Maelfu Ya Watu Kuwa Wasikivu Asilimia 100 ktk Mikutano Ya CHADEMA Inaashiria Nini? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Maelfu Ya Watu Kuwa Wasikivu Asilimia 100 ktk Mikutano Ya CHADEMA Inaashiria Nini?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by bagamoyo, Oct 8, 2010.

 1. b

  bagamoyo JF-Expert Member

  #1
  Oct 8, 2010
  Joined: Jan 14, 2010
  Messages: 4,531
  Likes Received: 2,113
  Trophy Points: 280
  Nimeona wasichotaka kukiona!

  Na Godfrey Dilunga wa Gazeti Raiamwema 06/Oktoba/2010

  NIMEHUDHURIA mikutano ya kampeni za awamu ya pili za mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa. Kwa nguvu za kampuni ya gazeti hili la Raia Mwema, nimefika katika mikutano ya Ifakara mjini, Lupiro-Mahenge, Songea Mjini, Njombe-Mjini, na Iringa Mjini.

  Ni baadhi ya mikutano tu. Kwa kuzingatia mikutano hiyo, nitajadili umuhimu wa nilichokiona ambacho kwa wengine hakionekani au hawataki kukiona na zaidi, hawataki kutoa tafsiri ya kimantiki.

  Tangu kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2010, vyombo vya habari vimekuwa vikizungumzia wingi au uchache wa watu katika mikutano ya wagombea husika.

  Ni kawaida kwa mwandishi wa habari gazetini kuandika mkutano ulihudhuriwa na maelfu au mamia ya wananchi.

  Ni kawaida sasa kwa mwandishi wa habari wa televisheni kuonyesha picha za wingi wa watu waliohudhuria. Kwa kadri ya mwenendo wa kampeni, waandishi wamekuwa wakilenga mambo matatu makubwa.

  Kwanza ni ujumbe wa mgombea husika kwa watu wanaomsikiliza. Pili, wingi wa watu. Tatu ikibidi vituko au mbwembwe zilizojiri eneo la mkutano.

  Ni kweli, yote haya yamekuwa yakijitokeza kwenye mikutano husika. Ni muhimu kuripotiwa.

  Binafsi, kwenye mikutano hiyo ya Dk. Slaa, sikushangazwa na wingi wa watu au ujumbe wa mgombea huyo kwa wananchi. Ni mambo yaliyoanza kujitokeza tangu kuanza kwa kampeni zake.

  Nilichoshuhudia, pengine ambacho kinaonekana lakini watu hawataki kukiona, ni utulivu na usikivu wa wahudhuriaji kwenye mikutano ya maeneo niliyotaja hapo awali.

  Kwa mtu makini, utulivu na usikivu wa asilimia 100 kwa watu zaidi ya 40,000 tena waliokusanyika pamoja kwa hiari yao, ni suala la kushitua.

  Katika mikutano hiyo, nimeshuhudia umati mkubwa watu ukiwa katika utulivu na usikivu wa asilimia 100. Ni utulivu na usikivu ninaoweza kuita chemchemu ya fikra mpya kwa viongozi au watawala.

  Nizungumzie mkutano mmoja kati ya mingi niliyopita. Huu ni mkutano wa Ifakara mjini. Nikiwa mkutanoni Ifakara mjini nilimwona mama muuza ndizi mbivu alizozipanga kwenye sinia.

  Kwa wakati huo, mkutano ulikuwa ukiendelea, Dk. Slaa anazungumza.

  Kwa kuwa utulivu na usikivu uwanjani pale ulikuwa kwa asilimia 100, huku sauti ya mtu mmoja tu ikisikika (Dk. Slaa), nilimsogelea yule mama, ambaye macho yake yalijielekeza kwa Slaa na sio sinia lake la ndizi alilokuwa ‘amelibwaga’ chini.

  Nilipomsogelea, nikainama kukwanyua ndizi mbivu ili nile kama mnunuzi wake. Hapa, kipaumbele changu hakikuwa ndizi bali kupima utulivu na usikivu wake kwa mtu anayemsikiliza. Je, anaguswa na anachosikia?

  Je, amefika uwanjani hapo kwa sababu kipaumbele chake ni kuuza ndizi? Na je, kama kipaumbele chake awali kilikuwa kuuza ndizi, kipaumbele hicho kimetekwa na hoja za Dk. Slaa?

  Je, kipaumbele cha mama huyu muuza ndizi mbivu kimegeuka kutoka uuzaji ndizi eneo la mkutano hadi kusikiliza hoja za Dk. Slaa? Kwa nini haya yamtokee mama huyu? Haya ni sehemu ya maswali niliyotaka kuyajibu kichwani mwangu.

  Nilipokwanyua ndizi ile ya kwanza, alinitazama na kisha kuendelea kumtazama na kumsikiliza mzungumzaji (Dk. Slaa). Nahisi aliniamini kwamba ni mteja nitakayemlipa bila matatizo.

  Nilikula ndizi nne bila yule mama kunitazama (macho na masikio yake yakitekwa na Dk. Slaa). Bado uwanja ni tulivu na usikivu wa maelfu ya watu ni mkubwa, ukiniondoa mimi ambaye bila shaka nimepunguza kiwango kutoka asilimia 100.

  Nilichukua ndizi nyingine. Nikamuuliza hivi unajua nimekula ndizi ngapi? Akajibu, wewe kula nitahesabu maganda; huku akiendelea kumsikiliza Dk. Slaa. Alijinijibu kwa haraka, nadhani alinichukulia kama mtu msumbufu na si mteja anayemtafuta juani kila kukicha.

  Hatua yake hiyo ilinifanya niwekeze zaidi fikra zangu kwake na kiasi fulani nihusishe na ujumbe wa Dk. Slaa kwa wakati huo.

  Kama ilivyo kawaida, masikio ya mwanahabari na macho yake hulazimika kufanya kazi ya ziada. Wakati nikila ndizi niligawa fikra zangu, nilikuwa nikisikiliza anachosema Dk. Slaa.

  Kwa hiyo fikra zangu zilibanwa na matukio matatu kwa wakati mmoja. Kwanza, kuwasiliana kifikra ‘kimya kimya’ na huyu mama kwa kuzingatia utulivu na usikivu wake uliomfanya apuuze biashara yake kwa muda.

  Pili, kuunganisha mawasiliano hayo ya kifikra na ujumbe wa Dk. Slaa ili nipate tafsiri sahihi kwa kutazama mwenendo wa nchi, siasa na mchakato wa kidemokrasia.

  Tatu, kwa kuzingatia ujumla wa mazingira hayo, nini nafasi ya watawala walioko madarakani? Je, ni kweli kuna mkatiko wa mawasiliano kati ya watawala na walalahoi mfano wa huyu mama?

  Naam, mkutano unaendelea. Sasa Dk. Slaa anazungumzia hoja mbili. Kwanza alikuwa akifafanua atapata wapi fedha za kufidia uamuzi wake wa kuondoa kodi kwenye vifaa vya ujenzi.

  Uamuzi unaotajwa kulenga kumwezesha mwananchi mwenye uwezo wa kati au wa chini ajenge; tofauti na hali ilivyo sasa.

  Lakini pia Dk. Slaa alikuwa akifafanua atapata wapi fedha za kugharimia elimu ya awali hadi chuo kikuu ili kumwondolea mzigo mzazi wa mwanafunzi au wanafunzi.

  Masuala haya mawili niliyaunganisha na utulivu ulioshiba na usikivu wa yule mama muuzaji ndizi. Ni mama wa makamu anayeonekana kuwa na familia. Tena ni familia yenye wanafunzi.

  Kuna mambo kadhaa niliyabaini kutoka kwa mama yule. Kwanza , licha ya kufanya biashara anaamini biashara husika haikidhi mahitaji lakini hana mbadala.

  Katika mazingira hayo, ni dhahiri mbadala pekee anaohitaji yule mama ni kuchagua kiongozi bora. Kiongozi atakayelinda maslahi yake, familia yake, jirani zake, wana-Ifaraka wenzake, wakazi wenzake wa Morogoro na Watanzania wenzake nchini.

  Nguvu ya usikivu na utulivu kutoka kwa mama yule na maelfu ya wakazi wengine uwanjani pale ilinielekeza niibue tafsiri mpya.

  Tafsiri hiyo ilizingatia masuala ya msingi, ikiwa ni pamoja na ukweli kuwa, wananchi walifika eneo la mkutano kwa utashi binafsi na si kwa ushawishi wa lifti au kingine chochote.

  Na kubwa zaidi, hata waliofika kwa ajili ya kufanya biashara ndogo ndogo walisahau biashara zao. Kwa kuzingatia mazingira haya, tafsiri niliyoipata ni kwamba viongozi walioko madarakani hawako salama hata kama watashinda uchaguzi kwa haki au mizengwe!

  Haina maana kwamba hawako salama kwa maana ya uhai wao, la hasha. Hawako salama kwa kuzingatia mfumo wao wa kiuongozi. Mfumo wa uongozi unaomtenga mama yule na wenzake kutia mkono ili naye anufaike na raslimali za Tanzania.

  Mfumo wa uongozi unaotanguliza kujuana katika mgawanyo wa raslimali na kulindana katika makosa ya ufisadi wa mali za umma. Hakika, kama mfumo huo hautavunjwa baada ya uchaguzi mkuu, mama yule na wenzake wakaendelea kusahaulika, viongozi hawatabaki salama. Siku zao zitaanza kuhesabika.

  Nguvu ya utulivu na usikivu ya mkusanyiko wa watu zaidi ya 40,000 niliyoshuhudia Ifakara ndiyo iliyojitokeza Lupiro-Mahenge, Njombe, Songea na Iringa.

  Kwa heshima zote, nawasilisha ujumbe kwa watawala kwamba; utulivu na usikivu ule wa hoja ni shinikizo kwenu kubadilika; kinyume chake siku zetu zitaanza kuhesabika.

  Ukweli ni kwamba, yeyote atakayeshinda Uchaguzi Mkuu 2010 na kuingia Ikulu, awe Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA, Jakaya Kikwete wa CCM au Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, usikivu na utulivu ule katika mkusanyiko wa maelfu ya walalahoi ni changamoto mpya kwao.

  Kama leo mkusanyiko wa walalahoi zaidi ya 40,000 katika kila mkutano wanakua watulivu, ipo siku utulivu na usikivu ule utafanyiwa kazi na walalahoi hao hao. Siku hiyo itafika kama watawala watazidi kujenga wananchi wa mfano wa mama muuza ndizi.

  Siku hiyo ikifika, watoto wa mama muuza ndizi na watoto wa majirani zake na wengine nchi nzima wataungana kutaka kujiondoa kwenye lindi la umasikini kwa kutumia nguvu na akili zao kwa taratibu zao. Atakayeshinda asiruhusu hilo.

  Hii ni changamoto inayoshinikiza kufumuliwa kwa mfumo wa uongozi wa kulindana katika ufisadi, kuenzi urafiki katika kugawana madaraka. Ni changamoto inayohitaji kufumua mfumo wa chama kwanza, Taifa baadaye.
  Sidhani kama yule mama ni mwana-CCM lakini nina hakina ni Mtanzania.

  Kuendeleza kauli za chama kwanza mtu baadaye, ni kuzidi kuwatenga katika ufalme watu mfano wa yule mama anayeshinda juani kusaka tonge.
  Nihitimishe kwa kumnukuu mwanzilishi wa taasisi ya kudhibiti uzito kwa watu (Weight Watchers Organization), Jean Nidetch, aliyewahi kusema: “It's choice -not chance - that determines your destiny.” Kwamba ni uamuzi na si fursa inayoangaza hatima yako.

  Kazi kwako. Nikipata nauli nitahudhuria mikutano ya wagombea wengine na nitakueleza nitakachoona bila wao kuona.

  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

  Source: Nimeona wasichotaka kukiona!
  [​IMG]
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Oct 8, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,345
  Likes Received: 418,852
  Trophy Points: 280  Hakuna mapana yasiyokuwa na ncha na ncha za CCM ni Dr. Slaa na Chademaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa
   
 3. TIMING

  TIMING JF-Expert Member

  #3
  Oct 8, 2010
  Joined: Apr 12, 2008
  Messages: 21,837
  Likes Received: 125
  Trophy Points: 160
  hii thread mbona imekua duplicate??

  si ziunganishwe tu?
   
 4. PakaJimmy

  PakaJimmy JF-Expert Member

  #4
  Oct 8, 2010
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 16,236
  Likes Received: 309
  Trophy Points: 180
  wANAFUNZI wa vyuo vikuu, tafuteni nauli mkapige kura mlikojiandikisha!...Oneni watu wanavyohangaika kwenda kutafuta mihadhara ya Dr Slaa!
   
 5. Mwanamayu

  Mwanamayu JF-Expert Member

  #5
  Oct 8, 2010
  Joined: May 7, 2010
  Messages: 7,944
  Likes Received: 2,091
  Trophy Points: 280
  because their minds see the light at the end of the tunnel now!!
   
Loading...