Maaskofu Katoliki watoa waraka mwingine 2010

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
*WATAKA VIONGOZI WALA RUSHWA WASICHAGULIWE, VYOMBO VYA DOLA KUTOTUMIA NGUVU KUPITA KIASI

Exuper Kachenje
Mwananchi

Wednesday, 07 July 2010

BARAZA la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), limetoa waraka wa Uchaguzi Mkuu huku likiionya serikali na vyombo vyake kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na kutaka vitumike kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.

TEC imetoa waraka huo ikiwa ni miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 31 mwaka huu. Mwaka jana, Kanisa hilo lilitoa ilaani ya Uchaguzi kwa waumini wake jambo ambalo lilipingwa vikali na serikali.

Waraka huo unafuatia mkutano wake mkuu wa 63 uliomalizika jana makao makuu ya TEC Kurasini jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha maaskofu wote 33 wa Kanisa hilo nchini.

Mbali na onyo hilo kwa serikali na vyombo ya dola, waraka huo umevionya vyama na wagombea wa nafasi mbalimbali kuheshimu kanuni za uchaguzi pamoja na kuhimiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) kujijengea imani na heshima kwa kusimamia uchaguzi kwa kuheshimu katiba na kanuni ili uwe wazi, huru, haki na usalama.

"Kwa hiyo sisi kama kadri ya nafasi yetu kama viongozi wa dini na raia wa nchi yetu ya Tanzania tunatambua kuwa tuna wajibu na haki ya kusema yafuatayo juu ya uchaguzi ujao:

Katika waraka huo, maaskofu hao walisema kuwa vyombo vya dola ni muhimu katika kulinda usalama hasa wakati wa kipindi cha uchaguzi, pamoja na kuwa mara kadhaa imetokea kwamba nguvu kupita kiasi zimetumika na vyombo hivyo kuliko inavyohitajika:

"Tunaviomba vyombo vya dola vitumie nguvu zake kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi, kwa kuzingatia maadili ya kazi yao pasipo kuegemea upande wowote Ili uchaguzi uwe kweli huru", ilisema sehemu ya waraka huo uliosainiwa na maaskofu wote 33 wa TEC wakiongozwa na Rais wao Askofu Yuda Thadei Ruwa'ichi wa Jimbo Katoliki Dodoma.

Waraka huo unawaelekeza wapigakura waliojiandikisha kutimiza wajibu na haki yao ya kuchagua viiongozi kwa umakini, kuwahoji na kuwapima wagombea udhati wa nia yao kwa kufuata vigezo vya hadhi ya utu wa mwanadamu na tunu za kimaadili.

"Kamwe wasimchague mtu kwa shinikizo, kwa msingi ya ukabila, dini, rangi jinsia, wala sababu ya takrima au rushwa", ulionya waraka huo.

Waraka huo ulibainisha kuwa suala la rushwa limejitokeza karibu katika kila uchaguzi, huku jambo baya zaidi likiwa baadhi ya wananchi kujenga tabia kuendesha maisha yao kwa kutegemea rushwa wanazopewa na wanasiasa.

Kutokana na hilo, waraka uliainisha kuwa uchaguzi unapofika na hata baada ya uchaguzi jambo linalosababisha baadhi ya wanasiasa kuendelea kubaki madarakani pamoja na kupoteza mvuto na ushawishi wa kiasiasa, uwezo hata sifa za uongozi.

Baraza la TEC lililaani kujitokeza kwa hali hiyo katika chaguzi zilizopita na baadhi ya watu kudaiwa kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura likieleza kuwa kuuza kura ni kusababisha utawala mbaya, kuuza uhuru na usaliti.

Kuhusu vurugu kuchafuana kwa baadhi ya wagombea TEC imesema vitendo hivyo vilikuwepo katika chaguzi ndogo zilizopita huku ikiviomba vyama vya siasa na wagombea kunadi sera zao zinazoweza kushawishi wagombea na siyo kushindana kwa maneno ya kashfa na matusi yanayosababisha uvunjifu wa amani.

Aidha, waraka huo wa TEC umezungumzia pia baadhi ya vyama na wagombea kukosa ukomavu wa kisiasa, unyofu na unyenyekevu wa kukubali matokeo hasa ya kushindwa katika uchaguzi ukiwataka watakaoshindwa kihalali kukubali matokeo na kuungana na wengine katika kujenga nchi.

"Tunahimiza vyama na wagombea watakaokuwa wameshindwa kihalali kukubali matokeo ya uchaguzi na kuungana na wengine katika kuijenga nchi,"ilieleza sehemu ya waraka huo huku ukiendelea kufafanua kuwa;

"Tunawaalika wagombea ambao wanadhani hawakushindwa katika uchaguzi kwa njia ya haki, watafute haki zao kwa namna inayokubalika kisheria, kuliko kuhamasisha vurugu na ghasia ambazo matokeo yake ni kusababisha uharibifu wa mali na pengine kupoteza maisha ya watu bila sababu za msingi."

Hata hivyo, waraka huo ulieleza kuwa mara nyingi vurugu zinazofanywa na vyama na wagombea mbalimbali au kukataa matokeo kusababishwa na hisia kwamba kanuni mbalimbali za uchaguzi kutoheshimiwa au kukosa uwazi katika uchaguzi.

TEC imetumia waraka huo wenye kurasa tano kuwataka viongozi wenzao wa dini mbalimbali kutoegemea upande wowote wala kushika uelekeo wa kundi lolote, badala yake kuwa sauti ya wasio na sauti wenye kupima mambo kwa ukomavu, upeo haki na ukweli bila kuathiri uadilifu wao huku likiwataka wananchi kuombea Uchaguzi Mkuu ili wapatikane viongozi wenye kujali maslahi ya wote na kujenga jamii yenye upendo, umoja, haki, amani na maendeleo ya kweli.

Hii si mara ya kwanza kwa Kanisa Katoliki nchini kutoa ujumbe kuelekea Uchaguzi Mkuu. Mwaka 2005 na miaka ya nyuma limekiuwa likifanya hivyo ambapo kwa mwaka huu waraka huo umebeba wazo lisemalo "Kanisa katika Tanzania na Huduma ya upatanisho, Haki na Amani.

Mwaka uliopita kanisa hilo kupitia chama chake cha wanataaluma Wakatoliki lilitoa ilani ya uchaguzi ambao ulivuta hisia za wengi na kuzua mjadala mzito kwa watu wa kada mbalimbali ikiwemo wabunge.

Wakati huo huo Festo Polea na Tumsifu Sanga wanaripoti kuwa Umoja wa Wakristo Tanzania (CCT) kwa kushirikisha masheikh na wanaharakati mbalimbali wa kutetea sekta ya madini nchini wanatarajia kutoa waraka elekezi kwa wananchi utakaoelekeza jinsi wawekezaji wa madini wanavyoinyonya serikali na kusababisha wananchi wake kutonufaika na migodi hiyo.

Waraka huo unatarajiwa kutolewa kabla ya uchaguzi ili wananchi waweze kutambua uwazi jinsi madini yao yanavyoibiwa na wahisani na kutoweza kuinufaisha serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa Umoja huo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Diyosisi ya Kaskazini Mashariki Dk Stephen Munga alisema waraka huo utaeleza taarifa zilizowazi kuhusu kiasi kinachochukuliwa na wawekezaji na kukipeleka nchini kwao huku serikali yetu ikikosa kunufaika.

Alisema waraka huo utaweka wazi mambo yote ya madini kuanzia mwaka 2002 hadi 2010, huku akidai kuwa katika waraka huo wataeleza jinsi kila kampuni inatoa kiasi gani katika kodi na inapokea kiasi gani kwa kuwa nyingi zinadanganya.

Habari zaidi soma=>Waraka: Kanisa Katoliki laandaa waumini uchaguzi 2010
 
Kuna waliloliona ila wanashindwa kusema waziwazi. Naona wameamua kwenda kwa mwendo wa waraka tuuuu
 
Kuna waliloliona ila wanashindwa kusema waziwazi. Naona wameamua kwenda kwa mwendo wa waraka tuuuu

...bora wabakie hivyo hivyo na kulinda balance iliyopo kati ya siasa na uumini, kusije kukatokea mambo yaliyomkuta Gen. David D. McKiernan wa jeshi la Marekani!!
 
wamekumbushia tu waliyozoea kutamka kila uchaguzi unapokaribia!
 
No one cares. Foreign forces should not be the deciding factor in Tanzania otherwise tutatawaliwa tuu. Watu wanajua mafisadi basi wasiwape kura. Its simple. When you let someone else do ur thinking for u.. U invite stupidity and with it colonialism. Fact
 
TEC mulikuwa wapi kipindi cha Mkapa?Maana madini yamechotwa sana kipindi hicho bila kelele...au ndio Kikwete kaleta uhuru wa maoni
Nina shaka sana uelekeo utabadilika 2015...CCM ikaanza kuwa tamu tena
 
Mwaka 2009 kulitokea mambo mawili makuu. Mwezi July Kanisa Katoliki kupitia wasomi wake yaani CPT lilitoa waraka uitwao ILANI KUELEKEA UCHAGUZI WA 2010.

Waraka ule ulipingwa sana na hadi Kingunge Ngombale Mwiru akaitisha press conference kukemea kwamba Kanisa Katoliki si chama cha siasa.

Ule waraka ulipomfikia askofu Kakobe, kama kawaida yake akaamua kuupeleka kanisani kwake na kuonyesha alivyouchukia akauchanachana mbele ya waumini wa kanisa lake.

Askofu msaidizi wa D'Salaam, Method KIlaini alipoulizwa kuhusu kitendo cha Kakobe alijibu "mimi siwezi kujibizana na mtu (Kakobe) ambaye hata sijui uaskofu wake kapewa na nani".

Hivyo ndivyo ilovyokuwa. Suala la waraka ule liliendelea hadikwenye kikao cha Halmashauri kuu ya CCM (NEC) kikaweka azimio kwamba nyaraka zote za makanisa zipitie kwanza serikalini. Ikalelekea kabisa ndivyo itakavyokuwa.

Hapa sasa ninakuja kwenye jambo la pili la mwaka huohuo 2009. Baada ya azimio hilo la NEC kikatokea kifo cha askofu Anthony Mayala wa Jimbo Katoliki la Mwanza. Wakati huo nikiwa bado niko Tanzania nilihudhuria mazishi yake kama sijasahau ilikuwa ni Agosti 26, 2009.

Kwenye mazishi yake misa iliongozwa na Polycarp Cardinali Pengo. Nakumbuka kuwaona Benjamin MKapa na ndiye alikuwa wa kwanza kupokea ekarist akifuatiwa na akina Chenge. Nakumbuka William Ngeleja waziri wa Mdini alikuwepo.

Rais Jakaya Kikwete alichelewa kidogo kufika na akakuta mambo mengi yameshachukua nafasi.

Kilichotokea ni nini kwenye misa ile. Kilichotokea ni kwamba kwenye mahubiri Polycarp Cardinali Pengo alitoa mahubiri makali ambavyo haijawahi kutokea. Kwa sababu ilishasikika kwamba nyaraka zote za mtamko ya maaskofu yatakuwa yanapitia kwanza serikalini ndipo yaende kwa waumini Polycarp Cardinali Pengo akakemea kwa vikali mkakati huo.

Polycarp Cardinali Pengo alitumia maneno haya "nchi za wakomunisti zilikuwa na kawaida kutaka nyaraka za maaskofu zipiti kwanza serikalini ndipo zisomwe. Je, Tanzania tunakoelekea hakuna tofauti na walichofanya wakomunisti."

Pengo akaendelea kuikemea serikali akisema "msiwafundishe maaskofu kuandika barua za kichungaji kwa waumini wao".

Kisha akageukiwa maaaskofu wenzake ambapo walikuwepo kama zaidi ya 25 akisema "Nanyi maaskofu, kama italazimika eti kupelekea nyaraka kwanza serikalini kana kwamba hamkutumwa na Mungu mmetumwa na serikali kuhubiri waumini wenu basi ni bora kutoandika nyaraka au kuacha kazi mliyotumwa na Mungu".

Pengo akamalizia na kusema "maaskofu hatutakubali kufundishwa cha kuwahubiria waumini wetu".

Kwa sababu Kingunge alilishabikia sana lile jambo Pengo akampiga dongo kwa kusema "wakomunisti tunafahamu kwamba hawana dini afadhali hata mabepari wanaamini kwamba kuna Mungu".

Kwa ujumla Pengo hakuwahi kuwa mkali kama siku ile.

Baada ya siku mbili Kakobe yuleyule aliyeuchana ule waraka akaibuka tena na kusema Polycarp Cardinal Pengo amemdharirisha Rais Jakaya Kikwete kwa kusema maneno yale mbele yake. Kanisa Katoliki lote nchini lilikaa kimya na hakuna aliyelumbana na Kakobe.

Zipo thread humu nimebishana na watu kuhusu Kakobe na nilichobishana nao ni jinsi wanavyoipnda hoja ya Kakobe wakati kuna hoja kama hii ya kumponda Kakobe kwa kumkumbusha.

Kakobe asione eti maaskofu wengine wamekaa kimya akumbuke kwamba wakati wenzake wanapambana mwaka 2009 yeye alikuwa wa kwanza kuchanachana nyaraka na kumkembehi Pengo kama nilivyokumbusha.

Hivyo watu wanaosema kwamba kuna mahala Kakobe kanaswa ingawa ni ngumu kuamini au kuthibitisha lakini kutokana na yeye kuwasaliti maaskofu wenzake ile mwaka 2009 ni wazi maaskofu hasa wa kanisa katoliki hawawezi kujitumbukiza katika vita aliyoianzisha.

Wasalaam
 
Ccm waliamini wakiimaliza chadema na wakina lissu basi hamna wakosoaji ndo kwanza wanaibuka wapya mjiandae kisaikolojia huwezi kuongoza watu zaid ya million 40 kama familia yako kila mmoja anawazo lake tofaut
 
Ccm waliamini wakiimaliza chadema na wakina lissu basi hamna wakosoaji ndo kwanza wanaibuka wapya mjiandae kisaikolojia huwezi kuongoza watu zaid ya million 40 kama familia yako kila mmoja anawazo lake tofaut
Na wala sio wagombeaji, ndo kinachowasumbua
 
Kwa Hiyo mkosoaji mliyemtuma huko CDM ni Likobe?
Ccm waliamini wakiimaliza chadema na wakina lissu basi hamna wakosoaji ndo kwanza wanaibuka wapya mjiandae kisaikolojia huwezi kuongoza watu zaid ya million 40 kama familia yako kila mmoja anawazo lake tofaut
 
Back
Top Bottom