Machafuko na Umwagaji damu Nigeria! Hiki Ndiyo Chanzo

Hashpower7113

JF-Expert Member
Sep 26, 2011
1,353
2,137
20NIGERIA-01-mobileMasterAt3x.jpg
Imeandaliwa na Hash Power kwa msaada wa mitandao

Nigeria is bleeding! Nigeria inavuja damu, maelfu ya wananchi wa nchi hiyo wanaandamana kuanzia kwenye mitaa ya Lagos, Port Harcourt, mpaka Abuja na kwingineko!

Jeshi katili la nchi hiyo, linaendelea kuwadhibiti waandamanaji kwa mtutu wa bunduki. Risasi za moto zinarindima, vijana wadogo, wasio na silaha, wanaoandamana mitaani, wanapigwa risasi za vichwa kama majambazi!

Tukio kubwa ni pale wanajeshi walipowafyatulia wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani, risasi za moto na kuwaua kikatili waandamanaji ambao bado idadi yao kamili haijafahamika huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya.

Mauaji yanazidi kuchochea hasira, waandamanaji sasa wanapambana na wanajeshi wenye silaha, ni patashika nguo kuchanika!

Vituo vya polisi vinapigwa moto, barabara zote zimefungwa, jeshi limetangaza amri ya mtu yeyote kutotoka nje kwa saa ishirini na nne lakini maelfu ya watu wapo mitaani wakiendelea kuandamana, afe beki afe kipa! Lazima mabadiliko yake! Ama kwa hakika, Nigeria inavuja damu.

Kama wewe ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii, utakuwa umekutana sana napicha za waandamanaji nchini humo zinazosambaa kwa kasi mithili ya moto wa nyika kwa wiki kadhaa sasa, zikisindikizwa na maneno hashtags kama #EndSARS, #EndPoliceBrutality na kadhalika.

Yawezekana bado hujajua ni nini hasa kinachoendelea nchini humo, kwa nini maelfu wanaandamana? Kwa nini wanajeshi wanawaua raia? Ufuatao ni uchambuzi wa kina kuhusu kinachoendelea Nigeria.

CHANZO CHA MACHAFUKO
Waswahili wanasema njiti moja inachoma msitu! Ndiyo, hicho ndicho kilichotokea nchini Nigeria.

Mambo yalianza kama masihara na hiyo ilikuwa ni baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii, ikiwaonesha polisi wa kitengo maalum cha SARS, wakimfyatulia risasi kijana mmoja nchini humo na kumuua.

Video hiyo iliamsha hasira kubwa miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo, hususan vijana ambao kwa miaka mingi wamekuwa wahanga wakubwa wa mateso, udhalilishaji, uonevu na mauaji yanayofanywa na polisi.

Kabla hatujaendelea, tukitazame kikosi hiki kinacholalamikiwa, SARS. SARS ni ufupisho wa maneno ya Kiingereza ya Special Anti Robbery Squad yakimaanisha kikosi maalum cha kupambana na ujambazi. Kikosi hiki kilianzishwa rasmi mwaka 1992 na hiyo ilikuwa ni baada ya kushamiri kwa ujambazi wa kutumia silaha nchini Nigeria.

Hata hivyo, tofauti na kusudi la kuanzishwa kwake, SARS ilianza kukumbwa na skendo za mauaji ya raia wasio na hatia, uporaji, ubakaji na mateso kwa rais. Askari wa kikosi hicho wakageuka na kuwa maadui wakubwa wa raia wema, huku wakituhumiwa pia kupokea rushwa kutoka kwa majambazi na kuwaachilia.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Binadamu, Amnesty International, kuanzia January 2017 hadi May 2020, zaidi ya visa 82 vya wananchi wasio na hatia kuuawa, kuteswa au kubakwa wakiwa mikononi mwa SARS viliripotiwa.

Manung’uniko ya miaka mingi dhidi ya mateso ya askari wa kikosi hicho, ndiyo yaliyoamsha machafuko yanayoendelea na kama nilivyoeleza, hiyo ilikuwa ni baada ya kuvuja kwa video ikiwaonesha askari hao wa SARS wakimtwanga risasi raia asiye na hatia!

Hasira hizo ndizo zilizowafanya maelfu ya Wanigeria kuingia barabarani, wakiishinikiza serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Muhammadu Buhari, kukifuta kikosi hicho mara moja lakini pia kuhakikisha mamia ya familia zilizowapoteza wapendwa wao kutokana na ukatili wa askari hao, zinalipwa fidia na wahusika wanafikishwa mbele ya vyombo vya habari.

Maandamano haya yaliyoanza kama masihara, yalianza kupata nguvu baada ya watu maarufu kutoka ndani na nje ya Nigeria kuanza kuyaunga mkono, kila mmoja akilaani ukatili wa polisi hao kwa raia.

Miongoni mwa watu maarufu wa mwanzo waliosimama mstari wa mbele, ni wasanii Wizkid, Burna Boy, Davido, Peter na Paul waliokuwa wakiunda P Square na wengine wengi.

Wasanii wakubwa duniani kama Beyonce, Rihanna, Drake, P Diddy Trey Songz na mwanzilishi na mmiliki wa Mtandao wa Twitter, Jack Dorsey nao wakajitosa kukemea ukatili wa polisi nchini humo, #EndSARS ikazidi kupata nguvu.

Wanasoka nao hawakuwa nyuma, Marcus Rashford na Odion Ighalo wa Manchester United wakapost kwenye mitandao ya kijamii wakiishutumu serikali kwa kushindwa kuwachukulia hatua polisi wa SARS, mambo yakazidi kupamba moto.

MWITIKIO WA SERIKALI

Baada ya serikali ya nchi hiyo kuona mambo yameanza kuwa mazito, iliamua kuchukua hatua ya kutekeleza matwaka ya wananchi, ya kukivunja kikosi hicho.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Mohammed Adam, Oktoba 11, 2020 wakati maandamano yakiwa yamepamba moto, alijitokea hadharani na kutangaza kuivunjilia mbali SARS.

Watawala wa nchi hiyo waliamini kwamba kitendo hicho kitamaliza maandamano na kurudisha amani lakini haikuwa hivyo! Wananchi waliona hatua hiyo kama ni danganya toto ili kuwapumbaza.

Waliendelea kuandamana na sasa wakawa wanadai kwamba kuivunja SARS pekee hakuwezi kumaliza ukatili wa polisi dhidi ya raia, badala yake jeshi zima la polisi lifumuliwe na kusukwa upya, askarti wote wenye kesi za mauaji wawajibishwe lakini kubwa zaidi, rushwa iliyotawala kila kona ya nchi hiyo, imalizwe.

Siku tatu baadaye, jeshi la polisi lilitangaza kuunda kikosi kingine, SWAT, Special Weapon and Tactics ambacho sasa ndiyo kingekuwa kikifanya majukumu yote yaliyokuwa yakifanywa na SARS, kelele zikazidi kuwa nyingi kwamba SARS na SWAT ni walewale, wakataka mabadiliko makubwa zaidi.

Matakwa ya msingi yaliongezeka na kufikia matano

1. Kuachiwa mara moja kwa waandamanaji waliokuwa wamekamatwa na polisi

2. Haki itendeke kwa familia za watu wote waliouawa na polisi kulipwa fidia

3. Kuanzishwa kwa uchunguzi maalum wa matukio yote ya mauaji na mateso yaliyofanywa na polisi na wahusika kufikishwa mbele ya mikono ya sheria

4. Kufumuliwa kwa jeshi lote la polisi na kuundwa upya huku askari wasio na makosa pekee ndiyo wakitakiwa kurudishwa kwenye jeshi jipya

5. Kuwaongeza mishahara polisi ili wafanye kazi zao kwa uadilifu.

Serikali ya Rais Buhari ikashupaza shingo na kuona madai yote hayo kuwa hayana msingi wowote, watu wakatakiwa kuacha kuandamana mara moja vinginevyo jeshi la Nigeria litaingilia kati ili kumaliza machafuko hayo, Wanigeria jinsi walivyo wabishi wakasema msitutanie, tutaendelea kuandamana mpaka matakwa yetu yatakapotimizwa!

Moto unazidi kuwa mkubwa, maandamano yanazidi kuwa makubwa, si vijana pekee wanaoandamana tena bali Wanigeria wote, wakubwa kwa wadogo, wanawake kwa wanaume, wazee kwa vijana!

Licha ya jeshi kuingilia kati na kusababisha maafa kwa waandamanaji, bado hali ni tete na maandamano yanazidi kupamba moto.

Nini itakuwa hatma ya Nigeria? Je, damu itaendelea kumwagika? Je, mataifa ya Magharibi yataingilia kati na kumng’oa Buhari madarakani? Je, maridhiano yatafikiwa? Ni suala la muda tu lakini kila mmoja kwa imani yake, aiombee NIGERIA kwani inavuja damu!
 
Back
Top Bottom