Madai kwamba wachaga wamelitawala kanisa katoliki yapanguliwa kwa hoja. Hajaitwa mtu hadharani bali yapanguliwa kisomi


Status
Not open for further replies.
M

Mdanganywa

JF-Expert Member
Joined
Jun 15, 2009
Messages
568
Points
250
M

Mdanganywa

JF-Expert Member
Joined Jun 15, 2009
568 250
Mwaka jana madai ya uchaga yaliibuliwa na gazeti la JAMVI LA HABARI likisema maaskofu wa kanisa katoliki huteuliwa kwa kufuata uchaga. Madai hayo haya hapa (bonyeza hapa)

Mtakumbuka madai haya yaliingia hadi bungeni gazeti hili kujadiliwa.

Jumatano iliyopita ina makala moja ya RAIA MWEMA inayoonyesha mchakato wa kuteua maaskofu unavyokuwa na kuonyesha isivyowezekana ukabila kupenya.

- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
TITLE: Je, unafahamu askofu mkatoliki anavyoteuliwa?
PUBLICATION: RAIA MWEMA
AUTHOR: JOSEPH MAGATA
DATE: MAY 08, 2019

- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
Jumapili atasimikwa “askofu mkuu” wa Mwanza, Renatus Nkwande. Kama kawaida TV na Redio zitarusha matangazo ya sherehe hiyo.

Katika sherehe hizi watangazaji wa TV na Redio wamekuwa wakiuliza askofu anateuliwaje? Watangazaji hawa wanastahili pongezi, tena waendelee kuuliza kwani sherehe kama hizi ni fursa ya kuelimisha wasikilizaji.

Mchakato wa zamani:
Zamani waumini kila jimbo walichagua askofu wao. Mwaka 374 waumini wa Milan walichagua Ambrose awe askofu wao.

Ambrose hakuwa amebatizwa hivyo hakuwa mkatoliki kamili. Hivyo akabatizwa Novemba 29, 374 na wiki iliyofuata akawa askofu wa Milan.

Watawala wa Ulaya walipolazimisha wateuwe maaskofu basi kuanzia mwaka 1122 Papa akaamua ndiye pekee awe anateua maaskofu hadi leo.

Kuujua mchakato:
Toka Papa aanze kuteua maaskofu watu wengi hawakujua mchakato. Wasomi waliutafiti lakini tafiti zao zilisomwa na wenzao tu vyuo vikuu vya kanisa.

Siku hizi mambo yalisomwa vyuo vikuu hii tu sasa yanasomwa na kuhojiwa hata na wasio wakristo.

Sheria za Uaskofu”:
Mambo mengi ya kanisa, ikiwemo uteuzi wa askofu hufanywa kwa kanuni zilizoagizwa.

Francis ni Papa wa 266. Ukikusanya hata maagizo manne tu ya kila Papa utapata kitabu chenye maagizo 1064 kinaitwa “Sheria za Kanisa”.

Hivyo, mwaka 1917 Papa Benedict XV alikusanya maagizo yakawa kwenye kitabu kimoja cha “Sheria za Kanisa”. Papa John Paul II naye akafanya hivyo mwaka 1983.

Hata hivyo hakikukamilisha kila jambo na kusababisha kanuni mahsusi za uaskofu zieendelee kubadilishwa.

Hivyo, June 28, 1988, John Paul II alileta mwongozo unaoitwa “Paster Bonus”. Ockotba 16, 2003 akaleta uitwao “Pastores gregis” na Januari 24, 2004 akaleta uitwao “Apostolorum Successores”.

Vigezo vya uaskofu:
Vigezo vinavyozoeleka siku hizi vya kumteua askofu baadhi ni hivi.

Awe na umri kuanzia miaka 35 na upadri kwa miaka mitano. Awe na imani thabiti, maadili safi, mpenda sala, busara, anayeheshimika na vipaji vingine.

Kama elimu yake si ya udokta (doctorate) basi walau iwe ya leseni (licentiate) ya maandiko au teolojia au “Sheria za Kanisa” toka chuo kilichoidhinishwa na Papa.

Papa John Paul II aliviweka vigezo hivi kwenye kanuni ya 378(1) ya “Sheria za Kanisa” za mwaka 1983. Hata hivyo haimzuii Papa kumteua mwingine akiridhika kaelimika kiwango hicho.

Uteuzi wa sasa:
Baada ya kuona sifa, elimu na maaskofu walivyoteuliwa zamani, sasa tuone askofu anavyoteuliwa siku hizi.

Kila miaka mitatu Papa hupokea majina ya mapadri wote duniani wanaopendekezwa kuwa askofu. Majina hutoka kwa kila askofu wa jimbo. John Paul II aliweka utaratibu huu kwenye kanuni ya 377(2) ya “sheria za kanisa”.

Askofu Mwandamizi
Ninaonyesha “askofu mwandamizi” anavyoteuliwa kwa sababu kanuni inamteua “askofu mwandamizi” sawa na inavyomteua “askofu wa jimbo”.

Jimbo linapohitaji “askofu mwandamizi”, mwakilishi wa Papa nchini anaelekezwa na kanuni ya 377(3) ya “sheria za kanisa” kukusanya mapendekezo ya maaskofu wa kanda yenye jimbo lile.

Hivyo, kumteua Renatus Nkwande kwenda Mwanza na Jude Thadaeus Ruwa’ichi kwenda D’Salaam kumeelekezwa na kanuni hii.

Hii maana yake ili kumteua “askofu mwandamizi” wa D’salaam, kanuni inaelekeza mwakilishi wa Papa akusanye mapendekezo ya maskofu sita yaani wa Zanzibar, Tanga, Morogoro, Mahenge, Ifakara na D’Salaam.

Hivyo, kumteua askofu wa Mwanza mapendekezo yanatoka kwa maaskofu saba yaani wa Musoma, Bunda, Shinyanga, Geita, Bukoba, Kayanga, Rulenge-Ngara.

Baraza la Maaskofu:
Kinachofuata ni mwakilishi wa Papa kuchukua mapendekezo ya Rais wa Baraza la Maaskofu.

Mwaka 2006 “askofu mwandamizi” wa Nyeri, John Njue alikuwa Rais wa Baraza la Maaskofu la Kenya, hivyo alipata haki hii ya kupendekeza jina la askofu wa jimbo lolote la Kenya.

Kuulizwa mapadri:
Baada ya hapo mwakilishi wa Papa atakusanya mapendekezo ya mapadri washauri wa askofu na ya baadhi ya mapadri na wamisionari.

Kuulizwa Walei:
Mwisho mwakilishi wa Papa huomba mapendekezo ya walei wanaoaminika. Hivyo, mchakato unaweza kuhusisha watu 20, wote wakitoa mapendekezo kisiri.

Kuteua “Askofu Mkuu:
Baadhi ya vitabu vinaonyesha kama anayeteuliwa ni “askofu mkuu” basi utaratibu ni huuhuu ila tu mwakilishi wa Papa sasa anakusanya pia mapendekezo ya “maaskofu wakuu” wote.

Kuchuja majina:
Hatua inayofuata mwakilishi wa Papa atapeleka majina Roma. Hapeleki yote aliyokusanya, bali anachuja yanabaki matatu tu. Je haya majina yanapokelewaje pale Roma?

Maana ya Kongregrasio:
Pale Roma hakuna “idara” bali zipo “Kongregrasio” au “sekretarieti” au “Tume” yaani “Commission”. “Kongregrasio” ni timu inayoongozwa na kardinali inayoshughulikia jambo fulani.

Kongregrasio ya Maaskofu”:
Masuala ya maaskofu duniani hushughulikiwa na “kongregrasio ya Maaskofu”. Hivyo ile orodha ya mapadri watatu hupelekwa Roma kwenye “kongregrasio ya Maaskofu”.

Propaganda Fide”:
Lakini bado kuna maeneo yanaangaliwa kama enzi wamisionari walipotumwa wakisimamiwa na “kongregrasio ya Uenezaji Injili”, maarufu kwa jina “Propaganda Fide”.

Maeneo hayo ni sisi Afrika pamoja na Asia na Ocenia. Hivyo orodha ile ya majina matatu toka Tanzania inatumwa Roma kwenye hii “Propaganda Fide”.

Kongregrasio” kujadili:
Kazi ya “kongregrasio” ni kuchambua sifa za yale majina matatu (“terni”) na kuchagua jina moja. Inaweza kuyakataa yote ikamuagiza mwakilishi wa Papa alete mengine.

Papa kukataa jina:
“kongregrasio” inapochagua jina Papa akalikataa, utaratibu utarudiwa kuanzia hatua atakayopenda. Papa anaweza asifuate utaratibu huu akachagua jina analolitaka.

Kukubali uteuzi:
Papa akilikubali jina anaanzisha hatua ya kumuuliza mteuliwa, anapeleka jina kwenye ile “kongregrasio”, nayo inamtaarifu mwakilishi wa Papa ili amuulize mteuliwa.

Novemba 1983, padri Polycarp Pengo alipewa muda wa siku moja tu kujibu kama amekubali au amekataa kuwa askofu wa Nachingwea: {Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ISBN: 978976893397, uk. 99}.

Kutangazwa uteuzi:
Mteule akikubali inapangwa tarehe ya kumtangaza. Tarehe ikifika mwakilishi wa Papa hutangaza uteuzi.

Kumpokea mteule:
Mara nyingi askofu hupokewa kwanza na makanisa ya mpakani mwa jimbo. Askofu Jude Thadaeus Ruwa’ichi alianza kupokewa kwenye seminari ya Visiga ya D’Salaam. Hivyo askofu Renatus Nkwande ataanza kupokewa kwenye Parokia za mpakani mwa Mwanza na Bunda.

Barua ya uteuzi (Bull):
Siku ya sherehe huanza kusoma barua ya Papa aliyoamuandikia mteuliwa.

Mwaka Aprili 591 Papa Gregory I alijiita “Servus servorum Dei”. Hivyo hadi le barua ya uteuzi inayoitwa “bull” huanza na maneno hayo na itasomeka “Franciscus episcopus Servus servorum Dei” yaani “Francis, askofu na mtumishi wa watumishi wa Mungu”.

Kupewa Daraja:
Hatua inayofuata ni kumpa daraja la uaskofu lakini kama alishaupata hatua hii haifanyiki.

Kusimikwa kitini:
Madaraka ya askofu ni kile kiti chake, “kathedra”. Hivyo hatua inayofuata ni kumkalisha madarakani, yaani kumkalisha kwenye “kathedra” na kupokea utii toka kwa mapadri wake.

“Kanda ya kikanisa”:
Ukristo ukishakomaa eneo hilo linaloitwa “jimbo” yaani “diocese”. Hata hivyo askofu husaidia ukristo kuenea eneo linalomzunguka ili siku moja pia pawe na majimbo.

Maeneo yale yakifaulu kuwa majimbo yeye sasa anaitwa “askofu mkuu” yaani “arch-bishop” na jimbo lake linaitwa “arch-diocese” yaani “jimbo kuu”, haya majimbo yanayomzunguka yanaitwa “suffragan-diocese”.

Eneo lote la “jimbo kuu” pamoja na haya majimbo “suffragan-diocese, kwa kiingereza linaitwa “ecclesiastical province”. Kwenye kamusi ya padri Stephano Kaombe wa D’Salaam analiita ni “kanda ya kikanisa”.

Jimbo kuu” la kwanza Tanzania ni Tabora na D’Salaam na wiki juzi limeanzishwa la Mbeya. Mengine ni Songea, Mwanza, Arusha na Dodoma.

Metropolitan”:
“Askofu mkuu” kama wa Mwanza si mtawala wa jimbo la pembeni (suffragan-diocese) kama Musoma au Bunda.

“Askofu mkuu” anaruhusiwa majukumu machache tu kwenye haya majimbo jirani na anapoyafanya anaitwa “metropolitan”.

Baadhi ya majukumu ni kumtaarifu Papa hali ya jimbo jirani ikitetereka na linapokosa askofu, siku ya tisa anamteua “msimamizi wa jimbo” kama bado hajateuliwa.

Majukumu haya Papa John Paul II aliyaweka kwenye kanuni ya 23(b) ya sheria ile “Apostolorum Successores”.

Heshima ya “Personal Title”:
Protase Rugambwa alikuwa ni askofu wa Kigoma. Papa Benedict XVI alimteua kuwa“askofu mkuu” japo hakumpa “Jimbo Kuu” lolote.

Huu “uaskofu mkuu” wa bila kupewa “Jimbo Kuu”, kama wa Protase Rugambwa, unaitwa “Personal Title”.

Protase Rugambwa sasa ndiye katibu wa “Propoganda Fide” pale Roma, yaani yuko hatua moja tu chini ya kardinali anayeongoza “kongregrasio” hiyo.

