Madaktari mmezidi kudharauliwa,Msiposimama pamoja, mtaangamia mmoja mmoja | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Madaktari mmezidi kudharauliwa,Msiposimama pamoja, mtaangamia mmoja mmoja

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Vancomycin, Jan 16, 2012.

 1. V

  Vancomycin Senior Member

  #1
  Jan 16, 2012
  Joined: Jan 7, 2011
  Messages: 171
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0  TUKIO la hivi karibuni la Serikali kuamua kuwafukuza madaktari wanafunzi waliokuwa wanadai mafao yao mbalimbali na nyongeza za mafao hayo, linahitaji kulaaniwa na kuoneshwa kuwa ni la kibabe. Madaktari wa Tanzania yawezekana ndio madaktari wanaofanya kazi katika mazingira mabovu zaidi wakitarajiwa kuhudumia maisha ya wananchi huku wanasiasa wa nchini wakiishi maisha ya juu zaidi, wakijiaminisha kuwa wanastahili zaidi! Tujadili suala hili katika maeneo mahsusi kama ifuatavyo.

  Tiba nchini India

  Mojawapo ya vitu ambavyo vinaonesha dharau na kukosekana kwa heshima ya hadhi ya madaktari wetu ni hili la kupeleka wagonjwa India, kwa matibabu ambayo yangeweza kufanyika hapa nchini. Niliandika juu ya hili miezi michache iliyopita lakini yafaa nirudie.

  Ningependa kujua kama viongozi serikalini wamewahi kukaa chini na kujiuliza swali jepesi (wengine wanaweza kuliita la kizushi) la ni kwa nini tunapeleka wagonjwa India na siyo kutibiwa hapa hapa nchini?

  Jibu la swali hili lina pande mbili – upande wa kwanza wapo wanaodai kuwa gharama ya kutibiwa India ni nafuu zaidi kuliko nchini. Sijui kama kuna ukweli wa hili na ni nani aliyewahi kufanya utafiti wa kupima hili.

  Ni kweli gharama ya nauli ya ndege kwenda na kurudi, chakula na malazi na mapumziko huko India ni ndogo kuliko kutibiwa hapa nchini?

  Binafsi sitaki sana kuamini hili kwa sababu gharama inasababishwa na vitu mbalimbali, je, Serikali yetu imeshindwa kabisa kufikiria namna ya kufanya gharama ya afya kuwa nafuu hapa nchini? Na ni kitu gani kinafanya gharama iwe juu Tanzania ambacho hakiwezi kuangaliwa na kushughulikiwa?

  Upande wa pili ni lile linalodaiwa ni ubora wa madaktari wa India. Wapo ambao wanaamini kuwa India ina madaktari wenye ujuzi mkubwa kuliko madaktari wetu. Watu wengi hawajui kuwa daktari wa Tanzania ili awe daktari kamili, anasomea kwa miaka saba wakati yule wa India anasomea miaka 5!

  Madaktari wa Marekani nao wanasomea miaka saba! Na nchi nyingine zina tofauti ya kati ya miaka mitano hadi saba, huku hadi kuwa Bingwa inakuwa ni miaka karibu tisa ya mafunzo. Sasa ubora wa madaktari wa India unatokana na nini ambacho Tanzania haiwezi kukifanya?

  Binafsi ningependa sana kuona chombo huru au taasisi huru kama walivyofanya watu wa taasisi za HakiElimu au Tunaweza, kwenye masuala ya elimu kupitia na kufanya ulinganifu wa madaktari wetu kulinganisha na India.

  Nadharia yangu ni kuwa karibu vitu vyote vinavyofanywa India vinaweza kabisa kufanywa Tanzania. Watu wanapenda kwenda India kwa sababu zaidi ni hisia ya kuwa wanaenda “nje” kutibiwa.

  Lakini nyuma ya hili ninaamini kuna hisia kuwa madaktari wa Tanzania hawaaminiki. Kuwa hawana uwezo – japo wanaweza kuwa wamesoma vizuri na hata kuzidi wale wa India na vile vile kuwa kutokana na maslahi yao duni hujikuta wakiendekeza taasisi zao binafsi zaidi kuliko kufanya kazi kwa weledi katika taasisi za ajira zao.

  Hili la mwisho laweza kuwa na ukweli zaidi kwani wapo watu ambao wamewahi kujikuta wanaambiwa waende hospitali ya dokta kwa uangalizi zaidi. Lakini kwenye nchi ambayo maslahi ya daktari ni duni sana, daktari huyo afanye nini zaidi ya kujipatia kipato chake cha ziada pembeni?

