Mabalozi wetu kumjibu Lissu, wametumwa na Serikali au ni utashi binafsi?

sammosses

JF-Expert Member
Jan 24, 2011
1,498
2,000
L

Takribani wiki sasa toka ndugu Tundu Antipas Mughwahi Lissu anze ziara ya Ulaya na Marekani kwa mwaliko maalumu. Tumeona akihojiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa akiwa pekee yake, lakini alipofika Marekani alipambanishwa na Balozi Wilson Masilingi katika kipindi cha straight talk cha VOA.

TUNDU LISSU, amekuwa akishitumu bunge na serikali kwa namna mbili. Moja serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kushindwa kufanya uchunguzi wa tukio la mh. Huyo kupigwa risasi hadharani mchana kweupe, pili bunge kushindwa kumlipa stahiki zake za matibabu ambazo ni haki yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za bunge.

Bahati mbaya sana, serikali imeshindwa kujinasua kwenye tuhuma hizo na kuja na majibu mepesi dhidi ya tuhuma ngumu za bwana Lissu. Tumeona jeshi la Polisi likitoa sababu zisizo na weredi dhidi ya tuhuma za Lissu. Haishi kusema Lissu amegoma kutoa ushirikiano ilihali hakuna juhudi zozote zinazo onyesha ufuatiliaji wa tukio hilo.

Haingi akilini uchunguzi wa kipolisi ujikite kwenye propaganda kuliko utendaji na uwajibikaji wa chombo hicho. Watanzania walitegemea jeshi lao la Polisi lingekuja na taarifa kuwa mpaka sasa tumefikia wapi na bado sehemu ndogo ya waathirika wenyewe kuhojiwa.

Bahati nzuri tuna uzoefu wa kiutendaji toka jeshi hilo toka sakata la mauaji ya Askari wetu huko MKIRU na utekwaji wa Mohammed Dewji, tuliona nguvu kubwa ya kiutendaji bila mtuhumiwa kupatikana na kupelekea kuonekana. Lakini kwa suala la Tundu Lissu imekuwa kizungumkuti.

Bunge limeonyesha kutojali maumivu ya mwenzao kama taasisi na kuitumia hisani ya wabunge binafsi kumchangia mwenzao, huku familia ya Lissu ikigonga mwamba hatima ya matibabu ya ndugu yao.

Turudi kwenye mjadala wenyewe, je MABALOZI wetu huko Ulaya na Amerika wametumwa na serikali kukanusha tuhuma za Lissu dhidi ya mihimili miwili!!

Kama ndivyo hivyo nini agenda yao kuhusu tuhuma za Lissu. Ukisikiliza malumbano ya Lissu (mb) na Mwanadiplomasia Balozi Masilingi, utaona ujumbe wa serikali umepwaya.

Kwanini;
Alichokifanya Masilingi ni kulivua nguo jeshi letu kutokujua majukumu yake kama chombo cha ulinzi na usalama. Lakini kinatoa tafsiri jinsi gani nchi yetu isivyo salama hali inayo sababisha maadui wa ndani na nje kufanya lolote bila hofu ya ulinzi wa nchi, kwa mantiki hiyo wananchi hawapo salama.

Kauli ya mh. Spika mkuu wa mhimili wa bunge kuingiza malumbano na kumtishia muathirika wa tukio la kupigwa risasi mh. Lissu, kuwa atanyang'anywa ubunge wake na kusimamishiwa mshahara wake kunalifanya bunge letu na serikali kujiweka njia banda hususani katika kipindi hiki, mihimili hiyo ikituhumiwa kutokumtendea haki mh. Lissu.

Nini kifanyike ;
Kwa kuwa serikali imeamua kumjibu Lissu kufuta tuhuma hizo, basi serikali ijipange jinsi ya kuzijibu tuhuma hizo kuliko kutumia njia ya malumbano yanayo ianika serikali.

Pili, kama majibizano hayo si maamuzi ya serikali bali ni utashi wa Posi na Masilingi ni msimamo wa serikali juu ya tuhuma hizi za mh. Lissu?

Mwisho, jeshi letu lijitazame upya kiutendaji, udhaifu au ukosefu wa weredi ndiyo pekee unao ianika serikali kimataifa na kuzua sintofahamu inayoendelea nchini.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom