Mafanikio ni nini? Na ipi tafsiri sahihi ya Mtu aliyefanikiwa?

Kanal Hilal

Member
Feb 4, 2017
62
121
Nimewahi kuzungumza maana halisi ya neno MAFANIKIO katika mijadala mbali mbali lakini mada imekuwa likileta mkanganyiko mkubwa sana.

Leo katika pita pita zangu nimekutana na vijana wakibishana kuhusu utajiri wa Diamond Platnumz. Vijana wote walikuwa wakitanabaisha kuwa magari na majumba anayomiliki mwanamuziki huyu ndio taswira halisi ya mafanikio yake. Hii inaweza kuwa ni sahihi kwa Diamond Platnumz kwasababu sote hatujui kile alichojipangia katika maisha yake. Katika ubishani huo hakuna hata mmoja aliyezungumzia juhudi na maarifa na namna mwnamuziki huyu wa bongo flavor anavyojituma katika kuufikisha muziki wa Tanzania katika level ya kimataifa. Pengine haya ndiyo yanaweza kuwa mafanikio tena makubwa sana kuliko nyumba na magari yake.

Unajua, MAFANIKIO yana uwanja mpana sana ambao unatoa fursa ya kila mmoja wetu kucheza katika "style" anayotaka na kuipenda. Tatizo letu tulio wengi aidha tunacheza katika style moja, au tunaiga na kuzipenda style za watu wengine namna wanavyo cheza.

Ukweli ni kwamba tafsiri ya mafanikio sio kama vile wengi wetu tunavyodhani au kuamini. Ni tofauti kabisa. Wengi tunaamini mtu akiwa na gari au magari, nyumba au majumba baaaaasi huyo mtu kamaliza. Eti ndio mtu aliyefanikiwa. Nooo, sio kweli kabisa. Hayati Dkt Reginald Mengi ni tajiri mkubwa sana na mashuhuri. Kila mmoja wetu anaamini kabisa kuwa Dkt Mengi alikuwa mtu mwenye mafanikio makubwa sana.

Ndio ni kweli, lakini je mafanikio yake yalitazama majumba au magari ya kifahari aliyomiliki?. Sidhani kuna mtu hapa anaweza kutaja hata aina moja tu ya gari alilomiliki mfanya biashara huyu kutoka uchagani. Nyumba yake aliyokuwa akiishi na mkewe Jackline Mengi Ntuyabaliwe iko Kinondoni Daressalaam tena bondeni. Ni mara kadhaa Serikali imemwambia aivunje na ahame ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza hasa yakitokea mafuriko maana hiyo nyumba iko kando kando ya mto.

Ni wazi kuwa mafanikio aliyokuwanayo Mzee Mengi hayakuakisiwa na idadi au thamani ya nyumba na magari anayomiliki. Bali ni thamani ya "status" aliyojiwekea kama mfanya biashara mashuhuri afrika na duniani. Na pengine ni kutokana pia na namna alivyokuwa akishiriki katika shida na matatizo ya wengine. Na pengine ni ile pesa anayomiliki katika akaunti yake kama ilivyo kwa Bakhresa, Mo Dewji na wengine.

Iko hivi, MAFANIKIO ni namna unavyotaka katika mtazamo na malengo uliyo jiwekea. Kama utakuwa na ndoto ya kuwa mfanya biashara mkubwa duniani, siku moja ukafanikisha ndoto yako basi hayo ni mafanikio. Ukiwa na mawazo ya kuwa na familia bora, na siku moja wazo hilo likatimia, tambua na hayo pia ni mafanikio. Na kama unaishi ukiamini siku moja atapata kazi itakayo kuingizia kipato. Siku ukipata kazi na ikakuingizia kipato basi hayo pia ni mafanikio. Ilimradi tu umetimiza malengo yako katika kila unacho kipigania. Haijalishi kina thamani kiasi kwa wengine. Kwako kina thamani kubwa sana ndio maana unakipigania.

Majarida yote makubwa duniani huwa yana mtazamo chanya katika kumuweka mtu katika orodha ya watu walio fanikiwa. Hayati Oliver Mtukudzi ni mwanamuziki mkongwe sana lakini alifariki akiwa hana utajiri wowote alioacha duniani. Pamoja na hayo Mr Mtukudzi anachukuliwa kama mwanamuziki aliye FANIKIWA kwa kiasi kikubwa sana kuutangaza muziki wa Afrika duniani.

Iko hivyo kwa Bob Marley na wengine wengi tu. Na hata baba wa taifa hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere mafanikio aliyokuwa nayo katika historia ya maisha yake hayakuwa ya "nyumba na magari" bali yalikuwa ni mafaniko ya kuwaweka watanzania na waafrika pamoja. Mwl Nyerere alifanikiwa sana kusaidia kuikomboa Afrika dhidi ya ukoloni.

Ndugu yangu mpendwa, sikufundishi kuacha kufikiria kujenga majumba au kununua magari. HAPANA. Nakufundisha kutambua thamani ya ulichonacho, au kile ukitakacho bila kutazama wengine wanamiliki nini au wanataka nini. Kamwe usiige mafanikio ya watu wengine. Tambua lengo lako na ulipe thamani hata kama si kile chenye thamani mbele ya macho ya wengine. Ikiwa unapambana katika njia za halali katika kukifanikisha basi hicho ndio kitu muhimu kwako.

Picha: Kwa hisani ya google.

2aa01329c2720449aa91ffc817942729-compressed.jpg
 
Mafanikio ni pale unapotimiza lenngo lako binafsi... liwe dogo au kubwa, ukiweza kulitimiza hapo utakuwa umefanikiwa katika jambo hilo
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom