Maaskofu Wakatoliki wataka Viongozi kuondolewa kinga ya kushtakiwa

Lady Whistledown

JF-Expert Member
Aug 2, 2021
1,023
1,609
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeshauri kuondolewa kinga ya kushtakiwa kwa viongozi wa Serikali ili kutoa haki sawa kwa Watanzania wote chini ya Katiba na matakwa ya Mwenyezi Mungu ili waweze kushtakiwa wanapokosea.

Baraza hilo limesema Ibara ya 12 (1) ya Katiba inasema binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, huku kifungu cha 13(1) kinafafanua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

Hata hivyo, Ibara ya 46 (2) kinasema haitaruhusiwa kufungua shauri dhidi ya Rais na kutoa masharti kadhaa.


TEC miongoni mwa taasisi za dini zilizotoa mapendekezo yake kwa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Mfumo wa Haki Jinai jana jijini Dar es Salaam.

Taasisi nyingine zilizotoa mapendekezo kwenye maeneo tofauti ni; Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).

Mara baada ya kutoka kuwasilisha mapendekezo, Dk Camilius Kassala, mkurugenzi wa hadhi ya utu wa binadamu, idara ya haki, amani na uadilifu wa TEC alizungumza na waandishi wa habari akifafanua suala la kinga kwa viongozi, likiwa miongoni mwa hoja nne walizoziwasilisha.

“Ndiyo maana kuna vuguvugu la Katiba Mpya ili hiyo kinga iondolewe, watu wanaelewa sasa binadamu wote tuko sawa, uwe Rais, bosi, tajiri au kamanda wa polisi wote tuko sawa,” alisema Dk Kassala.

Jambo jingine ni kuhusu mageuzi ya mfumo wa kisheria yaliyotokana na utawala wa kikoloni, uzito wa makosa uendane na adhabu za mahakama, ikiwamo utozaji wa faini ndogo katika ngazi za mahakama za chini ili kupunguza mianya ya rushwa kwa wananchi.

Vilevile, maaskofu hao walishauri kuimarisha mfumo utakaowaweka huru wanataaluma katika utekelezaji wa majukumu yao au wakati wa kuwajibishana bila kuingiliwa na mkono wa Serikali.

“Kwa kuwa Serikali inaundwa na wanasiasa, wanasiasa wana masilahi yao kwa sababu wanataka washinde uchaguzi unaofuata. Kwa hiyo watawatumia wanataaluma kwa masilahi yao kisiasa ili washinde chaguzi zijazo, matokeo yake taaluma zinatumikia siasa, badala ya siasa kutumikia taaluma,” alisema Dk Kassala.

Alisema haki ni msingi wa hadhi ya utu wa kila mwanadamu, hivyo mfumo wa haki jinai unatakiwa kuimarika kwa kuwa kukiuka msingi huo ni chukizo mbele za Mungu.

Hoja hiyo ya TEC kuhusu kuondolewa kinga imeungwa mkono na baadhi ya mawakili waliozungumza na gazeti hili, akiwemo, rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk Rugelemeza Nshala aliyesema, “mimi ni muumini wa usawa na watu wote wanapaswa kuwa na haki sawa kisheria.”

Vivyo hivyo, Wakili Patience Mlowe alisema ni Afrika pekee ndiko viongozi hutukuzwa mithili ya miungu watu, lakini mambo yapo tofauti kwingineko.

Alisema katika mataifa mengine nje ya Afrika viongozi huchukuliwa hatua kila wanapokosea, akitolea mfano Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson aliyeshtakiwa kwa kukiuka sheria wakati wa Uviko-19.

“Hiyo demokrasia tunayoiimba asili yake ni mataifa yaliyoendelea, sasa sisi tunatekeleza demokrasia gani kama tunawafanya viongozi kuwa miungu watu,” alihoji.

Kwa mujibu wa Mlowe, ili kuwa na kiongozi mwadilifu lazima kuwepo na mazingira yanayomjengea hofu ya kutenda kosa akijua kuna hatua atakazochukuliwa.

“Anakwenda kujilimbikizia mali si kutumikia watu, wakiondolewa kinga watakuwa na hofu maana watajua wakitenda kosa watachukuliwa hatua,” alisema.

Mwingine aliyeunga mkono ni mwanasheria nguli na rais wa zamani TLS, Fatma Karume aliyesema kwa kuwa hakuna mwananchi aliye juu ya sheria, hata Rais anapaswa kuondolewa kinga ili kuwe na usawa.

“Rais ni mwananchi kama wengine, hawezi kuwa juu ya sheria, anapokosea anapaswa kuwa chini ya sheria na achukuliwe hatua kama wengine,” alisema.

Akifafanua hilo, Wakili Fulgence Massawe alisema kabla ya marekebisho ya sheria, Rais alikuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya jinai na kwamba mabadililo hayo yaliondoa dhana ya uwajibikaji kwa viongozi hao.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom