Mabadiliko ya mawaziri: Mgonjwa Tanzania atapona?

baraka moze

Member
Apr 21, 2012
99
3
HAKUNA jambo baya katika maisha ya binadamu kama ugonjwa; hakuna anayependa kuugua.
Aidha, kila anayeugua anapenda apate tiba ya maradhi yake. Tena anataka tiba hiyo ipatikane kwa haraka na kwa kiwango cha juu. Hii ni kwa sababu afya ni jambo la msingi; bila afya mambo mengine yote katika maisha ya mwanadamu husimama. Kama unabisha, waulize wanasiasa wetu ambao hivi karibuni walikwenda kutibiwa India, Ujerumani, Afrika Kusini na kwingineko.

Waulize pia wagonjwa waliokimbilia kikombe cha babu kule Loliondo. Hata wanasiasa matapeli, kwa kutambua umuhimu wa afya kwa jamii nao walitumia fursa hiyo ya kikombe cha babu kujijenga wao au chama chao kisiasa! Shetwaan rajim hawa! Kila mmoja aliacha shughuli nyinginezo kufuata tiba!

Enzi zetu kulikuwa na kitabu cha shule za msingi kilichokuwa na msemo AFYA NI BORA KULIKO MALI na huu ndio ukweli. Watoto wote tuliaminishwa kuwa afya ni msingi wa yote, afya ni zaidi ya mali, cheo, siasa, n.k. Sina hakika kama watoto na vijana wa leo wanaaminishwa hivyo au wanaaminishwa kinyume chake?

Wengi ukiwasikiliza wanasema MALI NI BORA KULIKO AFYA! Hawajaugua hawa wakalazwa wakaona fedha isivyoweza kuwaondolea ugonjwa! Hawajaona matajiri waliosota na ambao bado wanasota hospitali kwa miaka kadhaa. Si kosa lao, ni kosa letu tuliopaswa kuwaongoza.

Afya ya mtu inapokuwa na matatizo, mgonjwa hufuata tiba na anategemea mtoa tiba awe na ujuzi wa kutosha, vifaa muafaka, n.k. Na wagonjwa wote wangependa tiba hiyo ipatikane jirani na makazi yao, kwa bei nafuu na kiwango cha hali ya juu ili wapone haraka.

Hapa ndipo inapojikiti makala yangu ya leo

Hakika kuna mgonjwa anaitwa TANZANIA. Mgonjwa huyu ni ndugu yetu na wote tunampenda na kwa mapenzi ya Muumba wetu, sote tunamtegemea mgonjwa huyu.

Alipokuwa mzima wa afya enzi za utoto na ujana wake, mgonjwa huyu Tanzania alikuwa na upendo nasi kweli kweli. Akitupatia mahitaji yote muhimu bila ubaguzi, kwa gharama nafuu na mara kadha wa kadha bure bilashi!

Hakika ndugu yetu huyu Tanzania alikuwa akikumbwa na maradhi enzi za utoto na ujana wake; kama ilivyo kwa binadamu yeyote. Lakini enzi hizo daktari wake na wauguzi walikuwa wepesi wa kugundua maradhi yake mapema kabla hayajasambaa mwili mzima.
Wakimpatia pia tiba madhubuti haraka bila kujali tiba hiyo itamuudhi mgonjwa, ndugu zake, marafiki zake au ndugu na marafiki wa wauguzi. Kilichopewa kipaumbile ni mgonjwa huyu TANZANIA apone haraka ili aweze kujiendeleza na kuendeleza wategemezi wake.
Lakini hali ilikuja badilika kijana huyu Tanzania alipo balehe na hasa pale daktari wake na wauguzi waliomlea toka utoto walipostaafu. Tatizo likaanza na mgonjwa mwenyewe na ndugu zake.

Hawa wakapoteza uwezo wa kutambua kwamba kijana Tanzania ameingiliwa na ugonjwa. Wakaacha ugonjwa ukakomaa weee hadi ukawa sugu. Kwa upande wa pili, madaktari na wauguzi wapya nao wakaona kuwapo na mgonjwa ni fursa yao kama wauguzi kunufaika.

Hawa wakaboresha mazingira yaliyochochea zaidi ugonjwa wa kijana. Wakakikana kiapo (Azimio la Arusha) cha udaktari. Kwa upande wa tatu, hata wale wauguzi wazuri waliokuwapo wakati mgonjwa Tanzania akiwa mtoto au kijana mdogo, nao wakaungana na matabibu wapya kumhujumu mgonjwa!

Kuna wachache kati ya matabibu wa zamani waliokasirishwa na hali ya mgonjwa na tabia ya matabibu wapya lakini nao kwa kuwa sasa hawamthamini mgonjwa kwa kiwango kilekile cha utoto na ujana wake, wakaamua hata kuzira kumtembelea mgonjwa hospitali!
Hawathubutu hata kuwaambia matabibu wapya jamani rudisheni kiapo cha madaktari! Sisi tulikitumia kiapo hicho na afya ya mgonjwa ilineemeka. Waapi, wamebaki kuzungumzia tabia chafu za matabibu kama kuiba mashuka ya wagonjwa tena kwa unyonge! Simameni, muenzini Mganga Mkuu wa awali kwa kupigana hata kwa damu zenu kurudisha kiapo cha madaktari!

