jyfranca
JF-Expert Member
- Oct 3, 2010
- 297
- 8
Nani alishinda Zanzibar ni CCM au CUF?
Padri Privatus Karugendo
KWA wanafiki na wenye uchu wa madaraka hili linaweza kuchukuliwa kama swali la uchochezi, swali la kutaka kuvuruga amani na utulivu wa Watanzania. Wenye upeo wa kuangalia Tanzania ya miaka ijayo, hili ni swali la msingi. Tusiangalie amani na utulivu wa leo na kesho na kusahau kwamba Tanzania itaendelea kuwepo miaka mingi inayokuja. Tunaweza kuweka pembeni maswali muhimu kwa lengo la kutaka leo hii tuishi kwa amani na utulivu huku tukijua kwamba kila lifunikwalo kwa nguvu hufumuka na kusababisha maangamizi. Historia haiwezi kutusamehe kwa kosa letu la makusudi la kuviandalia vizazi vijavyo maangamizi ya kuchinjana na kuikimbia nchi yao kuishi uhamishoni.
Ushindi wa CCM wa pointi moja unaacha maswali mengi zaidi ya majibu. Yako matukio mengi yanayowasukuma baadhi ya watu ndani na nje ya nchi kutilia mashaka ushindi huu.
Siku moja kabla ya kutangaza ushindi; wafuasi wa CUF kwa kujua wameshinda walizunguka kituo cha kutangaza matokeo ya kutangazia kura kwenye Hoteli ya Bwawani kwa lengo la kuishinikiza ZEC, iwatangaze washindi. Hali ya hewa ilibadilika; Jeshi likaanza kujiandaa.
Marais wastaafu wa Muungano Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa waliingia Zanzibar kimya kimya ili kuhakikisha kosa halifanyiki la CCM kuachia madaraka. Rais Jakaya Kikwete na vigogo wengine wa CCM walifika Zanzibar kwa lengo lile lile. Kilichokuwa wazi ni kwamba ushindi wa kura haukuwa na maana tena. Muhimu ilikuwa ni kuyalinda mapinduzi matukufu wa mwaka 1964. Wazanzibari wenyewe wanasema ushindi wa kura si neno; la msingi ni kupewa. Maana yake unaweza kushinda usipewe!
Pamoja na ukweli kwamba hata mimi wakati huo nilikuwa Zanzibar nikifuatilia matukio yote haya kwa karibu, sitajadili yote haya kwenye makala hii.
Siku za mbeleni baada ya vumbi kutulia na shughuli za kawaida kuendelea, baada ya kushuhudia baraza jipya la mawaziri na uteuzi mwingine nitajitosa kujadili Zanzibar, Muungano na hatima ya vyama viwili vikubwa vya CCM na CUF.
Juzi Rais Shein alifanya uteuzi wa Baraza la Wawakilishi kwa kuwachagua sita wa CCM na wawili wa CUF, kwa vyama vinavyozidiana pointi moja tu, uchaguzi huo haukuwa na uwiano hata kidogo. Bado ni mapema; subira yavuta heri! Leo nijadili jambo la wazi kabisa ambalo hata wachambuzi na vyombo vya habari makini vimekataa kulijadili. Nalo ni kwa nini Profesa Ibrahim Lipumba amepata kura nyingi kule Zanzibar zaidi ya Maalim Seif Sharif Hamad?
Wakati Lipumba ana zaidi ya asilimia 60, Seif Sharif Hamad ana asilimia 49.1. Hili ni muhimu sana kujadili, maana mwishowe linaweza kutujibia swali letu la
nani alishinda Zanzibar. Tunaweza kufahamu wazi ni nani alishinda na hakupewa na ni nani alishindwa akapewa.
Inawezekana kabisa kwamba watu waliompigia kura Lipumba, ambao wazi ni wale wa CUF, hawakumpigia kura Seif. Hili linawezekana maana kura ni siri ya mtu na inafuata mapenzi yake kwa yule anayemtaka, lakini si kwa Zanzibar ambako kura ya rais wa Zanzibar ni muhimu zaidi ya kura ya Rais wa Muungano. Inawezekana kabisa mtu akampigia Seif na asimpigie Lipumba na si kinyume chake. Kwa Wazanzibari, Zanzibar inakuja na muungano ni baadaye.
Hata hivyo kama CUF, walimpigia kura Shein na kumtosa Seif, basi CCM ingeweza kuchukua walau kiti kimoja kule Pemba. CUF, ilifanikiwa kujinyakulia viti zaidi ya vitatu unguja, lakini CCM ikaambulia patupu hata kule anakozaliwa Rais Shein mwenyewe. Hata kama mtu hukusomea sayansi ya siasa, anaweza kuona ukinzani unaojitokeza wazi wazi katika hoja hii ninayojaribu kuileta hapa.
Hoja ninayotaka kuijenga hapa ni kwamba kama kilichofanyika kule Zanzibar ni uchakachuaji, basi waliofanya hivyo ni wanafunzi wa kuchakachua na si watu makini, maana wangehakikisha wanaondoa utata huu ambao kama si leo hata kesho wenye akili timamu watasimama na kuhoji. Kwa nini Seif apate asilimia 49.1 na Lipumba apate zaidi ya 60, wakati wapiga kura ni wale wale wa Chama cha CUF? Haiwezekani watu wale wale wamchague mbunge wa CUF, mwakilishi wa CUF na diwani wa CUF na kukataa kumchagua rais wa nchi wakati shauku yao kubwa ilikuwa ni kuiongoza kwa mara ya kwanza serikali ya umoja wa kitaifa. Katika akili ya kawaida hili haliwezekani.
CUF wanajua wameshinda, lakini hawakupewa. CCM wanajua wazi kabisa kwamba CUF wameshinda lakini hawako tayari kuwapa; na si kweli kwamba CUF wameamua kunyamaza kwa vile wana imani ya kuingizwa kwenye serikali ya umoja wa kitaifa. Na si kweli kabisa kwamba Maalim Seif, amekuwa msaliti wa CUF kwa kujua kwamba ataingizwa serikalini kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kuwafikiria hivyo Maalim Seif na viongozi wenzake wa CUF ni kuwavunjia heshima na kuwakosea haki. Hawa wameonyesha uzalendo, busara na hekima. Wameitanguliza Zanzibar badala ya kutanguliza masilahi yao binafsi. Kama CUF, wangesimama kidete kudai ushindi wao kwa nguvu; Zanzibar ingeshuhudia machafuko makubwa zaidi ya yale ya 2002. Swali langu ni je, uvumilivu huu wa Maalim Seif wa kushinda akakubali kushindwa ili kuepusha shari utaendelea hadi lini? Vizazi vijavyo vitakuwa na uvumilivu huu? Na je, kwa nini uvumilivu huu uwe wa upande mmoja kana kwamba kule Zanzibar kuna watu ambao wana haki zaidi ya wengine? Kwanini CCM isijifunze kukubali kushindwa? Kwa nini dhana nzima ya Mapinduzi Daima isiwe na maana mpya ya mapinduzi katika maisha ya kila siku ya Mzanzibari; kufukuza umaskini, kufukuza ujinga kwa kuhakikisha kila Mzanzibari anapata elimu bora; kujenga uchumi bora na imara. Mapinduzi ya 1964 pamoja na umuhimu wake ambao unajenga historia isiyofutika umepitwa na wakati. Kuyalazimisha mapinduzi haya katika nyakati hizi tulizomo ni kutaka kuzalisha maasi ya leo na ya vizazi vijavyo.