Maaskofu Katoliki wamtaka Rais Magufuli kutumia busara

SeriaJr TW

JF-Expert Member
Oct 21, 2012
246
224
Taarifa iliyopewa uzito katika ukurasa wa mbele gazeti la Mtanzania la leo Juni 8 2016 linaelezea ushauri wa viongozi wa dini kwa Rais Magufuli katika namna nzuri ya kuongoza Serikali yake na kufanya maamuzi kwa busara.

1465358158579.jpg

========

Pg-1-300x198.jpg

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

BARAZA la Maaskofu Tanzania (TEC), limemtaka Rais Dk. John Magufuli atende haki na atumie busara na akili anapochukua hatua mbalimbali za utendaji zikiwamo za kupambana na ufisadi.

Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini kwa niaba ya TEC, alipozungumza na waandishi wa habari Mwanza jana.

Askofu Kilaini na wenzake wako jijini hapa kuhudhuria kongamano la tatu la taifa la Ekaristi Takatifu litakalofanyika kuanzia Juni 10 hadi 11 mwaka huu.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu utawala wa Rais Magufuli na matukio yanayojitokeza nchini, Askofu Kilaini alisema taifa lipo katika hofu.

Alisema ni kutokana na matukio ya mauaji yanayofanywa na watu wachache waliokosa hofu ya Mungu na akataka matukio hayo yashughulikiwe kwa uzito unaostahili.

Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho alisema TEC haiwezi kutoa tathmini au kutoa maoni ya uongozi wa Rais Magufuli kwa sasa kwa sababu ni mapema mno.

“Bado tunampa muda tutathmini utawala wake kwa kuwa kazi aliyoifanya kwa miezi saba haiwezi kutoa mwelekeo wa uongozi wake kwa vile bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania.

“Kazi ya Kanisa Katoliki ni kuwafundisha wananchi matendo mema yanayomfurahisha Mungu katika kutenda haki na usawa.

“Kwa hiyo tunaungana na Rais Dk. Magufuli na tunamuombea aweze kupambana na mafisadi kwa ukamilifu na uamuzi wake uwe unamfurahisha Mungu.

“Kazi ya kusafisha mafisadi ni ngumu na inahitaji kutenda haki, kutumia busara na akili katika uamuzi wowote.

“Ili rais wetu afanikiwe lazima tuungane na kumuombea afanye uamuzi sahihi na wa busara.

“Wanasiasa wao wanaweza kumlalamikia, lakini sisi Wakatoliki tunaendelea kumpa muda kidogo kwa sababu bado mambo ni mengi ya kufanya ndiyo maana tunafanya kongamano hili kuongeza matumaini mapya.

“Pamoja na hayo, TEC tumesikitishwa na vitendo vya mauaji ya watu vinavyoendelea nchini na tunapaswa kuungana bila kujali tofauti za madhehebu yetu ili kuimarisha amani kwa sababu bila kufanya hivyo, hatutawashinda mafisadi na wanaovuruga amani,” alisema Askofu Kilaini.

Kongamano

Awali, akizungumzia kongamano hilo, Askofu Kilaini alisema katika Kanisa Katoliki, Ekaristi Takatifu ndilo tukio kubwa kuliko yote na Wakatoliki wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja wakati wa kongamano hilo.

Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, wakati wa kongamano hilo, kutakuwa na mada mbalimbali juu ya ekaristi, ya matumaini ya kuleta amani kwa wote hasa waliokata tamaa na ekaristi kwa masikini kuwaletea heshima na uwezo kutoka kwenye umasikini wao.

“Pia kutakuwa na maombi kwa viongozi wa taifa hasa hasa Rais Magufuli aweze kuongoza nchi kwa weledi wa Mungu. Pia kutakuwa na maombi kwa familia ziweze kuishi katika upendo na amani,” alisema.

Wliwaomba waandishi wa habari nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na wawe makini kila wanapoandaa habari za kuwafikishia wananchi kwa lengo la kujenga Tanzania yenye amani.

Wakati huo huo, Askofu Kilaini alitangaza kuwa Juni 12, mwaka huu, Askofu Flavian Kasala wa Jimbo la Geita atasimikwa rasmi.


Chanzo: Mtanzania
 
Tatizo linalotusumbua ni KUTOJUA tafsiri ya neno maendeleo.
Maendeleo sio barabara na majengo tu.
Maendeleo ni dhana pana, maendeleo ya kidemokrasia, maendeleo ya kimfumo, maendeleo ya kijamii, maendeleo ya kiuchumi, n.k.
Pia utafiti unaonyesha maendeleo ya kidemokrasia ni muhimu zaidi kwani huchangia maendeleo ya nyanja nyinginezo.
N.B: Siungi mkono tamko hilo la maaskofu.
Mh. Rais wetu, kipenzi cha Watanzania bila kujali itikadi zao, anafanya kazi nzuri sana.
Naamini tunaenda hatua kwa hatua.
Hizi hatua anazochukua ni muhimu na hazikwepeki.
Ukiwa na nia ya kujenga hazina ni lazima uanze kwa kuua panya na kuziba matundu !
 
Sasa Busara si Mpaka awe nazo? Nakumbuka juzi niliandika Humu kuhusu Busara za Mama Janneth alipoenda kutembelea wazee Ruangwa na kuongea maneno ya busara sana baada ya Mumewe kutoa kauli kuwa wazee ni wala Rushwa na kumfananisha na Abigaili Mke wa Nabali .Kuna watu walikasirika humu.
 
Hata Kwa Mzee wa upako ameibua mchemko mwingine. Kila afanyalo anakosea
Huwezi tumia fedha za umma na kujipangia kujenga barabara kufurahisha kundi au mtu fulani ... Busara inahitajika

Hilo nalo nilisema atazua mambo makubwa.Madhehebu na Dini nyingine zitataka barabara za kuelekea makanisani mwao zijengwe.Rais sio father Christmass wa kugawa zawadi kila anapopita tena akitumia fedha za Umma
 
Hilo nalo nilisema atazua mambo makubwa.Madhehebu na Dini nyingine zitataka barabara za kuelekea makanisani mwao zijengwe.Rais sio father Christmass wa kugawa zawadi kila anapopita tena akitumia fedha za Umma
Hahahaaa ...father Christmas ,inaonekana viongozi wa dini wameona mapungufu katika uongozi,wametoa ya moyoni,kwa kuwa hapendi kukosolewa bungeni na jukwaani,sasa je atakubali kukosolewa makanisani ambako hivi karibuni alihamishia siasa zake?
 
Hata Kwa Mzee wa upako ameibua mchemko mwingine. Kila afanyalo anakosea
Huwezi tumia fedha za umma na kujipangia kujenga barabara kufurahisha kundi au mtu fulani ... Busara inahitajika

Barabara inayokwenda kwa mzee wa upako kimamlaka ipo chini ya Tan Road, au Halmashauri? Njia nzuri ambayo ingetumika ni kuagiza mamlaka husika kuitengea bajeti ili iweze kutengenezwa. Statement aliyotoa raisi haikuonesha wazi wajibu wa kitaasisi kuhusu barabara hiyo kwa hiyo ikaibua hoja kwamba Raisi anataka kuchukua fedha kwenye fungu lolote ajenge barabara hiyo. Barabara za namna hiyo zipo nyingi sana jijini Dar es Salaam na mikoa mingine- kitendo cha Raisi kupita barabara hiyo siku moja tu ili kufika kwenye kanisa hilo na kuahidi kujenga barabara hiyo kinaweza kutafsiriwa vibaya
 
Back
Top Bottom