Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,395
Naomba kujenga hoja kwamba ili tuweze kujenga uhalali wa kudai demokrasia ni muhimu sisi wenyewe tuoneshe mfano wa kuwa wanademokrasia kweli. Ninatumia dhana kwamba, mara zote, utawala wa nchi ni sura halisi ya utamaduni wa wananchi wake. Kwamba viongozi/watawala wa nchi hubeba tabia/ na hulka za jamii wanazoziongoza.
Haiwezekani kutarajia watawala wawe tofauti na wananchi wanaowaongoza kwa sababu utawala wa nchi huzaliwa na wananchi. Ndio maana, kwa mfano, wananchi wanaothamini elimu, hutafuta na kuchagua miongoni mwao viongozi wanaothamini elimu kama wao. Kinyume chake, wananchi wasiothamini elimu (wajinga) huweza, na kwa kweli hufurahia, kuchagua wajinga wenzao kuwa watawala wao. Kadhalika, wananchi wanaopenda njia za mkato kujipatia kipato, huthamini wenzao wajanja wenye kujua kutafuta fedha kirahisi na hatima yake wananchi hawa hujichagulia viongozi wanaokuja baadae kufahamika kama mafisadi. Ndio kusema viongozi hawawezi kuwa tofauti na wananchi.
Tukizitazama nchi zinazosifika kwa demokrasia tunabaini kuwa demokrasia katika nchi hizo ni utamaduni wa wananchi. Demokrasia ni maisha/mila inayoanza kwenye utawala wa familia. Kila mwanafamilia kwa kiasi kikubwa anajengewa mazingira ya kujisikia kuwa na uhuru wa maoni. Mtoto hupewa nafasi ya kufanya maamuzi kwa mwongozo wa mzazi. Mke hupewa fursa ya kushiriki katika maamuzi anayoyafanya mumewe kwa sababu demokrasia katika jamii hizo ni utamaduni unaoanzia kwenye familia na sio matamanio hewa ya kisiasa.
Ninapofikiria madai yetu haya ya kutaka watawala wetu wawe wana-demokrasia, maswali kadhaa yanajitokeza. Ninajiuliza, kwa mfano, tunaweza kweli kudai kuwa sisi ni jamii inayoamini katika demokrasia kuanzia ngazi ya familia? Je, demokrasia ni utamaduni wetu?
Je, sisi wanaume wa ki-Afrika hatutishwi na kukua kwa demokrasia kwenye ngazi ya familia zetu? Tunawashirikisha kweli wake zetu katika maamuzi bila kuwawekea mipaka? Tunaheshimu maoni ya watoto wetu kama tunavyotaka watawala wetu waheshimu maoni yetu? Ni lini kwa mfano wazazi hukaa na watoto wao kujadili bajeti ya familia?
Wanaume ili tuweze kujenga taifa linaloamini uhuru wa mawazo kweli kweli, tuanze kujenga demokrasia ya kweli ndani ya familia zetu
Tuanze kuwashirikisha wake zetu katika maamuzi bila kuogopa kuonekana 'tumeshikiliwa'. Tuanze kuthamini na kuheshimu maoni/mahitaji ya Watoto wetu na kuyasikiliza