  Namfahamu Daktari mmoja (sasa Marehemu) ambaye alisomeshwa na fedha za Watanzania lakini baada ya kujitahidi kujitolea sana kufanya kazi ya udaktari aliona kuwa hailipi na matokeo yake alianzisha biashara yake ya baa na maduka na hadi anafariki, alikuwa ni Daktari wa cheo tu akikataa kabisa kurudi hospitali kutoa huduma. Wapo madaktari ambao udaktari ni sehemu tu ya kazi zao lakini wanapotengeneza fedha zaidi ni kwenye miradi yao mbalimbali.

  Kutoboresha maslahi yao ni kejeli kwa utu wetu

  Ndugu zangu, ni kweli walimu ni muhimu (sitaki kuingia mjadala wa ‘nani bora kati ya daktari na mwalimu’) lakini katika kujenga taifa la kisasa na lenye watu wenye afya bora hakuna nafasi ya pekee kama ya madaktari.

  Ni wao ndio wanatupa nafasi ya kuishi na kutumikia taifa tukiwa na afya bora zaidi. Ni watu ambao kutokana na ujuzi wa kazi zao na vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu hujikuta wakiokoa maisha yetu (iwe katika ajali, magonjwa au dharura fulani).

  Ni watu muhimu sana kiasi kwamba katika Wagiriki na Wayahudi wa kale uponyaji ulikuwa ni sifa ya kimungu. Waebrania walimuita Mungu Yehova Rapha (yaani Bwana Anayeponya) wakati Wagiriki walikuwa na mungu aitwaye Askelpias ambaye alikuwa ni mungu wa tiba na uponyaji. Kati ya mabinti zake mmoja aliitwa Hygeia (tunapata neno la Kiingereza Hygiene – usafi) na Panacea yaani “tiba ya magonjwa yote”. Ile fimbo yenye nyoka hujulikana kama fimbo ya Asklepias. Hivyo basi, madaktari si watu wa kudharauliwa au kufanywa duni.

  Serikali inawaafanya madaktari wetu duni

  Sizungumzii suala la kufukuzwa kwa hawa madaktari wanafunzi tu, nazungumzia jinsi tunavyowaangalia madaktari na kuwatendea. Ni kweli hatuwezi kuwalipa sana lakini ukweli ni kuwa kutokana na idadi yao, madaktari wanastahili kulipwa zaidi kwa ajili ya kuwavutia zaidi lakini vile vile kuwafanya wafanye kazi yao ambayo ni wito wao kwa kweli.

  Unajua watu wengi hatuna wito wa kukaa na kufumua miili ya wanadamu, kuona uchafu wao na madamu yao na kuwapo pale kuwasaidia kurudi kwenye uzima au kuwasaidia wanapoelekea mauti. Ni wito wa ajabu sana ambao tusipoonekana kuuelewa tutaona kama “ajira nyingine tu”.

  Daktari wa Tanzania anayeingia kwenye ajira tu asingelipwa chini ya mshahara wa kama dola 5,000 hivi kwa mwezi pamoja na mafao mengine. Ni lazima tumtoe huyu daktari kutoka kwenye miradi yake ya nyumbani na vibarua na kumhakikishia usalama wa maisha yake.

  Hatuwezi kuwa na madaktari ambao ili wawahi hospitali kutoa huduma inabidi wadandie daladala au kununua gari mkweche. Haiwezekani leo tunajenga majumba ya wanasiasa lakini hatujawa na programu ya uhakika ya kuwajengea madaktari wetu nyumba za kudumu.

  Hivi katika miradi yote ya Jiji la Dar es Salaam ni wapi wana mpango wa kujenga nyumba za makazi kwa madaktari? Huko mikoani ni wapi ambapo wana miradi ya kujenga nyumba za madaktari karibu na hospitali au kwenye maeneo ya kisasa ambayo yatawapa nafasi ya kupumzika na kutulia na kujifunza kabla hawajarudi kukimbia kuokoa maisha ya wananchi wetu?

  Hivi watu wamewahi kujiuliza kuwa Tanzania ina madaktari wangapi? Katika Tanzania yetu hii ambayo watu wanaamini ina neema tuna daktari mmoja kwa kila watu kama 30,000 hivi. Marekani ina dokta mmoja karibu kwa kila watu 400 hivi. Sasa kweli tunaweza hata kufikiria kusimamisha madaktari wanafunzi zaidi ya 200 kwa sababu za kipuuzi – kwamba wamedai kuboreshewa maslahi yao? Kweli? Ni taifa gani ambalo tunajenga?

  Yaani, wanasiasa wanaweza kujiongezea posho bila kuhojiwa na yeyote tena kwa asilimia zaidi ya 300, lakini hawa madaktari wetu hata ‘kiduchu’ wanachodai imekuwa ni nongwa? Hivi, kuna mwanasiasa wa CCM anayeweza kusimama na kutuambia akiwa na macho makavu kuwa madaktari wa Tanzania wanalipwa vizuri na mazingira yao ni bora?

  Huyu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa CCM) aliyedai kuwa wamejiongezea posho kwa sababu maisha ni magumu Dodoma alikuwa hafikirii kuwa huko Dodoma nako kuna madokta? Nani atawapigania madaktari wetu?

  Naomba nitoe taarifa mbaya - madaktari wa Tanzania hawatopiganiwa na wanasiasa wetu! Wanajidanganya wale madaktari waliokaa Wizara ya Afya na ambao wanaishi maisha ya furaha kwa sababu wanakula na wakubwa! Hawa madaktari waliotupwa porini huko Katavi, Bukoba, Mbeya na sehemu nyingine waishi kwa kuombea kudura (kudra) tu! Hawana mtetezi. Na bahati mbaya sana hata vyama vyao haviwezi kuwatetea.

  Kuna wakati, madaktari lazima wasimamie maslahi yao kwani kwa kufanya hivyo watasimamia maslahi ya wagonjwa wao na wale watumishi wa afya wa kada nyingine. Na kuna namna moja tu ambayo italazimisha watawala wetu kuangalia maslahi ya madaktari na kuwarudisha mara moja wale wanafunzi na kuhakikisha kuwa madaktari wa Tanzania wanapewa heshima na hadhi wanayostahili – mgomo.

  Mimi si shabiki wa migomo ya aina hii lakini tulipofika sasa inaonekana hoja hazitoshi kuwashawishi watawala kufikiri. Mgomo siyo wa kukataa tu bali pia wa kudai kile kinachowezekana.

  Kama taifa linaweza kutenga posho ya karibu bilioni 28 kwa watu 350 hivi na wakahalalisha inawezekana, nina uhakika taifa hilo hilo lina uwezo wa kutenga kiasi kikubwa tu cha fedha kuboresha mishahara na posho za madaktari karibu 2,000 tu ambao tunao!

  Mgomo ni njia pekee na sahihi ya kutuma ujumbe wa kisiasa ambao umeshindikana kupokewa kwa njia za kidemokrasia na mazungumzo. Mazungumzo yamefanywa miaka nenda rudi lakini bado watawala wetu wanaona kama wanasumbuliwa na ‘madai’ ya madaktari.

  Nasema madaktari hamna cha kupoteza isipokuwa utu wenu na hadhi yenu kama waponyaji. Mtaendelea kudharauliwa, kunyanyasika na kudhulumiwa huku na ninyi mkitamani muwe wanasiasa!

  Si mmewaona madaktari wenzenu walivyoingia siasa wanavyonona. Hamna mtetezi wala wa kuwapigania isipokuwa ninyi wenyewe! Tangazeni mgomo na simameni pamoja mtasikilizwa. Msiposimama pamoja, mtaangamia mmoja mmoja!
  [/h]
   
 2. V

  Vancomycin Senior Member

  #2
  Jan 16, 2012
  Joined: Jan 7, 2011
  Messages: 171
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa raia mwema Rula wa Nzila
   
 3. N

  Ndinani JF-Expert Member

  #3
  Jan 16, 2012
  Joined: Aug 29, 2010
  Messages: 5,413
  Likes Received: 734
  Trophy Points: 280
  Ingawa kweli madaktari wetu wana madai yao ya haki ambayo serikali ni lazima iyashuhulikie, hata hivyo sio sahihi kumshutumu katibu mkuu wa wizara ya Afya kwa ucheleweshaji wa malipo stahiki kwani wizara ya Afya kama zilivyo wizara nyingine zinategemea mgao wa fedha kutoka Hazina, na pale hazina yetu inapokauka hakuna jinsi katibu mkuu wa wizara anaweza kufanya malipo kwa watumishi wa serikali!! Hapa sio suala la uzembe wa Katibu mkuu bali ni suala la serikali yetu kutokuwa makini juu ya kubalance mapato ya nchi na jinsi mapato hayo yanavyo tumika na pia vipaumbele vya serikali yetu. Serikali yetu inaona ni bora kutumia mabillioni ya fedha kwa sherehe kuliko luwalipa madaktari mishahara yao!! Sasa na kama hivyo ndivyo priorities za serikali ndio zilivyo, there is nothing that a permanent secretary can do to change those priorities even if she wanted To!!
   
 4. f

  frontline1 Member

  #4
  Jan 16, 2012
  Joined: Dec 4, 2011
  Messages: 53
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  ndugu yangu tunakushukuru sana kwa ushauri wako mahiri, madaktari wa taifa hili wako hoi katika kila nyanja!

  idadi
  madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali wanahesabika kwa vidole vya mikono na miguu unakuwa umemaliza idadi yao
  madaktari wa kawaida nao idadi yao ni ndogo sana kuilinganisha na mahitaji

  mazingira ya kazi
  kwa ujumla kuanzia makazi, usafiri, mawasiliano, vitendea kazi, mishahara, posho vyote kwa madaktari ni mambo ya aibu tupu
  katika muongozo wa serikali kwa watumishi wa umma wameainisha nyumba anayopaswa kuishi daktari nk lakini kwa hakika ni wachache mmno wanaoweza kukuonyesha makazi yao kwakuwa yamechoka sana hata house alowance hawapewi na wakipewa ni aibu tupu!

  wanasiasa wanajua kwa hakika madaktari tulionao ni wazuri na wana uwezo mkubwa wakiutendaji ila wanajua yakuwa hakuna vitendea kazi kwa mfano mashine zakutoa dawa za usingizi za kisasa, monitors, vyumba vya wagonjwa walizidiwa, dawa zakutosha, vyumba vya private, . hili wanalijua kwakuwa maombi ya vitu vyote hivi yamewakilishwa mezani mwao kwa utekelezaji lakini kwa kiburi chao hawajavinunua tofauti na kule india umeme wa uhakika upo na vitendea kazi vyote vipo.

  mafunzo ya madaktari wetu
  kuanzia miaka ya 2000 kushuka chini mafunzo yalikuwa murua kabisa kwa kuwa medical schools ilikuwa moja tu (muhimbili) wakufunzi walikuwa wakutosha na vnyenzo za kufundishia ziliilingana na idadi ya wanafunzi.

  kuanzia mwaka 2000 mpaka leo kumekuwa na siasa ndani ya sayansi, kama ilivyo mafuta na maji vitu hivi kamwe havichanganyikani.
  kukekuwa na shinikizo kubwa toka kwa wanasiasa kuongeza udahili wa wanafunzi wa udaktari sambamba na kuongezeka kwa vyuo vingi vya udaktari vingine vikiwa na sifa stahili na vingi vikikosa sifa. kwa kuwa hakuna tena swala la ubora bali wingi ndiyo hoja vyuo vyote vimeendelea kidahili idadi kubwa ya madaktari bila kujali wito wao, uwezo wao kielimu, matarajio yao nk.
  matokeo yake tuna wengi bora madaktari na madaktari bora wachache sana!

  wakufunzi wamelemewa na idadi ya watahiniwa kwa ujira ule ule na zaidi heshima na na marupurupu vimetoweka kabisa, madaktari wenzao walioko wizarani wamewasaliti nakuamua kujiunga na wanasiasa! inatisha kwa kuwa makufunzi wamepunguza nguvu yakufundisha na hari imewatoka matokeo yake wanatunga mitihani itakayo rahisisha kazi yakusahihisha na wakati huo huo wanhakikisha idadi kubwa inafaulu kukidhi matakwa ya wansiasa!

  umoja wa madaktari
  kwa nchi yetu ambapo siasa inaanza ikifuatiwa na vitu vingine hata watu waliopata mafunzo ya clinical officer kwa miaka mitatu au rural medical aid naye amepewa sifa ya kuwa daktari ila inapokuja wakati wakudai maslahin yoa hao wa kada ya chini hawajui wasimame wapi ndiyo maana wakati wote wanaposimama kudai maslahi yao mambo hayaendi kwa kuwa watu wa kada ya chini isiyo na umoja wala viongozi inaachwa ikiendelea kutekeleza majukumu ya madaktari hivyo nguvu ya umoja inakuwa imetoweka


  ushauri kwa madaktari
  kwanza waache kijibagua kwa viwango vyao vya elimu, uzoefu na umaarufu, wawe kitu kimoja na waanze kusimama kidete kupigania maslahi yao!
  wawahimize wanataaluma walioko chini yao kufanya kuanzisha vyama vyao na kuunganisha nguvu pamoja katika kudai maslahi yao
  kuwashawishi madaktari waliokimbia fani na kuingia kwenye siasa wajitambue nakurudi kundini kuanza kupigania maslahi yao
  waweke ajenda yakushirikisha watu wote wa idara ya afya kuleta mageuzi kwenye sekta ya afya kwa kudai kwa pamoja mazingira mazuri ya kazi yatakayowanufaisha wao na ,mwananchi wa kawaida asiyekuwa na uwezo wakwenda india

  MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU WAWEZESHE MADAKTARI NA WAFANYAKAZI WA SEKTA YA AFYA TANZANIA WAFUNGUKE WAWEZE KUSIMAMA KWA UMOJA NAKUDAI HAKI ZAO KWA UMOJA!
   
 5. W

  We know next JF-Expert Member

  #5
  Jan 16, 2012
  Joined: Sep 9, 2010
  Messages: 664
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Tunataka vitendo sasa, maneno basi!
   
Loading...