Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,470
- 911,173
Madiwani waliofukuzwa wamvaa Mkurugenzi Arusha | Send to a friend |
Thursday, 06 October 2011 21:12 |
Peter Saramba, Arusha MADIWANI watano waliofukuzwa uanachama katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamedai kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha,Estomih Changa, alikurupuka kutangaza kutowatambua kwa maelezo kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo bila kibali au maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa). Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, John Bayo aliyekuwa diwani wa Kata ya Elerai na Reuben Ngowi, aliyekuwa diwani wa Themi, walisema kitendo cha mtendaji huyo kutowaalika katika kikao cha kujitambulisha kwa viongozi na watendaji wa Wilaya na Manispaa ya Arusha, kilichoitishwa na mkuu mpya wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, kilikuwa ni cha kuwadhalilisha kwa sababu wao bado ni wawakilishi halali wa wananchi katika kata zao. Baada ya Chadema kutangaza kutufukuza uanachama na sisi kupinga mahakamani, waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa aliwaagiza meya na mkurugenzi, kuendelea kututambua na kuturuhusu kuhudhuria vikao vyote vya manispaa. Hakuna maagizo mengine hadi sasa na kama yapo tuna haki ya kuelezwa badala ya kuanza kubaguliwa kwenye shughuli za umma tunazoamini kuwa tuna haki nazo kuhudhuria, alisema Bayo. Alisema baada ya agizo la Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika la kutaka wao kuruhusiwa kuhudhuria katika vikao na kulipwa posho, Kaimu mkurugenzi hajapokea maelekezo mengi na kwamba kwa kutenda cha kutowaruhusu kuingia katika kikao cha kujitambulisha, ameonyesha utovu wa nidhamu kwa mamlaka yake ya ajira ambayo ni wizara. Alisema wakati mtendaji huyo akiwabagua kwa kutowaalika na hata kufuta majina yao kwenye orodha ya madiwani waliostahili kulipwa posho, siyo wao wala manispaa iliyokuwa imepokea nakala ya hukumu ya mahakama iliyotupilia mbali madai ya kuomba kurejeshewa uanachama wao. Kwa upande wake, Ngowi alisema baada ya kesi yao kutupwa, Hakimu Mkazi, Hawa Mguruta, aliwapa siku 30 za kukata rufaa na kwa msingi huo, haikuwa sahihi kwa Changa kuanza kutowatambua kabla siku hizo hazijamalizika na waziri kutoa maelekezo. Hali kadhalika kuitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi,kuhusu nafasi zao kuwa wazi ili kuruhusu uchaguzi mdogo kwenye katazao. Nakala ya hukumu ya kesi yetu tumeipokea mchana Septemba 28 na kwa taarifa tulizopata kutoka manispaa, hata wao waliipokea siku hiyo hiyo. Sasa mamlaka ya kutotutambua Kaimu mkurugenzi anayatoa wapi kama hakuwa na nakala ya hukumu wala maelekezo mapya kutoka kwa waziri, alisema na kuhoji Ngowi. Ngowi na Bayo ambao walisema wanazungumza kwa niaba ya wenzao Estomih Mallah, Charles Mpanda na Rehema Mohamed, walimtaka mkurugenzi huyo kuwajulisha kutowatambua kwa maandishi kama alivyofanya alipopokea barua ya waziri Mkuchika badala ya kufuta majina yao kwenye orodha ya wajumbe wa vikao. Hat hivyo Changa hakuwa tayari kuzungumzia madaia ya waliokuwa madiwani hao kwamba hana mamlaka ya kutangaza kutowatambua wala kuwazuia kuhudhuria vikao vya Baraza la madiwani. Kaimu Mkurugenzi huyo amekuwa kwenye mazingira magumu tangu kuanza kwa mgogoro wa umeya katika Manispaa ya Arusha ambapo awali alidaiwa kuvuruga uchaguzi na baadaye alituhumiwa kuwabeba madiwani waliofukuzwa na sasa amegeukwa na aliodaiwa kuwapendelea. |