Mgonjwa alipokuwa mahututi, zikazuka kelele, jamani mgonjwa Tanzania anakaribia kukata roho! Kelele hizi zikapigwa hata na matabibu wasaidizi ambao kwa kiwango kikubwa wananufaika na hali ya mgonjwa! Hawa wako katika jengo kuubwa. Wakiugua wanakwenda hospitali za nchi nyingine! Ubovu wa hospitali ni raha yao!

Kelele za wanafiki hawa zikaambatana na vitisho, Mganga Mkuu Msaidizi na Madaktari Waandamizi wameshindwa kazi, wafukuzwe! Ndugu wanaomtegemea mgonjwa nao wakadakia kwa nguvu na vitisho, ‘ndugu yetu anakufa'! ‘ndugu yetu anakufa'! ‘akifa mtamla nyama'!

Vilio na vitisho hivi vikamshtua Mganga Mkuu; naye akasema ‘basi kama ni suala la matabibu, nitawaondosha, lakini si wote'.
Sasa hapa ndo kuna tatizo; maradhi ya mgonjwa Tanzania hayakusababishwa na matabibu peke yao. Ni tatizo la jamii na mfumo wa utawala. Ndugu wa mgonjwa wanahusika pia kwa kuwa walimwona kipenzi chao ana dalili zote za ugonjwa lakini wakakaa kimya bila kumweleza. Hata wale wachache waliomueleza waliishia hapo. Hawakumpeleka hospitali. Wale wachache zaidi waliompeleka hospitali walimpeleka kusiko; wakampeleka kwenye kikombe cha babu Loliondo! Hakupona!

Kwa upande wa utabibu nako hawawezi kukwepa lawama. Mgonjwa yuko ICU wao wamebadili wauguzi wakitumai mgonjwa atapona! Tatizo si utaalamu wa matabibu peke yake, kuna suala la vifaa, taratibu za kazi ya utabibu, mtaala katika chuo cha utabibu, elimu ya afya kwa mgonjwa na ndugu zake, n.k. Ni mkusanyiko wa matatizo lukuki!

Kubadili matabibu peke yake hakutamponyesha mgonjwa! Kuwaacha matabibu walio vurunda katika chumba cha mgonjwa ni kuharakisha mauti ya mgonjwa Tanzania! Kuwaacha matabibu waliofukuzwa ICU waondoke na mikasi, bandeji, ada za wagonjwa, mablanketi ya hospitali, magari ya wagonjwa, n.k. bila kuwataka angalau warudishe ni sawa na kuwaambia matabibu wapya kwamba nao wanaweza kurejea makosa ya watangulizi wao bila hofu yoyote! Ni kulea tatizo!

Ndugu wa mgonjwa Tanzania, kuanzia sasa wanapaswa kuacha tabia ya kumwonea haya mgonjwa na matabibu wake. Lazima wajifunze namna ya kutambua magonjwa kabla hayajawa sugu kuliko kusubiri hadi ndugu yao anapokaribia kukata roho ndipo waanze kupiga mayowe. Lazima wawe na ujasiri wa kumwambia Mganga Mkuu, Mganga Mkuu Msaidizi na Matabibu Wasaidizi hivi mfanyavyo sivyo! Na la muhimu kabisa wajifunze namna ya kubadili mfumo mzima wa tiba hata ikibidi kumtosa Mganga Mkuu na wasaidizi wake.
Kwa jinsi Mwenyezi alivyo na mapenzi na wagonjwa, ametupa fursa ya kuandika kitabu cha Huduma ya afya upya! Baadhi wa ndugu wa mgonjwa waligundua kitambo kuwa kitabu ndilo chimbuko la magonjwa. Tatizo ni kwamba walikuwa wanaomba badala ya kulazimisha kitabu kiandikwe upya. Walioharibu kitabu wakajifanya hawaelewi somo! Mungu si Athumani au Richadi! Walioharibu kitabu wamekubali kiandikwe upya. Mungu ashukuriwe!

Kitabu kipya cha namna ya kumtibu mgonjwa Tanzania kimeanza kuandikwa. Nasikia kitabu hiki kitaitwa KATIBA (au kilistahili kuitwa KUTIBU?). Naona kingeitwa KITABU CHA AFYA YA NDUGU YETU TANZANIA! Ndugu wa huyu jamaa aitwaye Tanzania hawapaswi kupuuzia wajibu wao katika uandishi wa kitabu hiki muhimu.

Humu ndipo itakapoanishwa hospitali ziwe ngapi, za ubora gani, za umbali gani toka makazi yetu, kina nani wasomee utabibu, matabibu wahitimu wafanyaje kazi katika hospitali zetu, vifaa gani vinunuliwe kwa ajili ya matibabu ya Tanzania na nduguze, namna gani huduma za afya ziboreshwe ili tusiingie gharama za kupeleka wagonjwa India au kuparamia tiba zitokanazo na ndoto za mmoja wa wana ndugu, matabibu wakikiuka maadili ya kazi zao tuwashughulikie kwa utaratibu gani, n.k

Humo pia kutaandikwa kwa mistari myekundu ni magonjwa gani yatapewa kipaumbile; kuna UKIMWI (Ufisadi), Kansa (Rushwa), Malaria (Uvunjaji wa haki za binadamu), Matende (mamlaka ya utu mungu), homa (tume ya uchaguzi isiyo huru), mafua (waheshimiwa wasiojiheshimu), n.k. Na jukumu kubwa zaidi ni kuhakikisha kitabu kinaandikwa uzuri ili kiweze kutibu magonjwa; mkiacha wauguzi walioharibu kitabu cha awali waandike watakayo wao itakuwa balaa kwetu sote na mgonjwa TANZANIA.

Kitabu hiki kikiandikwa vibaya mgonjwa tunayempenda na kumtegemea atakufa! Hapo ndio itakuwa mwisho wa wimbo wa ‘mgonjwa huyu mstaarabu, toka aingie hospitali amelala tuli, hana vurugu' ‘Na hata nduguze nao wapoole, wao kazi kuleta uji kwa mgonjwa hata kama hospitali ilipaswa kumpa mgonjwa lishe bora'!

Ndugu wa mpendwa wetu Tanzania watakaopuuza wajibu wao katika zoezi la kuandika kitabu hiki hawatakuwa na haki hapo mbele ya safari ya kupiga mayowe kwamba ndugu yao Tanzania anachungulia kaburi! Na wakija msibani wanapaswa kutimuliwa kwani hawatakuwa na tofauti na wanga!

Wanajifanya wanakusikitikia kumbe ndo waliomuua marehemu!
Ujumbe kwa Mganga Mkuu: Mgonjwa Tanzania bado hajapona, nenda mbali zaidi. Wasaidie ndugu wa mgonjwa kushiriki na baadaye kupata kitabu bora kabisa kwa afya zao na za ndugu yao aitwaye TANZANIA. Kwa kipindi hiki cha mpito, tembelea hospitali mara kwa mara kwani hata hao Matabibu wapya na wale wa zamani waweza kumuua kabisa mgonjwa TANZANIA!

Kwa minajili ya kuwatia hofu, waadhibu matabibu uliowatimua toka chumba cha ICU hivi karibuni. Kwa kuanzia, wanyang'anye, mikasi, bandeji, magari ya wagonjwa mashuka ya hospitali waliyojitwalia kinyume cha sheria kabla ya kuwakabidhi kwa vyombo vya sheria.
Mtu mzima akikutwa na mke wa mtu gesti tena ya uchochoroni kuna haja ya kusibiri uchunguzi? Huyu si wakupigwa ‘Tanganyika jeki' yeye na mshirika wake watiwe pingu na kuelekezwa rumande ili siku hiyo hiyo au kesho yake wapandishwe kwa pilato? Unawaachia waende nyumbani wasubiri kuchunguzwa? Mama wee!

Pili, waondoe waganga wasaidizi wote ambao bado wako ICU, wodi ya wazazi, chumba cha sindano, chumba cha kufungia vidonda, chuo cha matabibu na sehemu nyinginezo ambao walibainika kushiriki uharamia huu dhidi ya mgonjwa.
Kinyume cha hapo, kitabu kitakamilika lakini mgonjwa atakuwa amekwisha kufa. Kadhalika, wagonjwa watarajiwa nao hawatakuwa salama. Ukoo mzima wa ndugu Tanzania utaisha.

Kumbuka kelele za ndugu zake kwamba AKIFA MTAMLA NYAMA! Hii ilikuwa kabla hujabadili baadhi ya matabibu, je, akifa yeye na ndugu zake baada ya wewe Mganga Mkuu kuwahakikishia umepata dawa ya ugonjwa wa ndugu yao na wao? Itakuwa balaa Daktari wangu!

Tatu, ili ukumbukwe milele, wasaidie ndugu wa mgonjwa na mgonjwa mwenyewe kitabu kiandikwe kwa uadilifu na nia njema.
Kitabu kikiandikwa vibaya utaingia katika kumbukumbu kama mganga mkuu aliyehalalisha mateso kwa mgonjwa TANZANIA na nduguze. Katika hili usiwasikilize wabetuaji wa mashuka, bandeji, dawa, mikasi, na magari ya wagonjwa!

Hawa ni watu waovu kabisa. Watazame usoni bila kupepesa kope; waambie kuanzia sasa ACHENI KUWAIBIA WAGONJWA! Nina hakika watatahayari na kukuacha uwapatie wagonjwa wako kitabu chema. Mungu akujaze nia njema na akutangulie katika zoezi hili Mganga Mkuu.


Yahya Msangi mwandishi wa makala hii
 
Back
Top Bottom