Maalim Seif Sharif: Uvumilivu sasa basi, wanachama lindeni ofisi na mali za chama

mshihiri

Senior Member
Jul 15, 2011
138
86
UVUMILIVU SASA BASI, WANACHAMA LINDENI OFISI NA MALI ZA CHAMA

MAELEZO YA MSHAURI MKUU WA CHAMA CHA ACT – WAZALENDO, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
OFISI KUU YA CHAMA ZANZIBAR – TAREHE 2 DESEMBA, 2019

Chama cha ACT – Wazalendo kinazo taarifa za uhakika za kuwepo njama za kufanya vitendo vya kihalifu vyenye lengo la kuvuruga amani na utulivu nchini kwa kuvamia majengo mbali mbali yanayotumika kama Ofisi za Chama visiwani Unguja na Pemba.

Njama hizo ambazo zilipangwa zianze jana Jumapili, tarehe 1 Desemba, 2019 kisiwani Pemba na kisha ziendelezwe hapa Unguja zimepangwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini kwa kuwatumia mawakala na vibaraka wao wa Chama cha CUF ambao wamehakikishiwa kwamba watalindwa na dola. Sehemu ya malengo ya mpango huo ni kutaka kuwakamata viongozi wa ACT – Wazalendo na kuwabambikia kesi.

Baada ya kupangwa, jana Pemba kulifanyika majaribio kadhaa ya kutekeleza mpango huo muovu na uliokusudiwa kuleta shari na kuvunja amani.

Watu kadhaa wakiwemo vijana walioletwa kutoka Tanzania Bara, maalum kwa ajili ya kutekeleza njama hizo waliingizwa katika gari na kuzungushwa katika maeneo ya Mkoa wa Kusini Pemba yakiwemo Mkoani, Mtambile, Kangani na Chake Chake wakijaribu kutaka kutekeleza kazi waliotumwa. Bahati nzuri waliwakuta wenyeji wako vizuri, na wakiwa tayari kwa lolote na hivyo kushindwa kutekeleza uovu wao huo.

Maandalizi ya njama hizo yalianza mapema lakini yamekuja kuongezewa nguvu kupitia ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally hapa Zanzibar baada ya kuwasili usiku wa tarehe 25 Novemba, 2019.

Kwa wanaofuatilia ziara hiyo watagundua kwamba Dk Bashiru anaonekana kama vile amechanganyikiwa na amekuwa akitoa maneno makali ya vitisho huku akionekana amejawa na jazba na hasira nyingi. Katika moja ya hotuba zake, alipandwa na jazba mpaka akajisahau na kuwatangazia Watanzania na ulimwengu kwamba alitoa maelekezo kwa Jaji Mutungi ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwamba hana ruhusa ya kushiriki mkutano aliokuwa amealikwa kuzungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Alisahau kwamba kwa mujibu wa Sheria, Msajili wa Vyama vya Siasa hapaswi kupokea maelekezo kuhusiana na utendaji wake kutoka kwa mtu yeyote seuze Katibu Mkuu wa chama kimojawapo cha siasa ambacho kinapaswa kusimamiwa na Ofisi hiyo. Kwa kauli ile akatuthibitishia Watanzania na ulimwengu kwamba kumbe CCM huwa inamuelekeza Jaji Mutungi kipi afanye na kipi asifanye. Hadi muda huu tunapozungumza hatujamsikia Jaji Mutungi akijitenga na kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa CCM.

Tukirudi kwenye njama nilizozitaja, hata kabla ya mpango huo unaolenga kuvunja amani na utulivu hapa nchini, vitendo vya uchokozi wa makusudi dhidi ya ACT – Wazalendo vilianza kutekelezwa na vijana wa UVCCM kila Mkoa uliotembelewa na Katibu Mkuu wa CCM katika ziara yake hii kwa kupachua bendera za Chama chetu katika matawi yetu.

Tukio la kwanza la upachuaji wa bendera ya ACT - Wazalendo lilifanywa siku ya Jumatano, tarehe 27 Novemba, 2019 majira ya saa 6:00 mchana kwenye Ofisi ya Tawi la Bandamaji, Jimbo la Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Tukio jengine la upachuaji wa bendera ya ACT - Wazalendo lilifanywa siku ya Ijumaa, tarehe 29 Novemba, 2019 majira ya saa 5:00 asubuhi kwenye Ofisi ya Tawi la Mbuyuni, Michamvi, Jimbo la Paje, Mkoa wa Kusini Unguja. Matukio haya yameripotiwa Polisi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.

Hata hivyo, inaonekana kwa vile malengo ya kutaka kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu hayakufanikiwa, ndiyo sasa kumeratibiwa mpango mkubwa zaidi wa kufanya hujuma na uhalifu katika Ofisi za ACT – Wazalendo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba ikiaminiwa na wanaosukuma mpango huo kwamba hatua kubwa kama hiyo itachochea hasira miongoni mwa viongozi na wanachama wa ACT – Wazalendo na kufanikisha uovu wao huo.

Maamuzi ya mwisho ya kuendelea na njama hizo yalifanywa katika kikao cha Katibu Mkuu wa CCM na viongozi wa chama hicho kilichofanyika usiku wa Jumamosi, tarehe 30 Novemba, 2019 hapo Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar iliopo Kisiwandui.

Mbali na njama hizo, kikao hicho pia kiliazimia kuiagiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi na kuufikisha kwenye mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea kipindi hichi kwa hati ya dharura, Mswada ambao utaweka sharti la kwamba ili mtu aweze kugombea Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani basi ni lazima mtu huyo awe mwanachama wa chama cha siasa anachogombea kupitia kwacho kwa angalau miaka mitatu (3) kabla ya tarehe ya uchaguzi. Lengo la njama hii lililoelezwa kwenye kikao hicho cha Kisiwandui ni kutaka kuwazuia wanachama wa ACT – Wazalendo waliojiunga na chama hichi kuanzia mwezi Machi mwaka huu wasiweze kugombea uchaguzi na kwa kufanya hivyo CCM wanadhani wataweza kujiondolea upinzani mkali unaowakabili hapa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.

Labda wananchi wanaweza kujiuliza kwamba nini kilichosababisha CCM na Katibu Mkuu wake, Dk Bashiru Ally kuchanganyikiwa kiasi hichi mpaka kujiingiza kwenye njama hizi. Sababu hasa ni hizi zifuatazo:

1. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Dola iliagiza kufanywa utafiti maalum kuhusu hali ya kisiasa na nguvu za vyama zilivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao Zanzibar. Utafiti huo ulionesha kwamba CCM inaungwa mkono na asilimia 36 tu ya wananchi wa Zanzibar huku ACT – Wazalendo ikiungwa mkono na asilimia 64 ya wananchi wa Zanzibar. Hali hii imewatia hofu na kiwewe Chama Cha Mapinduzi.

2. Baada ya kuyaona matokeo ya utafiti huo ulioendeshwa kimya kimya, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwaalika baadhi ya wachambuzi mashuhuri wa siasa za Zanzibar (kila mmoja kwa wakati wake peke yake) na kuwataka wampe mitazamo yao na maoni yao kuhusu kwa nini CCM inapoteza mvuto kila uchao Zanzibar. Wachambuzi hao walimueleza ukweli wa mambo kuhusu siasa za Zanzibar ambao ulizidi kumkatisha tamaa Dk Bashiru.

3. Jitihada za kuanzisha Kampeni na Mikakati mbali mbali ya kujaribu kuwavuta wapiga kura na hasa vijana kukiunga mkono CCM zilizoanzishwa na CCM Zanzibar kwa kushirikiana na SMZ zote zimekwama. Wametumika watu mbali mbali walioaminika kuwa wanaweza kuwa na mvuto kwa vijana na pia kutumika vishawishi kama ajira na nafasi za masomo lakini yote haya yameshindwa kufua dafu na CCM bado inakimbiwa.

4. Baada ya CCM Zanzibar kukataliwa katika Mikoa miwili ya Pemba na kisha kupoteza nguvu zake za kisiasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini Unguja, tegemeo lao lilibaki Mkoa wa Kusini Unguja. Bahati nzuri wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja hususan Vijana nao wameamka na wameamua kukipa talaka tatu CCM. Ukweli huo wameelezana mpaka kwenye vikao vya ndani vya chama chao vya Mkoa huo. Hata hizi kauli za vitisho zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Mkoa huo ni katika juhudi za mwisho za kujaribu kunusuru hali lakini bado wananchi wa Kusini Unguja wamewagomea na sasa wameamua kuungana na Wazanzibari wenzao kudai MABADILIKO.

5. Kushindwa kwa Serikali iliyojiweka madarakani kwa nguvu Zanzibar kutekeleza jambo lolote la maana la maendeleo tokea mwaka 2016 na kuyafanya maisha ya Wazanzibari yazidi kuwa magumu kumepelekea wananchi wa Zanzibar kuzidisha ari ya kutaka MABADILIKO na hasa baada ya kuonja ladha ya ushindi wa wazi wa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ambao CCM ilitumia Dola kuufuta. Wananchi wa Zanzibar wanashangazwa na wanawaona kioja watawala wanapopigana vikumbo kujisifia na kwenda kuzindua miradi ya watu binafsi baada ya watawala hao na Serikali yao kushindwa kutekeleza mradi wowote wa maana wa kunyanyua hali za maisha ya wananchi. Kama hilo halitoshi wananchi wanaona jinsi rushwa na ufisadi ulivyokithiri Serikalini ambapo wakubwa wanajitajirisha wao na familia zao huku wakiwaacha watumishi wengine wa umma na wananchi kwa ujumla wakiangamia.

Ni sababu hizo na nyenginezo, ambazo kwa kutotaka kuwachosha sikuzieleza hapa, ndizo zilizomfanya Dk Bashiru Ally kuja Zanzibar kwa kile alichokieleza kwamba kaja “kukijenga Chama”. Nilimtegemea Dk Bashiru kwa kutumia elimu yake ya Sayansi ya Siasa angeweza kutambua kwamba hakuna chama cha siasa kinachoweza kujengeka kwa siku

10. Na pengine ameliona hilo na ndiyo maana sasa wameamua kuandaa njama nilizozitaja.

MAELEKEZO YETU
CCM inatambua kwamba haijawahi kushinda uchaguzi mkuu wowote Zanzibar tokea uchaguzi mkuu wa mwanzo wa vyama vingi mwaka 1995. Imeshatufanyia maovu na mabaya mengi Wazanzibari ili kulazimisha kubakia madarakani huku wakitambua kwamba Wazanzibari tumewakataa.

Kwa kutambua mitafaruku tuliopitia kama nchi na kuona haja ya kutibu majeraha ya historia, mimi na mwenzangu, Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Mheshimiwa Dk Amani Karume, mwaka 2009 tulianzisha Maridhiano ambayo hatimaye yaliungwa mkono na asilimia 66.4 ya Wazanzibari walioridhia mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tulifanya hivyo kwa kuamini kwetu kwamba amani na utulivu wa Zanzibar utapatikana tu kwa Wazanzibari kufanya kazi pamoja.

Bahati mbaya CCM ya sasa imeyahujumu hata Maridhiano hayo ya Wazanzibari.
Kama hayo hayakutosha, CCM ikitumia Dola imeuhujumu uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 na kujitwalia madaraka kinyume na ridhaa ya Wazanzibari, ikamtumia Msajili wa Vyama vya Siasa (ambaye sasa inajigamba uwanjani kwamba inamuelekeza) kutuingizia mgogoro kwenye chama tulichokuwepo, na mwisho kuitumia Mahakama kukamilisha malengo yao.

Tumewaachia chama vibaraka wao lakini inaonekana bado hawajaridhika. Sasa wamepanga kuwatumia vibaraka wao huo kuzusha fujo na kuvunja amani ya nchi wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Tunasema IMETOSHA, SASA BASI!
Kwa namna ya pekee, na kwa niaba ya Chama, nawapongeza viongozi na wanachama wetu walioko Pemba kwa kujipanga na kujiandaa kikamilifu jana kuzihami Ofisi za Chama chao.

Wameonesha mfano halisi wa jinsi tunavyopaswa kwenda na tutakavyokwenda kuanzia sasa katika kukabiliana na upuuzi wowote utakaopangwa dhidi yetu.

Baada ya maelezo hayo, sasa kupitia mkutano huu na waandishi wa habari, maelekezo yetu ni kama ifuatavyo:

1. Chama cha CUF kimefungua Kesi ya Madai Nam. 16 ya 2019 na kupitia kesi hiyo pia Ombi la Madai Nam. 19 la mwaka 2019 katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kuhusiana na majengo hayo, na huko wametakiwa kuthibitisha umiliki wa majengo hayo iwapo ni ya chama chao kama wanavyodai. Shauri hilo bado linaendelea. Kujaribu kuwatumia CUF kusababisha fujo kwa jambo ambalo tayari CUF wenyewe wamelipeka Mahakamani hakukubaliki na sisi HATUTOLIKUBALI hilo.

2. Hatutakubali majengo yanayotumika kama Ofisi za ACT – Wazalendo kusogelewa seuze kuvamiwa na kuchukuliwa na wahuni. Tutayalinda kwa njia zote na zozote majengo hayo ambayo ni mali za watu mbali mbali waliyoyakabidhi kwa Chama chetu kuyatumia kama Ofisi halali za ACT – Wazalendo.

3. Tunawataka viongozi na wanachama wetu wa ngazi zote Unguja na Pemba, mjini na mashamba kuanzia muda huu kuzilinda Ofisi zote za Chama chao na kutoruhusu mhuni yeyote au kikundi chochote cha wahuni kuzisogelea, achilia mbali kuzivamia na kuzichukua Ofisi hizo za Chama.

4. Uvunjifu wowote wa amani utakaosababishwa na wahuni hao kujaribu kuyasogelea majengo tuliyokabidhiwa kihalali iwe kwa kuazimwa au kwa kukodishwa kuyatumia kama Ofisi za Chama chetu jukumu lake litabebwa na wahuni hao na wale wanaowatuma na kuwalinda.

5. Tumevumilia mambo mengi tuliyofanyiwa. SASA BASI!

Ahsanteni

Seif Sharif Hamad
Mshauri Mkuu wa Chama.
ACT-Wazalendo.
 
Lini ACT wakawa na ofisi?

Huyo bwana Zitto anajua muda wake wa kuwa mbunge umeisha anatapa tapa
 
FB_IMG_1575294419931.jpg


Mpaka mwaka mmoja uliopita CCM ilikuwa inaungwa mkono na Wazanzibar 13% tu, lakini Alhamdulillah, safari hii wamepanda hadi 36% huku CUF ikiwa imepotea kabisa.

Chama kinachoungwa mkono na Wazanzibar wengi 64% ni ACT Wazalendo.
 
sijasoma maelezo yote kwa sababu ya ufinyu wa muda ila swali la msingi je ACT WAZALENDO wametoa taarifa kwenye vyombo vya dola kuhusu hizo tetesi? na je ikigundulika ni udaku na propaganda za kisiasa wako tayari kuchukuliwa hatua kuhusu huu uvumi
 
Takwimu hii haiwezi kuwa kweli CCM ipendwe zb kwa lipi Yani itoke 13 mpk 30+ kwa lipi ? Labda kwasababu shein ni mpole na mtaratibu ila wazenz wakiiangalia CCM kwa jicho la kumtazama meko asilimia zinatakiwa zishuke hakuna lolote atakalolifanya meko duniani na mbinguni litakalokuwa na kibali chema machoni pa mbingu na Ardhi.
 
Takwimu hii haiwezi kuwa kweli CCM ipendwe zb kwa lipi Yani itoke 13 mpk 30+ kwa lipi ? Labda kwasababu shein ni mpole na mtaratibu ila wazenz wakiiangalia CCM kwa jicho la kumtazama meko asilimia zinatakiwa zishuke hakuna lolote atakalolifanya meko duniani na mbinguni litakalokuwa na kibali chema machoni pa mbingu na Ardhi.
Mkuu mimi nimenukuu Maalim
 
Na baada ya Bashiru kutoa povu alilolitoa huko hata hiyo 34% lazima iwe imeshuka, maskini Lipumba katumika vibaya kweli bora angelowea ughaibuni nae leo angekuwa balozi.
 
Lakini pamoja na kuungwa mkono na asilimia 36% ukifanyika Uchaguzi lazimaCCM ISHINDE kwa asilimia 99.9%
 
"Alhamdulillah , safari hii wamepanda hadi 36% , huku cuf ikiwa imepotea kabisa"

Yaani Maalim Seif anamshukuru Mungu kwa "mafanikio" ya ccm?! Tunaposema huyu mzee ni ajenti wa system tunazodolewa kwa vile kuna "wapinzani" wanamkubali sana!
 
mshihiri, Kwa mahali tulipofikia kisiasa tunahitaji kauli thabiti kutoka kwa viongozi thabiti katika kutetea haki zilizopo kikatiba na kisheria. Hakuna kupindisha maneno, ifike mahali iwe basi.
 
Back
Top Bottom