Mabalozi waikamata Serikali ya JK pabaya

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,889
Mabalozi waikamata Serikali ya JK pabaya

na Tamali Vullu
Tanzania Daima

MSIMAMO wa mashirika na mataifa mbalimbali wa kuitaka serikali kuchunguza tuhuma za ubadhirifu zinazoikabili, zimeonekana dhahiri kuishtua Serikali ya Awamu ya Nne.

Mshtuko huo wa serikali ulidhihirishwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, muda mfupi baada ya kurejea kutoka kwenye ziara ndefu nchini Marekani, alikokuwa na Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Membe, alisema mabalozi hao wapo nchini kwa shughuli za kidiplomasia, na si kujihusisha na masuala ya kisiasa, huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni uchochezi.

Kauli hiyo ya Membe inakuja siku chache tu baada ya mabalozi wa mataifa makubwa ya Ulaya Magharibi na wawakilishi wa taasisi za fedha za kimataifa kuitaka serikali kuzifanyia kazi tuhuma zote za rushwa dhidi ya viongozi na zile za ubadhirifu katika Benki Kuu.

Membe ambaye alitangaza msimamo wake huo kwa waandishi wa habari jana asubuhi kabla ya kukutana na mabalozi hao jana hiyo hiyo mchana, alisema iwapo mabalozi hao wanakerwa na masuala mbalimbali nchini, wanapaswa kufuata taratibu zao za kazi, kwa kutoa maoni na kuwasilisha kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa au katika vikao halali.

“Kuna taratibu za mabalozi kutoa maoni yao, si kuzungumza majukwaani. Wanapaswa kufuata taratibu za mkataba wa Vienna…wanatakiwa kutoa maoni yao kwa maandishi wizarani ama katika vikao halali. Sasa wanapozungumza, sijui wanazungumza kwa niaba ya wakubwa wa nchi zao au wao.

“Lakini tulipokuwa katika ziara na Rais Kikwete, viongozi wa huko wamekuwa wakitupongeza kwa juhudi za kupambana na rushwa, lakini huku mabalozi wao wanatulaumu,” alisema.

Waziri huyo alisema katika nchi mbalimbali walizopo mabalozi, watu hawazungumzii masuala kama hayo na iwapo watafanya hivyo watafukuzwa katika nchi hizo kwa kuwa wamevunja sheria.

Alisema, mabalozi hao wanapaswa kufanyia kazi mambo ya kidiplomasia, na kuongeza kuwa atawaeleza suala hilo mabalozi hao atakapokutana nao, kwa kuwa uongozi wake ni imara.

Hata hivyo, alisema wananchi wana haki ya kulalamikia hatua zinapochelewa na si mabalozi.

Aidha, alieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa watu wanaishinikiza serikali kuwachukulia hatua watu waliotajwa kuhusika na tuhuma za ufisadi, wakati bado tuhuma hizo zinafanyiwa uchunguzi.

“Huwezi kupambana na suala la rushwa bila kufanya uchunguzi…baada ya tuhuma hizo kutolewa, serikali inafanyia uchunguzi tuhuma hizo na utakapokamilika watakaobainika watachukuliwa hatua stahili kwa kuwajibishwa au kufukuzwa.

“Serikali ya Awamu ya Nne ambayo imedhamiria kupambana na rushwa, haitaweza kukaa kimya bila kuwachukulia hatua watu watakaobainika kujihusisha na ufisadi iwapo uchunguzi utabaini hivyo,” alisema.

Waziri huyo katika kudhihirisha kuwa Rais Kikwete amedhamiria kupambana na rushwa, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), imeboreshwa na baadhi ya maofisa wamepelekwa masomoni kujifunza jinsi ya kuchunguza tuhuma za rushwa.

Membe, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati uchunguzi wa tuhuma hizo unafanyiwa kazi, ili utakapokamilika, Rais Kikwete awachukulie hatua waliobainika.

“Lazima tuwe wavumilivu, ripoti ikiwa tayari na ikifika mezani kwa bwana mkubwa, walengwa watawajibishwa, kwani Serikali ya Awamu ya Nne tumedhamiria kupambana na rushwa…mkiona kuna ucheleweshaji, basi kuna contradiction sehemu, lakini ukiwepo ushahidi, hatua zitachukuliwa,” alisema.

Aidha, katika hatua nyingine, waziri huyo alisema haoni ubaya wa mawaziri kufanya ziara mikoani kuelezea bajeti, na kuongeza kuwa hiyo ndiyo siasa, kwani mpinzani anapokwenda kufukua, chama tawala kinakwenda kufukia.

“…hata mimi kesho nakwenda Arusha kufukia mashimo yaliyoachwa wazi na wapinzani…hii ndiyo siasa. Pia nitakutana na mabalozi kujitetea na kuwakumbusha kufuata miiko yao ya kazi. Sisi ndio tunajua zaidi kuhusu rushwa nchini, hivyo wao hawawezi kutuzungumzia,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwashauri wapinzani kutafuta hoja ya kwenda nayo katika uchaguzi wa mwaka 2010, kwani tuhuma walizozitoa hazitakuwa na nguvu baada ya watu watakaobainika kuhusika kuchukuliwa hatua.

Wakati huo huo, Waziri Membe, alieleza kuwa ziara ya Rais Kikwete anayetarajiwa kurejea nchini leo, imekuwa ya mafanikio makubwa.
 
"Lakini tulipokuwa katika ziara na Rais Kikwete, viongozi wa huko wamekuwa wakitupongeza kwa juhudi za kupambana na rushwa, lakini huku mabalozi wao wanatulaumu," alisema.

Haya ndio maajabu ya Mussa! Hivi kweli JK alipokuwa akipongezwa kwa kupambana na RUSHWA ni kitu gani hasa alichokifanya hadi kuwa kigezo cha sifa zote hizi!..Ni wapi JK kaweza kupigana na RUSHWA!..
Can someone explain this!
 
Ameunda Takukuru yenye meno ya Hosea kama serikali inavyojigamba

Takukuru ambayo yeye ndo anaiamrisha na kuichagulia nani imchunguze na nani imuache? kwa lugha nyingine JK mwenyewe ndo TAKUKURU kwani ndiye anaye amua nani achunguzwe na nani aachwe!
 
Membe hajui kwamba taarifa zinazotumwa kwa wahisani zinatoka ktk serikali hii hii tunayoituhumu kwa ufisadi, na kama wanajua kuudanganya ulimwengu basi ajue kuwa hao mabalozi wanaishi na kufanya kazi nchini humuhumu na wanayo macho ya kuona kisha wanazo taaluma za kujua nini kinaendelea na upi ni ukweli na upi ni uzushi....

nilipomwona membe ktk tv anavyowabembeleza mabalozi wasiibane serikali kupitia vyombo vya habari nilimhurumia sana maana hata yeye ametumia media kujaribu kuwabana hao wanadiplomasia... na ama kwa hakika membe hajui atendalo.
 
Haya ndio maajabu ya Mussa! Hivi kweli JK alipokuwa akipongezwa kwa kupambana na RUSHWA ni kitu gani hasa alichokifanya hadi kuwa kigezo cha sifa zote hizi!..Ni wapi JK kaweza kupigana na RUSHWA!..
Can someone explain this!

Inanikumbusha kupongezwa kwa Mkapa na akina WB na IMF kwamba alikuwa anafanya vizuri katika awamu yake, wakati huo huo alikuwa busy "akifanya mavitu yake" na asilimia kubwa ya Watanzania ikiendelea kuishi katika umaskini wa kutisha.

Kiongozi kama anafanya uongozi wake ni mzuri wanaostahili kumpongeza ni wananchi waliomchagua ambao ndio wanaona hali halisi katika tofauti ya maisha yao ya kila siku, na sio Wamarekani wanaoishi Washington au New York ambao hawajui lolote kuhusiana na hali halisi ndani ya Tanzania.

Hakuna mfano wowote unaonyesha kuna jitihada zozote za kupambana na rushwa na mifano ya kuthibitisha hili ipo mingi tu.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom