SoC01 Mabadiliko ya hali ya hewa na Kilimo cha Umwagiliaji

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Jun 3, 2021
544
558
Dunia ilipofikia hivi sasa kilimo cha kutegemea mvua ambazo kwa mwaka huja mara moja au mara mbili kimepitwa na wakati na kinaonekana kutokua na tija kwa jamii. Jambo ambalo limeilazimu jamii kuhamia kwenye kilimo cha umwagiliaji. Na hii ni matokeo ya kuongezeka kwa shuguli za binadamu ambazo zimesababisha kuwe na mabadiliko ya hali ya hewa na kutotulizana kwa majira ya mwaka katika hali moja.

Mabadiliko ya hali ya hewa na majira ya mwaka yamekua ni changamoto kubwa kwa wakulima wanaotegemea mvua pekee kunywesheleza mazao yao. Lakini pia ongezeko la mahitaji ya vyakula vya shamba kwa kipindi chote cha mwaka mzima kimewasukuma wakulima wengi kujikita kwenye kilimo cha bustani ambacho kwa kiasi kikubwa huendeshwa kwa umwagiliji ili waweze kukidhi mahitaji ya soko. Maendeleo ya viwanda na ongezeko kubwa la viwanda ambavyo malighafi zake hutoka shamba yameongeza mahitaji ya wakulima kuhamia katika kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi hizo kwa wakati.

Kwa nchi zetu za daraja la tatu kilimo ndio uti wa mgongo, bali kilimo kimeajiri watu wengi sana hasa vijana wenye elimu na wasio na elimu. Kubwa zaidi kilimo kina nafasi kubwa katika kukuza pato la mtu mmoja mmoja na pato la taifa kwa ujumla. Watu wengi wanaojishugulisha katika shuguli za kibiashara na hata wafanyakazi wa serikali na wale wa kwenye sekta binafsi wamejiingiza katika kilimo, na pale ambapo biashara zao zinapozorota au mishahara yao inapochelewa kilimo huwainua. Kwa hapa kwetu Tanzania tunaona na kushuhudia hata viongozi na wanasiasa wakubwa wakimiliki mashamba makubwa na kuajiri kundi kubwa la nguvu kazi kuendeleza sekta ya kilimo. Hivyo tukisema kilimo ndio sekta mama hatukosei.

Katika nchi zilizoendelea walishajiingiza kwenye kilimo cha umwagiliaji takribani miongo mitatu iliyopita au zaidi. Lakini kwa nchi zetu zinazoendelea ni hivi karibuni katika miaka ya milenia ya pili ilipoanza ndio tumeingia katika kilimo cha umwagiliaji. Mbali na gharama kuwa kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji, lakini ndio kilimo chenye tija na kimekua tegemezi kwa wakulima wa dunia ya sasa. Mashamba yaliyo pembezoni mwa mito ya kudumu inayotiririsha maji yake kwenye mabonde hulimwa kipindi chote cha mwaka mzima. Na katika maeneo ambayo vyanzo vya maji viko mbali au sio vya kudumu wakulima hutumia njia mbadala za kurina na kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji. Na kwa wale wenye nguvu za kiuchumi huyavuta maji kutoka huko yalipo mpaka shambani kwa kutumia mashine.

Sambamba na faida kemkem, kilimo cha umwagiliagi bado kimekua na changamoto hasa kwa wakulima wadogo. Yafuatayo ni miongoni mwa mambo yanayowakwamisha wakulima wadogo wasifikie malengo;-

  1. Ukosefu wa pembejeo za kutosha
    Kilimo cha umwagiliaji ni kilimo cha kisasa, kinacho hitaji ufuatiliaji wa hali ya juu. Matumizi ya viuatilifu na madawa mbalimbali dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa rejareja ya mimea ni jambo la kawaida. Hivyo kufanya kilimo hicho kuwa ni cha gharama kubwa kama nilivyoashiria hapo awali. Hivyo wakulima wengi hasa wakulima wadogo hushindwa kugharamia mashamba yao jambo linalopelekea kupungua kwa uzalishaji.

  2. Ushindani katika masoko
    Kwa kuwa kila mkulima amejiingiza katika kilimo cha umwagiliaji, na kwa bahati mbaya wengi wao hulima mazao ya aina moja; unafika wakati wa mavuno bidhaa/mazao yao yanafurika sokoni jambo linalopelekea kushuka kwa bei na kuwalazimu wakulima kuuza mazao yao kwa hasara. Lakini pia kutokana na kushindwa kuhudumia mazao yao yakiwa shambani wakulima hao huvuna mazoa yasiyo na ubora na kufanya yakakosa soko na kuuzwa kwa bei isiyo na maslahi.

  3. Sera za serikali iliyopo madarakani
    Igawa kilimo ndio sekta yenye kutegemewa, lakini kwa wakati mwingine serikali hushindwa kuwa na sera madhubuti za kuendeleza sekta hiyo. Bali hata katika bajeti za serikali kilimo hakipewi kipaumbele, mwisho wa siku hata wakulima wanakosa ari ya kufanya kazi na kupelekea kupungua kwa uzalishaji.

  4. Miundombinu dhaifu
    Kwa kawaida mashamba makubwa huwekwa huko msituni mbali na miji ili kuepusha mambo mengi yanayoweza kuathiri uzalishaji. Hata hivyo kuna changamoto ya miundombinu kufika katika maeneo hayo ya mashamba. Barabara za kuwafikisha watu shambani sio za uhakika, hivyo kufanya zoezi la kusafirisha mazao kuja viwandani au kwenda sokoni kukwama. Lakini pia miundombinu ya nishati ya umeme kufikia mashamba ni changamoto nyingine. Kwa kilimo cha umwagiliaji nishati ya umeme ni muhimu sana katika kuendesha mashine za umwagiliaji. Wakulima wadogo hawawezi kugharamia vyanzo binafsi vya nishati, hivyo kuwarudisha nyuma katika kufikia malengo yao ya kufanya mapinduzi ya kijani.
Changamoto hizi na zingine nyingi zinarudisha nyuma jitihada za wakulima wetu kufikia malengo yao ya kuwa na matokeo makubwa.

Hali ya hewa itaendelea kubadilika kadri siku zinavyozidi kusonga kwa sababu mwanadamu anaendelea kuvumbua vitu vipya kila siku ambavyo ndio vichocheo vikubwa katika kuathiri mabadiliko ya hali ya hewa, hali ya nchi na uoto wa asili. Hivyo haiwezekani kaendelea kubakia katika kilimo cha kutegemea mvua pekee. Kilimo cha umwagiliaji ndio kinaanza kuwa kilimo mama katika dunia ya sasa. Hatuna budi kukipa kipaumbele, kupanga mipango mikubwa na midogo, ya muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinapiga hatua katika kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo.

MAPENDEKEZO

Wito wangu kwa serikali kupitia wizara husika, iendelee kuwasaidia wakulima wadogo katika kuwapatia pembejeo kwa gharama nafuu au hata kwa kuwakopesha. Serikali iweke mipango ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kutoa elimu kwa wakulima ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha. Serikali isimamie na ihamasishe raia kuhifadhi vyanzo vya maji na ziwekwe sheria kali kwa wanaoharibu vyanzo vyetu vya maji ambavyo ndio tegemeo kwa wakulima wa kilimo cha umwagiliaji.

Lakini pia kwa taasisi za fedha na benki, watoe mikopo yenye masharti mepesi kwa wakulima ili kuwasaidia katika kutatua mahitaji yao ya shamba. Kadhalika mashirika na taasisi za wahisani na wao wawaangalie wakulima ili wawape misaada ya mbegu, pembejeo, zana, elimu, nk.

Nawashauri wakulima wadogo wadogo waanzishe vikundi kwani kupitia vikundi ndio inakua rahisi kupata misaada kutoka kwa wahisani, na hata serikalini. Lakini pia vikundi hivyo vinaweza kutumika kama saccos wakulima wakawa wanaweka fedha na kukopeshana kwa ajili ya kuwawezesha kuhudumia mashamba yao.

Kwa wabunge na wanasiasa wengine wasio wabunge, kumbukeni katika majimbo yenu idadi kubwa ya wapiga kura wenu ni wakulima wadogo wadogo. Ambao wanahitaji msaada mkubwa sana kutoka kwenu kuwasemea kwa serikali yao. Ingawa kuna vyama vya wakulima lakini ninyi mna nafasi kubwa sana katika kufikisha kero zao mahala husika. Lakini pia mnapofanya ziara majimboni mwenu mkumbuke kukutana na wakulima ili muweze kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zao.



Imeandikwa na;-

DustBin
 
Back
Top Bottom