Mafanikio ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara

Wizara ya Afya Tanzania

Official Account
Oct 1, 2020
58
124
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA



Nembo ya taifa.png




WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO



TAARIFA KWA UMMA

MAFANIKIO YA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA.


Ndugu Wananchi, Disemba 2021 nchi yetu inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru tangu tarehe 09 Desemba, 1961 tulipoanza kujitawala hivyo, maadhimisho haya ni tofauti na miaka mingine kutokana na haja ya kutafakari kwa pamoja tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Maadhimisho haya yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “MIAKA 60 YA UHURU; TANZANIA IMARA, KAZI IENDELEE”.

Tangu mwaka 1961, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitekeleza Sera, Miongozo na Sheria mbalimbali kulingana na maboresho ya muundo wa wizara kwa wakati husika. Kufikia mwaka 2016 Wizara mbili ziliunganishwa ambazo ni Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, hivyo kutengeneza Idara Kuu ya Afya inayoshughulikia masuala yote ya Afya na Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inayoshughulikia Masuala yote ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Ndugu Wananchi, huduma za tiba ya magonjwa pamoja na maendeleo ya jamii zimekuwepo kwa karne nyingi huku huduma za tiba ya asili zikiitangulia tiba ya kisasa. Aidha, baada ya karne ya 10 huduma ya tiba za kigeni iliingizwa na wafanyabiashara wa Kiarabu, Kireno, Kifaransa, n.k. Hata hivyo, Tiba asili na tiba mbadala pamoja na tiba ya kisasa zimeendelea kutolewa hadi sasa karne ya ishirini na moja. Aidha, maendeleo makubwa katika huduma za afya na maendeleo ya jamii yamejitokeza zaidi baada ya uhuru na katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru ukilinganisha na kipindi cha takribani miaka 71 ya ukoloni (Utawala wa Wajerumani, 1889 -1916 na Utawala wa Waingereza, 1916 – 1960).

Napenda kuanza kuangazia huduma za afya kabla ya Uhuru; kabla ya uhuru makabila yote 126 yalitumia tiba asili katika kutibu na kujikinga na magonjwa na kwa mara ya kwanza huduma za tiba za kigeni (Western Medicine) ziliingizwa nchini mwaka 1887 na kuanza kutolewa mwaka 1889-1916 na wamisionari kipindi cha utawala wa wajerumani. Vilevile, huduma za kinga hususan Chanjo ya Ugonjwa wa Ndui ilianza kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1891. Hata hivyo, bado tiba asili iliendelea kuwepo hata wakati wa Utawala wa Mkoloni (Ujerumani na Uingereza) huku baadhi ya huduma za tiba asili zikipigwa marufuku na nyingine kuruhusiwa baada ya kukidhi masharti ya Mkoloni. Aidha, zile zilizopigwa marufuku ni zile zilizohusishwa na imani za kishirikina au uchawi. Kutokana na changamoto hizo, mwaka 1928 Sheria ya kwanza ilitungwa ya kuruhusu uhusishwaji wa tiba asili katika kutoa matibabu na kuwakinga wananchi.

Ndugu Wananchi, huduma za afya za kisasa zilizokuwa zinatolewa wakati huo zilikuwa ni pamoja na Malaria, Chanjo ya Ndui, huduma za afya dhidi ya Tauni, Malale, Ukoma na Magonjwa ya akili. Hata hivyo, huduma hizo zilikuwa zikitolewa zaidi kwa Watumishi wa Serikali ya Kijerumani, Wafanyabiashara na Askari wa Kiafrika huku Vituo vya kutolea huduma hizo za tiba vikijengwa zaidi katika miji na makazi ya wajerumani na hospitali ya kwanza ikijengwa Mamboya, Mpwapwa.

Kwa kifupi, upatikanaji wa huduma za afya za kigeni au kisasa enzi hizo haukuwa na usawa kwa wote (equity) na huduma zilikuwa chache na mbali na wananchi walio wengi.

Ndugu Wananchi, sura hii ya huduma za afya iliendelea hivyo hata baada ya vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914 ambapo, nchi ya Tanganyika ilitawaliwa na Mwingereza kuanzia mwaka 1916-1960. Ni katika kipindi hicho ambapo, huduma za tiba zilizidi kuendelezwa kwa kiasi kikubwa huko huko maeneo ya mijini ikilinganishwa na maeneo ya vijijini huku zikitoa kipaumbele kwenye tiba zaidi kuliko kinga licha ya uwepo wa idara ya tiba na usafi kwa ajili ya afya ya jamii. Kwa upande Mwingine, watumishi wa afya waliongezeka kwa idadi na aina ya kada zikiwemo madaktari wa kigeni, matibabu (medical assistants), watoaji dawa (dispensers), wasaidizi maabara (African Laboratory assistants), wahudumu wa tiba (medical auxiliaries), wafunga vidonda (tribal dressers), wakaguzi wa usafi (urban sanitary inspectors), wauguzi, n.k



Aidha, juhudi zingine katika uboreshaji wa huduma za afya zililenga katika upatikanaji wa maji, huduma za utupaji taka, kuangamiza mazalia ya mbu huku vituo vingi vya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na hospitali vikijengwa.

Ndugu Wananchi, Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliyoanza mwaka 1939 ilirudisha nyuma maendeleo ya huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya zilizokuwa zinasimamiwa na Wizara ya Afya na Kazi huku huduma hizo zikitolewa zaidi kwa wageni waliokuja nchini, hususan watumishi wa utawala wa kikoloni, wafanyabiashara na askari. Kwa hali hii ilikuwa vigumu kwa wananchi walio vijijini kupata huduma hizo. Aidha, katika kipindi hicho, kulikuwepo na uchache wa raslimali za kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya hasa watumishi, dawa, vifaa tiba na vituo vya huduma.

Ndugu Wananchi, zifuatazo ni baadhi ya takwimu za hali ya upatikanaji wa raslimali kwa ajili ya huduma za afya kabla ya uhuru;

  • Idadi ya hospitali na zahanati kwa pamoja ilikuwa 1,343 zikiwa na jumla ya vitanda 18,832.
  • Aidha, hadi kufikia mwaka 1960 kulikuwa na hospitali kubwa 12 tu zikiwa na jumla ya vitanda 3,046. Kati ya hospitali hizo, Saba (7) zilikuwa zinamilikiwa na Serikali, Nne (4) Mashirika ya Kidini na Hospitali moja (1) binafsi. Hospitali hizo zilikuwa katika maeneo ya Dar es Salaam (Jimbo Mashariki), Tanga (Jimbo la Tanga), Moshi (Jimbo la Kaskazini), Peramiho (Jimbo la Kusini), Mwanza (Jimbo la Ziwa), Tabora (Jimbo la Magharibi), Morogoro (Jimbo Mashariki), Bumbuli (Jimbo la Tanga), Ifakara (Jimbo la Mashariki), Dodoma (Jimbo la Kati), Ndanda (Jimbo la Kusini) na Sumve (Jimbo la Ziwa).
  • Uwiano wa wagonjwa kwa vitanda ulikuwa ni kitanda 1 kwa kila watu 1,000 (1:1000). Ikumbukwe, hadi kufikia mwaka 1956 kulikuwa na uwiano wa vitanda 0.6 kwa kila watu 1,000 chini ya lengo la kitanda 1 kwa kila watu 1,000.
  • Uwiano wa vituo vya afya kwa idadi ya watu ulikuwa kituo cha afya 1 kwa watu 40,000 au 50,000.
  • Aina ya watumishi kwenye vituo hivyo ulikuwa:
  • Mganga Msaidizi mmoja (1),
  • Mkaguzi wa Afya mmoja (1),
  • Wakunga kijijini wawili (2),
  • Wauguzi wawili (2),
  • Mhudumu wa Afya mmoja (1), na
  • Watumishi wa kawaida wawili (2).
  • Watumishi waliofuzu shahada ya udaktari walikuwa 400 tu huku watanzania wazawa wakiwa chini ya 20.
  • Jumla ya madaktari waliosajiliwa na wenye leseni na kufanya kazi hadi mwaka 1961 walikuwa 403 tu (182 walikuwa katika vituo binafsi; 140 wakiwa serikalini; na 81 waliajiriwa na Mashirika ya Afya ya Kujitolea). Aidha, jitihada za kuongeza watumishi zilifanyika katika kipindi cha miaka 5 ya mwisho katika kipindi cha ukoloni wa Waingereza.
Ndugu Wananchi, kwa mara ya kwanza mwaka 1960 zilianzishwa huduma za kinga kwa njia ya chanjo kwa watoto. Katika kipindi hiki Mashirika ya Kujitolea yalitoa mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za mama na mtoto huku mama 1 kati 6 ndiye aliweza kupata huduma za uzazi kutoka kwa mtumishi wa afya aliyepata mafunzo.

Hadi kufikia Desemba 1961 hali ya utumiaji wa huduma za Mama na Mtoto ilikuwa kama ifuatavyo;- Jumla ya Kiliniki zilifikia 412 ambazo zilikuwa chini ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Kujitolea na ziliweza kutoa huduma za Kiliniki kwa jumla ya wajawazito 177,214.

  • Serikali Kuu ilikuwa ikimiliki Kiliniki 71 ambapo mahudhurio ya kwanza kwa mama wajawazito yalikuwa 48,667,
  • Serikali za Mitaa ilikuwa ikimiliki Kiliniki 204 ambapo mahudhurio ya kwanza ya Mama Wajawazito walikuwa 68,601; na
  • Mashirika ya kujitolea yalikuwa yakimiliki Kiliniki 137 ambapo akinamama wajawazito 59,946 walihudumiwa.
Ndugu Wananchi, kipindi hicho (Disemba, 1961) pia kulikuwa na Kliniki za watoto zipatazo 454 ambapo;

  • Serikali Kuu ilimiliki 69 na watoto 29,715 walihudhuria hudhurio la kwanza;
  • Serikali za Mitaa ilimiliki Kiliniki 195 na watoto 52,635 walihudhuria hudhurio la kwanza; na
  • Mashirika ya Kujitolea yalimiliki Kiliniki 190 ambapo watoto 54,154 walihudhuria udhurio la kwanza.
Kwa ujumla wake Kliniki hizi za watoto ziliweza kutoa huduma za Kiliniki 136,504 tu.

Ndugu Wananchi, endeshaji wa huduma za Afya Serikali Kuu ulikuwa katika ngazi tatu ambazo ni Wizara, Mkoa na Wilaya. Huduma za afya ziliendeshwa chini ya Wizara ya Afya na Kazi na Kiongozi Mkuu alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali akiwa na wasaidizi wa aina tatu: Madaktari Waandamizi (Principal Medical Officers) 3; Muuguzi Mkuu (Principal Matron), na Mkaguzi Mkuu wa Afya (Chief Health Inspector). Huduma maalumu zilizosimamiwa zilikuwa: Mafunzo (Medical training); Huduma za maabara na dawa (pathology and pharmaceutical services); Huduma za afya ya akili (psychiatric services); na Vitengo maalumu: Malaria, Elimu ya Afya na Lishe.

Ndugu Wananchi, sasa naomba nijielekeze kwenye hali ya Huduma za Afya baada ya Uhuru wa Desemba 9, 1961; tunapotimiza miaka 60 tangu kupatikana kwa Uhuru tunashuhudia mabadiliko na mafanikio makubwa ya maendeleo kwenye huduma za afya ukilinganisha na kabla ya uhuru.

Maendeleo au mafanikio haya yametokana na msingi mzuri na thabiti uliowekwa na Rais wa kwanza na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo alielekeza nguvu za Taifa katika kukabiliana na adui watatu wakubwa, yaani Ujinga, Umaskini na Maradhi huku viongozi wengine wa taifa hili awamu zote wakiendelea kupambana kutimiza ndoto hizo. Vilevile, mafanikio hayo yametokana kazi kubwa ya Serikali za Chama cha Mapinduzi na Ilani zake nzuri awamu zote sita za uongozi zilizowezesha kupata Marais mahiri na wenye uthubutu, kuwa na utashi wa kisiasa kwenye maendeleo nyakati zote, kuunda Serikali zenye uongozi bora na kupata Sera nzuri za Afya.

Pia, mafanikio haya yametokana na uboreshwaji wa ushirikiano na mashirika ya dini na binafsi, wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja wananchi wa taifa hili kwa ujumla wake.

Kwa ujumla wake, mazingira haya yamewezesha utekelezaji wa masuala ambayo huko nyuma yalikuwa yanaoneka kama ndoto.



Ndugu Wananchi,
mafanikio ya miaka 60 baada ya uhuru ni mengi na ni vigumu kuyaeleza kinagaubaga na kumaliza hivyo nitafupisha kwenye maeneo muhimu kama ifuatavyo; miaka 60 baada ya uhuru;-

  • Idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote imeongezeka hadi kufikia vituo 8,537 ikilinganishwa na vituo 1,343 Mwaka 1960. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 84.26. Aidha, kati ya vituo hivyo, Serikali inamiliki asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27.
  • Mtandao wa vituo vya huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi ambapo; zahanati ni 7,242; vituo vya afya 926; na Hospitali za Wilaya ni 178, Hospitali zingine ni 151. Aidha, hospitali za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda Sita (6), hospitali za ubingwa maalumu ni Tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH).
  • Vituo vyote hivi vina jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na asilimia 79.18. Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa watu 6,751.5 (1: 6,751.5) tofauti na 1:40000-50000 kabla ya uhuru. Hivyo, Tanzania imefikia malengo ya umoja wa mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na jiografia.
  • Aidha, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni kitanda kimoja kwa watu 637 (1:637) ukilinganisha na 1:1000 kabla ya uhuru. Hadi mwaka 2020 uwiano wa wagonjwa kwa vitanda umekuwa kitanda kimoja kwa watu 19 (1:19).
  • Idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu kwenye vituo vya huduma umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao awali ulikuwa haufanyiki.
  • Idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi takribani 71,365 na usajili unaendelea kila siku. Hawa ni baadhi tu ya kada zinazojumuisha madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu. Hii ni hatua kubwa sana.
  • Hadi kufikia Juni, 2021 huduma za chanjo zimepanuka na kuimarika na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza kwa ufanisi eneo hili hususan chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja (1) huku utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 101. Aidha, kila kituo cha huduma za afya kina huduma ya chanjo kwa ajili ya Kinga ya ugonjwa wa Polio (OPV3), PENTA-3 kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda (tetanus), homa ya ini na homa ya uti wa mgongo na chanjo ya Surua/ rubella.
  • Idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya uzazi na mtoto.
  • Mifumo ya uongozi na uendeshaji wa vituo vya huduma za afya imeboreshwa kiasi kwamba wananchi nao ni sehemu ya bodi za ushauri, uendeshaji na kamati za ushauri na uendeshaji kuanzia hospitali za kitaifa hadi zahanati. Hii ni pamoja na taasisi zote katika sekta ya afya. Hivyo, mipango, utekelezaji na tathmini vinafanywa siyo na wataalamu tu bali na wananchi wenyewe, fedha za mipango ya maendeleo na uendeshaji kwenye sekta ya afya sasa zinapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za vituo zinazosimamiwa na wananchi wenyewe (DHFF kwa ajili ya uendeshaji na kwa miradi ya ujenzi kupitia Force Account). Maendeleo haya ni makubwa yanahitaji kusimuliwa kwa sauti kubwa na kukumbukwa daima huku tukijivunia, kuyafurahia na kuyaenzi.
Ndugu Wananchi, Hata sasa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kazi ya kuboresha huduma za afya inaendelea kwa kasi kubwa Kama mlivyosikia hivi karibuni, juhudi za Mheshimiwa Rais katika kupambana na madhara ya UVIKO-19 zimewezesha Nchi kupata mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 567.25 sawa na Shilingi trilioni 1.362 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo, tarehe 10/10/2021 wakati akizindua kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19 alitenga Shilingi Bilioni 466.781 (34%) kwa ajili ya Sekta ya Afya ziende;

  • Kuimarisha huduma za dharura, wagonjwa mahtuti na wanaohitaji uangalizi maalum; itakayogharimu Shilingi bilioni 254.4.
  • Kuimarisha huduma za maabara, mionzi na tiba mtandao; itakayogharimu Shilingi bilioni 111.5
  • Kuimarisha huduma za chanjo dhidi ya UVIKO - 19 na elimu ya afya kwa umma dhidi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo; itakayogharimu Shilingi bilioni 43.2
  • Kuimarisha miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za Afya; itakayogharimu Shilingi bilioni 41.8
  • Kufanya tafiti za kitaalam kuhusu Virusi vya Korona pamoja na kuwajenga uwezo watoa huduma za Afya; itakayogharimu Shilingi bilioni 15.9.
Hii ni kudhihirisha kuwa, mapambano dhidi ya adui maradhi bado yanaendelea hata kwenye serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa JMT.

Ndugu Wananchi, mapambano haya miaka kadhaa iliyopita baada ya uhuru yalipelekea kuzaliwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM-2007-2017) uliochangia;

  • Kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya nchi nzima;
  • Kupungua kwa vifo vya watoto;
  • Kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyote;
  • Kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi;
  • Kuongezeka kwa ajira ya wataalam waliopelekwa katika ngazi zote za vituo vya kutolea huduma katika Halmashauri, Mikoa, Kanda na Taifa.
Vilevile, mapambano dhidi ya adui maradhi baada ya uhuru yaliifikisha nchi kwenye kuanzishwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ambapo kama nilivyosema awali hivi sasa tunazo hospitali 12 za ubingwa daraja la juu zinazotoa huduma ikiwemo;

  • Upasuaji mkubwa wa moyo,
  • Huduma za usafishaji na upandikizaji wa figo,
  • Matibabu ya kisasa ya Saratani,
  • Matibabu ya mifupa na huduma nyinginezo nyingi ambazo zimepunguza rufaa ya wagonjwa kwenda nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zingetumika kuhudumia rufaa hizo.


Ndugu Wananchi,
katika kuendeleza mapambano na adui maradhi, Serikali ya Awamu ya Sita katika mwaka huu wa 60 pia imetenga jumla ya Shilingi bil 149 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (META), Hospitali ya Kanda Chato Awamu ya Kwanza pamoja na hospitali mpya za Rufaa za Mikoa ya Njombe, Simiyu, Geita, Songwe, Katavi na Sekou Toure, Mwanza. Vilevile, Manyara, na Mara – Hospitali ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa), Kazi inaendelea.

Ndugu Wananchi, ukiacha maendeleo ya miundombinu baada ya Uhuru, vilevile, maendeleo makubwa yamepatikana kwenye vifaa tiba vya kisasa na wataalamu bobezi wa tiba ambao, wamefanya kazi nzuri iliyopunguza rufaa za nje ambapo katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Juni 2021, ni wagonjwa 2 tu walipatiwa rufaa nje ya nchi, ukilinganisha na wagonjwa 554 waliopatiwa rufaa nje ya nchi mwaka 2015/16. Haya ni mapinduzi makubwa kwa kipindi cha miaka 60 tangu tupate uhuru.

Zifuatazo ni baadhi ya alama za mapinduzi haya kwenye baadhi ya hospitali za ubingwa bobezi nchini Tanzania kama ifuatavyo kwa ufupi;



Hospitali ya Taifa Muhimbili huduma mpya zimeanzishwa zikiwemo;


  • Kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo (Dialysis) ambazo pia zimeenea hospitali mbalimbali nchini hadi hospitali za rufaa za mikoa;
  • Kuanza upandikizaji Figo (Renal Transplant) ambapo hadi sasa wananchi 64 wamenufaika na huduma hiyo pia huduma hii inapatikana katika hospitali zingine kama BMH na zingine ziko mbioni kuanza;
  • Upandikiza vifaa vya kusaidia watoto kusikia (Cochlear Implant) kupitia Hospitali za umma katika ukanda wa Afrika Mashariki na zaidi ya watoto 32 na watu wazima wawili wamenufaika na huduma hizi; na
  • Tiba Radiolojia (Interventional Radiology) ambapo kwa miaka mingi wagonjwa waliokuwa na uvimbe kwenye kinywa na mataya walianza kufanyiwa upasuaji hapa nchini.
Hospitali ya Saratani Ocean Road (ORCI);

  • Sasa tunazo mashine za kisasa za teknolojia ya 3D za tiba mionzi za LINAC na CT simulator zilizogharimu Tsh 9.5 Bilioni zinazotibu saratani kwa sayansi ya kisasa na sahihi zaidi.
  • Serikali Imetoa jumla ya Tsh 14.5 Bilion za Mradi wa Jengo, na Mashine za Cyclotron na PET CT scan ili kuimarisha vipimo vya ugunduzi na uchunguzi wa saratani ambapo kwa sasa havifanyiki nchini wala Ukanda wa Africa mashariki na Kati.
Aidha, kuimarishwa kwa utoaji wa huduma hasa tiba mionzi, kumeendelea kuwavutia wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja nchini kwa ajili ya tiba. Katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Juni, 2021 jumla ya wagonjwa wapya 55 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za uchunguzi na tiba ya saratani. Maboresho yote haya yamepunguza rufaa za wagonjwa wa saratani nje ya nchi kwa asilimia 90% na Serikali imeokoa takribani Tshs 10 bilioni ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi.



Hospitali ya tiba ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamo (MOI);
hivi karibuni serikali imenunua na kufunga mashine ya kupasua ubongo bila kufungua kichwa (Angio Suite iliyogharimu bilioni 7.9). Ikumbukwe, kufikia Januari 2021 mashine hii ilipofungwa hakukuwa na kama hii Afrika Mashariki bali ilikuwepo Afrika Kusini. Kufikia leo imeshawafanyiwa operesheni ya ubongo wagonjwa 68 bila kufungua kichwa.



Hospitali ya tiba ya moyo (JKCI);
huduma nyingi mpya za kisasa za matibabu ya moyo zimeendelewa kutolewa na pia upo mtambo wa kisasa wa Cathlab na Carto 3 wa uchunguzi na kutibu magonjwa ya moyo wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 ambapo, wagonjwa 6,513 wameshafanyiwa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo na 2,436 wametibiwa matatizo ya mishipa ya damu.





Hospitali ya Rufaa Kanda ya Ziwa (Bugando);
huduma mbalimbali mpya za kibingwa zimeendelea kutolewa na zaidi;

  • Hospitali imenunua mashine ya tiba ya mionzi inayoitwa brachytherapy, mtambo wa kusafisha damu (renal dialysis), CT-Scan na mtambo wa kuzalisha maji tiba.
  • Umefanyika ununuzi wa MRI yenye Thamani bilioni 2.43 (Euro 900,000) katika Hospitali hii vilevile, imeanzisha huduma za upasuaji kwa Watoto wachanga waliozaliwa na ulemavu (Congenital Malformations).


Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini (KCMC).


  • Imewezeshwa kwa mashine za kisasa za uchunguzi wa magonjwa ikiwa ni pamoja na MRI, CT-Scan yenye ukubwa wa Slice 128.
  • Serikali inatekeleza mradi wa bilioni 4 wa ujenzi wa idara ya matibabu ya saratani kwa mionzi.


Hospitali ya Kanda ya Kati ya (BMH) Dodoma;
Pamoja kuanza huduma mwaka 2017, imekua kwa kasi na kuanza kutoa huduma za ubingwa bobezi mathalani;

  • Imeshapandikiza figo wagonjwa 23 na kati ya hao 16 wamepandikizwa na madaktari wazawa.
  • Inatoa matibabu ya magoti kwa kutumia matundu madogo kwa watu wenye matatizo ya miguu,
  • Inazo huduma za kuondoa mawe kwenye figo kwa kutumia vifaa maalumu bila kulazimika kufanya upasuaji kwa mgonjwa;
  • Imeweza kutoa huduma ya kupandikiza Betri kwenye moyo kwa watu wazima wawili (2).








Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya).


Hii ilifunguliwa mwaka 1985 na Mtoto wa Malkia wa Uingereza (Prince Anne) na kufikia miaka 60 baada ya uhuru imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo;-

  • Kutoa huduma za kibingwa kama upasuaji wa kawaida na upasuaji kwa njia ya vitundu “Laparascopic Surgery” pamoja na usafishaji wa figo (haemodialysis).
  • Kumiliki maabara ya kisasa iliyopewa Ithibati “Accredation” yenye uwezo wa kufanya vipimo vya ngazi ya kimataifa pia ina uwezo wa kupima magonjwa ya Ebola na mengine yanayofanana na hayo.
  • Kuanzisha huduma ya Mkalimani wa Viziwi jambo ambalo limepelekea mafanikio kwa Taasisi na Jamii kwa ujumla. Imeweza kutoa huduma ya upasuaji mkubwa kwa viziwi sita (6) na kutoa huduma ya elimu ya uzazi wa mpango na kuepusha mimba zisizo tarajiwa kwa watu wenye matatizo ya kusikia.
  • Imeboresha miundombinu kwa kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa MAJI TIBA (Infusion).


Aidha, hospitali zote hizi pia zinatumia mifumo ya kisasa ya kidigitali katika kuhudumia wateja na kuweka kumbukumbu zao pia kudhibiti mapato na matumizi ya taasisi hivyo, kwa kiasi kikubwa zimepunguza utegemezi kwa serikali lakini pia zimeboresha huduma kwa mteja ukilinganisha na miaka kdhaa nyuma.



Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe (Dodoma).


Kabla ya Uhuru huduma za Afya ya Akili zilikuwa duni sana ikilinganishwa na hivi sasa. Aidha, idadi ya Wataalam wauguzi “Mental Nurses” katika eneo la Afya ya akili walikuwa 12. Wagonjwa kutoka sehemu mikoa yote ya Tanganyika walikuwa wakipelekwa Hospitali ya Mirembe na Isanga (Broadmoor).

Wagonjwa walisongamana sana katika hospitali hiyo na wengi walitibiwa mbali na ndugu zao bila mawasiliano na nyumbani kwao.

Baada ya Uhuru Serikali imefanikiwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo.


  • Kuanzisha kozi za “certificate na diploma in psychiatric nursing” katika hospitali ya Mirembe mwaka 1973 – 1980s. Katika miaka hiyo ya 1980 ikaanzishwa kozi ya AMO Psychiatry.
  • Kuanzishwa kwa masomo ya udaktari na udaktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili ambapo hadi sasa tuna madaktari bingwa zaidi ya 40.
  • Kuanzishwa kwa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 “The Mental Health Act, 2008. Act No 21, 2008”. Sheria hii ina madhumuni ya kuratibu na kusaidia Wagonjwa wa afya ya akili nchini na kuweka huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya akili, na kushirikisha jamii katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa akili.
  • Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni ilanzisha mpango wa Huduma ya Afya ya Akili Ngazi ya Msingi. Mradi huo ulifanywa kwa majaribio mikoa ya Kilimanjaro na Morogoro na ukawa wa mafanikio makubwa.
  • Kati ya 1980 hadi 1990, mikoa ilieendelea kuhimizwa kuanzisha wodi za wagonjwa wa akili pamoja na vijiji vya utengemao.
  • Vitengo vya wagonjwa wa akili vilianzishwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Tabora, Mwanza, Kigoma, Kagera na Kilimanjaro ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Mirembe.
  • Mikoa yote Tanzania bara sasa ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa akili katika wilaya zao, hadi ngazi ya zahanati. Mafunzo ya kueneza stadi za kuwahudumia wagonjwa ngazi ya msingi zinapatikana katika vituo vya afya na zahanati.
  • Kuanzishwa tiba ya saikolojia ambayo inasaidia wagonjwa wanaoendelea na tiba za kibaolojia waendelee kuimarika na kurudi kataka kazi zao za kijamii.




Hospitali ya Udhibiti wa Maambuki Kibong’oto (Kilimanjaro).

Hospitali hii
ilianzishwa mwaka 1926 kwa lengo la kukinga na kudhibiti kifua kikuu na magonjwa ambukizi. Aidha, mwaka 1952 ilibadilishwa rasmi kuwa hospitali ya TB na Lady Twining – Mke wa Gavana wa Tanganyika. Mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo;-

  • Kabla ya uhuru ilikuwa na wodi 3 zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa sasa hospitali ina wodi 7 zenye vitanda 300 vya kulaza wagonjwa, ambapo vitanda 120 ni kwa ajili ya wagonjwa wa TB sugu, vitanda 120 wagonjwa wa TB ya kawaida na vitanda 60 kwa wagonjwa wengine
  • Hospitali iligatua matibabu ya kifua kikuu sugu toka hospitali 1 ya kibongoto 2009 hadi kufikia vituo 179 nchini
  • Serikali imenunua mashine maalumu ya kisasa (Migit) yenye uwezo wa kupima usugu wa dawa za kifua kikuu na kuotesha vimelea vya kifua kikuu cha kawaida na kifua kikuu sugu ndani ya muda mfupi (wiki 3 hadi 4) badala wiki nane mpaka 10 kwa kutumia njia ya kawaida ilivyokuwa kabla uhuru.
  • Uboreshwaji wa huduma za uchunguzi wa vinasaba (whole genomic sequencing) na kuweza kubainisha anuai ya virusi vinavyosababisa corona nchini ambako kabla ya uhuru huduma hii haikuwepo
  • Pamoja na huduma hizi katika hospitali, inatoa huduma za kijamii kwa njia ya mkoba kwa kutumia gari maalumu la kisasa lenye kiliniki tembezi.
  • Serikali inaendelea na ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa ya afya ya jamii yenye hadhi ya Biosafety level 3 ambayo inagharimu jumla ya shilingi 11,337,672,870.88.


Ndugu Wananchi,
katika kuzingatia upatikanaji wa huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi na kwa uwiano wa kijiografia nchini tofauti na kabla ya uhuru au miaka kadhaa iliyopita, Serikali inajenga zingine mpya ikiwemo Hospitali ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara.



Aidha, inapanua miundombinu kwenye Hospitali kongwe za Mikoa, Kanda, Maalumu na Taifa kama ifuatavyo;

  • Mbeya; ujenzi wa jengo la ghorofa Sita (6) la afya ya uzazi na mtoto Mbeya (META).
  • KCMC; Ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa saratani, upanuzi wa Idara ya kusafisha damu na figo (Hemodialysis) na kitengo cha Endoscopy
  • Kibong’oto; Ujenzi wa Maabara ya Afya ya Jamii ngazi ya tatu (BSL3). Jengo la Maabara husika lina ghorofa tatu (Ground + 3 floors)
  • Mawenzi; jengo la afya ya uzazi na mtoto pia jengo la huduma za dharura.
Ndugu Wananchi, katika kipindi hiki cha baada ya uhuru ukiacha ujenzi wa hospitali mpya za mikoa nilizotaja awali za Njombe, Songwe, Simiyu, Geita, Manyara, Songwe na Mara – Kwangwa na upanuzi wa hospitali kongwe za rufaa za mikoa, maendeleo mbalimbali yanafanyika ikiwemo;

  • Usimikaji wa mitambo ya kuzalisha hewa tiba kwa thamani ya shilingi bilioni 8.7 unaendelea katika Hospitali za Rufaa za Mikoa Saba (7) ambayo ni Geita, Manyara, Dodoma, Dar es Salaam-Amana, Mtwara, Ruvuma-Songea na Mbeya.
  • Ufungaji CT scan, Ultra Sound na vifaa vya mama na mtoto, upasuaji, utakasaji, incinerator umefanyika katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure kwa thamani ya Shilingi. 2,228,448,375.00.
  • Ununuzi na usimikaji wa CT Scan yenye thamani ya shilingi bilioni 1,444,500,000 umefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Mwananyamala RRH).
  • Ununuzi na sambazaji wa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 6 vya Mradi wa ORIO (Fluoroscopy, Digital X-ray, ultrasound, incinerator n.k) unaendelea kwenye hospitali tisa (9) hapa nchini; (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Kitete - Tabora, Shinyanga, Kigoma (Maweni), Bukoba - Kagera, Mara, Hospitali ya Wilaya Bukombe, Chato na Misungwi).
  • Ununuzi wa mashine za kidigitali za X-ray katika hospitali zote 28 za rufaa za mikoa kupitia mradi wa ORIO unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi.
  • Umefanyika ununuzi wa mashine za kisasa “GeneXpert” 239 za kupima Kifua kikuu zinazotoa majibu ndani ya masaa mawili ikilinganishwa na hadubini zinazotoa majibu baada ya masaa 24.
  • Baadhi ya miundombinu inayopanuliwa iweze kutoa huduma bora zadi kwenye hospitali hizi za mikoa ni pamoja na;
  • Ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala lenye ghorofa nne na pia Mawenzi Kilimanjaro.
  • Ujenzi wa jengo la kutolea huduma za dharura (EMD katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
  • Ujenzi wa jengo la Methadone lenye ghorofa tatu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga.
  • Ujenzi wa jengo la huduma za upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma – Maweni.
  • Ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa
  • Ujenzi wa jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora – Kitete
  • Ujenzi wa Jengo la Wodi ya wagonjwa walio chini ya uangalizi maalum, Wodi ya Upasuaji, jengo la huduma ya Upasuaji na utakasaji vifaa tiba pamoja na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya


Ndugu Wananchi,
Serikali haikuzisahau hospitali za ngazi ya halmashauri, vituo vya afya na zahanati ambapo, baada ya uhuru kupitia MMAM ilitoa msukumo mkubwa kwa ufupi kama ifuatavyo;

  • Ukilinganisha na kabla ya huru, hivi sasa kuna jumla ya Zahanati 7,242 Vituo vya Afya 926 na Hospitali za Halmashauri 178. Jumla ya Vituo vya Afya 487 kati ya vilivyopo vinafanya upasuaji wa dharura kwa maana hiyo, watumishi wa kada mbalimbali muhimu wanapatikana hadi ngazi ya vituo vya afya tofauti na kabla ya uhuru.
  • Huduma za uchunguzi wa maabara na mionzi nazo zimeimarika. Umefanyika ununuzi wa Xray za kidigitali (Digital X-ray 18) kwa gharama ya Shilingi za kitanzania 5,290,000,000.00 sawa na shilingi 264,500,000.00 kila moja na kusambazwa hospitali 14 za halmashauri; (Mangaka, Tunduru, Mbinga, Kasulu, Nyamagana, Butiama, Makambako, Makete, Mbarari, Tukuyu, Itumba, Nkasi, Usangi, na Same) na hospitali 4 za Wilaya (Kisarawe, Songwe/ Mwambani, Namtumbo, na Musoma/ Mwl.Nyerere memorial Hospital). Ununuzi huu umefadhiliwa wadau wa maendeleo Global Fund.
  • Huduma za uchunguzi kupitia Ultra Sound zimeanza kutolewa kwenye vituo vya afya 125 katika Halmashauri mbalimbali nchini.
  • Vipimo mbalimbali vya maabara vinafanyika ngazi zote za vituo vya afya ya msingi.
Ndugu Wananchi, katika miaka sitini (60) ya Uhuru Serikali inaratibu uendeshaji wa huduma za afya kidigitali kupitia mkakati wa TEHAMA (Digital Health Strategy 2019-2024) ambapo mpaka sasa;

  • Imepeleka Mkongo wa Taifa wa mawasiliano (fiber optic cable) na kujenga miudombinu ya mtandao (Loca Area Network) kwenye hospitali zote za rufaa kuanzia ngazi ya Taifa, Kanda, Mkoa na hospitali maalumu (specialized hospital).
  • Imeboresha upatikanaji wa mtandao wa uhakika katika vituo vya ngazi ya msingi.
  • Imesambaza vifaa vya TEHAMA kama Kompyuta, “Server “, printer na vishikwambi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kurahisiha matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kutolea huduma na kukusanya taarifa.
  • Kwa mifumo hii, udhibiti wa raslimali fedha na bidhaa za afya na uwajibikaji pamoja na upatikanaji wa taarifa kwa wakati unaendelea kuimarika ulikinganisha na miaka kadhaa iliyopita.


Ndugu Wananchi,
katika kuimarisha huduma za afya baada ya uhuru serikali imefungua taasisi mbalimbali saidizi kama ifuatavyo;



Taasisi ya Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya;
Kabla ya uhuru huduma za matibabu zilikuwa bila malipo hadi kufikia miaka ya 1997 zilipoanza kutolewa kwa sera ya uchangiaji na msamaha kwa wasio na uwezo. Hata hivyo, mfumo huu ulibainika kupitwa na wakati hivyo serikali kuanzisha bima za afya ili kuwawezesha wananchi wananchi kumudu gharama za matibabu. Hivi sasa, Serikali inayo Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na Bima ya Afya ya Jamii (CHF). Aidha, zipo na Bima mbalimbali za binafsi.

Kupitia mifuko hii ya bima za afya;

  • Hifadhi ya jamii imeimarika ambapo jumla ya watanzania 8,224,271 sawa na asilimia 14.7 ya watanzania wote wananufaika na huduma za mifuko ya bima ya afya. Kati ya wananchi waliojiunga na mfumo wa bima ya afya, asilimia 8 wamesajiliwa na NHIF, asilimia 5.4 wanahudumiwa na iCHF, asilimia 0.3 wananufaika na huduma kupita SHIB-NSSF na asilimia 1 wamejiunga na bima ya afya inayotolewa na makampuni ya bima binafsi za afya.
  • Hadi kufikia Juni 2021 jumla ya vituo 8,482 vya ngazi ya Zahanati hadi Taifa, vya Serikali, Mashirika ya Dini na Binafsi vinahuhumia wanachama wa NHIF ikilinganishwa na vituo 3,197 vya mwaka 2001/02. Mwanachama wa NHIF kwa kutumia kadi yake anatibiwa popote Tanzania Bara na Zanzibar katika vituo hivi vilivyosajiliwa. Hivyo, Kadi ya NHIF haina mipaka ya kimikoa.


Ndugu Wananchi,
Hivi sasa Mfuko umeweka utaratibu rahisi kwa kila kundi kuchangia, kujiunga na kuanza kunufaika kwa hiari ikilinganisha na kundi la watumishi wa umma tu ambalo liliwezeshwa kujiunga wakati Mfuko unaanzishwa.

Wanachama wa mfuko wa taifa wa bima ya afya wanapata manufaa mbalimbali ikiwemo;

  • Kupata huduma kuanzia za afya ya msingi hadi za kibingwa ikiwemo matibabu ya moyo, figo, saratani, upandikizaji wa viungo, vipimo vikubwa kama CT Scan na MRI. Awali huduma kwa wanachama zilikuwa chache mathalan idadi ya vipimo ilikuwa 9 na dawa 440 wakati mfuko unaazishwa mwaka 2001.
  • Sasa hivi kitita cha huduma kina jumla ya dawa 975 zikiwemo za magonjwa ya Sukari, Moyo na Saratani na vipimo 354 vikiwemo vikubwa na vidogo kulingana na maendeleo ya teknolojia ya tiba. Huduma za upasuaji mkubwa 210 na mdogo 167 na wa kibingwa 148. Aidha huduma za kulazwa, kujifungua, macho, meno, n.k zinatolewa kwa wanachama wa NHIF kulingana na miongozo ya tiba iliyopo.
  • Kulingana na mahitaji ya wanachama waajiri, Mfuko umeweka utaratibu unaowezesha waajiri kulipia watumishi wao huduma za ziada (Suplimentary package) ambazo hazipo kwenye kitita cha mafao cha NHIF. Mathalani, Huduma za Uokozi (Air and ground evacuation), dawa za majina ya kibiashara, huduma za miwani, n.k
Ndugu Wananchi, kwa kutambua kuwa wananchi wengi (takriban asilimia 85.3) wako nje ya mfumo wa bima ya afya, Serikali inaendelea kukamilisha muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote na imefikia hatua kubwa. Huu ni mwelekeo mzuri wa nchi katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru.



Taasisi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD);


Ndugu Wananchi,
Ili kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, baada ya uhuru serikali ilianzisha taasisi ya MSD ambayo imeendelea kuboresha utekelezaji wake kwenye mambo makubwa kama ifutavyo;

  • Kuagiza dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji; hatua hii imewezesha kupata bidhaa hizo kwa gharama nafuu ambapo hadi sasa upatikanaji wa bidhaa za afya umeimarika kwa asilimia 55.
  • Kuingia mikataba na watengenezaji wa vifaa vya maabara na vitendanishi vyake, na mashine za kuchuja damu. Hatua hii imepunguza gharama za bidhaa hizo kwa asilimia 50 -100 na hatua hii inatarajiwa kuokoa shilingi bilioni 9.7 kwa mwaka.
  • Ujenzi wa kiwanda cha barakoa ambapo bei ya barakoa moja imeshuka kutoka kuuzwa shilingi 1,600 hadi kuuzwa shilingi 600 na kuokoa shilingi milioni 683,980,500 ambazo zingetumika kwa kuagiza kutoka nje ya nchi;
  • Kuanza uzalishaji wa bidhaa za afya ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Keko Pharmaceutical Limited (ambacho MSD imepewa jukumu la kukisimamia), Kiwanda cha Keko Pharmaceutical kina uwezo wa kuzalisha aina 10 za vidonge ambavyo kati ya hivyo, aina mbili ni vya maumivu na nane ni vya kuua vimelea vya magonjwa, yaani Antibiotics na moja ya kutibu fangasi.
  • Kujenga viwanda vinne vya uzalishaji dawa na vifaa tiba huko Idofi Makambako. Kiwanda cha mipira ya mikono, Vidonge, vidonge vya rangi mbili na dawa za majimaji (syrup) ambapo vitaipinguzia gharama Serikali kwa kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 33 kwa mwaka.
  • Serikali imeongeza bajeti ya fedha za kununulia dawa hadi kufikia shilingi Bilioni 277.49 mwaka huu.
  • Taasisi ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa tiba (TMDA); taasisi hii imepata mafanikio makubwa yakiwemo;
  • Hadi kufikia Juni, 2021, Mamlaka ilikuwa imesajili jumla ya viwanda vya ndani 36, ambapo 11 vya dawa, viwanda 14 vya vifaa tiba na 11 vya gesi tiba vinavyofanya kazi ukilinganisha na kiwanda kimoja cha dawa kilichokuwa kimesajiliwa wakati wa Uhuru mwaka 1961.
  • Idadi ya bidhaa za dawa, zilizosajiliwa hadi kufikia mwaka 2020/21 ni 16,467 ikilinganishwa na 265 zilizosajiliwa mwaka 2003/04 ikiwa ni ongezeko 6,214%.
  • Idadi ya majengo yaliyosajiliwa ya biashara za bidhaa za dawa zinazodhibitiwa na Mamlaka hadi mwaka 2020/21 ni 11,156 ikilinganishwa na majengo 1,504 yaliyosajiliwa mwaka 2007/2008 sawa na ongezeko la 742%.
  • Taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA); taasisi hii inahusika na kufanya uchunguzi wa kimaabara juu ya masuala mbalimbali ya kisayansi. Taasisi hii imeendelea kuimarika kutoka utumiaji wa mbinu duni za makaratasi ya uchunguzi hadi mbinu zinazotumia mitambo na vifaa vya kisasa. Mitambo hii imeifanya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ya pili katika maabara zenye vifaa vya kisasa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati, Kusini mwa Afrika ikitanguliwa na maabara chache za Afrika Kusini.
  • Taasisi ya Utafiti Afya (NIMR); taasisi hii inahusika na Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ambapo imeweza kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuhusu Malaria, kifua kikuu (TB), UKIMWI, afya ya mama na mtoto, magonjwa ya kitropiki yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza, muungano wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza (co-morbidities), viashiria vya afya vya kijamii pamoja na, magonjwa mtambuka ya binadamu na wanyama (One Health). Pia Taasisi imeendelea kutekeleza miradi ya utafiti inayolenga kuimarisha mifumo ya afya na tafiti hizo zililenga katika kutafiti na kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa hata pale ambapo madawa katika bohari ya dawa yanapatikana.

  • Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC); Taasisi hii inahusika na kuishauri serikali, wananchi pamoja na wadau wote wa lishe nchini namna ya kupambana na aina zote za utapiamlo.
  • Katika miaka 60 ya Uhuru, TFNC kwa kushirikiana na sekta nyingine imechangia kutekeleza afua ambazo zimepelekea kupunguza viwango vya utapiamlo kwa kiasi kikubwa kama ifuatavyo;-

  • Udumavu kwa Watoto chini ya miaka mitano kutoka zaidi ya asilimia 50 kabla ya uhuru kufikia asilimia 31.7 mwaka 2018;
  • Ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 6 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2018;
  • Uzito pungufu kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 29 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 14 mwaka 2018:
  • Upungufu wa damu kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa (miaka 15-49) kutoka asilimia zaidi ya 50 hadi kufikia asilimia 28 mwaka 2018.
  • Pia Taasisi imewezesha kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wenye umri chini ya miezi sita kutoka asilimia 24 hadi kutikia asilimia 59 mwaka 2018.


Ndugu Wananchi,
zifuatazo ni takwimu chache za utumiaji wa vituo vya kutolea huduma kwa rejea ya Huduma za Afya ya Uzazi (Mama) na Mtoto;-

  • Ongezeko la wajawazito waliohudhuria mahudhurio manne au zaidi ya kiliniki hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2021, asilimia 93.4 ya wajawazito walihudhuria kliniki.
  • Ongezeko la akinamama kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya limefikia hadi asilimia 83.1 mwaka 2020 ambayo ni zaidi ya lengo la Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP IV) la asilimia 65.
  • Idadi ya akinamama waliojifungua na kurudi kiliniki siku mbili baada ya kujifungua imefikia asilimia 62. Mwitikio huu ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto, kwa kuwa asilimia 60 ya vifo vitokanavyo na uzazi hutokea kipindi cha baada ya kujifungua kutokana na matatizo ya kupoteza damu, kifafa cha mimba na maambukizi ya bakteria.
  • Hadi kufikia Machi 2021, jumla ya akina mama 332,620 walifanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi kwenye vituo 794 vya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi.


Baadhi ya vashiria vingine vya mafanikio ni pamoja na;

  • Chanjo kwa watoto vhini ya miaka mitano imeendelea kutolewa kwa wastani wa 95% kwa miaka mitano mfululizo kutoka mwaka 2015.
  • Ugonjwa wa Polio (Acute Flaccid Paralysis) (kupooza ghalfa kwa watoto) tumefanikiwa kuumaliza kwa chanjo na hivyo Tanzania kutangazwa kuwa huru dhidi ya ugonjwa huu toka mwaka 2015 na kupewa cheti cha kuwa huru miaka mitano baadae yaani mwaka 2020.
  • Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 112 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2004/05 hadi vifo 50 kila vizazi hai 1000 mwaka 2020. Tukumbuke mwaka 2013 Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi ambazo zilifanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kufikia malengo ya milenia ya nne (MDG 4).
  • Vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja (Infant Mortality) vimepungua kutoka 94 kwa vizazi hai 1000 mwaka 1992 hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2020 (DHS projection 2020).
  • Vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28 (neonatal mortality) vimepungua kutoka vifo 32 kwa kila vizazi hai 1000 (2004/05) hadi vifo 20 kwa kila vizazi 1000 (2020).
  • Vifo vya wajawazito vimepungua kutoka vifo 870 kwa kila vizazi 100,000 (1990) kufikia vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 (2020).
  • Kuenea kwa malaria (prevalence) kumepungua kwa 50% kati ya miaka ya 90s hadi kufikia 7.5% mwaka 2017 (MIS - 2017). Vilevile, idadi ya wanaofariki kwa malaria imepungua kwa 61% kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 2,460 mwaka 2020.
  • Hali ya ugonjwa wa Ukoma imepungua kutoka wagonjwa 1889 (2015) mpaka wagonjwa 1217 kwa mwaka 2020.
  • Hali ya matibabu ya Kifua Kikuu nchini inazidi kuimarika ambapo tumeongeza uibuaji wa wagonjwa kutoka 62,180 (2015) mpaka 85,597 (2020). Aidha vifo vimepungua kutoka 55,000 (2015) mpaka 26,800 (2020). Hii inatokana na uwepo wa njia zilizoboreshwa za uchunguzi na elimu kwa jamii na Serikali kupeleka huduma za uchunguzi na tiba mpaka kwenye ngazi ya jamii.
Mafanikio haya pia yanajieleza kwa kuongezeka kwa umri wa kuishi wa mtanzania toka miaka 36 mwaka 1961 hadi miaka 66 mwaka 2020 ambayo inaashiria kuimarika kwa mifumo ya utoaji huduma za afya nchini. Hili ni ongezeko la mara mbili kwenye umri wa kuishi mtanzania.



Ndugu Wananchi,
katika kipindi hiki cha baada ya uhuru serikali imejiendeleza na kujiimarisha zaidi katika kukabiliana na magonjwa yanayozuilika (kinga) yakiwemo yanayoambukiza na yasiyoambukiza. Kwa upande wa mgonjwa yanayoambukiza mifumo ya kubaini, kuzuia na kudhibiti imeimarika hadi sehemu za mipakani ambapo sasa tuna vituo 40. Maabara kuu ya taifa imeimarika na ina vifaa vya kisasa na imefungua matawi yake manne katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha.

Kuhusu magonjwa yasiyoambukiza serikali imejielekeza kwenye mkakati mtambuka shirikishi wa sekta zote ili kuimarisha mapambano eneo hili. Hivi sasa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na Ukoma ndiyo imepewa na jukumu la kusimamia magonjwa yasiyoambukiza. Huu ni mtazamo chanya na shirikishi kwenye vita hivi tofauti na awali kabla ya uhuru.



Baadhi ya changamoto.


  • Kuongezeka kwa wimbi la magonjwa mapya yanayoambukiza (Communicable Disease) na yasiyoambukiza (NCD).
  • Uchache wa raslimali kwa ajili ya uendeshaji huduma za afya hususan watumishi, dawa, vifaa Tiba na vipimo.
  • Baadhi ya Wananchi kushindwa kumudu gharama za tiba kutokana na kukosa Bima.
  • Utendaji wa mazoea wa baadhi ya waliopewa fursa ya kuwa watumishi wa umma sekta ya afya jambo linalohitaji maboresho makubwa kwenye mifumo ya motisha na uwajibikaji.


Mwelekeo mpya.


  • Kuwekeza kwenye ubora wa huduma baada ya uwekezaji wa miundombinu (software engineering) sambamba na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji wenye matokeo kwa kupima viashiria vya matokeo (performance merits by scorecards).
  • Kuimarisha Mifumo ya Tehama ili kuweza kuimarisha udhibiti wa raslimali na uwajibikaji pia kuharakisha huduma kwa mteja.
  • Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI)
  • Kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi katika Huduma za tiba na Viwanda vya dawa na vifaa tiba.
  • Kuendelea kupanua huduma za kibingwa na bingwa bobezi sambamba na raslimali watu na hivyo kufungua njia ya medical tourism.
  • Sambamba na kuendelea na maboresho ya afya ya msingi, kujikita kwenye afya kinga dhidi ya magonjwa yanayoepukika kwa kuimarisha ushirikishaji wa jamii katika kumiliki huduma za afya.
  • Kuongeza uwekezaji na Ugunduzi katika Tafiti za Tiba, Chanjo na Tiba Asili.
IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII;

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAFANIKIO YA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA MIAKA 60 YA UHURU WA TANZANIA BARA



Ndugu Wananchi

Kwa upande wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yafuatayo yamefanyika;-

Ndugu Wananchi,
Tangu miaka ya 1960 hadi 1980 Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii walikuwa chachu ya kutekeleza kampeni mbalimbali za kitaifa zinazohitaji ushiriki wa jamii ikiwemo Uhuru na Kazi; Siasa ni Kilimo; Kisomo Chenye Manufaa; Azimio la Arusha; Mtu ni Afya; Elimu kwa Wote; Chanjo ya Watoto wenye Umri Chini ya Miaka Mitano; Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mtoto. Miaka ya 2019-2021 wataalam hawa wanaendelea kuamsha ari ya jamii kuboresha makazi yao kupitia Kampeni ya Ujenzi wa Nyumba Bora ambapo hadi sasa jumla ya nyumba 4,008 zimejengwa.

Ndugu Wananchi, Katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi 2020 Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wamewezesha kaya 617,100 kuboresha vyoo, kaya 305,724 kuboresha maeneo ya kunawa mikono, kujengwa madarasa ya shule za msingi 6,521 na sekondari 2,499, hospitali 67 za Halmashauri na miradi mingine vijijini na mijini.

Aidha, jamii ya sasa ina mwamko wa kujiletea maendeleo kwa kuanzisha miradi inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili mfano ujenzi wa barabara, maboma ya madarasa, zahanati, vituo vya afya. Pia, jamii imeanza utaratibu wa kujitafutia mitaji kwa ajili ya uzalishaji na kujiwekea akiba kupitia vikundi vya VICOBA, Benki za kijamii na SACCOs. Vile vile kuna mwamko mkubwa wa jamii kutumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano kupeana taarifa mbali mbali zikiwemo za masoko

Ndugu Wananchi, Serikali, kupitia wizara hii baada ya Uhuru, imeendelea kuzalisha wataalam wa Maendeleo ya Jamii ambao ni muhimu katika kuchochea mabadiliko na kufanya mageuzi ya kifikra miongoni mwa jamii ili kuwawezesha wananchi kushika hatamu ya maendeleo yao. Katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Serikali imepanua wigo wa kutoa mafunzo ya wataalam wa maendeleo ya jamii ambapo miaka ya 1960 kulikuwa chuo kimoja tu cha Tengeru na leo hii kuna jumla ya vyuo 63 ambapo, kati ya hivyo vya Serikali ni 12 na vya binafsi ni 51. Kati ya vyuo 12 vya Serikali 9 vinasimamiwa na Wizara ambapo mafunzo hayo yanatolewa kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Shahada ya uzamili.

Ndugu Wananchi, Ili kuongeza thamani ya mafunzo yanayotolewa na vyuo vilivyo chini ya Wizara, imeanzishwa programu za uanagenzi zinazomuandaa mhitimu kujiajiri na kuajiriwa, programu za ubunifu zinazotoa fursa kwa wanafunzi na jamii inayozunguka vyuo kufanya kazi za ubunifu unaosaidia kutatua changamoto mbalimbali na ajira. Hadi sasa vimeanzishwa vituo Tisa (9) vya ubunifu wa kidigitali na programu za ushirikishwaji jamii kutatua changamoto zinazowakabili kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka zimeanzishwa.

Ndugu Wananchi, baada ya Uhuru Serikali imejielekeza kwenye kuimarisha Ustawi wa Watoto ambapo, katika miaka ya mwanzo ya 1970 Wizara ilikuwa inaratibu na kusimamia upatikanaji wa haki na ulinzi wa mtoto kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Ili kuimarisha upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi wa mtoto, Serikali imeongeza wigo wa kutekeleza masuala ya watoto kwa kuridhia na kusaini mikataba ya kikanda na kimataifa.

Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (1990). Kupitia mikataba hii Wizara imeendelea kunufaika na usaidizi wa kitaalamu pamoja na rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa masuala yanayohusu upatikaji wa haki na ustawi wa watoto.

Ndugu Wananchi, baada ya Uhuru, Serikali imepanua wigo wa majukwaa ya watoto katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo, katika kipindi cha mwanzo cha Uhuru wa Tanzania Bara, jukwaa pekee la watoto la kujadili masuala yanayowahusu na kufikisha ujumbe ilikuwa ni kupitia shule ikijumuisha majukwaa kama chipukizi. Mfumo huu ulijumuisha watoto wale tu waliopo shule na kuwaacha watoto wasiokuwa shule na hivyo kutokutoa fursa sawa ya kushirikisha watoto wote.

Ndugu Wananchi, Ilipofika mwaka 1991 Tanzania iliridhia na kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki ya Mtoto ambapo moja ya matakwa ya mkataba ni kuanzisha majukwaa ya watoto ili kujadili masuala yanayowahusu ikiwemo upatikanaji wa haki na ulinzi dhidi yao. Jukwaa hili huwajengea watoto uwezo katika nyanja za uongozi na uzalendo, uadilifu, ujasiliamali, stadi za maisha na masuala mtambuka yakiwemo utunzaji wa mazingira, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI

Mnamo Disemba, 2002, Serikali iliratibu uundwaji wa mabaraza ya watoto katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa hadi Taifa. Aidha, Wizara inaratibu uanzishwaji wa Madawati ya ulinzi wa watoto shuleni kwa lengo la kuwashirikisha watoto katika kutoa taarifa za ukatili dhidi yao ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wakosaji. Kupitia madawati haya watoto wanajengewa ujasiri, uwezo wa kujieleza, kujiamini ili kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.

Ndugu Wananchi, Mara baada ya Uhuru, Serikali ilihakikisha uwepo wa Sera, Sheria, Miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto ili kuimarisha mifumo ya kusimamia haki, ulinzi na ustawi wa watoto na kuwakinga dhidi ya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia. Sera ya kwanza ya Maendeleo ya Mtoto iliandaliwa mwaka 1996 na kurejewa 2008 ambayo imeainisha haki tano za msingi kwa watoto; haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki na haki ya kutobaguliwa.

Aidha, Sheria mbalimbali za kumlinda mtoto zilitungwa ikiwa ni pamoja na Sheria ya mtoto Na 21 ya mwaka 2009 inayosimamia upatikaji wa haki za mtoto na kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za ukatili. Hadi sasa, Wizara inaratibu huduma ya simu bila malipo kwa kutumia Na. 116 kwa ajili ya utoaji wa taarifa za matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na ushauri wa namna ya kukabiliana na matukio hayo.

Ndugu Wananchi, Katika kuimarisha huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto, Wizara imeratibu uandaaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (2021/22-2025/26) yenye lengo la kumlea na kumkuza mtoto kwa utimilifu wake. Katika kutimiza azma hiyo, Wizara imenzisha vituo vya kijamii 30 vya mfano ambapo lengo ni kujenga vituo hivyo katika Vijiji/Mtaa yote nchini.

Vilevile, Serikali imesajili jumla ya vituo 2,133 vya kulelea watoto wadogo mchana kwa ajili ya kutoa huduma za malezi na uchangamshi wa awali. Aidha ili kukabiliana na changamoto za afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe Wizara iliratibu uandaaji na inasimamia utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe (2021/22 – 2024/25), lengo likiwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana balehe wenye umri wa 10-19 katika ya maeneo ya VVU/UKIMWI, mimba za utotoni, Ukatili, Lishe bora, Kuendelea kuwa shuleni na kujengewa ujuzi ili kupata fursa za kiuchumi.

Ndugu Wananchi, Katika kuimarisha malezi ya watoto na familia katika mazingira ya sasa, Wizara kwa nyakati tofauti imekuwa ikiratibu upatikanaji wa huduma za malezi kwa watoto. Mnamo 2019, Wizara ilizindua Ajenda ya Kitaifa ya Malezi ya Watoto na Familia ijulikanayo kama “Familia bora, Taifa imara” lengo likiwa ni kuhimiza wazazi/walezi na jamii kwa ujumla katika kutekeleza jukumu lao la msingi la malezi na utoaji wa matunzo kwa watoto na familia ili hatimaye kuwakuza katika maadili mema na uzalendo kwa Taifa lao.

Vilevile, Katika kuimarisha mahusiano katika familia na jamii, Serikali imeendelea kuratibu utoaji wa huduma za unasihi na msaada wa kisaikolojia. Aidha, huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia na msaada wa kisaikolojia zimekuwa zikitolewa kwa njia ya mtandao ili kuweza kuwafikia wananchi wengi wanaokabiliwa na changamoto hizo.

Ndugu Wananchi, Vilevile Serikali imeimarisha huduma za malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi kwa kuhakikisha uwepo wa programu za malezi mbadala kama vile huduma za malezi ya kambo, uasili wa watoto, malezi ya watu wa kuaminika kwa watoto walio nje ya malezi ya kifamilia na wale ambao wanakabiliwa na vitendo vya ukatili katika familia; pamoja na afua za utengemano na marekebisho ya tabia kwa watoto walio katika mkinzano na Sheria na wale wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya makao ya watoto, Serikali inaratibu na kusimamia jumla ya makao ya watoto 239 ikilinganishwa na makao moja yaliyokuwepo mwaka 1960. Kwa upande mwingine, Serikali kwa kushirikiana na shirika la ABBOT FUND imejenga Makao ya Watoto katika Eneo la Kikombo Mkoani Dodoma ambayo yalizinduliwa na Mhe. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 16 Juni 2021. Makao haya yanachukua Watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwemo wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa lengo la kuwapatia huduma za msingi, kurekebisha tabia zao kwa lengo la kuwaunganisha na familia zao.

Ndugu Wananchi, Serikali pia imeweka utaratibu wa Maafisa Ustawi wa Jamii kusimamia upatikanaji wa haki kwa watoto katika mahakama 147 za watoto ambazo zilianzishwa hapa nchini kupitia Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2019. Mahakama hizi zimesaidia kuharakisha upatikanaji wa haki kwa watoto waliokinzana na sheria pamoja na wale waliofanyiwa vitendo vya ukatili na wenye changamoto mbalimbali za malezi na uangalizi. Katika kipindi cha mwaka 2019/20, jumla ya watoto 737 walihudumiwa katika Mahakama za Watoto nchini. Kati yao, watoto 516 waliachiwa huru na watoto 221 walikutwa na hatia.

Ndugu Wananchi, Serikali vilevile, imeendelea kuimarisha huduma za malezi, matunzo na ulinzi kwa Wazee katika makazi ambapo imeboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma za msingi kama vile chakula, mavazi, malazi, matibabu n.k. kwa sasa Serikali inasimamia na kuratibu jumla ya makazi 15 yanayomilikiwa na Serikali yenye jumla ya wazee 277 (Me-166, Ke- 111) na makazi 20 yanayomilikiwa na taasisi binafsi yenye jumla ya wazee 537 (Ke-242,Me-295). Serikali imeimarisha ulinzi na usalama kwa wazee kwa kutekeleza afua mbalimbali ambazo zimesaidia kupunguza vitendo vya ukatili ikwemo mauaji kwa wazee.

Ndugu Wananchi, Ushiriki wa Wazee katika masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo umeimarika baada ya Serikali kuweka utaratibu wa kuwa na Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote, ambayo yameanzishwa kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003. Mabaraza 26 yameundwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na kufanya Mabaraza kufikia 20,748. Mabaraza haya yanatumika katika kusaidia jamii kuimarisha malezi ya vijana pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali kwenye jamii.

Vilevile, wakati wa Uhuru mifumo ya utoaji huduma za afya kwa wazee imeboreshwa ambapo Serikali imekuwa ikifanya utambuzi wa wazee wasiojiweza na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo. Aidha, Serikali imewezesha uundwaji wa timu za uratibu na usimamizi wa huduma katika hospitali na vituo vya afya nchini ili kutoa usaidizi na kuhakikisha wazee wanapata huduma. Timu hizo zinajumuisha wataalam watatu (3) ambao ni Daktari, Muuguzi na Afisa Ustawi wa Jamii. Aidha, Serikali imehamasisha na kuhakikisha kila kituo kinaweka utaratibu wa kuwa na bango linalosomeka ‘Mpishe Mzee Kwanza’ ili kukumbusha na kuhamasisha wajibu wa watoa huduma kujali wateja wa kundi hili pamoja na jamii kuona umuhimu wa kuwapisha wazee ili wapate huduma mapema

Ndugu Wananchi,
Katika kushughulikia Maendeleo ya Wanawake na Jinsia, Serikali imefanya Jitihada za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ndani na nje ya nchi. Wakati Baraza la kwanza la Mawaziri linaundwa mara baada ya uhuru halikuwa na mwanamke hata mmoja. Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri ilikuwa mwaka 1965 ambapo Bi Lucy Selina Lameck Somi aliteuliwa kuwa waziri mdogo wa Shirika na Maendeleo ya Jamii. Tangu kipindi hicho wanawake wameendelea kuaminiwa ambapo kwa sasa idadi ya Mawaziri wanawake imefika saba (7), Wabunge wanawake imeongezeka kutoka wabunge 127 mwaka 2015 hadi kufikia wabunge 145 mwaka 2020.

Ndugu Wananchi, Kutokana na jitihada hizo, kwa mara ya kwanza nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Rais wa Awamu ya Sita ambaye ni mwanamke Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na pia amewahi kushika nyazifa mbalimbali kabla ya kuwa Rais. Wengine ni Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Kwanza mwanamke wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Tulia Akson ambaye ni Naibu Spika wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndugu Wananchi, Kimataifa nchi inajivunia Mheshimiwa Getrude Mongela aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu masuala ya wanawake Duniani uliofanyika mwaka 1995 Jijini Beijing China, Profesa Anna Tibaijuka alikuwa Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UNHABITANT) kuanzia mwaka 2006 hadi 2010; Dkt Asha Rose Migiro amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoka kwaka 2007 hadi 2012 na Dkt Stergomena Lawrance Tax alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya SADC kwa kipindi cha miaka nane kutoka 2013 hadi 2021. Kwa sasa Dkt. Stergomena Tax ni mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa.

Ndugu Wananchi, Katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru imewezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi ikiwemo kuwezesha nyenzo mbalimbali ikijumuisha kutoa mikopo isiyo na riba inayotokana na kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, Dirisha la mikopo kwa wanawake kupitia Benki ya Wanawake na sasa Benki ya Posta, VICOBA, SACCOS, Sekta binafsi, taasisi za fedha na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo huwezesha wanawake kiuchumi.

Serikali pia imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya ukatili wa wanawake na Watoto kwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA (2017/18 2021/22). Jitihada hizi zimewezesha kamati 18,186 mpaka sasa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa. Aidha, yameanzishwa Madawati ya Jinsia na Watoto 420 katika vituo vya Polisi, Madawati ya Jinsia 153 katika Jeshi la Magereza na Dawati katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono kupitia Kampeni ya “Vunja Ukimya.

Ndugu Wananchi, Serikali kupitia Wizara hii ina dhamana ya kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Sekta ya Mashirika yasiyo ya kiserikali haikutambulika katika kipindi cha uhuru kwani taasisi zilizojulikana kipindi hicho ni taasisi za Dini na vyama vya wafanyakazi. Mashirika haya yalianza kuibuka kwa kasi kuanzia miaka ya 1990 baada ya mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi.

Hivyo, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa mashirika haya kwa kutunga Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo ndiyo ilianza kuweka Taratibu za uratibu na usajili wa Mashirika hayo. Aidha, katika kuimarisha utoaji wa huduma za usajili na uratibu Serikali imefanikiwa kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NIS) kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika uratibu wa Mashirika hayo.

Ndugu Wananchi, Mfumo huu umesaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikitumiwa na wadau wa Mashirika kupata huduma mbalimbali kutoka Ofisi ya Msajili na kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu zikiwepo taarifa za fedha na taarifa za utekelezaji za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pia kuongezeka kwa usajili kutoka Mashirika 404 mwaka 2005 hadi kufikia Mashirika 11,731 tarehe 29 Oktoba, 2021. Mashirika hayo yamechangia kuleta maendeleo kwa kutoa huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya, elimu, kilimo, maji, mazingira, haki za binadamu, jinsia, na utawala bora.

Aidha, Serikali imeendelea kujenga na kuimarisha uhusiano kati yake na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuboresha mazingira ya Mashirika hayo kufanya kazi pamoja na kujenga uelewa kwa Mashirika hayo kuhusu masuala ya kodi, uhamiaji na uratibu wa pamoja wa mashirika katika ngazi zote zikiwemo Wizara za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa, Mashirika yenyewe na Sekta Binafsi.

Ndugu Wananchi, Katika kuimarisha uhusiano huo, kwa mara ya kwanza katika historia, Serikali imefanikisha Mkutano wa sekta ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ambao ulihutubiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mafanikio makubwa kwa Sekta hii ambapo Serikali imeonesha dhamira ya kushirikiana nayo na kutambua mchango wao ambapo kwa mwaka 2020 jumla ya trillioni 1.1 zilitumika na mashirika hayo katika Miradi ya maendeleo na ajira za wazawa 6194 zilizalishwa na Mashirika hayo.

Vilevile, Serikali imefanikiwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na.3/2019 pamoja na kutunga kanuni tatu zenye lengo la kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa sheria hiyo. Kuwepo kwa Sheria hii pamoja na kanuni zake imewezesha Mashirika mengi kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu, Mila na Desturi za Nchi na kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa mashirika hayo.

Mwisho niwatakie kila la Heri watanzania wote katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu. “MIAKA 60 YA UHURU; TANZANIA IMARA, KAZI IENDELEE”.

Imetolewa na;

Dkt. Dorothy Gwajima
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii
Jinsia, Wazee na Watoto
08/11/2021
 
Haa aliye soma yote atuwekee summary maana nimefeli
Kwa kweli angekua anatuletea vipande tunajadili lol

Mimi naomba kuwasiliana moja kwa moja na wewe mkuu wa wizara ya afya,nafanyaje mwenye kunisaidia mawasiliano
 
Wizara ya Afya Tanzania watu wenu mnaothibitishaga wamekufa na jamii ikawazika wanarudi huku
Mnaliongeleaje hili? Msije kusema halina ushahidi maana records zao mnazo, wafufuka wapo, wazikaji wapo na makaburi yapo pia

 
Back
Top Bottom