Maendeleo yetu hayawiani na muda wa Uhuru wetu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
ALHAMISI, Desemba 9, mwaka huu, Watanganyika tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 49 ya uhuru wa nchi yetu Tanganyika ambayo kwa sasa haipo katika ramani ya uso wa dunia.


Zilikuwa sherehe za kukumbuka tukio la kujikomboa kutoka katika makucha ya wakoloni, baada ya wazungu-Waingereza waliokuwa wamepewa nchi yetu waitawale kwa kisingizio cha kutuandaa kujitawala wenyewe, waliporejesha mamlaka ya kiuongozi na kiutawala mikononi mwa wazalendo wa nchi yetu.

Kuondoka kwa wezi hawa wa kizungu, kulitokana na harakati za wazalendo wa nchi yetu kuwapinga na kuwataka kuondoka, ambazo ziliongozwa na mwasisi wa taifa letu, hayati Baba wa taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere na chama chake cha Tanganyika National Unity (TANU).

Kwa hakika siku hiyo ilikuwa ya furaha kwa watanganyika wote, kwa maana ni siku walioisubiri kwa hamu na kwa miaka mingi, ilikuwa ni kama ndoto iliyotimia, maana watu wengi hawakuamini kama harakati za Mwalimu na wenzake zingefanikiwa, waliwaona kama watu wenye kuota ndoto za Alinacha.

Hatahivyo, leo tunapoadhimisha miaka 49 tangu Waingereza hawa waondoke, wananchi wengi hawana la kujivunia, wengi wanaishi maisha ya dhiki kubwa pengine kuliko hata kipindi cha utawala wa wakoloni, wengi wanakandamizwa na kunyimwa haki zao kushinda kipindi cha waingereza, kwa kifupi watanganyika wengi hawaoni maana ya uhuru, ni kama tupo katika utawala wa wakoloni weusi.

Inasikitisha na kuuma mno kuona kuwa katika kipindi cha miaka 49 ya kuwa huru, watanzania wengi hawamudu hata mlo wa siku moja, hawana uhakika wa matibabu wanapougua, huduma za elimu ni mbovu kupindukia, na matatizo mengine mengi yametukaba koo.

Maendeleo tuliyopata ni kidogo sana na hayana uwiano na muda ambao tumekuwa huru, na ni bahati mbaya sana kwamba sasa tumeanza kupiga hatua kurudi nyuma tulikotoka, tunarejea katika ukoloni, ukoloni wenye ubia kati ya wazungu wezi na weusi wenzetu vibaka waliovalia majoho yenye maandishi ya "wanasiasa", dhidi ya wananchi walio wengi-maskini au walalahoi.

Baada ya miaka 24 ya uongozi wa awamu ya kwanza wa hayati Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere, ambayo bila shaka ulikuwa wa matumaini kwa watanganyika, kipindi ambacho wananchi walio wengi tuliona dhahiri tofauti za utawala wa kikoloni na ule wa wazalendo, kutokana na kuwepo mabadiliko makubwa katika kila nyanja ya maisha yetu ya kila siku, kiuchumi na kijamii, kipindi cha miaka 25 iliyofuata kimekuwa cha kusikitisha na kukatisha tamaa, kwani nchi imeshindwa kusonga mbele na badala yake sasa tunarejea katika enzi za kutawaliwa na wageni, sasa tupo chini ya ukoloni wa watu weusi, waswahili wenzetu wanaoshirikiana na wageni.

Uongozi wa Baba wa taifa ulifanikiwa kuongeza na kuboresha huduma mbali mbali za kijamii kwa watanganyika wote, kama vile elimu, afya, maji, makazi bora, miundombinu, nk. Huduma za elimu, afya, na maji zilipatikana bure kwa watanganyika wote.

Huduma za afya ziliongezeka na zilikuwa bora, kila mwananchi alikuwa na uhakika wa kupata matibabu ya bure anapougua. Madawa yalipatikana kwa urahisi katika hospitali na zahanati zetu, na hapakuwa na tatizo la kulazimishwa kuhonga madaktari na manesi ili kupata huduma za afya kama ilivyo leo.

Serikali ilifanikiwa kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na zingine tuliuza nje na kujipatia fedha za kigeni. Mpango huu ulituwezesha kupunguza gharama za kuagiza bidhaa kutoka nje, na hivyo kusaidia kukua kwa uchumi wa taifa na kuongeza nafasi za kazi kwa watanganyika wengi.

Kilimo kiliwekewa mkazo wa hali ya juu, ambapo serikali ililenga kuongeza uwezo wa kuuza mazao nje ya nchi na kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula kwa wananchi wake. Matokeo yake, miaka ya 1970, tulifanikiwa kuwa nchi inayoongoza Afrika kwa kuuza mazao nchi za nje na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi yetu.

Wakati wa uongozi wa Mwalimu, serikali haikutegemea michango ya mataifa ya nje katika bajeti yake, tulijitegemea kwa asilimia 100 na kuweza kuheshimika duniani kama taifa huru kweli. Waliotupatia msaada wa fedha au mali, walifanya hivyo kwa mapenzi yao, hatukuwapigia magoti na kuwalilia kama tunavyofanya leo.

Rasilimali zetu tulizilinda kwa uaminifu mkubwa, hatukuruhusu wazungu wezi waliojipamba jina zuri la "wawekezaji", kutulaghai na kutupora madini yetu, mbuga zetu za wanyama, misitu yetu, viwanda na mashirika yetu ya umma kwa mgongo wa ubinafsishaji.

Kwa ujumla enzi za utawala wa Mwalimu, nchi yetu ilidhihirisha kwa ulimwengu kuwa ilikuwa huru kweli, hakuna aliyetuchezea au kutudharau, na sherehe za kumbukumbu ya uhuru zilikuwa za maana kweli na wananchi wengi walijitokeza na kusherehekea wakitembea vifua mbele na mabega juu, walikuwa na haki ya kufanya hivyo, waliwekwa huru kweli.

Lakini mambo yalianza kwenda mrama kuanzia mwaka 1985, wakati Mwalimu alipong'atuka uongozi na kumwachia rais mstaafu mzee Alli Hassan Mwinyi, aliyeongoza taifa letu kwa kipindi cha miaka kumi (1985-1995). Wakati huo ndipo misingi ya uhuru wetu ilipoanza kuvunjwa, na imeendelea kuvunjwa na marais wengine waliomrithi mzee Mwinyi, yaani rais mstaafu Benjamin Mkapa (1995-2005) na rais wa sasa Jakaya Kikwete aliyeingia madarakani mwaka 2005.

Kwa sasa huduma za jamii hususan elimu na afya zimedorora mno, mashule ya serikali yamebaki majengo tu, walimu hawatoshi, vitendea kazi kwa walimu havitoshi na zana za kujifunzia vya wanafunzi havikidhi mahitaji halisi, madawati hayatoshi na hivyo watoto wengi wanakaa chini wakati wakisoma, na michango na ada sasa ni kero na vikwazo kwa watoto wengi kupata elimu. Kwa sasa shule za serikali zimekuwa kama biashara, ada na michango inaanzia shule za msingi mpaka chuo kikuu.

Ubaguzi katika elimu sasa ni rasmi, kwani kuna shule za matajiri na zile za watoto wa maskini, shule za matajiri zina huduma zote muhimu na ni za kisasa, wakati zile za walalahoi ziko hoi bin taaban. Watoto wengi wa maskini sasa hawaendi shule na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, ambapo sasa inakadiriwa kuwa watanganyika karibu asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika.

Mahospitali na zahanati za serikali sasa si mahali pa kuokoa maisha ya watu bali ni mahali pa kufia, kwani hakuna dawa na huduma zingine muhimu za matibabu, watumishi wa afya hawana ari ya kufanya kazi kwani hawalipwi vizuri, imefikia hatua wagonjwa wanakufa mikononi mwa manesi na madaktari kwa kukosa huduma!

Uchumi wetu tumeukabidhi mikononi mwa wageni, ni wageni sasa wanaomiliki vilivyokuwa viwanda na mashirika yetu ya umma baada ya kuwauzia kwa bei ya kutupwa, wazalendo sasa ni watu wa kutumwa tu, wengi wao ni vibarua, yale yale ya wakati wa ukoloni yamerejea, kwa hakika tumerejea katika ukoloni.

Rasilimali zetu kama vile madini, mbuga za wanyama, misitu, mazao ya bahari na maziwa sasa vinadhibitiwa na wageni wezi, baada ya kuuziwa kwa bei chee na viongozi wetu vibaka, sasa wananchi wengi ni wapagazi katika migodi ya dhahabu, katika meli za uvuvi na viwanda vya samaki vya wageni.

Serikali yetu sasa ni tegemezi, bajeti ya serikali inategemea misaada na mikopo kutoka kwa wakoloni wa zamani kwa asilimia 35, na hili limesababisha manyanyaso na kuingiliwa kwa uhuru wetu kwa kupangiwa mambo ya kufanya na hawa wakoloni wanaojiita "wafadhili".

Kila kukicha viongozi wetu wanapiga mguu kwenda Ulaya na Marekani kuwapigia magoti watawala wa huko kuwabembeleza watupatie misaada na mikopo, huku wanatukanwa na kusimangwa, lakini hawakomi, wamekubali aibu na udhalili.

Siku hizi viongozi wetu wanasikia fahari kusifiwa na hawa wakoloni wezi, kwamba wanaongoza vizuri na wameleta maendeleo makubwa kwa nchi zao, wakati sifa hizo hazina ukweli wowote, wanavikwa vilemba vya ukoka ili waendelee kuruhusu rasilimali za nchi yetu kuporwa.

Huu ni ukoloni kwa tafsiri yoyote ile, tunatawaliwa kifikra na kivitendo, tumewasaliti wazee wetu waliohangaika miaka mingi kupigania uhuru wa taifa letu na hata wengine kupoteza maisha yao.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom