MADA FIKIRISHI: Ingekuwa vipi kina Ertugrul wangezaliwa Tanzania?

Ferruccio Lamborghini

JF-Expert Member
Apr 15, 2020
1,231
2,000
etuugupicc


Angalia tamthilia za kituruki za Azam TV; tangu Sultan, Wounded Love na hata sasa Ertugrul utagundua kitu kimoja tu.

Kwamba tamthilia hizi ni simulizi za historia ya nchi yao ya Uturuki. Kihistoria Uturuki ilikuwa sehemu ya himaya kubwa ya Ottoman ambayo ilianza mnamo karne ya 13.

Himaya hii ambayo ilianza kidogokidogo ilipanuka na kuwa kubwa zaidi wakati wa utawala wa Sultan Suleiman Khan au Suleiman The Magnificent kama ambavyo wazungu walimuita.

Ertugrul ni jina la mtu ambaye ni baba mzazi wa Osman au Othman wa kwanza ambaye ndiye mwanzilishi wa himaya ya Ottoman.

etuguuupiccc

Na himaya hii iliitwa Ottoman kutokana na watu kulikosea jina la mwanzilishi wake Osman au Othman, wakasema Ottoman. Ndiyo likawa jina la nchi.Osman au Othman alianza na kanchi kadogo ambako alikakuza kwa kuwavamia majirani zake na kuwapora ardhi yao. Ndiyo maana kwenye tamthilia hizi kila siku kuna vita, vita vita.

Utawala wa kisultani ni wa kurithi. Kwa hiyo alipokufa Osman au Othman wa kwanza akarithiwa na wengine tisa kisha akaja wa kumi ambaye ndiyo Sultan Suleiman Khan - yule mume wa Hurem.

Alitawala kuanzia 1520 hadi 1566. Alirithi usultani kutoka kwa baba yake, Selim wa kwanza na ndiye aliyeipanua zaidi himaya ya Ottoman.

Alipigana vita nyingi sana ikiwemo dhidi ya Wakristo kutoka Ulaya Magharibi. Pia aliteka na kutawala sehemu nyingi za Bara la Asia hadi Afrika Kaskazini.

Sultan Suleiman Khan naye akafa na kurithiwa na utitiri wa masultan hadi sultan wa mwisho Abdulmejid wa pili aliyetawala kwa mwaka mmoja na miezi mitatu tu - Machi 1922 hadi Novemba 1924. Kuanguka kwa himaya hii ndiyo simulizi ya tamthilia ya Wounded Love ambayo ni simulizi ya vita vilivyoisambaratisha kabisa himaya hii na kuzaliwa mataifa mengi sana likiwemo la Uturuki.

etuguuupiccc

Unapokaa na kuangalia tamthilia hizi ujue unaangalia historia halisi ya himaya ya Ottoman iliyozaa Uturuki na hata Saudi Arabia ya sasa na Libya, Morocco na kadhalika.

Na hii ndiyo inayonisukuma kutamani kina Ertugrul Beyi wangezaliwa Tanzania. Tamaa yangu inatokana na ukweli kwamba nchi yetu ina mikasa mingi zaidi ya ile iliyopo Uturuki ambayo kina Ertugrul wanatamba nayo.

Hii nchi ina makabila zaidi ya 120 na kabla ya Tanzania kuwa taifa kama lilipo leo, asilimia kubwa ya makabila yalijiendesha kama nchi kamili.

Mkwawa na Wahehe wenzake pamoja na Wabena walikuwa katika nchi yao. Mazengo na Wagogo wenzake walikuwa kwenye nchi yao.

Mirambo na Wanyamwezi wake walikuwa kwenye nchi yao. Hawa wote wana simulizi nzuri sana ambazo zingeweza kuwa tamthilia tamu na za kuvutia.

Vipi ikitokea JB akiigizia tamthilia ya ujio wa Wangoni nchini? Hivi ni nani aigize tamthilia ya vita vya Wangoni chini ya Chifu Mputa Gama na Songea Mbano dhidi ya Wahehe chini ya Munyigumba baba yake Mkwawa vilivyopiganwa pale Makambako?

Nani aigize kuhusu asili ya jina la mji wa Mpwawa. Mkwawa alienda pale kusimikwa uchifu na mjomba wake Chifu Mazengo wa
Dodoma.

Mkwakwa alikuwa mtoto wa dada yake Mazengo. Mtoto wa dada ni mpwa. Kwa hiyo wakati akisimikwa neno mpwa lilitajwa mara nyingi sana - yaani mpwa mpwa mpwa ndiyo ikazaa Mpwawa.

Nani aigize tamthilia ya kipigo cha kwanza kabisa cha Wajerumani dhidi ya Mkwawa pale Lugalo Iringa? Kambi ya jeshi ya Lugalo - Dar es Salaam imerithi jina la eneo ambalo Mkwawa aliwashinda vita Wajerumani mwaka 1891.

Hivi ndivyo vita vya kwanza kihistoria Wajerumani kushindwa na kamanda wao Zelewski kuuawa. Yaani Mjerumani alishindwa kwa mara ya kwanza katika ardhi yetu halafu tunachukulia poa tu.

Nani aigize tamthilia ya Mtemi Mirambo kuushinda nguvu msafara wa Sultan Barghash wa Zanzibar pale Tabora walipokataa kulipa kodi. Barghash akaungana na Mwingereza Sir Henry Morton Stanley ambaye alikuja Afrika Mashariki kumtafuta Dk Livingstone.

Mirambo alifunga njia hadi walipe kodi, wakakataa na kuanzisha vita. Aliwanyoosha hadi Sir Henry akamuita Mirambo “The African Bonaparte” yaani Bonaparte wa Afrika akimfananisha na mtawala wa Ufaransa aliyegopewa sana kwa vita.

Nani aigize tamthilia kuhusu Kilwa - dola imara sana ya kuanzia karne ya 10 hadi karne ya 14. Dola hii ilianza mwaka 957 hadi 1513. Makao yake makuu yakiwa Kilwa Kisiwani. Dola hii ilikuwa kubwa kiasi cha kutengeneza pesa yake yenyewe.

Endapo kina Ertugrul Beyi na Cevdet wangekuwa wamezaliwa Tanzania tungeweza kuwa na tamthilia nyingi sana zinazosumbua duniani.

Lakini bahati mbaya hapa kwetu wamezaliwa kina Wema Sepetu, Kajala, JB, Idrisa Sultan na kadhalika ambao kazi zao nyingi ni za mapenzi tu kama stori za kazi. Hakuna hata moja inayowaza kuichimbua historia ya Tanzania na kupata tamthilia kama kina Ertugrul.©Mwananchi
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom