Machozi yao ni zao la tamaa na hulka zetu za kimwili

Jul 18, 2020
14
12
Na; Norbert Mporoto.
27.01.2021 ¦ 12:36 PM
Tanzania.

Siachi kustaajabu namna ambavyo thamani ya ukarimu unaotoka katika vyanzo visivyosadifu jambo hilo unafanyika kuwa halali tofauti na uasilia wake. Kinachoogofya zaidi ni namna ambavyo mboni zinatetwa, si machozi bali woga unaosahaulisha asili na ukweli wa yale yanayotia woga huo. Hakika, huu ni unafiki mkubwa kwani imekuwa ni kawaida watu kuyakarimu matatizo yanayotokana na uzembe, upumbavu, na matendo mabaya tunayoyatengeneza kwa kigezo kwamba tumeumbwa na udhaifu wa kutenda makosa. La hasha! Huu si ufikiri sahihi, bali ni furaha ya kuvibebesha vichwa na mioyo yetu mzigo wa tamaa na hulka za miili yetu.

Hivi sasa tunashuhudia ongezeko kubwa la watoto wa mtaani, wakiwepo wasio na baba (japo baba zao wako hai), wakiwepo wasio na mama (vile vile mama zao wako hai), ama wale wanaohangaika na mlo mmoja kwa siku wakiwa chini ya mbawa za mzazi mmoja baada ya sintofahamu kati ya wazazi wao, na wale tuliowazoea ambao hawana wazazi wote (yamkini wazazi wao walipotea kupitia sababu za wazi na ambazo zinaepukika kwa sisi ambao bado tuko hai). Poleni sana wote mlio katika makundi haya.

Kimsingi, ongezeko kubwa katika kundi hilo huenda sambamba na ongezeko la kesi za mimba zisizotarajiwa (naimani wale ambao tamaa imetangulia umri wao wanaelewa zaidi lugha hii), wazazi kukana watoto, kutupwa na kutelekezwa kwa watoto kinyemela, au kutalakiana kwa wazazi. Haya yote huwa ni chanzo cha vilio vya watoto hawa visivyokwisha, wala kufutika vichwani mwao milele. Kiukweli haya yote hutokana na udhaifu tunaojitengenezea kwa makusudi.

Pasipo kutafuta kichaka cha kujificha, ukweli ni kwamba huu ni msiba wa kujitakia, na hauna mahusiano yoyote na dhana potofu ya wakosaji ya kwamba "HAKUNA ALIYEKAMILIKA, WOTE TUNAKOSEA NA MAKOSA TUMEUMBIWA BINADAMU". Kuisimamia dhana hii kujadili mambo nyeti kama haya ni kuendelea kuchuma dhambi kwa kumkwaza Mwenyezi Mungu na mizimu yetu, kwani wao hawahusiki na huu utaratibu wetu wa kuishi nje ya misingi na kanuni zao juu yetu. Hii ni jeuri tunayochuma kwa kujitakia, hivyo tumeshindwa kuusimamia utu na ubinadamu wetu.

Sina kichwa cha panzi kiasi cha kusahau kwamba tunaishi katika ulimwengu wa mawazo huria, pia si jambo geni watu wakashangaa kwanini naumiza kichwa na kuhofia dhoruba ndani ya kikombe cha chai ili hali wao ni manahodha hodari katika bahari zilizonawiri dhoruba tena zenye kina kirefu. Labda! Kwa kuwa wanatumia ustaarabu wa jani kavu mtini kulilaumu lililo chini kwa kelele. Kamwe siwashauri kusadiki ujinga wa manahodha hao.

Tathimini yangu ni kwamba, ufahamu wa matatizo haya umetukutanisha katika vilio vya kuomboleza kuona nani atatunusuru na kadhia hii, hakuna aliyejaribu kutazama chanzo chake. Labda tumezongwa na imani kwamba haya ni matatizo ambayo sisi binafsi hatuijui asili yake. Tafadhali, naomba niangazie hili kwa ufupi kuanzia pale ambapo umetupwa ukomo wa kimtazamo wa walio wengi.

Kwa miaka kenda tumezijenga jamii zetu kwa misingi isiyosadifu utu, heshima, wala maadili yetu. Katika maandishi yangu mengi huwa siachi kuzungumzia namna ambavyo tumepoteza thamani ya utu wetu na heshima inayolinda mhimili wa maadili. Jamii kupitia watu wetu imeridhia kufanya suala la maadili kuwa mwafaka wa kifamilia na si jukumu la wanajamii. Kwani jitihada za wazazi wengi zimejikita katika kujisahaulisha majukumu yao, na hivyo kuruhusu mgawanyiko wa misingi ya maadili kutamalaki. Hii imepelekea ufa mkubwa na myumbo wa kitabia unaorasimisha matendo mabaya kutokana na ubinafsishaji wa mihimili ya malezi katika ngazi ya familia.

Ufa huu mkubwa ndiyo unaopelekea idadi kubwa ya watoto walioko mtaani, hii inatokana na mwingiliano mkubwa wa kitabia ambao si rafiki kwa familia moja na familia nyingine. Wazazi wa hao watoto wamejikuta katika hali ya kutenda makosa kutokana na misingi ya malezi iliyowakuza. Wengi wao wakijikuta katika mahusiano yasiyo na mantiki yeyote isipokuwa kutimiza haja na tamaa za miili yao. Lakini jambo kubwa la haya yote ni wanajamii kukosa dhamiri thabiti itayowaunganisha katika kuujenga vyema mhimili huu wa maadili.

Ndani ya jamii zetu usasa umeleta dhana potofu yenye mtafaruku wa kiuelewa kuhusu haki na uhuru wa mtoto ambao hautaki kuguswa na mihimili ya malezi ya kiafrika. Aina ya malezi anayopata mtu ndiyo huamua mwafaka wa kitabia wa maisha yake. Jamii zetu hususani kipindi hiki cha utandawazi zimekuwa zinazongwa na mapokezi ya sera tofauti ambazo hazina ufanani na mazingira ya kiutekelezaji katika nchi husika. Yamkini sera hizo si mbaya, ila mapokezi yake yana madhara makubwa mawili. Kwanza hutaka anayepokea atupe mbali kile alishoshika, pili sera hizi huleta ugeni kwa wapokeaji wake kitu ambacho huwafanya kuwa watumwa kutokana na ugeni huo, hivyo ufanisi wa utekelezaji huwa hauwezi fikika pasipo madhara kwa wahusika.

Sera hii ya uhuru na haki za watoto imekuja kulegeza baadhi ya misingi na mihimili ya malezi ya kiafrika ambayo watangulizi wetu waliishi. Ulegezwaji wa misingi hiyo huenda sambamba na kuvalishwa matendo mapya yasiyosadifu uafrika wetu, kisha kuagiza watoto wetu wapewe uhuru ili wayavae matendo haya kwa kivuli cha uhuru na haki usioainisha manufaa yake katika nyakati hizi na mazingira yetu. Kwa lugha nyepesi sera hizi ni kama chatu, hivyo wanetu katika taswira hiyo ya utumwa wamekuwa mithili mbwa wanaojikabidhi kinywani mwa chatu.

Ni wazi kwamba hakuna utumwa mbaya kama kujiona uko huru, hivyo pasipo kupepesa macho, kuna ukweli kwamba sera hizi zimechagiza uwepo wa vilio vya watoto hawa wa mtaani kwani ndizo zilizo (zinazo) wapa wazazi wao ujasiri wa kuyavaa matendo mabaya yanayokiliza kizazi hiki na kijacho maana uzembe, upumbavu, na tamaa vyote kwa pamoja viko hai kuendeleza upuuzi huu. Ashakum si matusi.

Kinga huliwa tumboni, lakini si sababu ya kuruhusu fisi aongoze kundi la mbuzi machungani. Mateso wanayopata watoto hawa yanatokana na udhaifu wa wazi kabisa, hakika yanawatesa mno. Busara yetu imekuwa ni kutengeneza kizazi kinachohaha kwa kushindwa kuzihimili hisia zetu? Je nini mwafaka wa jamii na taifa letu kwa kuzalisha kizazi cha bahati mbaya? Lazima ifahamike kwamba uzazi ni kutimiza majukumu, na kabla ya hilo huwa ni matokeo ya kuafikiana baina ya watu wawili tena kwa wakati sahihi, nje ya hapo tutakuwa tunajitoa kuliangamiza taifa. Ipo siku tutakuwa na bajeti kubwa ya kugharimia upuuzi huu ambao leo hii jamii zetu zinauchelea. Hatupaswi kuficha fimbo, amkeni wanetu wanapotea.

Fisi hawezi kumla mwanae, basi nami busara hiyo naitumia kutowanyooshea kidole watu fulani, ila ninachoweza ni kuwakumbusha juu ya mienendo yetu. Haifai kuona kijana aliyetoka kuvuta bangi na kunywa pombe anatuletea mtoto na binti aliyeko kujiuza kisa tamaa za mwili. Hili sio taifa tunalotazamia kuwa nalo, hatuhitaji kuwaanda vijana wetu kuishi maisha ya kuomba kwa majirani na wahisani. Yapo yakutusumbua, lakini si haya tunayoyatengeneza.

#MakalazaMporoto #watotowamitaani #UhuruniFikra #Tanzania

NB: Picha imetumika kutoa fasiri tu na si umiliki.

Screenshot_2017-11-03-01-31-38.jpg
 
Back
Top Bottom