kichwa mafisadi kufikiri kwamba Mheshimiwa Rais yuko upande wao?

Wanaopinga ufisadi nao wanapenda kumsemea sana Rais kuwa yuko upande wao. Tumemsikia mara nyingi Mama Kilango akisema vita hii ina baraka za Rais. Mh. Rais hawezi kukanusha kauli kama hiyo maana ni ya kizalendo na yeye anapenda aonekane ni mzalendo haswa. Mpaka hapa tukubaliane kuwa upande atakaojiunga nao Mh. Rais ndio utakaoshinda.

Kuna watu wamekuwa wanafuatilia nyendo na kauli za Mh. Rais na kubaini kuwa labda yuko upande wanaoitwa wa mafisadi. Kauli yake kuwa kilichompata Lowassa ni ajali ya kisiasa, kusita kuwachukulia hatua wanaosakamwa na tuhuma za ufisadi kwa kisingizio cha utawala wa sheria, na hotuba yake kwa wamiliki wa viwanda CTI akiwatuhumu kuwa wao ndio wanaolea rushwa ni ushahidi wa mazingira kuwa labda Rais wetu yuko upande wa mafisadi na mantiki yangu, upande huo ndio utakaoshinda.

Wako wanaofikiri kwamba Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, anakaa kimya ili kila mtu ajimalize mwenyewe. Kusema kweli Rais wetu ni mtu mwenye marafiki wengi. Pia anawakumbuka marafiki zake hata kwa majina! Wakuu wa wilaya wote anawafahamu kwa majina na kila mtu na kituo chake. Marafiki wengine waliotapakaa nchi nzima anawafahamu kila mtu kwa jina lake.

Wale wote walioshiriki kwenye kampeni zake na kutoa misaada mbali mbali anawafahamu kila mtu kwa jina lake. Hivyo eti yeye ameamua kuwaacha hata wale wapambe wake, ambao hawakufanya vizuri kazi zao na kujiingiza kwenye ufisadi wajinyonge wenyewe. Hana mpango wa kummaliza mtu wala kumsaidia mtu. Anaacha uhuru wa kila mtu kuuchukua msalaba wake mwenyewe. Eti ndo maana anakaa kimya bila kuonyesha anaunga mkono upande upi.

Ni wazi Rais Jakaya Kikwete, anajua nguvu za wale wenye fedha. Anajua wazi kwamba akiendelea kukaa kimya wenye fedha watashinda. Lakini pia yeye kama Mwanaharakati, anajua nguvu za wale wenye fikra – kawaida fikra inaungwa mkono zaidi na wananchi. Fikra inaweza kugandamizwa kwa muda, lakini si milele yote. Hapo ni lazima kupima vizuri, maana ushindi wa mafisadi unaweza kuwa wa muda tu, au ukasabisha vurugu na umwagaji damu. Hivyo ukimya wake au msimamo wa kuacha kila mtu kujinyonga mwenyewe utakuwa umeleta maafa kwa Taifa zima.

Kama kuna mshauri mzuri anayehitaji sasa hivi kwenye taifa letu, ni yule wa kumweleza Mheshimiwa Rais wetu, kuonyesha upande wake katika kupambana na mafisadi. Huu ni wakati wake kujitoa muhanga, huu ni wakati wake kukubalil kuwapoteza marafiki ili kuliponyesha taifa zima. Ni kazi ngumu kuwapoteza marafiki – maana kuachana na mtu si kama vile kuvua nguo na kuiweka pembeni.

Lakini pia ni kazi ngumu kuirudisha amani ya nchi ikishavurugika. Hapa ni lazima Rais wetu apime na kuchagua fungu lililo bora; kuwapoteza marafiki wachache nchi ikapata amani na utulivu ama kuwakumbatia marafiki wachache na nchi ikaingia katika machafuko.

Mpaka sasa hakuna mwandishi (Ukiacha wa Uhuru na Mzalendo) ambaye amemsema kuwa Rais yuko upande wa wanaopiga vita ufisadi. Hata hao waliojaribu kama sharti muhimu la ajira yao, waliishia kutoa ushahidi wa kumfukuza kazi Balalli, kumteua Zitto Kabwe katika kamati ya madini na kuridhia kujiuzulu kwa Lowassa. Na Labda Rais kukubali kuwapatia waheshimiwa wabunge taarifa ya Tume ya Madini.

Waandishi hawa hawana ushahidi wa maneno kutoka kwa Mh. Rais kudiriki hata kutamka neno ufisadi. Kinachoonekana wazi ni kuwa Rais hakuwa na uhakika na matokeo ya Kamati ya EPA. Kama ana uhakika, basi asingekuwa na kigugumizi kuchukua hatua za haraka.

Kuna ushahidi mkubwa wa kumsaidia Mheshimiwa Rais. Kuna baadhi ya viongozi wa Serikali wana mali nyingi kupindukia. Kwa nini hili lisimsaidie kusimama imara? Watumishi wa serikali wanapata wapi utajiri wa kupindukia? Kwa nini asiwatoe serikalini na kuwalazimisha kurudisha kiasi cha fedha kwenye mfumo wa taifa – na fedha hizo zikasaidia kuleta maendeleo ya wananchi wote?

Nani sasa anaongoza vita hii ambayo mafisadi wanaelekea kushinda? Kama Rais wetu anaonyesha kusita na kuwa na kigugumizi, ni nani ataongoza mapambano haya? Ni mapambano makubwa! Wengi wanasema Spika Sitta? Lakini kuna tetesi kwamba “vigogo” wa Chama Cha Mapinduzi wana njama za kumshughulikia na kumwondosha kwenye kiti chake cha uspika!

Akitoka kwenye kiti chake ndo mwisho wake wa kupambana! Wengine wanafikiri mapambano haya yataongozwa na Komredi Slaa na wapinzani wenzake? Tatizo ni kwamba nguvu za mafisadi zinawadhoofisha pia wapinzani. Fedha kitu kingine! Kuna wenye mawazo kwamba vita hii ya mafisadi itaongozwa na mabaki ya Baba wa taifa katika CCM? Wengine wanasema itaongozwa na chuki iliyotokana na uchaguzi mkuu wa 2005? Wengine bado wanaamini kwamba vita hii inaongozwa na Kikwete mwenyewe bila hata yeye kujua kuwa anaiongoza. Nisemee zaidi hili la mwisho.

Makovu ya yale yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu wa 2005, hayakutafutiwa dawa. Hivyo baada ya uchaguzi makovu haya yaliendelea na bado yanachimba na kusimika mizizi. Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, alifikiri dawa pekee ni kuendelea kuongoza bila kutibu makovu. Nina mashaka kama alifanya juhudi binafsi za kuyamaliza makundi ndani ya CCM, kuwapatanisha wanamtandao na wale waliokuwa nje ya mtandao.

Kutamka kwamba makundi yamekwisha, si dawa! Panahitajika kazi ya ziada. Nafikiri Rais wetu alipaswa kuelekeza kwanza nguvu zake katika kutibu makofu ndani ya CCM na taifa kwa ujumla kuliko kujenga mahusiano yetu na nchi za nje.

Watu kama Malecela, Sumaye, Salim, Mwandosya, Butiku, na wengine walipata makovu makubwa. Baada ya uchaguzi Rais alifanya makosa ya kiutendaji kwa kuwateua baadhi yao kuingia katika vyombo muhimu bila kwanza kuponya makovu na kuhakikisha yamepona kweli. Hawa ni mwiba na sitaki kusema zaidi. Yeye anadhani wanaongoza kumkwamisha lakini kimsingi yeye anajikwamisha kwa kuamua kufa na tai shingoni.

Wazee hawa ni Hazina ya nchi na wanaona Rais anavyobabaika kukaa katikati ya pande hizi mbili. Rais kukosa upande au kutojulikana anasimama wapi katika suala muhimu kama hili ni hatari zaidi kuliko ufisadi wenyewe. Ukimya wa Rais wetu unaweza kusababisha mafisadi kujipanga na kwa vile wana nguvu za fedha wakafanikisha mipango yao. Ndiyo maana nadiriki kusema ufisadi umeshinda, lakini huko ndiko kushindwa kwake (Kikwete) pia.

Kama ni kweli kuna watu wanaotaka kuanzisha CCM B, wafanye haraka kujitangaza. Wasiogope kuitwa wapinzani. Kuliokoa taifa letu na majanga yanayolinyemelea ni muhimu zaidi ya mtu kuitwa mpinzani. Hata hivyo wapinzani ni Watanzania na baadhi yao wamehakikisha kuwa ni wazalendo wa kweli!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa S. L. P. 114 Magu, Mwanza. Simu: 0754 633122
 
Back
Top Bottom