Maandamano ya UVCCM yazua maswali mengi...

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,173
Maandamano UVCCM yashtukiwa

*Ni yale ya kutaka bodi ya mikopo ivunjwe
*Yahojiwa mbona hawakuwatetea kupiga kura


Na Tumaini Makene

MAANDAMANO yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yakilenga
kuwajumuisha wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu nchini, yameshtukiwa yakielezwa kuwa ni mkakati kufunika udhaifu wa kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwapatia wanafunzi mikopo.

Maandamano hayo ni yale yenye nia ya kutaka kuishinikiza serikali kuvunja Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB), kwa kuondoa uongozi uliopo na kuiunda upya kwa madai kuwa imeshindwa kuwahudumia wanafunzi hao kulingana na mahitaji yao.

Baadhi ya wananchi, wadadisi wa masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, wamesema kuwa huo ni mkakati wa UVCCM kutaka kurudisha imani ya kundi kubwa la vijana nchini, hususan wanafunzi, ambao wameonekana kuanza kuipa kisogo CCM na hata kuonesha kukerwa na mwenendo wa serikali yake, katika kushughulikia kero mbalimbali katika jamii.

Wiki iliyopita Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Bw. Beno Malisa alikubaliana na ombi la wanafunzi wa vyuo vikuu walio wanachama wa CCM mkoa wa Dar es Salaam juu ya kuitisha maandamano hayo.

Nia hiyo ilifuatia tamko la hivi karibuni la Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM lililosomwa Dar es Salaam, ambalo nalo lilisema kuwa tatizo la migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu, moja ya sababu zake kubwa ni ukiritimba wa bodi ya mikopo, ukisema hauko tayari kuona hilo likiendelea, bali watendaji 'wapinduliwe' mara moja.

Tamko hilo la UVCCM taifa, lilijibiwa na HESLB, ambapo Mkurugenzi Mtendaji, Bw. George Nyatega, alisema vijana hao walitoa taarifa za 'uzushi na kukurupuka' bila kufanya uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha migomo ya vyuo vikuu, huku akitaka bodi hiyo isigeuzwe 'jimbo la uchaguzi' na wanasiasa.

Akizungumza hali hiyo, mmoja wachambuzi mahiri wa masuala ya kisiasa na kijamii, Bw. Bashiru Ally ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa, alisema kuwa bodi ya mikopo ni dalili ya tatizo kubwa nchini kwa sasa.

Bw. Bashiru alisema kuwa ni vigumu kuzungumzia tatizo dogo bila kujikita katika suala la msingi, ili kupata majibu ya uhakika, badala ya 'majibu mepesi kwa matatizo magumu.'

"Unajua sekta ya elimu ina matatizo mengi tofauti tofauti ambayo yamekuwa yakiibuka kwa nyakati tofauti kwa sura tofauti, leo utasikia Dodoma wamegoma kwa sababu ya mishahara au wanafunzi kukosa fedha, au wanafunzi wengine wanapata kidogo kuliko wanavyohitaji.

"Lakini pia mfumo wa kutambua umaskini wa wanafunzi na kuwapata wanafunzi wahitaji bado ni tatizo kubwa hapa nchini...hivi kwanza unawekaje madaraja ya kuwatambua maskini katika nchi maskini kama hii. Hao wanaomudu kulipa kutokana na utajiri wao, wameupataje huo utajiri.

"Hata bodi ikivunjwa leo nini kinafuata...hata kama bodi ikipewa fedha...kwanza hizo fedha zinatoka wapi katika uchumi unaokufa huu. Uchumi huu unakufa...lakini bodi ya mikopo ni kiashiria tu cha mfumo mbovu ambao umewaparanganyisha watu," alisema Bw. Bashiru.

Huku akisema kuna kila haja ya jamii kukaa chini na kuutafakari ubepari, aliongeza kuwa mfumo huo ni chanzo cha jamii kuhangaika kila siku na suala moja baada ya jingine bila kupata majawabu yanayotosheleza kuhitimisha kila mjadala au kashfa inayoibuka.

Alisema Watanzania wamegeuka kuwa jamii ya watu wanaohangaika na 'kashfa na mijadala mipya' kila siku, bila kupata muda wa kujadili undani wa matatizo yao na kutafakari kwa kina nchi inakotoka, ilipo na inakoelekea.

Alisema vijana wote nchini bila kujali itikadi za vyama, wala kutumikia makundi ya watu wachache kwa maslahi ya muda mfupi, wanapaswa kuwa chachu ya kuibua mijadala ya kitaifa, juu ya msambaratiko wa kijamii kwa sababu ya kukumbatia mfumo aliouita wa kinyama, yaani ubepari.

"Vijana hawa wananishangaza kwani bodi ya mikopo ina-exist (iko) nje ya mfumo huu mbovu wa kinyama tulioamua kuukumbatia. Mbona wameshindwa kuwazungumzia wamachinga waliojaa barabarani au huko Kariakoo, wale si vijana wala hawana mwelekeo...wanapaswa kuwa chachu ya mjadala mpana wa kitaifa juu ya tatizo la msingi linalosumbua jamii.

"Tumekuwa watu wa ajabu, leo kashfa hii, kesho mjadala ule, tulikuwa na Dowans, mara matokeo ya kidato cha nne, hatujamaliza hilo ghafla watoto 10 wamekufa Mwananyamala, mara mauaji ya albino, mara wananchi huko Babati wamevamia mashamba, sasa wanasumbuana na polisi...yaani ni confusion (mkanganyiko) tu katika jamii.

"Ubepari ni mfumo ambao tayari umejionesha kwa sura halisi ya unyama, mfumo unaotoa fursa kwa kakundi kadogo kunufaika, huku kundi kubwa likibakia kuwa fukara, mfumo unaoua vijiji, ukiua hata kilimo kinachotoa ajira kwa wengi na kukuza miji, sasa ukikuza miji bila watu kuwa na ajira, unategemea nini.

"Sasa wanaonufaika wanaendelea kunufaika, maskini wanaendelea kuwa maskini...sasa katika mazingira ya nchi maskini kama hii unawapimaje maskini...wanafunzi sasa wanasoma wakiwa njaa, hawana uhakika wa malazi...mfumo wa kinyama unazalisha watu wanyama pia.

"Mfumo wa kinyama utazalisha watu watakaokuwa wanyama, kwa sababu wamesumbuka sana, unategemea wakija kuwa wabunge au wakuu wa wilaya, wataacha kujitengea mafao makubwa yanayozidi hata profesa kama ilivyo sasa! Haya ndiyo vijana kama UVCCM walipaswa kutafakari kabla ya kutoa tamko, nchi haitaendelea kwa watu kutoa matamko kwa malengo ya kisiasa.

Alitoa rai kwa vijana nchini na jamii kwa ujumla kuacha kutafuta majibu mepesi kwa mambo magumu ambayo yanahitaji mjadala na tafakuri inayoendana na muktadha wa kuangalia nchi inatoka wapi, iko wapi na inaelekea wapi.

"Hao UVCCM wote nawafahamu nimewafundisha hapa, wanafiki tu...mbona wamechagua bodi ya mikopo tu, mbona hawataki kushughulikia uchafu wa uchaguzi, watu walinunua kura, mbona hawazungumzii huko Babati wananchi wanahangaika sasa...mbona hawakutoa tamko juu ya vijana wenzao elfu sitini waliokosa haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita, hatukusikia.

"Waende kwenye Azimio la Arusha watapata majibu ya hayo mambo wanayotaka, wajifunze kutafakari kwa upana kabla hawajatoa matamko, matamko ya vyama mbalimbali hayatatusaidia, vijana wa chama hiki, mara wa chama kile, mpaka tutafakari kwa kina chanzo cha mparanganyiko wetu,

"Tatizo la bodi ni la kimfumo zaidi si kiutendaji...tusiangalie maslahi ya kiitikadi, wala makundi ya watu wachache...nchi hii ikisambaratika, itasambaratika na watu wote bila kujali ikitikadi zetu," alisema Bw. Bashiru kwa kirefu.

Akitumia uzoefu wa kuwa kiongozi wa wanafunzi kama waziri wa mikopo na baadaye waziri mkuu, Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bw. Julius Mtatiro ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) alisema kuwa tatizo la mikopo nchini ni la kimfumo zaidi si bodi pekee.

Akiweka wazi kuwa bodi ya mikopo inayo matatizo yake, Bw. Mtatiro alisema kuwa kuna mambo mengi juu ya mfumo wa utoaji mikopo nchini hayawekwi wazi, hivyo katika hali ya kawaida ni rahisi kuisukumia bodi ya mikopo lawama zote juu ya matatizo yanayowakumba wanafunzi.

"Ninaposema mfumo namaanisha mfumo wa serikali, hapa UVCCM inatumika tu, tatizo ni serikali imeshindwa kubuni mbinu za namna ya kufadhili elimu ya juu, hata kwa kupitia bodi hiyo hiyo, kwa mfano hakukuwa na haja ya wanafunzi wote kupatia fedha zao Dar es Salaam, wala Mwanza au Morogoro wangeweza kupata fedha zao huko huko waliko.

"Hivi kwa nini watu hawajiulizi, kila bodi inapolalamikiwa kwa nini serikali huwa inakaa kimya, wanakaa kimya kwa sababu wanajua ukweli uko wapi, wanajua wakiwabwekea bodi, bodi watasema ukweli, mbona serikali kila siku wanakuwa wepesi kuzibwekea agents (wakala) zingine zinapoboronga.

"Kwa mfano kuna wakati serikali inafanya projection (makadirio) ya idadi ya wanafunzi itakaowakopesha kwa mwaka husika, inaweza kuweka elfu themanini, lakini ukifika wakati husika, wenye sifa stahili wako 140,000, bodi ya mikopo wanakwenda kimya kimya kuwaambia, serikali nayo kimya kimya inatafuta fedha," alisema Bw. Mtatiro.

Kwa maoni yanayotokana na uzoefu wa kushughulikia matatizo ya mikopo akiwa chuoni, alisema bodi ya mikopo inachangia asilimia 5 ya matatizo yaliyopo huku asilimia 95 zote zinachangiwa na serikali, akiongeza kuwa hiyo ndiyo sababu wanafunzi wengi huchelewa kupata fedha mpaka vyuo vinafunguliwa au 'wakati wa mwisho mwisho'.

"Tatizo ni ukosefu wa mbinu sahihi, serikali imeishiwa mbinu sasa wanawatumia UVCCM...wakishamaliza kuvunja bodi hii ambayo imeanza kupata uzoefu wataunda kitu kingine katika mfumo huo huo mbovu, serikali yenyewe iko kwenye matatizo makubwa ya fedha, kulipa Dowans na vitu vingine..." alisema Bw. Mtatiro.

Naye mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), Sunday Charles, alisema kuwa kushughulika na bodi pekee, katika suala zima la mfumo wa utoaji mikopo nchini ni kutaka kufanya propaganda kwa manufaa ya kisiasa kwenye matatizo ya wanafunzi.

Alisema ni vigumu kuitofautisha bodi na serikali moja kwa moja, kwani pamoja na kwamba serikali kupitia bunge hupitisha bajeti za mikopo, kiuhalisia si fedha yote huenda bodi kwa wakati mwafaka, baada ya kupitia hazina.

"Cha kwanza lazima tutambue kuwa bodi wana-implement (wanatekeleza) matakwa ya serikali...bunge hupitisha bajeti za fedha za mikopo in terms of figures (mahesabu ya kwenye karatasi) lakini ki-uhalisia sio pesa inayopitishwa hufika yote bodi, hata hivyo kiasi kidogo hicho kinachopatikana bado hupitishwa hazina, na hazina pia hutoa pesa hizo kwa kibaba.

"Lakini kingine hakuna clear link (uhusiano wa wazi) kati ya management (uongozi) ya chuo na bodi ya mikopo, suala la mikopo manejimenti nyingi za vyuo zinalitazama kama ni mkataba wa mwanafunzi na bodi yenyewe...

"Tumewashtukia muda tuu, na kama ukitaka kuona kwamba ni propaganda ya kukamata wanafunzi wa elimu ya juu, kwa nini iwe ni mikopo tu, ili hali kuna matatizo makubwa nchini...kuna suala la Dowans wanapitia tuu juu juu, mgao wa umeme, kupanda kwa bei ya nishati ya umeme, gesi, wako wapi UVCCM, mbona hawasemi.

"Tatizo letu kwa sasa ni kupandishiwa pesa za kujikimu walau 5000 mpaka 10,000, hawasemi wao wanafumba watu macho eti tatizo ni bodi, UVCCM lazima watambue kuwa wanafunzi wa elimu ya juu wana-reason (wanatafakari)," alisema Bw. Charles.
http://majira-hall.blogspot.com/201...howComment=1296654344656#c4094040544237742104
 
Mwarobaini wa taasisi dhaifu nchini humu ni katiba mpya......kuvunja kwa Bodi ya mikopo ni kuahirisha tu tatizo..................................lakini siyo kulitatua........................................................UVCCM wangeeleweka kama wangelijikita katika kupinga DOWANS na kudai katiba mpya...................mengine ni dalili ya tatizo na wala siyo tatizo....................................
 
Ushauri wa bure:
Tuwaache waanzishe hayo maandamano, halafu tuyageuze katikati yawe ya kudai serikali itoke madarakani. Then tufanye kama Tunisia!
 
Ushauri wa bure:
Tuwaache waanzishe hayo maandamano, halafu tuyageuze katikati yawe ya kudai serikali itoke madarakani. Then tufanye kama Tunisia!
nadhani hili ni sahii kuyapora haya maandamano na kuprotest against the government. Hawa watoto wa nyoka hawawezi kuwa mjusi wametumwa tu na wazee wao. Wanataka kuangalia ni vijana wangapi bado wanaunga mkono chama cha mafisadi. CCM ni mafia, wako tayari kuwasacrifice hata hawa UVCCM ili kufanikisha malengo yao. Vijana mlioko vyuoni kuweni makini na hawa watoto wa mafisadi. Wanataka kuwateka vijana kwa changa la macho.

Nashauri cdm vyuoni wawaelezee wanafunzi juu ya hii janja ya nyani. Hakuna mabadiliko ya kweli yatakayoka kwa watoto wa mafisadi. Nguvu ya umma ndiyo mabadiliko yetu. Wasitutoe kwenye focus ya kuleta madiliko kwa maandamano ya changa la macho.

Kimsingi bodi ya mikopo ni agenti wa serikali haiwezi ikatenda kinyume na wateule wake. Yanayofanywa na bodi ni maelekezo kutoka serikalini.

Nani asiyejua kuwa seikali haina helakwa sababu ya mabango ya JK. Bodi inapata wapi pesa? Hata wakivunja bodi mara mia bado haitasaidia maana kiini hakijaharibiwa JK and co must go to make sense of our living.
 
Wazo la kutumia hayo maandamano kudai haki zaidi ni Mawazo mazuri sana lakini yanapaswa kutumika vyema hasa katika kujipanga kuakikisha kuwa wanazidiwa hoja na mantiki wakati wa kuongea na wanafunzi
 
Hofu ya vijana wanapojipanga kuingia mitaani. Wakati huu hata vijana wa sekondari nao wanaangalia Egypt na Tunisia na vijana wanajua wakiandamana kupinga "Regime ya Kikwete na CCM" CCM will go down softly, sasa tunaona njama za UVCCM kutaka kuanzisha maandamano bila kujiangalia kwenye kioo.

Tatizo si UVCCM na CCM nzima? Hii ni sawa na mbwa kutaka kuushika mkia wake na kuanza kipiga mduara. Wanalipwa mishahara na CCM ambayo inatoka humo humo Dowans na makampuni kama hayo, Je watakataa mishahara inayotokana na wizi wa mali za Taifa?

Sijaona mtu ana adui au jambazi kamwingilia ndani halafu anatoka nje kumtafuta wakati kamwona kabisa yumo ndani - JK na Rostam na Mafisadi wengi?
 
Wasomi waishushua UVCCM

• Wafichua serikali inavyokwamisha mikopo kwa wanafunzi

na Waandishi wetu

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umeendelea kupingwa kwa hatua yake ya kutoa tamko linalotaka Bodi ya Mikopo (HELSB) ivunjwe bila kueleza njia mbadala ya kumaliza matatizo ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Jana wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kupitia kwa mwakilishi wao katika bodi hiyo, Chitage Edwin, walitoa rasmi msimamo wa kupinga tamko la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) la kutaka Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe na badala yake wamefichua kuwa serikali ndiyo inayopaswa kulaumiwa na kuwajibika kwa kusababisha matatizo ya mikopo kwa wanafunzi.


Viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) hivi karibuni walinukuliwa wakitoa tamko lao la kutaka Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe kwa madai ya kukwamisha na kuchelewesha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini huku wakisisitiza kuwa isipovunjwa watafanya maandamano yatakayohakikisha inavunjwa.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mwakilishi wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu katika bodi hiyo, Chitage Edwin, alisema wao kama wasomi fikra zao zipo tofauti kabisa na fikra potofu za UVCCM wanaotaka bodi hiyo ivunjwe wakati matatizo yote yamesababishwa na serikali yenyewe.


Alisema utaratibu mbaya wa serikali kutenga na kutoa pesa kidogo kwenda Bodi ya Mikopo (HESLB) ndio uliosababisha kwa kiasi kikubwa matatizo ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.


"Fedha inayotengwa na serikali haikidhi mahitaji, kwa sababu hiyo idadi kubwa ya wanafunzi wenye sifa ya kusoma elimu ya juu hawapati mikopo, kwa mfano wanaopata daraja la tatu hawapati mikopo isipokuwa tu wanaposoma ualimu na masomo ya sayansi.


"Hata hao wanaopata mikopo bado wanawekwa katika madaraja, kwa bahati mbaya sana hakuna mazingira yanayowezesha kufahamu kwa usahihi uwezo wa kiuchumi wa kila mwombaji.


"Pia ni utaratibu mbaya wa serikali kutoa pesa kidogo kidogo kwenda bodi ya mikopo," alisema mwakilishi huyo.


Wakipinga zaidi kile walichokiita "hatua ya vijana wa CCM kutaka kuugeuza mgogoro wa mikopo kuwa turufu yao ya kisiasa", mwakilishi huyo alisema jambo linalopaswa kufanyiwa kazi ni mfumo mzima wa utoaji wa mikopo na upungufu wake, ambao mhimili wake ni serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu na Hazina.


Akiukosoa mfumo huo, alisema kukosekana kwa usimamizi na udhibiti wa ada kwa wanafunzi kumetoa mwanya kwa mamlaka ya vyuo kupandisha ada kiholela, jambo ambalo lingeweza kudhibitiwa kama serikali ingekuwa makini.


Akiwasilisha mapendekezo ya nini kifanyike ili kutatua matatizo yaliyopo, alisema: "Serikali iweke utaratibu utakaowezesha fedha za mikopo kuifikia bodi kwa haraka kwa kiasi cha kutosha, iwe na dira iliyo wazi juu ya malengo ya taifa hususan katika idara ya wataalamu katika fani mbalimbali.


"Izingatie kuongeza fedha za kujikimu sambamba na mahitaji mengine kwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha.


"Iweke utaratibu wa usimamizi na udhibiti katika viwango vya ada za wanafunzi, iwajumuishe wanafunzi waliopata daraja la tatu wenye sifa za kusoma chuo kikuu wapate mikopo na iache kutoa mikopo kidogo kidogo."


Wakati huo huo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga, juzi alilazimika kutumia salamu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuwashawishi wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST) waweze kumsikiliza.


Kitwanga alilazimika kukikubali japo kwa muda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na hatua ya wanafunzi wa chuo hicho kuguna kila alipoitaja ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi wakati akizungumza nao kuhusu inavyotekeleza sera ya elimu.


Waziri huyo alilazimika kuwasalimia wanafunzi hao akisema: "CHADEMA hoyee!!" Na ukumbi mzima ulirindima kwa mayowe na vifijo vya wanafunzi waliopaza sauti zao wakimjibu: "Oyeeee" huku kila mmoja akimpungia alama ya vema kwa kuonyesha vidole viwili.


Kitendo cha Waziri Kitwanga kutumia jina la CHADEMA katika kibwagizo hicho kilitokana na hatua ya wanafunzi hao kuguna pale alipoanza kujibu maswali yao kwa kusema: "katika manifesto ya CCM….." bila kumalizia kusema alishtushwa na miguno.


Akionyesha wazi kuwa amezisoma nyuso za wanafunzi hao, waziri huyo alibadili mwelekeo naye na kuwasalimu kwa salamu hiyo ya CHADEMA.


Baada ya hapo aliwataka wanafunzi hao waanze kueleza kero na changamoto zinazowakabili ambapo alisimama Makamu wa Rais wa serikali ya wanafunzi ambaye alieleza kero inayowasumbua kuwa ni pamoja na chakula kinachotolewa si kizuri na hakina usalama.


"Hapa tuna tatizo la chakula kwani tunapewa chakula ambacho hakilingani na kiwango halisi na wakati mwingine tunapewa nyama ambayo tayari imeharibika, hivyo tunashauri tuwe tunapewa fedha ili tujitafutie chakula wenyewe," alisema.


Mwanafunzi Jacob Mambo alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa maabara za taasisi hiyo zimechoka, haziendani na mfumo wa sasa, maktaba iliyopo haitoshelezi na miundombinu yake sehemu kubwa imechakaa.


"Tunashindwa kuielewa hii serikali yetu kwani tunaeleza matatizo yetu tunaambiwa serikali haina pesa, sasa hizo fedha za kuilipa Dowans zinatoka wapi?" alihoji Mambo.


Mwananfunzi mwingine, Charles Gabriel, alisema kuwa hali ya mabweni ya wanafunzi ni mbaya na kwamba wamekuwa wakilipwa fedha pungufu kwa ajili ya kwenda kwenye mazoezi ambapo mwaka jana kilitolewa kiasi cha sh 360,000 badala ya sh 444,000 tofauti na Taasisi ya Arusha ambayo wanapewa kiasi cha sh 480,000.


Akijibu kero hizo, Naibu Waziri huyo alianza kwa kusema kuwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini kabla ya kuendelea kilianza kizaazaa cha wanafunzi kupaza sauti na kubeza wakisema: "Aaaaaaa!….Aaaaaaa!" Hali iliyomfanya waziri huyo ajikute akinadi salamu ya CHADEMA kwa kusema: "CHADEMA Oyee!" Ndipo wanafunzi zaidi ya 1,000 waliokuwa kwenye ukumbi huo wakaitikia kwa kupaza sauti: "Oyee!" Huku wakipiga makofi na kumpungia alama ya chama hicho ya vidole viwili.


Waziri huyo aliwataka wanafunzi hao kuwa na subira ingawa ni kweli taasisi hiyo ina tatizo la vitendea kazi.


Pia alikiri kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya mahitaji ya chakula ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi na kuahidi kuwa serikali itajitahidi kuhakikisha kero hizo zinakwisha kwa wakati.


Baada ya kumaliza mkutano huo, Kitwanga alilazimika kutembelea mabweni ili kuweza kujionea hali halisi huku wanafunzi wakimzonga na kusema: "Bado huku, bado chooni." Kitendo ambacho hakusita kwenda sehemu zote alizotajiwa na wanafunzi hao.
 
Jana wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kupitia kwa mwakilishi wao katika bodi hiyo, Chitage Edwin, walitoa rasmi msimamo wa kupinga tamko la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) la kutaka Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe na badala yake wamefichua kuwa serikali ndiyo inayopaswa kulaumiwa na kuwajibika kwa kusababisha matatizo ya mikopo kwa wanafunzi.
Viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) hivi karibuni walinukuliwa wakitoa tamko lao la kutaka Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe kwa madai ya kukwamisha na kuchelewesha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini huku wakisisitiza kuwa isipovunjwa watafanya maandamano yatakayohakikisha inavunjwa.
Lengo la UVCCM ni kupoteza lengo na watu wasahau DOWANS na udhaifu uliomo ndani ya serikali ya CCM ambayo hata hivyo sisi hatukuichagua ila ipo madarakani kwa ridhaa ya TISS na NEC tu.................................
 
Back
Top Bottom