Maandalizi Thabiti ya Uzee/mwisho wa mwisho

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,327
51,831
MAANDALIZI THABITI YA UZEE

Anaandika, Robert Heriel.

Kutokana na kuishi na wazee tangu utoto wangu mpaka napata nuru ya akili, nimeona niyaandike haya, ikiwa ni muhtasari wa mengi niliyoyaona na kujifunza kutoka kwao.
Andiko hili lamfaa yeyote mwenye kuishi, na mambo niliyoyaandika ni amini na kweli kutokana na yale yote niliyoyaona. Hata hivyo, nimeandika nikiwa na ubongo wenye umri wa miaka ishirini na saba tuu, hivyo nastahili kurekebishwa endapo nitapuyanga.

Niite Taikon wa Fasihi, Mwana kutoka Nyota ya Tibeli.

Kabla ya nguvu za mwili kupungua, nguvu za akili hutangulia kuchoka, kumbukukumbu hupepesuka kama unyoya, hamasa ya kutenda inaongezeka lakini nguvu ya mwili iliyeyuka, hamu ya maisha huzidi lakini utamu hupungua, kila unachokitamani unaweza kupewa lakini unakiona hakikufai. Majuto na majivuno hugeuza moyo uwanja wa mapigano, leo ashinde huyu kesho ashinde huyu, basi kila siku huwa na mshindi wake, usiku usingizi hukimbia na uchovu unakukumbatia, macho hata ukiyafumba ndoto kamwe hazitokufikia, kutetemeka pasipo baridi, nguvu ndizo zimetoweka. Huo ndio uzee, mwisho wa mwisho katika maisha.

Hao wazee niliokaa nao, wakakaa nami, nikawaona wakinifunza yale waliyoyaona ni mafunzo, wakinionya yale walioona ni mtego enzi zao, hata hivyo neno moja nisisahau kulisema, ile sumu ya zamani kwao, leo ndio dawa, na hii dawa ya leo; kesho ndio sumu, hayo nayo niliyaona kwao hao wazee, waliozeeka.

Maandalizi ya Ujana huanzia uzeeni, na yauzeeni huanzia ujanani, hata hivyo maandalizi ya utoto huanzia kwenye mahusiano ya wazazi wawili, wakipendana au wakichukiana.

Uzee ulioandaliwa vyema ni faida kwa vijana watakaojifunza. Kuanguka kwa wazee ni kuanguka kwa vijana, Ukoo wenye wazee walioanguka moja kwa moja ukoo huo umeanguka, vijana wameanguka, na watoto wameanguka.
Wazee mashujaa huzalisha vijana mashujaa, maandalizi ya uzee ni mkakati wa miaka mingi kama ulivyo uzee.

Mtu huweza kuwa mzee kabla hajawa mzee kiwakati, yaani kiumri. Ingawaje maana ya msingi ya Uzee ni hali ya mtu/kiumbe kuwa na umri mkubwa hasa umri wa tamati.

Mimi ninaweza kueleza nadharia yangu niliyoipa jina UZEESHI hivi; Uzeeshi ni kile kitendo cha kuuona ujana kwa macho ya akili, kuuona uzee kwa macho ya akili na kujua namna ya kuishi kwa utulivu na uzoefu hata kabla hujafika huko. Yaani kijana wa miaka 25 awe na uwezo wa kuyaona na kuyaishi maisha ya utu uzima iwe ni miaka 45-90 kwa utulivu na uzoefu.
Kwa maana hiyo Uzeeshi humfanya mtu awe mtulivu, mzoefu, mwenye busara, hekima, na Imani.
Uzeeshi ni ule uwezo wa kijana kuwa na jicho kuna mwisho akiwa mwanzo, kuona mwanzo akiwa mwisho. Uwezo wa kufanya mambo kwa kuangalia hatma ya kila jambo atakalolifanya.

Wazee hata kama wanaukabili ukingo wa maisha yao kwa huzuni, lakini tayari wanayopicha halisi ya kule walikotoka na kule waendako, tayari wameshajua nini kiliwaleta na wapi sasa wanaelekea.
Hii ni tofauti na vijana wengi ambao mpaka wakifikisha miaka 50 hawajui ni wapi walipotoka, na ikiwa ni hivyo hawajui wapi walipo na wapi wanaenda, na ikiwa ni hivyo bado watakuwa na papara ya maisha.
Siku zote jambo lolote usilolijua vyema, na usilo na uhakika nalo lazima ulipaparikie.

Maandalizi ya Uzee ni muhimu na lazima kwa kijana yeyote anayehitaji familia na ukoo atakaouleta dunia uishi maisha salama yasiyo na hofu na mashaka,
Maandalizi hayo huanzia pale kijana anapofikisha umri wa kujitambua, na sio kipindi akiwa anatambulishwa yeye ni nani, ispokuwa ni kipindi ambacho maisha yatamfanya ajitambue yeye ni nani.
Hata hivyo hakuna muda mahususi wa mtu kujitambua, wapo wanaochelewa, wapo wanaowahi, na wapo ambao kamwe hawatawahi kujitambua mpaka siku wanalamba mchanga kuzimu.

Maisha pekee ndio humfanya mtu ajitambue,

MAISHA YANAKUFANYA UJITAMBUE KWA NJIA ZIFUATAZO;

1. MATATIZO, MIKOSI, CHANGAMOTO N,K
2. MAFANIKIO, KUFAULU, USHINDI nk

Mambo hayo mawili huletwa na wahusika aidha ni watu au wanyama au mimea.

Sehemu muhimu za mtu kuandaa uzee wake ni kama ifuatavyo;
1. AKILI
2. ROHO
3. MWILI
4. HISIA



Ukiwa kijana jambo la kwanza kulilinda ni Akili yako, akili ndio inayoongoza maisha ya mwanadamu, akili ndio hukufanya uwe na roho safi au chafu, mwili msafi au mchafu, hisia chafu au safi.

Lazima akili yako uipe chakula muhimu kitakachoshibisha bongo lako. Uwe na uwezo mzuri wa kutafakari, kuchambua mambo, kufanya maamuzi, kuwa na mtizamo chanya, falsafa na maarifa yenye manufaa.

Ukiwa kijana jambo muhimu kuliko yote unalopaswa kuwekeza ni kwenye akili, kwa sababu akili ndio utadumu nayo kwa muda mrefu kusaidia familia na ukoo wako.
Hakuna maisha pasipo Akili,
Hakuna kitu kinachoweza kutokea pasipo IMANI/ROHO, hata hivyo imani pasipo Akili ni upumbavu, ni maafa,
Akili ndio hujenga imani/roho, kuyafanya yale yasiyoonekana yaonekane kwa macho ya nyama, yawe mambo mazuri au mabaya, hiyo ndio akili.

Maisha ya mwanadamu yalivyo yanatokana na akili yake ilivyo, vile mtu anavyoishi ndivyo akili yake ilivyo, na bila shaka ndivyo roho yake ilivyo.

Ili akili ifanye kazi lazima iwe Falsafa, na mtizamo/attitude. Katika maandalizi ya Uzee lazima mtu aandae mtizamo na falsafa njema ambayo itamfanikisha, na ambayo watoto na kizazi chake watafanikiwa kupitia hiyo.

Mzee mwenye hekima humrithisha Mwanaye akili njema ili aweze kuishi maisha mazuri ayatakayo.
Kinachomfanya mtu/ukoo uwe tajiri sio mali walizorithi bali ni mtazamo na falsafa walizopewa na mababu zao.

Maandalizi ya Uzee ni kuishi kwa furaha. Na kuishi kwa furaha ni kuhakikisha dunia inakutumikia na sio uitumikie dunia.
Kuifanya dunia ikutumikie ni jambo kubwa sana linalohitaji akili zaidi, watu wengi duniani hawana raha kwa sababu wanaitumikia dunia, wamekuwa watumwa wa pesa, wamejigeuza misukule kwa kufanya kazi pasipo kuishi, lakini hii inapaswa iwe tofauti, dunia ndio ikutumikie wewe na sio wewe uitumikie. Sasa hapo kunahitaji akili ambapo kimsingi kuitumia inahitaji kujitoa.


Tuishia hapa

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Morogoro
 
Vijana mmepatwa na nini? Mbona mnaushikia bango uzee? Mtafika tu haina haja ya kukata denge.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom