Maalim Seif: Haki ya Wazanzibari itapatikana baada ya miezi 3, RITA kufikishwa Mahakamani

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,789
11,931
Heshima kwenu wakuu,

Leo maalim Seif anaongea na Waandishi wa Habari.

Ntawaletea Updates.
f7d5e955457e05657e125cf327ec40d7.jpg
5edd35dae9c80c0eb17ddc41c2036db6.jpg

========

UPDATES

=========

11:40Hrs

Maalim Seif: Nawashukuru wahariri wa vyombo vyote vya habari

=> Tarehe 9 April nlitoa maelezo ya kutosha kuhusu mbinu chafu za RITA kwa maelekezo ya dola na msajiri wa vyama vya siasa.

=> RITA imekubali kutumiwa katika mpango haramu, kwani RITA imetekelezwa walichoagizwa kusajiri wajumbe fake wa CUF. Baada ya RITA kuona watu wanalalamika, wameanza kusema wanafanyia kazi watu waliofanya hivyo.

=> Tunazotarifa kwamba mkurugenzi wa RITA ameshinimizwa kupitisha majina ya watu feki wa prof. Lipumba. Aliandika barua kwa katibu mkuu wa CUF alisema alifanya usajili huo kutokana na barua mbili alizoandikiwa na Msajili wa vyama vya siasa. Wakati akihojiwa na Gazeti la Mwananchi kwanini amesajili najina feki ya bodi ya CUF, Mama Emmy alisema wa kuulizwa ni Msajili wa vyama vya Siasa. Lakini sheria hamuambii kufanya kazi kutegemea msajili wa vyama vya siasa.

=> Bodi ya CUF ilisajiliwa Mwaka 1993 na kupatiwa namba ya Usajili. CUF tunafanya mabadiliko kila inapobidi na kulipia ada ya bodi ya wadhamini kila mwaka hadi 14May 2017 RITA. CUF kupitia baraza kuu la taifa la mwaka 2014 ikifanya mabadiliko machache ya bodi ya Wadhani.

=> RITA si kwamba amefanya kitu ambacho hakifahamu, bodi ilipomfungulia kesi msajili wa vyama vya siasa, msajili aliwasiliana na RITA ili kujinusuru tarehe 14/11/2016 akiomba kusaidiwa kugushi barua ya ya bodi ya CUF kwamba hailipii ada na haipo kihalali na RITA walitii. Msajili wa vyama vya siasa alifuta vyama ambavyo havikidhi vigezo lakini CUF haijafutwa. Huu ni mwendelezo wa RITA kwa CUF.

=> Baada ya kugundua chama kina nyaraka halali za Malipo hadi 2016. Wamebuni mbinu mpya;

Kwanza wanataka kufuta kesi zote

Mbili kufungua acc. Mpya ili kumuezesha kibaraka Lipumba kupata Luzuku na kumuondoa katibu mkuu wa CUF.

=> Vibaraka wa Lipumba walianza kuandika kwenye mitandao kwamba Mambo yote yamekwisha.

=> Azimio la bodi feki ni kufuta kesi zote dhidi ya Msajili na kesi zote zinazomkabili Kibaraka Lipumba. Sisi CUF tumeshitushwa na vitendo vinavyofanywa na Taasisi kubwa kama RITA. RITA wanasukumwa na utashi binafsi wa kifisadi

HATUA TUNAZOZICHUKUA

Kamati tendaji ya taifa ilikutana Zanzibar na kuazimia yafuatayo

1. Tutafungua kesi dhidi ya RITA kwa kutofuatilia majina bodi

2. Kuitaka mahakama kuu kusimamisha kesi zote hadi maamuzi ya RITA yatakapo amuliwa.

Amemaliza Maalim Seif.

Hapa wapo Wabunge 40 kati ya 42 wabunge wa CUF.

Maswali

1.Kila siku mnasema haki ya Wazanzibar inakuja, je itakuja lini?

Je hakuna njia nyingine ya haraka zaidi ya hii ya mahakamani?

Mumesema mnaenda mahakamani, kuna tofauti gani na wale wanaofuta?

Seif anajibu:

Tuanze na swali la Nyamla kuhusu kuwapora Wazinzabar

Nasema haki inakuja na si muda mrefu. Mimi nina hakika haizidi miezi mitatu haki itapatikana.

Kwanini sikubali kukaa na Lipumba? Je nikae na Lipumba kama nani? Lipumba alikuwa mwenyekiti wetu wa CUF mwenyewe akajiuzulu. Yeye si mwenyekiti wa CUF. kutokana na fujo alizofanya ubungo kwa kuleta wahuni juchafua mkutano, baraza kuu la CUF la taifa lilimfukuza uanachama. Huyu ni mwenyekiti wa Msajili. Ndo maana anafanya hujuma dhidi ya CUF.

Kumbuka maamuzi hakuyachukua Maalim Seif bali baraza kuu la Uongozi la Taifa na Mkutano mkuu, mimi kama Seif sina uwezo wa kubatilisha maamuzi ya vikao vya kuu.

Henry: Je hakuna njia nyingine? Kama una ushauri tushauri, sisi hatuoni kama kuna njia nyingine zaidi ya Mahakama. Hata ikachukua muda mrefu. Haki haizami wala haiozi. Ila tunapokea mawazo cha kufanya.

Recho: Sisi tunaenda kusimamisha kesi, wale wanaenda kufuta kesi. Kuna bodi ya wadhamini halali na bodi ya wadhamini feki iliyopelekwa na Lipumba. Nasema ni bodi feki sababu mamlaka ya kuteua bodi yapo chini ya baraza kuu la CUF. eti Msajili naye kamshauri naye ateue wake. Akaenda kuwachukua adc, ccm nk. Ndo maana twaita feki.

Wanafikiri kwa kutuhangaisha huku wazanzibar hawatapata haki yao. Mimi nina uhakika kabisa na sina Wasiwasi haki ya Wazanzibar itapatikana. Msajili tunamshitaki Msajili kaiba fedha zetu za Luzuku wakagawana na Lipumba ndo maana anahaha kesi zifute. Thomas ana kesi mbaya sana ya kugushi.

Bi hawa kauliza, Cuf imegawanyika pande mbili na luzuku anapewa lipumba je mnaishije? Anajibu kwamba hakijagawanyika mara mbili bali wajumbe wa baraza kuu ni sitini wanaomfuata lipumba ni watano. Wabunge ni 42 wanamfuata Lipumba ni 2.

Hakuna pande mbili bali chama cha CUF dhidi ya kikundi cha wahuni wa Lipumba. Lipumba alipewa luzuku mara moja mahakama ikazuia. Sisi ni chama cha wananchi, tuna wabunge 40 tunawashukuru sana wabunge wamejitolea kwa hali ya juu na wanachama wanachangia. Hiki ni chama mtu kaingia mwenyewe kwa mapenzi hivyo wanakichangia. Luzuku yetu imehifadhiwa tu. Tutaanza kuzunguka kifua mbele.

Kila siku tulisema tunaheshimu maamuzi ya mahakama, lakini sasa tumeshawaagiza hii RITA ishughulikiwe kwa mjibu wa Sheria, hatutavunjika moyo na maamuzi ya mahakama ya kesho. Hatuwezi kuchezewa na kibaraka mmoja. Mapambano yanaendelea. Kitu tusichotaka ni fujo na Vurugu, tunataka kufuata sheria ya nchi na sheria ipo upande wetu.

=======

FULL TEXT

=======

MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CUF, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA WA WATANZANIA KWA UJUMLA JUU YA MUENDELEZO WA HUJUMA ZINAZOFANYWA NA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI JAJI FRANCIS MUTUNGI DHIDI YA CUF KWA KUTUMIA WAKALA WA USAJILI, UFILISI NA UDHAMINI (RITA)

PEACOCK HOTEL, DAR ES SALAAM, TAREHE 28 JUNI, 2017

Ndugu zangu wahariri na waandishi wa habari,

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana leo hapa. Nitumie fursa hii pia kuwapa mkono wa Eid Mubarak Waislamu wa hapa nchini pamoja na Waislamu wengine duniani wanaoendelea na maadhimisho ya sikukuu ya Eid-el-Fitr kufuatia kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Pili, nawashukuru na nyinyi Wahariri na waandishi wa habari kwa kupokea mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano huu. Siku zote mmetupa mashirikiano makubwa katika shughuli zetu na kuufikisha ujumbe wetu kwa umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla. Ahsanteni sana.

Ndugu Wahariri na waandishi wa habari, mtakumbuka vyema tarehe 9 Aprili, 2017 katika ukumbi wa Hotel ya Ramada Encore Dar City Centre jijini Dar es Salaam, nilitoa maelezo ya kutosha kuhusu mbinu chafu iliyopangwa kufanywa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa maelekezo ya Dola kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa lengo la kumnusuru kibaraka wao Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuhakikisha kwamba Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini feki waliopelekwa na kibaraka Lipumba wanasajiliwa baada ya kuona Bodi halali ya CUF - Chama Cha Wananchi ni kikwazo katika kufanikisha mipango yao haramu ya kufungua akaunti mpya ya benki ili kuwezesha wizi wa ruzuku ya Chama.

Katika mkutano huo, nilifafanua pia na kueleza kwa kina hujuma zinazofanywa na dola dhidi ya CUF - Chama Cha Wananchi hasa baada ya mafanikio makubwa na ushindi wa kutosha uliopatikana Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba, 2015. Sitoyarejea tena hapa niliyoyaeleza siku ile.

RITA YAKUBALI KUTUMIWA KATIKA MPANGO HARAMU

Niseme tu kwamba yale tuliyoyaeleza tarehe 9 Aprili yamethibitika wiki iliopita kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kutekeleza alichoagizwa kufanywa ambacho ni kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini ya CUF. Mtaona utekelezaji umechukua muda kwa sababu inaonekana baada ya kuzieleza njama zile hadharani na nyinyi vyombo vya habari kuziandika, RITA walishtuka na kudai bado wanayafanyia kazi maombi yaliyowasilishwa na wanahitaji kujiridhisha juu ya uhalali wa vyombo vilivyofamya mabadiliko yaliyowasilishwa kwao.

Nilieleza siku ile kwamba tokea kuanza kwa njama ovu na mbinu chafu hizi, moja ya vinavyoonekana vikwazo vikubwa vinavyokwamisha kufanikiwa malengo ya wanaomtumia kibaraka Ibrahim Lipumba imekuwa ni Bodi ya Wadhamini ya THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - Chama Cha Wananchi) ambayo imechukua hatua madhubuti za kukilinda Chama na; hususan, rasilimali zake kupitia Mahakama na taratibu nyingine za kiutawala na kisheria. Hatua hizo zilizochukuliwa na Bodi ya CUF ni kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya mwaka 1992(Toleo la 2014) kifungu cha 98(4) ambayo nanukuu:

"98(4) - Bodi inaweza kushtaki au kushitakiwa kwa niaba ya Chama"


Aidha mamlaka hayo yamebainishwa katika Sheria ya Wadhamini (The Trustees' Incorporation Act Cap.318), kifungu cha 8(1)(b), nanukuu:

"8(1) Upon the grant of a certificate under subsection (1) of section (5), the trustee or trustees shall become a body corporate by the name described in the certificate, and shall have;-

(b) power to sue and be sued in such corporate name"

Tunazo taarifa zisizo na shaka kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA amepata shinikizo kubwa kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini ya CUF kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na kibaraka Lipumba ili kuhujumu majina halali yaliyopitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kupitia kikao chake kilichofanyika Makao Makuu ya Chama Zanzibar, tarehe 19 Machi, 2017. Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa RITA amenukuliwa na vyombo vya habari kukiri hivyo alipohojiwa akiwa Dodoma kama ilivyonukuliwa na gazeti la Mwananchi toleo Na.6176 la tarehe 25 Juni, 2017. Aidha katika barua aliyomwandikia Kaimu Katibu Mkuu (cheo ambacho hakipo kwenye Katiba ya CUF), amebainisha wazi wazi kuwa usajili huo wa wajumbe feki wa Bodi ya CUF umezingatia barua mbili alizoandikiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa zenye Kumb. Na. CHA.322/362/14/23 ya tarehe 4/4/2017 na Kumb. Na. CHA.322/362/14/30 ya tarehe 11/5/2017. Wakati akihojiwa na gazeti la Mwananchi, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Mama Emmy Hudson, amejitetea na kuweka wazi kuwa mtu mahsusi wa kutoa majibu ya kwa nini yamesajiliwa majina feki ya Bodi ya CUF ni Msajili wa Vyama vya Siasa.

Pamoja na kwamba utetezi huo haumwondoi Mama Hudson kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka kutokana na kwamba anayesajili Bodi sio Msajili ya Vyama vya Siasa bali ni yeye (RITA) na sheria inamtaka kujiridhisha na nyaraka zinazowasilishwa kwake na waombaji. Suala hilo limefafanuliwa vizuri na yeye mwenyewe kupitia taarifa yake kwa umma ya tarehe 29 Machi, 2017. Katika ibara ya (3) ya taarifa hiyo Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA, Mama Emmy K. Hudson anasema (nanukuu):

"Tarehe 27 Machi, 2017 Wakala ulipokea maombi ya Usajili wa Bodi mpya ya Wadhamini ya CUF. Kwa mujibu wa utaratibu, maombi hayo yakipokelewa hupitia katika hatua ya uchambuzi wa taarifa zilizowasilishwa ili kujiridhisha sababu za mabadiliko hayo, na kuangalia iwapo taratibu zilifuatwa katika upatikanaji wa wadhamini hao kwa kuzingatia maamuzi ya mkutano uliohusika kupitisha mabadiliko hayo, hii ni kwa mujibu wa kifungu 17(a). Hatua hii bado haijakamilika."

Maelezo hayo yamenukuliwa kutoka kwenye Sheria ya Wadhamini (The Trustees' Incorporation Act Cap. 318), kifungu cha 17(a) kinachotamka ifuatavyo:

"17 - No changes of the names of a person who is or who were trustee or trustees of a body corporate or organization incorporated under this Act shall be authorised by the Registrar-General unless he is satisfied that-

a) There were held a lawful meeting of the body corporate or organization for the purpose of electing a person or persons as trustees of such a body corpotate or organization."

Ndugu Wahariri na waandishi wa habari, kwa sababu ya kutaka uelewa fasaha wa hujuma iliyofanywa na RITA akishirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa na kibaraka wake Lipumba kuhusiana na Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF - Chama Cha Wananchi), naomba kutoa maelezo ufafanuzi.

Bodi ya Wadhamini ya CUF ilisajiliwa mwaka 1993 kwa kufuata taratibu zote za kisheria (Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258 na The Trustees' Incorporation Act Cap. 318) na kupatiwa hati ya usajili Na. ADG/T.1/1127. Sheria ya Wadhamini (The Trustees' Incorporation Act Cap. 318) kifungu cha 8(1a) kinasema Bodi iliyosajiliwa ni endelevu isipokuwa kama imefutwa. Hapa nanukuu:

"8(1). Upon the grant of a certificate under subsection (1) of section (5) the trustee or trustees shall become a body corporate by the name described in the certificate, and shall have;-

(a) perpetual succession and common seal"

CUF - Chama Cha Wananchi kimeendelea kuheshimu na kutekeleza matakwa ya sheria hiyo kwa kuweka sawa kumbukumbu za Bodi yake na kufanya mabadiliko kila ilipobidi kwa mujibu wa Katiba ya Chama kifungu 98(1) na kuwalipia wadhamini ada ya kila mwaka (return of trustees) ambayo kwa sasa ni Tshs. 50,000/=. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF walifanyiwa mabadiliko madogo mara ya mwisho mwaka 2012 na imeendelea kulipiwa ada ya wadhamini ya kila mwaka hadi tarehe 24 Mei, 2017 kwa mujibu wa kumbukumbu ya stakabadhi ya malipo iliyotolewa na RITA tarehe 24 Mei, 2016 yenye Na.105888047. Kwa mantiki hiyo mabadiliko mengine ya wajumbe wa Bodi yalipaswa kufanya mwaka huu wa 2017.

CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililochaguliwa kihalali kupitia Mkutano Mkuu wa Taifa wa mwezi Juni mwaka 2014 na kwa kufuata masharti mapya ya Katiba ya 1992 (Toleo la 2014) ilifanya mabadiliko machache ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini tarehe 19 Machi, 2017 na kuyawasilisha kupitia barua ya Katibu Mkuu Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/RT/001 ya tarehe 24 Machi, 2017 kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA). Aidha pamoja na barua hiyo Fomu T.I.4 (Notification) na T.I.5 (Return of Trustees) na malipo ya Tshs. 100,000/= yalifanywa na kupatiwa stakabadhi mbili; Na.14995169 (Notification) na Na.14995170 (Return of Trustees) zote za tarehe 27 Machi, 2017.

Kuthibitisha kupokelewa kwa mabadiliko hayo, Msimamizi wa Wadhamini RITA alikiri kwa barua Kumb. Na.ADG/T.1/1127/29 ya tarehe 31 Machi, 2017 aliyomwandikia Katibu Mkuu wa CUF - Chama Cha Wananchi. Katika barua hiyo, Msimamizi wa Wadhamini alimjulisha Katibu Mkuu kuwa pindi taratibu zitakapokamilika atamtaarifu. Mpaka ninapozungumza nanyi hapa, Katibu Mkuu hajataarifiwa chochote, jambo ambalo linakinyima Chama chetu hata haki ya kukata rufaa kwa Waziri kwa mujibu wa sheria ya Wadhamini (The Trustees' Incorporation Act Cap. 318), kifungu cha (27) kama kilivyonukuliwa hapa:

"27. Appeals

Any person aggrieved by the refusal of the Administrator-General to grant a certificate of incorporation or to approve a change of name, or by any conditions or directions inserted in any certificate of incorporation, or by the revocation of the incorporation of any body corporate may within twenty-one days after the notification of such refusal, conditions or directions or revocation, as the case may be, appeal to the Minister responsible for legal affairs and the Minister may make such order as the circumstances may require and except as aforesaid no appeal shall lie against any such refusal, conditions or directions or revocation."

Hata hivyo, mara baada ya kuwasilisha mabadiliko hayo, kibaraka Ibrahim Lipumba naye akatakiwa na Msajili haraka aandae majina yake na kuyafikisha RITA na kwamba Ofisi ya Msajili itatoa maelekezo kwa RITA nini wafanye. Ni dhahiri barua mbili za Msajili wa Vyama vya Siasa za tarehe 4/4/2017 yenye Kumb. Na. CHA.322/362/14/23 na tarehe 11/5/2017 yenye Kumb. Na. CHA.322/362/14/30 zilizonukuliwa na RITA katika barua ya kuitambua Bodi feki ya kibaraka Lipumba zinahusika na maelekezo hayo.

Lakini pamoja na maelekezo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, RITA si kwamba amefanya kitu ambacho hakifahamu. Mwezi Novemba, 2016 baada ya Bodi kumfungulia kesi Msajili wa Vyama vya Siasa (Shauri Na. 23/2016 ambalo liko Mahakama ya Rufaa), Msajili wa Vyama vya Siasa katika hatua za kutaka kujinusuru na mkono wa sheria aliwasiliana na RITA kupitia barua Kumb. Na. HA.322/362/14/30 ya tarehe 14 Novemba, 2016 akiomba kusaidiwa kughushi kumbukumbu za Bodi ya CUF ili ionekane Bodi imepita muda wake na hailipii ada zake tangu mwaka 2010.

Msajili wa Vyama vya Siasa akiwa Jaji wa Mahakama Kuu alifanya hivyo akijua fika kuwa anachomshawishi RITA kufanya ni kosa la jinai na ikizingatiwa kuwa mwezi Oktoba, 2016 alikamilisha uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili kwa vyama vya siasa vyote nchini, ambapo alivifuta vyama kadhaa visivyokidhi masharti hayo na CUF - Chama Cha Wananchi hakikuwa miongoni mwa vyama visivyokidhi masharti. Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa Kumb. Na. HA.322/362/01/21 ya tarehe 24 Oktoba, 2016 kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu ni ushahidi wa zoezi hilo la uhakiki.

Baada ya kupata taarifa hizo za muendelezo wa hujuma za Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia RITA, Katibu Mkuu wa CUF aliandika barua Kumb. Na. CUF/HQ/BRT/005/016/12 ya tarehe 10 Oktoba, 2016 kuitahadharisha RITA juu ya mipango hiyo iliyokuwa ikiratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Barua hiyo ya Katibu Mkuu iliambatanishwa na nyaraka za kughushi za Msajili wa Vyama vya Siasa na mfuasi wa kibaraka Lipumba anayeitwa Thomas Malima akijitambulisha kama Katibu wa Bodi zilizopelekwa Bank ya NMB Ilala katika harakati za kutaka kuiba fedha za ruzuku ya Chama.

Jambo la ajabu RITA licha ya kuwa na jopo kubwa la wanasheria, ilikubali ombi la Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa barua Kumb. Na. ADG/T.1/1127/16 ya tarehe 15 Novemba, 2016 iliyosainiwa na Afisa wake anayeitwa Gilbert P. Bubelwa iliwasilisha nyaraka za kughushi zilizoambatanishwa kwenye hati ya kiapo ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kupinga kufunguliwa kwa shauri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Jambo la kushangaza wameghushi mpaka sahihi ya kibaraka Lipumba licha ya kwamba ni mshirika wao.

Ndugu wahariri na waandishi wa habari, baada ya kugundua kuwa Chama kinazo nakala halisi na stakabadhi za malipo hadi mwaka 2016 na kwa hivyo nyaraka zao za kughushi haziwezi kuwasaidia, ndipo wakaja na njama hii ya pili ya kusajili Bodi feki kwa malengo makuu manne yafuatayo:-

1) Kufuta kesi zote zilizofunguliwa na ambazo zinawaelemea licha ya kutumia nguvu kubwa ya dola.

2) Kufungua akaunti mpya ya benki ili kumwezesha kibaraka Lipumba kupata ruzuku.

3) Bodi hiyo kuwezesha udhibiti wa Ofisi za Makao Makuu, Zanzibar.

4) Kumwondoa madarakani Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na hivyo kufanikisha njama za kuwapokonya haki yao Wazanzibari kwa maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015.

Baada ya kupata taarifa za uhakika juu ya njama hizo ovu, na kupata stakabadhi ya malipo ya kibaraka Lipumba ya mabadiliko ya wajumbe wa Bodi yenye Na. 14995179 ya tarehe 27 Machi, 2017 iliyotolewa na RITA, Katibu Mkuu wa CUF alimwandikia tena barua RITA yenye Kumb. Na. CUF/HQ/AKM/003/017/01 ya tarehe 28 Machi, 2017 kumtahadharisha juu ya njama hizo kama alivyokuwa amefanya awali mwezo Novemba, 2016.

Aidha, Katibu wa Bodi halali ya Wadhamini, Mhe. Joran Bashange alikwenda RITA na kukutana na wanasheria Gilbert P. Bubelwa na Mwakatobe na kuwaeleza juu ya njama hizo ovu lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuikabili hali hiyo. Jambo hilo linadhihirisha wazi kuwa njama, hujuma na mipango yote ya kuihujumu CUF ni ya dola. Kwa hali ilivyo ya utawala wa serikali ya awamu ya tano haingii akilini kama mtumishi yeyote wa umma anaweza kuwa na ujasiri wa kufanya makosa makubwa ya kijinai wazi wazi namna hii. Watawala wanafanya hivyo kwa kujidanganya kuwa wataweza kuidhibiti CUF na hivyo khofu yao ya madai ya Wazanzibari juu ya haki yao ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 itakuwa imetoweka. Aidha wanadhani kuwa Watanzania wanaoiamini CUF kama taasisi imara ya kuwaletea mabadiliko ya kweli watasambaratika.

Ndugu Wahariri na waandishi wa habari, taarifa za kusajiliwa Bodi feki ya kibaraka Lipumba kwa shinikizo la dola kupitia Msajili wa vyama vya Siasa na RITA zilipatikana tarehe 20 Juni, 2017 ambapo mawakili wa Chama walitaarifiwa kwa njia ya simu na karani wa Mahakama kuwa Shauri Na. 21/2017 mbele ya Jaji Wilfred Dyansobera, dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililokuwa limepangwa tarehe 3 Agosti, 2017 ghafla limerudishwa nyuma hadi Jumatano ya tarehe 21 Juni, 2017 (hakuna summons zilizotolewa). Aidha Jumanne, tarehe 20 Juni, 2017 wafuasi wa kibaraka Lipumba walianza kuandika kupitia mitandao ya kijamii wakihamasishana kukusanyika Ofisi Kuu Buguruni tarehe 21/6/2017 wakitangaza kwamba mambo yote yamekwisha. Baadaye CUF - Chama Cha Wananchi kikapata taarifa za uhakika kuwa RITA imesajili Bodi feki ya Lipumba, na kwamba tayari imekwishamtaarifu Jumamosi ya tarehe 17 Juni, 2017 na kwamba wanakwenda kufuta kesi zote ili pia Msajili aweze kuanza kuwapatia ruzuku.

Jumatano, tarehe 21 Juni, 2017 siku ambayo kesi ilipangwa kusikilizwa Afisa mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Bw. Sisty L. Nyahoza alifika Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es salaam na kufanya mazungumzo ya siri na uongozi wa Mahakama. Wakati mazungumzo hayo yanaendelea ilikuwa ikitangazwa kuwa mashauri yote mbele ya jaji Wilfred Dyansobera, yataanza kusikilizwa saa 4.00 asubuhi hivyo wenye mashauri waendelee kusubiri.

Jumatano hiyo ya tarehe 21 Juni, 2017 saa 3.20 za asubuhi (muda mfupi kabla ya shauri kuitwa) ndipo mawakili wetu walipopatiwa barua mbili zilizosainiwa na mfuasi wa kibaraka Lipumba anayeitwa Thomas Malima akijitambulisha kuwa eti ni Katibu wa Bodi. Barua aliandikiwa Msajili wa Mahakama Kuu na kunakiliwa kwa Jaji Wilfred Dyansobera.

Ø Ya kwanza ikimtaarifu kuondolewa kwa mawakili wetu wasomi Juma Nassor, Daimu Halfani na Hashim Mziray na eti kumuajiri wakili msomi Makubi Kunju Makubi.

Ø Ya pili ikiomba kufutwa kwa Shauri Na. 21/2017 linalomkabili Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi la wizi wa fedha ya ruzuku ya Chama takriban Tshs.369 milioni. (Thomas Malima ambaye aliomba ajumuishwe kama mlalamikiwa "RESPONDENT" kwenye shauri hilo ghafla amejigeuza kuwa mlalamikaji na anawasilisha barua mahakamani kufuta kesi).

Kupitia muhtasari wa kugushi wa kilichoitwa kikao cha Bodi feki ya kibaraka Lipumba, kilichoketi Jumamosi tarehe 17 Juni, 2017 na kuhudhuriwa na wajumbe Jumatano tarehe 21 Juni, 2017 lakini barua kupelekwa kwa Msajili wa Mahakama Jumatatu tarehe 19 Juni, 2017, azimio la Bodi feki ni kufuta kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kibaraka Lipumba na wafuasi wake. Ni wazi nyaraka hizo zote ni za kughushi.

Ndugu Wahariri na waandishi wa habari, Chama chetu kimepatwa na mshtuko mkubwa sana, kuona taasisi kubwa na nyeti yenye dhamana kubwa katika nchi inaweza kufanya vitendo vya ovyo vya kughushi nyaraka kama hivyo. RITA ni taasisi inayobeba maisha ya watu ya kila siku. Licha ya kusajili Bodi za Wadhamini, inasajili vizazi na vifo, ndoa, talaka na inatunza WOSIA kwa ajili ya mirathi. Katika mazingira ya kujihusisha na vitendo vya ovyo, vilivyokosa maadili ya utumishi wa umma na vya kijinai kama hivi, itaaminikaje kwa wananchi na taasisi nyingine? RITA wameacha kuongozwa na weledi katika kutekeleza majukumu yao badala yake wamesukumwa na utashi binafsi wa kifisadi na hujuma dhidi ya taasisi ya CUF. Ukiipitia barua ya RITA kwa kibaraka Lipumba unajiuliza maswali kama imetoka kweli kwenye taasisi hiyo iliyosheheni wasomi na wanasheria waliobobea. RITA imedhihirisha kuwa sio chombo cha kutenda haki na kusimamia misingi yake. Yumkini ndiyo sababu Jaji Wilfred Dyansobera ameamua Mtendaji wa RITA afike mahakamani kutoa ushahidi.

Ni aibu kubwa maana pamoja na kupokea majina feki ya kibaraka Lipumba tuliamini angetimiza ahadi aliyokuwa ameitoa kwenye taarifa yake mwenyewe kwa umma kwamba atafanya uchambuzi na kujiridhisha kama yalivyo matakwa ya sheria na si kushirikiana na mhalifu Francis Mutungi ambaye RITA wanafahamu wazi kuwa ni mlalamikiwa kwenye kesi na amekwisha waingiza kwenye mgogoro na Mahakama kufuatia nyaraka za kughushi alozoambatanisha pamoja na hati ya kiapo kwenye shauri Na. 23/2016.

Katibu Mkuu ameandika barua tatu kati ya 31 Machi na 6 Juni, 2017 akiomba kukutana na Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA, bila ya mafanikio yoyote. Katibu Mkuu ndiye mtunza kumbukumbu zote za wajumbe wa vikao vyote vya kitaifa na jinsi wanavyopatikana. Kitendo cha RITA kukataa kumpa nafasi Katibu Mkuu kukutana naye wakati akifanya hivyo kwa kibaraka Lipumba kunadhihirisha kuwa alichokifanya hakikuwa cha bahati mbaya bali alidhamiria. Ni dhahiri RITA wamejiunga na Jaji Francis Mutungi sio tu kuivuruga CUF bali kuzizamisha ndoto za Wazanzibari juu ya haki yao ya maamuzi waliyoyafanya Oktoba 25, 2015 kwa lengo la kuididimiza demokrasia nchini.

HATUA TUTAKAZOCHUKUA:

Baada ya kupata taarifa hizi kupitia Mahakama Kuu tarehe 21 Juni, 2017, Kamati ya Utendaji ya Taifa ilikutana mjini Zanzibar tarehe 22 Juni, 2017 na kuazimia yafuatayo:

1. Kufungua kesi dhidi ya RITA kwa kukiuka taratibu za Sheria ya Wadhamini (The Trustees' Incorporation Act Cap. 318) kama nilivyonukuu vifungu mbali mbali hapo juu, kwa kutojiridhisha juu ya uhalali wa majina ya Bodi ya Wadhamini ya CUF yaliyofikishwa kwake na iwapo yamefanywa na kikao halali cha Chama chenye mamlaka hayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama.

2. Kuwasilisha maombi mbele ya Mahakama Kuu kuitaka isimamishe kesi nyengine zote tulizozifungua kuhusiana na kadhia hii hadi hapo shauri linalohusu uhalali wa maamuzi ya RITA litakapoamuliwa.

Ni imani yangu na imani ya CUF kikiwa ni chama chenye wanachama wapatao milioni mbili na mamilioni ya wafuasi hapa nchini kwamba Mahakama Kuu zitaona umuhimu wa kulitendea haki suala hili ili kuiepusha nchi yetu na mgogoro usio na sababu zaidi ya malengo ya muda mfupi ya baadhi ya watu wanaodhani kwamba kwa kuihujumu CUF watafanikiwa.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.
 
RITA wanadai walisajili hiyo Bodi baada ya Msajili kuipa baraka-Gazeti moja la siku chace zilizopita ndio liliandika hii habari.
 
Hawa akina professor pumba na washirika wake wanaacha wana nchi wanakufa huko kibiti wao wanahangaika na vyama vya tu hii nchi hii !!!
 
Soon Maalimu Seif atakosa sifa za kuwa Katibu mkuu wa CUF ....haiwezekani katibu mkuu ukainua sharubu kwa mwenyekiti wako ukabaki salama.
 
Hvi kwan ni lazima maalimu awe katibu mkuu wa cuf,si aunde chama chake awe boss kama atakavyo!
 
Seif hana jipya. Hataki kusikiliza ushauri wa watu.

Hivi anajitambua kuwa bila kukaa na Lipumba hamna CUF kama anavyosema? Akae na lipumba ndo atafika anakotaka,

Zaidi ya hayo, atafute njia zingine za kuwa kiongozi tena. Aulize ZZK mbinu zingine.
 
Oneni ccm inavyoharibu maprofesa wa nchi hii, huko dodoma nako tumeambiwa ccm imemteua Profesa kuwa Diwani, lipumb wamemuharibu akili kabisa
 
  • Thanks
Reactions: Mj1
Hujuma za msajili kwa kushirikiana na RITA dhidi ya maalim seif zinaendelea
 
Back
Top Bottom