Madereva wenye makosa zaidi ya 15 kunyang’anywa leseni badala ya viboko

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,658
55,484
DCMa53DXoAILCv-.jpg

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limesema litanyang’anya leseni za udereva madereva watakaokutwa na makosa ya usalama barabarani zaidi ya kumi na tano waliyofanya kwa nyakati tofauti, badala ya kuwachapa viboko kama ilivyoagizwa na viongozi wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani hivi karibuni.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari, leo Juni 13, 2017 jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Fortunatus Muslimu amesema kupiga bakora madereva wanaofanya makosa ni kinyume na sheria, na kwamba baraza hilo liliagiza askari kutoa adhabu kali ifananayo na kuchapwa viboko.

“Kupiga viboko ni kinyume cha sheria, ila sheria zitakazotumika sasa ni sawa na kupiga viboko. Tutaanza kufungia leseni kwa mfumo wa nukta, na kila dereva anapofanya makosa tunamuhesabia alama ambazo tutaziweka katika leseni yake, akifikisha alama 15 tunamfungia leseni,” amesema.

Sambamba na adhabu hiyo, amesema Jeshi la Polisi halitasita kuwafikisha mahakamani madereva wasiofuata sheria na kanuni za usalama barabarani, wazembe na wale wanaotembea kasi zaidi ya kilomita 90 kwa saa.

“Sasa uzembe wa madereva hautafumbiwa macho, tutachukua hatua kali dhidi yao. Lengo letu ni kuwafanya madereva kuwa na utii bila shuruti, kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu na kuharibu miundombinu ya nchi,” amesema.

Na Regina Mkonde
 
Kwa hiyo ile kauli ya viboko yule aliyoitoa ALIKURUPUKA...? Nalipongeza jeshi la polisi kwa hatua hiyo nzuri
 
Back
Top Bottom