Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza kuwa iko siku atakuwa Rais wa Zanzibar, licha ya kuwepo watu wanaomwombea kifo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, alitoa tamko hilo jana, alipokuwa katika ziara ya siku tano inayoendelea kisiwani Pemba, kuelezea hali ya kisiasa Zanzibar, baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, uliofutwa na wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
Akizungumza na watendaji na viongozi waandamizi wa chama hicho katika Wilaya ya Micheweni, Kaskazini Pemba, Maalim Seif alisema baada ya afya yake kuzorota na kupatiwa matibabu nchini India na baadaye Hindu Mandal, Dar es Salaam, kuna watu walimwombea kifo kupitia mitandao ya kijamii.
"Nashukuru Mungu baada ya kupatiwa matibabu India na kurudi salama salmini, nilipata matatizo na kutibiwa Hindu Mandal. Madaktari walijitahidi nikapata nafuu na sasa niko ngangari kinoma pamoja na taarifa za mitandao kuwa nipo mahututi. Wapo walioomba nife wakati hakuna anayeweza kufa bila matakwa ya Mwenyezi Mungu," alisema.
Alisema anamwomba Mwenyezi Mungu amuweke hai hadi aiongoze Zanzibar na wakati umefika kutokana na mabadiliko makubwa ya utawala yanaoendelea tangu kuanzishwa kwa vyama vingi nchini.
Aliongeza kuwa pamoja na kufanyika uchaguzi wa marudio na kuundwa kwa serikali, mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar bado haujamalizika kwa kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulifutwa kinyume cha Katiba na CUF itaendelea kupigania uamuzi wa wananchi walioutoa Oktoba 25, mwaka jana.
Alisema mgogoro wa sasa kuhusu uchaguzi wa mwaka jana, umekuwa tofauti na miaka yote kwa vile CUF ina ushahidi wa vielelezo vya matokeo kinyume cha uchaguzi wowote uliopita, kwa sababu walikuwa wakilalamika bila ushahidi.
"Wasidhani mambo haya yamekwisha. Tuna ushahidi wa kutosha kuwa tulishinda kwa kura 28,000 na hatutakubali hadi haki itendeke kupitia uchaguzi huo kama walivyokuwa wameamua wananchi," alisisitiza.
Alisema CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi imeamua kuweka azimio la kutoitambua serikali ya Zanzibar chini ya Dk. Ali Mohamed Shein na kwamba mwanachama au kiongozi atakayekwenda kinyume, atachukuliwa hatua, ikiwamo kufukuzwa, kwa sababu atakuwa msaliti.
Kuhusu wabunge wa upinzani, alisema wamefanikiwa kuichachafya serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, ndiyo maana wameamua kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya bunge ili kuficha aibu inayotokea juu ya utendaji wa serikali.
Alisema hiyo inadhihirisha kuwa waunge wa upinzani wanaendelea kufanya kazi nzuri ya kupigania maslahi ya wananchi ndani ya bunge.
Source: Nipashe