Maduro: Tumemkamata Jasusi wa Marekani

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Nicols Maduro.jpg

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amesema kuwa wamemkamata jasusi wa Marekani aliyekuwa akipeleleza kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi nchini humo.

Maduro aliutangazia umma wa Wavenezuela kupitia televisheni ya taifa katika matangazo ya moja kwa moja akimweleza jasusi huyo kuwa ni mwanajeshi wa Marekani aliyekuwa kaihudumu katika kambi ya Shirika la Upelelezi la Marekani (CIA) nchini Iraq. Amesema kuwa jasusi huyo alikamatwa katika jimbo la Falcon lililopo Kaskazini Magharibi mwa taifa hilo, akipeleleza viwanda vya kuchakata mafuta ghafi vya Amuay na Cardon.

"Amekamatwa akiwa na vifaa vya kisasa, fedha nyingi - dola nyingi na vitu vingine," alisema Maduro. Hata hivyo hakutoa taarifa zaidi akibainisha kuwa kwa sasa jasusi huyo yupo kizuizini akiendelea kufanyiwa mahojiano.

Marekani bado haijatoa taarifa yoyote kumhusu jasusi huyo. Mwezi mmoja uliopita, mahakama nchini Venezuela iliwahukumu kifungo cha miaka 20 gerezani wanajeshi wawili wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Marekani (Green Beret) waliohusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini humo.

Licha ya Marekani kukana kuhusika na jaribio hilo mwezi Mei, Marekani inamuunga mkono kiongozi wa upinzani, Juan Guaido anayetaka kumpindua Maduro.

Maduro amesema pia kuwa wametibua njama ya kulipua kiwanda kingine cha kuchakata mafuta cha El Palito katika jimbo la Carabobo siku ya Jumatano, akiwatahadharisha wafanyakazi katika viwanda vyote vya mafuta kuchukua tahadhari dhidi ya mashambulio mengine yaliyopangwa.

Venezuela, taifa lenye utajiri mkubwa zaidi wa mafuta Amerika, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta na hali mbaya ya uchumi, wengi wakimlaumu Rais Maduro kwa uongozi mbaya uliopelekea kuporomoka kwa uchumi wa taifa hilo. Vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela vinaathiri pakubwa sekta ya mafuta ambayo ndiyo kiungo muhimu zaidi kwa uchumi taifa hilo.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom