SoC01 Maendeleo ni jambo ambalo sio la kuja kwa pupa, ila ni mchakato laini ambao jamii zote hufuata kwa usawa

Stories of Change - 2021 Competition

Jmwacha0076

New Member
Sep 8, 2021
1
1
MAENDELEO KATIKA TAIFA LA TANZANIA

Katika mtazamo wa kawaida, maendeleo ni hali ya kuwa na mabadiliko chanya kukoka hatua moja hadi nyingine katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Hali ya maendeleo katika taifa hupimwa kwa kuangalia mambo mbalimbali kama vile uwepo wa amani, gharama za maisha, utawala bora, usalama wa raia, upatikanaji wa chakula pamoja na kiwango bora cha elimu na ajira kwa wananchi.

Aliyewahi kuwa mshauri wa usalama wa taifa la marekani Wolt Whitman Rostow aliwahi kusema kuwa ‘’maendeleo ni jambo ambalo sio la kuja kwa pupa, ila ni mchakato laini ambao jamii zote hufuata kwa usawa’’.

Hivi karibuni maendeleo ya taifa la Tanzania yameongezeka kidogo ukilinganisha na kipindi cha nyuma, hali hii inadhihirishwa kupitia ongezeko la pato la taifa kwa robo ya mwaka wa fedha 2020 kutoka mwezi Januari hadi mwezi Machi kutoka shilingi ya fedha za kitanzania trilioni 36.4 mpaka trilioni 38 kwa robo ya mwaka wa fedha 2021, taarifa hii ni kutoka kwenye ofisi ya taifa ya takwimu ‘‘National Bureau of Statistics (NBS)’’ Hivyobasi, ili kuzidi kuchochea maendeleo, taifa letu litahitaji kufanya yafuatayo;

Uchumi na biashara, ni mojawapo ya sekta ambayo huchangia kwa kiasi fulani katika maendeleo ya taifa, kwani ni kupitia kodi na tozo mbalimbali taifa hujipatia mapato ambayo hutumika katika kukidhi matakwa ya bajeti ya taifa. Maendeleo katika nyanja hii yanaweza kuchochewa zaidi kwa kutunga na kuboresha sera ambazo zitaendana na mfumo na uhalisia wa hali ya sasa kwa taifa letu, mfano uwepo wa utoaji wa elimu na mafunzo ya kibiashara na ujasiriamali hasa kwa vitendo katika taasisi za elimu ili kuweza kuwaanda vijana kuwa katika nafasi na hali ya kuweza kuanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji ingali bado wapo katika vyuo na hata baada ya kumaliza.

Jambo lingine ni uwepo wa punguzo katika tozo na makato kwani litapelekea ongezeko la uwekezaji wa miradi mbalimbali, kwani ni bora kukusanya mapato kidogo kidogo kwa watu wengi kuliko kukusanya kiasi kikubwa kwa watu wachache.

Maendeleo katika jamii yoyote na suala la afya ni mambo mawili ambayo huambatana kwa pamoja, ili jamii iweze kupata maendeleo inahitaji watu wenye afya iliyo njema na salama. Katika taifa la Tanzania yapo baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kufanyika katika sekta hii ya afya, mfano wa mambo haya ni kuongeza kasi ya utoaji wa elimu juu ya namna mbalimbali za kuweza kujikinga na magonjwa kama vile homa, malaria na utapia mlo, licha ya kukazania kujenga vituo vingi vya afya ili kutatua matatizo ya kiafya na wakati chanzo chake bado kipo pale pale kama vile matumizi ya pombe, madawa ya kulevya na kutokuzingatia lishe bora.

Mfano mwingine, pawepo na utoaji wa elimu juu ya afya ya uzazi ili kupunguza tatizo la mimba zisizotarajiwa, jambo ambalo limekuwa likiwasumbua watu wengi hasa wale wanaoishi vijijini, tatu ni kuhimiza kufanya mazoezi ili kujikinga na maradhi madogo madogo ambayo yalikuwa siyo yenye ulazima wa kutumia dawa au kwenda hospitalini, na badala yake vituo vya afya viwepo kwa ajili ya wale wenye matatizo makubwa na yenye uhitaji wa utabibu kama vile makundi yenye uhitaji maalumu (walemavu), seli ya mundu na wenye magonjwa ya kurithi.

Kilimo ni sekta nyingine ambayo inachangia sana katika maendeleo ya taifa, kwani kutokana na taarifa kutoka shirika la chakula na kilimo ‘’Food and Agriculture Organization (FAO)’’ kilimo kimechangia kwa takribani asilimia 26.7 ya pato la taifa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na vilevile kutoa ajira kwa asilimia takribani 41.49 ya watanzania katika mwaka 2020.

Upatikanaji wa masoko yenye utayari ni jambo ambalo wakulima wanapaswa kuhakikishiwa ili kuwa na moyo katika kazi zao, uboreshwaji wa maendeleo ya sekta ya kilimo yataweza kufikiwa kwa kuhakikisha kuwa wakulima wanapatiwa ruzuku zao ndani ya muda muafaka, uwepo wa miundombinu mizuri kama barabara na maghala ya kuhifadhi mazao, vilevile uwepo wa ukaguzi na udhibiti wa viwatilifu hatarishi na vilivyokwisha muda wake wa matumizi na ufanisi ili kuwafanya wakulima kupata mazao yaliyo safi na salama zaidi.

Jambo lingine ni kuhimiza na kuwapa watu elimu ili kuwawezesha kuanzisha kilimo katika maeneo madogo madogo, jambo ambalo halihitaji gharama kubwa za uanzilishi na uendeshaji.

Sayansi na teknolojia ni mojawapo ya sekta muhimu sana katika kuchochea maendeleo ya jamii yoyote, kwani sayansi na teknolojia ndio huja na njia mpya zenye maboresho ambayo hupelekea na kuchochea maendeleo ya taifa. Katika taifa la Tanzania kuna mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kufanyika kwa ufasaha ili kuikuza teknolojia ya nchi yetu, baadhi ya mambo hayo ni kama vile kuongeza idadi ya wawekezaji wenye nia kutoka nchi za nje ili waweze kuja na teknolojia ambazo ni za hali ya juu zaidi ukilinganisha na zilizopo nchini kwa sasa, vilevile suala la kuwainua wabunifu wazawa kutoka nchini kutapelekea maendeleo ya kasi katika taifa kwani waswahili husema kuwa ‘’jambo jema siku zote huanzia nyumbani’’.

Ongezeko la uanzishwaji wa mashindano mbalimbali kama vile Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi na Ubunifu (MAKISATU) kutapelekea kuwapa vijana nafasi mbalimbali za kuendeleza fumbuzi na gunduzi zao.

Maendeleo katika taifa au jami yoyote huambatana na uwepo wa utimizwaji wa haki za kibinadamu kwa wananchi wote pasipo kujali dini, kabila, rangi wala jinsia, kwani ni kupitia utoaji sawa wa haki za binadamu kutapelekea wanajamii kupata huduma na nafasi mbalimbali kama vile elimu ambayo itawafanya kuwa katika nafasi ya kujikomboa na umasikini, haki ya umiliki wa mali kama vile ardhi na nyumba hasa kwa wanawake itawapa nafasi ya wao kuweza kujishughulisha na shughuli mbalimbali za uwekezaji kama vile kilimo na biashara, jambo ambalo litapelekea zaidi kasi ya ukuaji na maendeleo ya taifa.

Suala la demokrasia, utawala bora pamoja na uwajibikaji wa viongozi na wananchi ni jambo ambalo lisilo la kuepukika kwaajili ya maendeleo ya taifa, kupitia uwepo wa demokrasia ya kweli, katiba mpya na ya haki tutaweza kupata viongozi ambao wako tayari katika kulitumikia na kuliongoza taifa letu kwa haki na amani, vilevile demokrasia ndiyo chimbuko la amani, upendo na mshikamano katika jamii yeyote.

Hivyo basi, kwa kuhitimisha, ushirikiano wa jamii katika kuleta maendeleo unaangaliwa kwa kina zaidi katika matukio kama vile ulipaji wa kodi stahiki ili kuchangia pato la taifa, matumizi na utunzaji wa mazingira, ushiriki katika matukio ya kijamii na utunzaji wa miundombinu ambayo ipo katika mazingira yetu. Hivyo basi suala la maendeleo ya taifa ni jambo ambalo kila mwananchi anapaswa kushiriki katika kutekeleza mipango na matarajio ya taifa na sio kuwaachia serikali na taasisi zinginezo.
 
Back
Top Bottom