Mafisadi sasa kufilisiwa mali zao na kusweka jela miaka 30

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,487
JELA.jpg


BUNGE la jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha marekebisho ya sheria ya kuundwa kwa divisheni maalum ya Mahakama Kuu ya kesi za rushwa na uhujumu uchumi kwa kesi ambazo thamani yake haipungui Sh. bilioni moja.

Sheria hiyo inapendekeza kifungo kisichopungua miaka 20 na isiyozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja kwa atakayekutwa na hatia na pia hatua za kijinai za kutaifisha mali zilizopatikana kutokana na makosa hayo.Hivi sasa, adhabu za makosa ya uhujumu uchumi ni kifungo kisichozidi miaka 15, na yanaipa Mahakama mamlaka ya kutoa adhabu ndogo zaidi ilimradi haizidi miaka hiyo.

Katika mapendekezo yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, bungeni mjini Dodoma, inaelezwa kuwa adhabu iliyopo kwa sasa ni ndogo kulinganisha na uzito wa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanayopendekezwa.

"Kwa ujumla ,hatua hii ni njia mojawapo ya kuwafanya watu waogope kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, na kuhakikisha kuwa mhalifu hanufaiki na uhalifu alioutenda kwa kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa au ufisadi na uhujumu uchumi," alisema Mwanasheria Mkuu Masaju.

Aidha, sheria hiyo inapendekeza kuwa mshtakiwa mwenye mali yenye thamani ya fedha taslimu aruhusiwe kutoa badala ya ilivyo sasa aambapo natakiwa kulipa fedha nusu na inayobaki kuwa ni thamani ya mali, lakini kwa mapendekezo hayo, iwapo mali haihamishiki , atapaswa kutoa hati au ushahidi unaothibitisha umiliki wa mali.

Masaju alisema inapotokea uwezekano wa kuingiliwa kwa kutishwa shahidi, Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka wataweka utaratibu wa kulinda usalama wa shahidi huyo pamoja na familia yake.

Mwanasheria huyo alitaja mapendekezo mengine kuwa ni masharti ya ufilisi au maamuzi ya kufilisi kampuni kutumika kwa mali inayochunguzwa chini ya makosa ya uhujumu uchumi.

"Marekebisho hayo yanalenga kukabili vitendo vya watu au kampuni kujifilisisha pindi uchunguzi unapoanza dhidi yao na pia kuhakikisha mali zote zinazohusika na kosa linalochunguzwa au linaloendelea mahakamani zinaendelea kuwapo hadi uchunguzi au kesi husika utakapohitimishwa," alisema.

Alisema hatua hiyo itaiwezesha serikali kuitaifisha mali kesi itakapokamilika na ikathibitika mahakamani kuwa ina uhusinao na kosa la rushwa na uhujumu uchumi.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom