Mafanikio ya Rais Samia kuelekea 2025, Roma locuta, causa finita!

Ngaliwe

Senior Member
Dec 30, 2015
161
364
KATIKA karne ya tano ilitokea sintofahamu katika Kanisa Katoliki Jimbo la Hippo, eneo hilo leo linaitwa Annaba, nchini Algeria, lililokuwa likiongozwa na Mtakatifu Augustine. Mtafaruku huo umeacha alama na funzo kubwa kwa jamii yetu hata leo.

Katika mafundisho ya Kanisa na kwa mtazamo wa Mt. Augustine, ukamilifu wa mwanadamu unapatikana kwa Neema ya Mungu. Lakini wafuasi wa mtazamo wa mtawa wa Kiingereza Pelagius wakiitwa Pelagians wao walikuwa wakiamini kwamba mwanadamu anaweza kuwa mkamilifu wa umahili na uwezo wake tu bila kuhitaji neema ya Mungu.

Ili kuondokana na mkanganyiko huo mabaraza ya Milevi na Carthage yalituma shauri hilo Roma, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, ili kupatiwa ufumbuzi wa mkanganyiko huo. Majibu toka Roma yaliporudi Mtakatifu Augustine aliwaeleza wafuasi wake kwamba baada ya shauri hilo kufika kwa Baba Mtakatifu, limeamuliwa kuwa ukamilifu wa mwanadamu haupatikani isipokuwa kwa Neema ya Mungu tu, kwa hiyo hakuna mjadala tena, suala hilo limekwisha.

Ni katika hukumu hiyo toka Roma ndipo ulipozaliwa msemo maarufu alioutumia Mtakatifu Augustine kwa wafuasi wake kwamba Roma locuta, causa finite est, kwamba Roma imesema, shauri limefungwa (Rome has Spoken, the matter is finished).

Ndani ya CCM huwa kawaida kwa rais na mweyekiti wake kutopingwa anapowania kuongoza kipindi cha pili kukamilisha miaka kumi ya ukomo wa urais wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba. Ndiyo ilivyokuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, uliomweka madarakani aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli na aliyekuwa Makamu wake Samia Suluhu Hassan.

Ni wazi kwamba wapo watu ndani ya chama walishajiandaa kujitokeza kuomba kuwania Urais wa Tanzania kupitia chama hicho ifikapo 2025, lakini katika maisha yetu Mola ndiye mpangaji wa yote. Machi mwaka huu Rais Samia kwa mujibu wa Katiba akawa ndiye Rais wa Tanzania baada ya kifo cha mtangulizi wake, Hayati Rais Magufuli.

Katiba ya nchi inaelekeza kuwa ikitokea Makamu wa Rais anachukua nafasi ya Rais kwa sababu zozote kwa mujibu wa katiba hiyohiyo, ikiwa imebaki miaka minne kabla ya kufikia uchaguzi mkuu unaofuata, atahesabiwa kuwa ameongoza kwa kipindi kimoja, na hivyo kubakiza awamu moja kama atataka kuendelea, ikiwa atashika nafasi ya rais chini ya miaka mitatu, ataruhusiwa kugombea kwa mihula miwili mizima ya miaka mitano mitano. Rais Samia bado anayo nafasi ya kuomba tena kipindi cha pili cha miaka mitano.

Kulizuka taarifa mkanganyiko za watu kuendelea na mikakati ya kuelekea 2025 bila kujali utamaduni kiliojiwekea Chama Cha Mapinduzi kwamba Rais anayekuwa madarakani ikiwa hajakamilisha kipindi chake cha awamu ya pili hapingwi ndani ya chama. Vuguvugu lilishaanza kushika kasi, tetesi na uzushi ukawa mwingi kiasi cha kuanza kuwachanganya wananchi na wananchama wa CCM.

Hatimaye katika madhimisho ya siku ya Demokrasia Rais Samia amevunja ukimya na kuweka bayana kuwa kwa majaaliwa ya Allah, yuko kiringeni 2025. Waliokuwa na mashaka, waliokuwa wanatamani iwe na waliokuwa kinyume chake huu sasa si wakati wa hisia na tetesi, ukweli uko dhahiri shahiri, Rais Samia anagombea mwaka 2025. Na kama ulivyo utamaduni mzuri wa ndani ya CCM inatarajiwa wana CCM wote wamauunge mkono kwa nguvu zote, mjadala nani ni nani sasa umefungwa rasmi, kilichobaki sasa ni namna gani ushindi wa tufani unapatikana ifikapo 2025.
 
Back
Top Bottom