Padri kuwa “askofu mkuu”:
Si lazima “askofu mkuu” atokane na mmoja wa maaskofu.

Tanzania imeshatoa mapadri wawili walioenda moja kwa moja kuwa “askofu mkuu”. Mmoja alikuwa ni Marko Mihayo wa Tabora aliyekuwa mwafrika wa kwanza kuwa “askofu mkuu”.

Mwingine ni Novatus Rugambwa ni ambaye ni mwakilishi wa Papa nchini New Zealand .

“Askofu msaidizi”:
Tumeona “askofu mwandamizi” anavyolingana na “askofu wa jimbo” katika utaratibu wa kumteua.

Uteuzi wa “askofu msaidizi” ni tofauti, jimbo linamupohitaji anayependekeza ni “askofu wa jimbo” tu na Roma wanashughulikia pendekezo lile.

Mwaka 2004, utaratibu huu wa kumteua “askofu msaidizi”, Papa John Paul II aliuweka kwenye kanuni ya 70 hadi 71 ya ile sheria “Apostolorum Successores”.

Pallium ya Askofu Mkuu:

Hatua ya mwisho kwa “askofu mkuu” ni kusubiri siku ya kumvika shingoni utepe unaoitwa “pallium”. Kwa karne nyingi “pallium” imekuwa na utaratibu ufuatao.

Kondoo wa “Pallium”:
“Pallium” imeanza kuvaliwa karne ya tano. Hufumwa kwa manyoya ya kondoo anaowapokea Papa kila Januari 21 kwenye kanisa liitwalo “ Agnes” pale Roma.

Kuvalishwa Pallium:

“Pallium” ina historia ndefu ya kuivalisha. Mwaka 2004 kwenye kanuni ya 23(b) ya sheria (“Apostolorum Successores”) John Paul II aliagiza kila “askofu mkuu” mpya afike Roma Juni 29 avalishwe “pallium”.

Jude Thadaeus Ruwa’ichi na Denis Dallu ndiyo watanzania wa mwisho Papa kuwavisha “pallium” kwani Januari 12, 2015, Papa Francis aliamua kila “askofu mkuu” mpya avishwe “pallium” jimboni kwake.

Hivyo “pallium” ya askofu Isack Amani, aliyovalishwa Desemba 04, 2018 na Marek Solczynski, mwakilishi wa Papa, ndiyo ya kwanza kuvalishiwa hapa nchini.

Natumaini mchakato huu ukifafanuliwa kama hivi utaeleweka kiurahisi.

Hata anayeeneza tuhuma za ukabila unaweza kumuumbua kwa kumuuliza ukabila unawezaje kupenya hatua zote hizi za mchakato.
- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
Imetayarishwa na:
Joseph Magata
Cell: 0754-710684
Email: josephmagata@yahoo.com
- - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - - -
 
idawa

idawa

JF-Expert Member
Joined
Jan 20, 2012
Messages
21,917
Points
2,000
idawa

idawa

JF-Expert Member
Joined Jan 20, 2012
21,917 2,000
Asante kwa hii elimu adimu kuipata kirahisi.
 
Aikambee

Aikambee

JF-Expert Member
Joined
Sep 27, 2017
Messages
2,494
Points
2,000
Aikambee

Aikambee

JF-Expert Member
Joined Sep 27, 2017
2,494 2,000
Kanisa ni moja tu.

Kanisa Takatifu Katoliki la Mitume, Ushirika wa Watakatifu, Maondoleo ya Dhambi, Ufufuko wa Miili na Uzima wa Milele, Amina!
 
B

bagamoyo

JF-Expert Member
Joined
Jan 14, 2010
Messages
6,204
Points
2,000
B

bagamoyo

JF-Expert Member
Joined Jan 14, 2010
6,204 2,000
Hii ndiyo JamiiForums, inatoa elimu endelevu kwa wote ktk jamii.
 
Samwel Ngulinzira

Samwel Ngulinzira

Verified Member
Joined
Aug 5, 2017
Messages
893
Points
1,000
Age
26
Samwel Ngulinzira

Samwel Ngulinzira

Verified Member
Joined Aug 5, 2017
893 1,000
Asante kwa ufafanuzi mzuri.
 
Status
Not open for further replies.

Forum statistics

Threads 1,295,677
Members 498,336
Posts 31,219,350
Top