Maandamano ya waandishi yatikisa nchini;Wamtaka Rais Kikwete, MCT wakutane haraka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Maandamano ya waandishi yatikisa nchini;Wamtaka Rais Kikwete, MCT wakutane haraka

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Sep 12, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Sep 12, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  JUMATANO, SEPTEMBA 12, 2012 05:25 NA WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI


  [​IMG]

  Marehemu Daudi Mwangosi

  *Walaani vikali mauaji ya Daudi Mwangosi
  *Wamtaka Rais Kikwete, MCT wakutane haraka
  *Polisi Iringa wakimbia maandamano ya waandishi
  *Mashushushu, TAKUKURU wamwagwa Jangwani

  MAANDAMANO makubwa yaliyoitishwa na waandishi wa habari jana kutoka vyombo mbalimbali nchini, yametikisha nchi, huku vikiazimia kutoandika taarifa zozote za Jeshi la Polisi ndani ya siku 40 za maombolezo.

  Maandamano hayo, yalilenga kulaani mauji ya mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu, wakati akitekeleza majukumu yake katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.

  Licha ya maandamano kuwa ya waandishi, yalitawaliwa na askari wengi kutoka idara mbalimbali, ikiwamo Idara ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

  MAANDAMANO BARABARANI
  Maandamano yalianzia katika kituo cha Televisheni cha Chanel Ten majira ya saa 3.00 asubuhi, kupitia Mtaa wa Jamhuri na kushika barabara ya Morogoro hadi Jangwani.

  Waandishi hao, walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali uliokuwa ukilaani mauaji hayo na wengine wakiwa na mfano wa bunduki, huku wakionyesha maigizo namna ambavyo polisi walimkamata, kumtesa na hatimaye kumuua Mwangosi.

  Pamoja na maandamano hayo kuwa ya amani, yaliongozwa na askari wengi, wakiwamo wa kikosi cha usalama barabarani, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), huku baadhi ya barabara zikifungwa kwa muda, ikiwemo ya Morogoro.

  Kufungwa kwa baadhi ya barabara, kulisababisha kuwapo kwa msongomano mkubwa wa magari yaliyokuwa yakitokea maeneo mbalimbali kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

  Waandishi wa habari, walionekana wazi kuonyesha hasira dhidi ya polisi kila walipokutana nao, waliwazomea na kuwaonyesha mabango.

  Baadhi ya mabango yalisomeka hivi, ‘IGP Mwema si mwema tena kwa waandishi wa habarii', ‘Chagonja, RPC Kamuhanda, hatuna imani na polisi tena', ‘Polisi waliohusika wanyongwe'.

  Mengine yalisomeka, ‘Muda umefika polisi kufukuzwa uraiani', ‘Mchuna ngozi umeonekana Nyololo', ‘Polisi rudisheni kamera, laptop na kalamu za Mwangosi, ‘RPC Kamuhanda apelekwe the Hague' na mengineyo.

  Ujumbe wa mabongo hayo pamoja na kauli za waandishi, zilizokuwa zikitolewa mbele ya askari polisi hao zilionekana kuwagusa na kuonyesha sura za kuwakera, kitendo ambacho kiliwafanya kuzungukazunguka huku na kule na kushauriana wenyewe.

  MICHANGO YA TEF NA WAANDISHI

  Akizungumza katika mkutano huo, Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, alisema marehemu Mwangosi ni mwandishi wa 46 kuuawa duniani na wa kwanza kuuawa Tanzania hadharani.

  Aliwasisitizia waandishi wengine kutorudi nyuma kutokana na kifo cha mwenzao.

  "Hakuna kuogopa au sio, hebu hao wanaotuua wafikirie wakiamka asubuhi halafu wanakuta hakuna redio inayoongea, katika meza za magazeti hakuna magazeti, watajisikiaje," alihoji.

  "Hiyo itakuwa siyo dunia wala nchi, sisi ni watu muhimu sana katika taifa hili," alisema.

  Naye Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu, alisema ni jambo la kusikitisha kuona uhai wa mtu unakatishwa ghafla.

  "Mwangosi angekuwa ametwaliwa kwa njia ya kawaida isingekuwa tatizo, lakini ameuawa na polisi kinyama, damu yake iliyomwagika kikatili itakuwa mwanzo wa kubadilisha mwenendo wa Jeshi la Polisi.

  "Wananchi wanalipa kodi zao mnunue magwanda, buti na bunduki ili kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuua raia."

  Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Jane Mihanji, alisema dunia itambue waandishi ni kama wafanyakazi wengine, huku akisisitiza polisi kupewa mafunzo zaidi ya kazi zao.

  UTPC

  Mkurugenzi wa Umoja wa Vilabu vya Wandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan, alisema atahakikisha polisi waliohusika na tukio hilo, wanatunza familia ya marehemu Mwangosi.

  Naye Rais wa UTPC, Keneth Simbaya, alisema marehemu Mwangosi, aliaga kwenda kazini lakini hakuweza kurudi.

  "Hii ni changamoto kubwa huko tunakoelekea, kwani tumeambiwa matendo kama haya yanafifisha demokrasia ya tasnia ya habari, hivyo Serikali inapaswa kututetea kwa nguvu zote," alisema.

  Kwa upande wake, Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena, alisema tukio hilo limegusa wanataaluma wote nchini na linatuma salamu dunia nzima kwamba wanahabari Tanzania hawana usalama sehemu za kazi.

  "Waandishi wana nguvu kuliko wanavyofikiria polisi, wana uwezo wa kuwadhibiti polisi, jana (juzi) nilimshangaa RPC wa Ilala, Herieth Komba ananipiga mkwara kuninyima kibali, lakini baadaye alinikubalia.

  "Tukiamua kutumia taaluma na kalamu zetu, tutafanikiwa kufanya jambo lolote nchini, kwani wananchi wanatuamini, tulianza kusema kwa kulaani kisha leo (jana), tumeandamana na kinachofuata ni kutaka polisi waliohusika wachukuliwe hatua zaidi, tutazidi kusema hadi kieleweke.

  "TEF tumeamua kuunda tume nyingine huru ambayo ina watu kutoka TEF, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Baraza la Habari Tanzania (MCT), hii itatoa majibu kabla ya kamati nyingine.

  MAAZIMIO

  Wakizungumza na wanahabari kwa vyakati tofauti katika Viwanja vya Jangwani, viongozi wa TEF walilaani mauaji ya marehemu, Daudi Mwangosi, huku wakitoa maazimio ya kutoandika habari zinazohusu Jeshi la Polisi ndani ya siku 40 za maombolezo.

  Azimio hilo, lilitamkwa mbele ya waandishi na kiongozi mwandamizi wa TEF, Masoud Sanani na kuwataka waandishi na wahariri kutekeleza tamko hilo.

  "Ndani ya siku 40 za maombolezo ya marehemu Daudi Mwangosi, habari zote zinazohusu Jeshi la Polisi zisiandikwe, hata akiongea IGP, RPC, RCO na wengine wote wanaofuata, hatutaki habari zao," alisema na kushangiliwa na waandishi wote.

  HARAMBEE YA WAANDISHI

  Kutokana na tukio hilo, waandishi wa habari waliamua kufanya harambee ya kuchangia kiasi chochote walichokuwa nacho mfukoni ambapo walifanikiwa kupata Sh 526,500 katika mkutano huo wa Jangwani.

  ARUSHA

  JESHI la Polisi wilayani Arusha,jana limezuia kwa muda maandamano ya kimyakimya ya waandishi wa habari mkoani Arusha.

  Zuio hilo, lilitokana na kuwepo shughuli za mkutano mkubwa wa mazingira unaowajumuisha zaidi ya wageni 3,000, wakiwemo mawaziri wa mazingira 52 kutoka nchi za Afrika.

  Barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, (OCD) Lotson Mponjoli kwenda Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), ilidai maandamano hayo yalipaswa kusitishwa ili kupisha shughuli za kitaifa zinazoendelea jijini hapo.

  Katika barua ya OCD Mponjoli yenye namba AR/B.5/VOL.II/75, kwenda APC ilidai, maandamano hayo yalipaswa kusitishwa kutokana ugeni mkubwa uliopo kwa sasa.

  "Wiki yote hii, tutakuwa na shughuli za kiserikali, tuna ugeni mkubwa wa uongozi wa Serikali na kimataifa wanaohudhuria mkutano wa mazingira."

  Hata hivyo wakati barua hiyo ikiahirisha kufanyika kwa maandamano hayo, tayari baadhi ya waandishi wa habari, walikuwa wamekusanyika jirani na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, kwa ajili ya kufanya maandamano yao.

  Awali waandishi wa habari walikutana karibu na Ofisi za CCM Mkoa wa Arusha tayari kwa kuanza maandamano yao, kulaani mauaji ya Mwangosi, huku wakiwa na mabango mbalimbali.

  Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa APC, Eliya Mbonea, alilazimika kutoa ufafanuzi kwa waandishi ambao tayari walikuwa wameingia barabarani.

  Alisema juzi, Kamati ya Utendaji ya APC pamoja na wanachama watatu walifanya kikao na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, ambaye aliomba kusitisha maandamano kutokana na ugeni mkubwa uliopo

  Maandamano hayo, yalipangwa kuanza Saa 4:00 asubuhi kupitia Barabara ya Makongoro, ambayo inapita mbele ya ofisi za Polisi, Ofisi za Mkuu wa Mkoa Manispaa, kisha kuingia Barabara ya Boma.

  KIGOMA WAMPA NENO JK

  Huko mkoani Kigoma, wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari, wamelitaka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Muungano wa Vyama vya Habari Tanzania (UTPC) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) wakutane na Rais Jakaya Kikwete ili waweze kujadili changamoto zinazowakabili waandishi wa habari.

  Akisoma maazimo yaliyofikiwa na wanachama wa klabu hiyo, kufuatia kikao kilichokutana kumjadili Mwangosi, walisema hiyo ndiyo njia pekee ambayo inaweza kumaliza tofauti zilizopo.

  Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Kigoma, Deogratius Nsokolo, alisema kuna umuhimu mkubwa wa Rais Kikwete kukutana na taasisi hizo, ili kujadili kwa kina matatizo ya waandishi wanayowapata, hasa wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kila siku.

  Alisema pamoja na wanachama wa Klabu ya Kigoma kumtaka Rais kukutana na taasisi hizo, lakini wanachama hao wameazimia kwa pamoja kulaani kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi cha kutumia nguvu kubwa dhidi ya marehemu Mwangosi.

  MWANZA WALAANI

  CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), kimelaani mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na kutaka wahusika wa tukio hilo, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

  Tamko la MPC, lilitolewa na Mwenyekiti wake, Deus Bugaywa, wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuandamana kimya kimya kutoka viwanja vya Ghand hadi uwanja wa michezo wa Nyamagana.

  Alisema chombo huru cha uchunguzi, kinapaswa kuundwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya tukio la kuuawa kwa Mwangosi, kisha matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe mbele ya umma wa Watanzania.

  Alisema wanahabari wanaamini, Mwangosi aliuawa kwa makusudi na inaonyesha wazi kulikuwa na mpango wa polisi kuwashughulikia waandishi wa habari watatu, Mwangosi akiwa ni mmoja wao.

  MUSOMA WAWASUSIA POLISI

  Licha ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi kuandamana na kulaani mauaji ya kinyama dhidi ya Mwangosi, waandishi wa habari mkoani Mara, waliandamana kwa amani.

  Mapema jana asubuhi, waandishi hao walifika katika ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), wakiwa wametawaliwa na huzuni.

  Waandishi wakiwa katika mnaandalizi ya kuanza maandamano hayo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Musoma (OC CID), Mahamudi Banga, kwa niaba ya Mkuu wa Polisi ya Wilaya, alikuwa na barua yenye kumbukumbu MUS/A.3/VOL 11/.378, ikitaka kuzuia maandamano hayo kwa kwa kile kilichoelezwa kuvunja kifungu namba 43(1) cha Polisi na wasaidizi Polisi 2002 ya kutoa taarifa kwa masaa 48.

  Kutokana na katazo hilo na unyeti wa maandamano ambayo yalikuwa ya amani, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Emanuel Bwimbo, alishinikiza kufanyika kwa maandamano hayo na kukabiliana kwa chochote ambacho kingetokea.

  Baada ya maandamano hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, Bwimbo alitangaza kusitisha kuandika habari za jeshi hilo.

  IRINGA

  Mkoani Iringa, waandishi huko waliungana na wenzao kulaani vikali mauaji hayo.

  Maandamano hayo, yalifanyika kwa amani katika barabara kuu za mjini hapa.

  Katika hali ya kushangaza, polisi hawakujitokeza kulinda maandamano hayo, yaliyoanzia ofisi za Iringa Press Club (IPC) bustani za Manispaa ya Iringa.

  Katika maandamano hayo yaliyowavuta baadhi ya wananchi, waandishi walionekana wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali kama "Rais umeyaona haya", RPC kaa pembeni" na wananchi wakiwa wamebeba magazeti yenye habari za kifo cha marehemu Daudi Mwangosi.

  Mwenyekiti wa maandamano ya waandishi wa habari Iringa, Zulfa Shomari alisema "W waandishi mkoani Iringa tunataka RPC Michael Kamuhanda akae pembeni ili kupisha uchunguzi."

  SHINYANGA

  CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), kimelaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya waandishi wa habari yaliyopangwa kufanyika jana mkoani humo, kwa ajili ya mauaji ya Mwangosi.

  Tamko hilo, limetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Shinyanga (SPS), Shija Felician, alipokuwa akizungumza na waandishi.

  Uamuzi huo, ulifikiwa na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarsti Mangala, kuzuia maandamano hayo.

  Alisema kitendo hicho, hakitavumiliwa na kusisitiza kuwa chama hicho hakiko tayari kuandika habari zozote zinazohusu jeshi hilo.

  Alimtaka Rais Kikwete, kumwajibisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

  Habari hii, imeandaliwa na John Maduhu (Mwanza), Benjamin Masese, Elizabeth Mjatta (Dar), Eliya Mbonea (Arusha), Editha Karlo (Kigoma), Shomari Binda (Musoma), Mercy Mwalusamba, Sam Bahari na Editha Edward (Shinyanga).

   
 2. Ye Soya

  Ye Soya Senior Member

  #2
  Sep 12, 2012
  Joined: Nov 24, 2011
  Messages: 187
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  safi sana kwa taarifa kamili
   
 3. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #3
  Sep 12, 2012
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
Loading...