SoC01 Madhara yanayotokana na msongo wa mawazo (sonona). Je, tunajali?

Stories of Change - 2021 Competition
Jan 22, 2020
5
1
Kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio ya watu kuchukua maamuzi magumu ya kujitoa uhai. Vilevile kumekua na ongezeko la watu kuishi mtindo wa maisha usiofaa ambao huweza kuleta madhara kwenye maisha yao na jamii inayowazunguka, mfano tabia ya ukahaba, matumizi ya pombe kupindukia au madawa ya kulevya na vilevi vingine. Hali hii kwa sehemu kubwa inasababishwa na msongo wa mawazo ambao umekosa tiba. Mtu huamua kujitoa uhai au kuishi mtindo wa maisha usiofaa kama njia ya kuondokana na msongo wa mawazo.

Kwa mtazamo wangu ninaamini kabisa madhara ya msongo wa mawazo yanaweza kupunguzwa au kumalizwa kabisa katika jamii yetu. Kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu nimewahi kumsaidia mtu ambaye alikua kwenye hali ya msongo wa mawazo na kukata tamaa kabisa na hatimaye akafanikiwa kuvuka katika tatizo lililokuwa linamkabili. Nitaeleza kwa ufupi nilivyomsaidia mtu huyo katika sehemu ya mbele ya makala hii.

Msongo wa mawazo (sonona) ni nini? Msongo wa mawazo ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, taabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku. Mtu hupata msongo wa mawazo (sonona) baada ya akili kuwaza sana na kukosa utatuzi au majibu ya tatizo au hali inayomkabili. Hali ya kukosa utatuzi au majibu ya tatizo humfanya mtu kuwaza zaidi, jambo ambalo huongeza tatizo zaidi kwani kisaikolojia unavyowaza zaidi ndio unasababisha tatizo kuwa kubwa zaidi na kutengeneza tatizo ambalo halikuwepo mwanzoni. Kuna msemo wa kiingereza unaosema “Overthinking is an art of creating problems which were not existing”, ikiwa na maana kwamba kufikiria sana kuhusu jambo fulani (overthinking) kunaweza kumfanya mtu kutengeneza matatizo mengine ambayo hakua nayo kwa sababu kunaongeza ukubwa tatizo.

Hali hii husababisha mtu kuwa mpweke na kuwa na huzuni (depression) na kuhisi dunia imemtenga. Hii ndio sababu watu wenye msongo wa mawazo hupendelea kujitenga na kukaa peke yao tu. Mtu akishafikia hatua hii huwa ni ngumu sana kujinasua kwenye tatizo bila kupata msaada. Ni ngumu sana kwa sababu ni ngumu sana akili iliyoko kwenye tatizo kukutoa kwenye tatizo hilohilo. Kuna msemo wa kiingereza unaosema “You cannot solve the problem with the same level of thinking/mindset that created the problem”, ikiwa na maana kwamba huwezi tatua tatizo kwa kutumia akili ileile iliyoko kwenye tatizo. Hivyo bila kupata msaada, akili hufika mwisho kabisa wa kufikiri na kuchoka kabisa, hali ambayo hupelekea mtu kutamani kupumzika na mateso anayoyapata baada ya kuwa katika hali ya msongo wa mawazo kwa muda mrefu.

Katika kipindi hiki mtu huwa katika hali ya kukata tamaa kabisa na kuona hakuna chochote cha maana katika maisha yake, hata uhai wake mwenyewe. Hivyo hufikia uamuzi mgumu wa kujitoa uhai ili apumzike, au kutumia vilevi kama pombe na madawa ya kulevya kama namna ya kumfanya asahau matatizo yanayomkabili, au pia kuishi mtindo wa maisha usiofaa kwa sababu ya hali ya kukata tamaa. Kwa ujumla kisaikolojia ni ngumu sana kushinda dhidi yako wewe mwenyewe, ndio maana asilimia kubwa ya watu wanaokuwa kwenye msongo wa mawazo bila kupata msaada huishia kuchukua uamuzi mgumu wa kujitoa uhai. Hii ni kwa sababu wanakosa mawazo mbadala ya kuwatia moyo na kuwabadilisha mtazamo kwamba wanavyofikiria sivyo ilivyo.

Kuna siku moja mchana mwaka 2016 nikiwa bado mwanafunzi wa chuo, nilikua nimekaa nje karibu na bweni la wanafunzi. Muda huo nlikua nina maongezi kwa njia ya simu. Pembeni yangu umbali wa mita kumi alikua amesimama kijana wa kiume, sikujali sana hivyo niliendelea na mazungumzo kwenye simu. Nilipomaliza tu maongezi yule kijana alikuja na kuniangukia miguuni huku analia machozi. Nikamuinua na kumsihi asilie aniambie ana shida gani. Kichwani nilikuwa nafikiri labda ana shida ya kifedha, alivyoanza kunielezea nikagundua sio hivyo. Kwa ufupi alikuwa ana changamoto ya kimapenzi ambayo ilikua inamkabili na hakua na njia ya kujinasua hivyo alikua amekata tamaa kabisa. Kwa ufupi tu mpenzi wake ambaye alikua ni mwanafunzi mwenzake, alikua anaonyesha kutokumjali tena licha ya yeye kujitoa sana kwake.

Kwa kutumia uelewa wangu mkubwa wa saikolojia na mahusiano kwa ujumla nilimshauri yule kijana, na hatimaye nilifanikiwa kumnasua kwenye tatizo ambalo kabla ya kukutana na mimi lilionekana kwazo kubwa kwake, na pengine kama sio kukutana na mimi pengine angeweza kuchukua uamuzi ambao ungeleta madhara makubwa kwenye maisha yake bila ulazima. Baada ya muda kidogo kupita, siku moja nilikutana na yule kijana maeneo ya palepale chuoni, sikumkumbuka ila yeye alinikumbuka na kunishukuru sana na kuniambia anaendelea vizuri sana baada ya kuyafanyia kazi yale niliyomshauri.

Kuna jambo kubwa sana la kujifunza kutokana na hadithi ya huyu kijana. Huyu kijana alipata bahati ya kupata mtu wa kumueleza matatizo yanayomsibu, na hatimaye akapata msaada. Kama nilivyoeleza awali kwamba ni ngumu sana kujinasua katika msongo wa mawazo bila msaada, ni vema unapopitia changamoto yoyote ambayo umekosa majibu, ukatafuta msaada haraka sana kabla hali haijawa mbaya kwa sababu utakavyoendelea kukaa na tatizo na kuliwaza sana, kisaikolojia utaongeza ukubwa wa tatizo na kupelekea kufanya uamuzi ambao unaweza kuwa na madhara kwenye maisha yako.

Msaada unaweza kuwa mtu wako wa karibu, ndugu, rafiki au mtu yoyote ambaye utakua huru kumueleza. Hii itakusaidia sana kwa sababu utakavyoeleza tatizo kisaikolojia itakusaidia kuondoa upweke na kutua mzigo kwa kiasi fulani, hivyo kukupa ahueni. Lakini pia kueleza tatizo kutakusaidia pia kupata mawazo mbadala ambayo yatakinzana na vile unavyofikiri. Hii ndio njia ambayo wanaisaikolojia huitumia kumtibu mtu mwenye msongo wa mawazo. Lakini pia kuelezea tatizo kunaweza kukusaidia ikiwa yule unayemueleza pengine ana uelewa mkubwa kuhusu tatizo linalokukabili. Pia kama alishawahi kupitia changamoto kama hiyo anaweza akakushauri njia za kujinasua kwenye changamoto inayokukabili. Kwa ujumla njia pekee ya kuepukana na msongo wa mawazo ni kuepukana na msongo wa mawazo wenyewe, kwa kutafuta msaada wa haraka sana unapokutana na changamoto ambayo umekosa utatuzi wake.

Kama jamii tuna mchango katika kuepukana na madhara yatokanayo na msongo wa mawazo, kwanza kwa kukubali kwamba tatizo hili lipo na lina madhara kama kupoteza nguvu kazi ya taifa kupitia vifo au mitindo ya maisha ambayo humfanya mtu kutochangia katika ujenzi wa taifa. Kama jamii tunatakiwa kutafuta msaada haraka sana pale tunapokutana na tatizo ambalo limekosa ufumbuzi.

Lakini pia wazazi tuwafundishe na kuwajenga kisaikolojia watoto na vijana wetu kuwa changamoto kama kuachwa au kusalitiwa na mpenzi, kufeli mitihani, magonjwa yasiyotibika na changamoto zingine zozote katika maisha ni sehemu ya maisha na inaweza kumtokea mtu yoyote. Hivyo wanapokutana na changamoto hizo wasione kuwa dunia imewatenga na mwisho wa maisha umefika, au kwamba wana upungufu fulani. Kuwajenga watoto na vijana kisaikolojia kuanzia wakiwa wadogo itatujengea jamii ambayo ina nguvu kisaikolojia na hivyo kuweza kupambana na changamoto mbalimbali za maisha.

Hii itasaidia sana kwa sababu changamoto kwenye maisha ni kitu ambacho hakikwepeki, ila namna unavyopambana na changamoto ndio itaamua matokeo. Pia tuwafundishe kuwa wepesi kusema matatizo yanayowakabili na kwamba kupambana na tatizo peke yako hakuonyeshi kwamba una nguvu au uwezo mkubwa sana.

Kwa kuhitimisha ningependa kutoa wito kwa serikali kulichukulia kwa uzito tatizo hili kama yalivyo matatizo makubwa mengine yanayotukabili. Na pia kuchukua hatua za makusudi dhidi ya tatizo hili, kwani linasababisha madhara ambayo yanaweza kuepukika. Kuna jitihada ambazo zimechukuliwa dhidi ya tatizo hili lakini hazijazaa matunda kwa sababu kwanza jamii yetu ina uelewa mdogo sana juu ya hili tatizo na bado serikali na jamii haijaona kama ni tatizo kubwa na kulipa ukubwa unaostahili.

Serikali inaweza kuanzisha mitaala mashuleni kuhusu elimu ya saikolojia na afya ya akili, hii itasaidia watoto wetu kukua wakiwa na uelewa mkubwa kuhusiana na saikolojia na afya ya akili hivyo kutengeneza jamii yenye nguvu kisaikolojia na kupunguza au kuondoa kabisa madhara yatokanayo na matokeo ya msongo wa mawazo. Lakini pia serikali inaweza kuanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya kuijengea jamii ufahamu na uelewa juu ya tatizo hili na namna ya kukabiliana nalo. Hii itasaidia sana kwa sababu ni ukweli ulio wazi kwamba jamii yetu ama haina uelewa kabisa au ina uelewa mdogo sana kuhusiana na tatizo la msongo wa mawazo na madhara yake.

Serikali pia inaweza kuanzisha vituo maalumu kwa ajili ya kusaidia watu ambao wanakutana na changamoto za msongo wa mawazo. Hii itasaidia watu kupata msaada wa haraka sana kabla msongo wa mawazo haujawaletea madhara. Katika maisha ya kila siku wapo watu wanaokutana na changamoto za msongo wa mawazo kila siku lakini hawajui wapi pa kwenda kupata msaada hivyo wanakaa na msongo wa mawazo mpaka unawaletea madhara katika maisha yao.

Madhara yatokanayo na msongo wa mawazo katikati ya jamii yetu yanaweza kupungua au kuisha kabisa kama tutaamua kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hili. Hii itasaidia kuzuia madhara yanayotokana na msongo wa mawazo ikiwemo maamuzi ya kujitoa uhai, mitindo ya maisha isiyofaa kama ukahaba, uvutaji wa madawa ya kulevya na matumizi ya pombe kupitiliza na vilevi vingine. Madhara haya kwa ujumla yanapoteza nguvu kazi ya taifa, taifa ni watu ambao ndio nguvu kazi ya kuendeleza taifa,bila watu hamna taifa. Pia ningependa ifahamike kwamba ubongo wa mwanadamu ni kiungo muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu. Lakini kisipotumika vizuri kinaweza kumletea mtu shida kubwa sana, ikiwa na maana kwamba kutegemea na mawazo unayowaza ubongo wako mwenyewe unaweza kukuingiza kwenye tatizo kubwa sana na ukashindwa kujinasua.

Ifuatayo ni picha kutoka mtandao wa google inayoonyesha jinsi ambayo ubongo wako mwenyewe unaweza kukuletea shida hata ya kuamua kujitoa uhai kutokana na unavyowaza.
1632385746986.jpeg



 
Back
Top Bottom