Maalim SEIF akutana na waandishi wahabari leo kutoa ufafanuzi juu ya utoaji wake wa maoni kwa katiba

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Maalim Seif akutana na waandishi wahabari leo kutoa ufafanuzi juu ya utowaji wake wa maoni kwa katiba mpya aliotoa jana







++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

(
HOTUBA KAMILI ya MAALIM SEIF)

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI HUKO HOTELI YA BWAWANI TAREHE 14 JANUARI 2013, KUHUSU MAONI YAKE BINAFSI ALIYOYATOA MBELE YA WAJUMBE WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA ILIYOFIKA NYUMBANI KWAKE MBWENI ZANZIBAR, SIKU YA TAREHE 13 JANUARI, 2013

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana tena leo hapa hoteli ya Bwawani, ikiwa ni mara ya kwanza kwangu kufanya mkutano kama huu kwa waandishi wa habari tokea kuanza kwa mwaka huu mpya wa 2013. Naomba nichukue nafasi hii kukutakieni kheri na Baraka tele katika mwaka huu wa 2013. Aidha, sina budi kutoa shukurani zangu nyingi na za dhati kabisa kwenu nyote waandishi mlioweza kuhudhuria hapa kwa wingi, licha ya kupewa taarifa kwa muda mfupi, juu ya kuwepo kwa mkutano huu, lakini mkaukubali na mkasema muje kusikiliza wito wetu.

Waheshimiwa waandishi wa habari
Kama ambavyo mnaelewa hivi sasa nchi yetu imo katika mchakato muhimu wa mabadiliko ya katiba. Mchakato huo ni jambo muhimu sana kwa sababu hii ni mara ya kwanza kabisa wananchi wa Tanzania wanashirikishwa kikamilifu katika kuamua aina ya katiba wanayoitaka, tokea katiba hiyo ilipotungwa mwaka 1977.

Tume ya mabadiliko ya Katiba katika kufanikisha kazi yake tayari imemaliza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar na Tanzania Bara, na baada ya kumaliza hatua hiyo ya kukusanya maoni ya wananchi, tume hiyo ilianza kazi ya kukutana na makundi maalum, kwa ajili ya kuyasikiliza na kuchukua maoni ya makundi hayo, ambapo vyama tafauti vya siasa makundi mengine muhimu ya kijamii, zikiwemo taasisi za kidini yaliweza kupata fursa kama hiyo.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya tume hiyo ya mabadiliko ya Katiba kumaliza kuchukua maoni ya makundi maalum, jana tarehe 13 Januari, 2013 ilianza kukutana na viongozi mashuhuri kwa ajili ya kupata maoni.

Waheshimiwa waandishi wa habari na furaha kukujuilisheni kuwa kwa mujubu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, mimi ndiye niliyepata bahati ya kuwa wa kwanza katika kundi la viongozi mashuhuri kupewa nafasi ya kutoa maoni yangu mbele ya Tume hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Warioba na Makamu wake, Jaji Augostino Ramadhan jana asubuhi walifika nyumbani kwangu Mbweni, kwa ajili ya kuja kunisikiliza kuchukua maoni yangu kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo nimeona ni jambo la busara wananchi nao wafahamu japo kwa uchache ni kitu gani nilichokizungumza katika maoni yangu binafsi, kama Seif Sharif Hamad.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama ilivyojitokeza kwa Wazanzibari walio wengi, nami nimeona ni jambo la busara kabisa katika maoni yangu nizungumzie moja kwa moja suala la Muungano wa Tanzania, kwa vile nikiwa kama Mzanzibari niliwaeleza wajumbe wa Tume hiyo kuwa, hilo ndilo jambo linalonigusa zaidi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Nukta muhimu nilizozizungumzia katika maoni yangu ni kama ifuatavyo:

1. Asili na Sababu za Muungano
2. Misukosuko katika Muungano
3. Kiini cha matatizo katika Muungano
4. Uvunjwaji wa mkataba wa Muungano
5. Matatizo yatokanayo na kiini cha tatizo
6. Nafasi ya Zanzibar katika Muungano
7. Vipi tutoke hapa tulipo
8. Mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba

ASILI NA SABABU ZA MUUNGANO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Maoni yanayotolewa kuhusu asili na sababu za Muungano yamekuwa yakitofautiana mno. Wapo wanaouleza Muungano huu kuwa ni wa pekee katika bara la Afrika, kwani ndiyo pekee ulioweza kudumu katika kutimiza azma na malengo ya kuleta umoja wa Afrika (Pan-Africanism), na pia wapo wanauona kuwa ni "jaribio la kusisimua la ukoloni mdogo wa nchi moja ya Kiafrika kuiteka na kuitawala nchi nyengine ya Kiafrika".

Hivyo basi, si rahisi kusema moja kwa moja kuwa maelezo yepi au hoja ipi ni sahihi. Utangulizi (Preamble) wa Mkataba wa Muungano wa 1964 wenyewe unataja sababu kuu ya kuunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika kuwa ni "maingiliano ya muda mrefu ya watu wa nchi mbili hizi na mahusiano yao ya kidugu na kirafiki na kuendeleza umoja wa watu wa Afrika. Lakini miaka 49 sasa baada ya uzoefu wa Muungano huu, Wazanzibari wanajiuliza kweli haya yalikuwa ndiyo madhumuni ya Muungano huu?

Tukiangalia kwa undani tutaona kuwa wakati ule wa miaka ya 1950 na 1960 waasisi na wakuu wa harakati za kupigania Uhuru waliiona mipaka ya nchi zao iliyowekwa na wakoloni kuwa ni ‘mbinu za kibeberu'zilizotekelezwa kwa ajili ya manufaa na maslahi yao. Kutokana na hisia hizo, mazungumzo ya kuanzisha aina fulani ya umoja miongoni mwa nchi huru za Afrika yalitawala duru za siasa.

Nadharia mbili zilijichomoza. Ya kwanza, ikishadidiwa na Kwame Nkrumah wa Ghana, ilikuwa ikitaka kuasisiwa kwa nchi moja tu ya Afrika nzima iliyoungana ikiwa na Serikali moja kwa bara zima. Nadharia hii ilipingwa na baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, ambao walisisitiza haja ya kuanza na miungano ya maeneo (regional unions) chini ya mfumo wa Shirikisho badala ya kuwa na mpango wa Serikali moja.[1]

Katika kulifikia lengo hilo, viongozi wa kisiasa wa nchi tatu za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanganyika – walikuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kipindi chote cha kati ya mwaka 1961 na 1963 kuona jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto hiyo. Mfumo wa Muungano uliokuwa ukiandaliwa ulikuwa ni ule wa Shirikisho.

Ijapokuwa Zanzibar haikuwakilishwa katika mkutano wa kuanzishwa umoja wa Afrika Mashariki, viongozi wan chi tatu hizo walisema kuwa"tunapaaswa kuweka bayana kwamba nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika mikutano yetu kwa ajili ya uundwaji wa Shirikisho.

Wakati juhudi za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki zikiwa zinafifia, Mwalimu Nyerere aliona Zanzibar kama fursa ambayo hakutaka kuipoteza. Katika mazungumzo ya siri kati yake na Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wakakubaliana kuziunganisha nchi mbili hizi. Hakukuwa na ushirikishwaji wa aina yoyote ule wa wananchi wa nchi hizi mbili katika maamuzi haya makubwa. Usiri uliogubika hatua hii kubwa unafichuliwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe pale aliposema:

"Tanganyika tulipeleka Polisi wetu Zanzibar. Baada ya kuyashinda matatizo kadhaa tukaungana. Sisi wenyewe kwa khiyari zetu tulikubaliana kuungana. Karume na mimi tulikutana. Peke yetu wawili tu tulikutana. Nilipomtajia wazo la Muungano, Karume hakufikiri hata mara mbili. Pale pale alinitaka kuita mkutano wa waandishi wa habari kutangaza azma yetu. Nilimshauri asubiri kidogo kwani ilikuwa bado ni mapema mno kuweza kuviarifu vyombo vya habari.

Taarifa hizi ziliendelea kubaki kuwa siri hadi tarehe 26 Aprili, 1964 pale Redio ya Tanganyika ilipotangaza kwamba siku hiyo Marais wawili hao watakutana katika Bunge la Tanganyika kubadilishana Hati za Muungano ambazo zimeunganisha Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja.

MISUKOSUKO KATIKA MUUNGANO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umepita katika masaiba kadhaa tokea kuasisiwa kwake takriban miaka 49 iliyopita lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa sana. Ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi zake kama nchi? Hilo limekuwa ndiyo suala kubwa linaloulizwa na Wazanzibari hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.

Muungano huu umekuwa gumzo kuu katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa
katika nchi yetu. Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mwaka 1964 – 1966.

Mengine ni wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi kwa mwandishi wa maoni haya na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka 1988, katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano huo mwaka 1989/90, wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka 1991.

Kama hayo hayatoshi misuko suko mingine mikubwa ilijitokeza katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka 1994/95, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar, harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na pia baada ya kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyofanywa mwaka 2010.

Tume na Kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda Tume na Kamati zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala haya:

1. Kamati ya Mtei
2. Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)
3. Kamati ya Shellukindo (1994)
4. Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
5. Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
6. Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
7. Kamati ya ‘Harmonization'
8. Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
1. Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
2. Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997
3. Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
4. Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
5. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
6. Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
7. Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
8. Kamati ya Mafuta
9. Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
10. Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
11. Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
12. Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
13. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)

Ukiacha Tume, Kamati na Ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.

Utaratibu huu uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo sasa imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

KIINI CHA MATATIZO YA MUUNGANO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama tulivyokwisha kuona kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union). Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya Zanzibar, tarehe 22 Aprili, 1964.

Mkataba wa Muungano wa 1964 ni Mkataba wa Kimataifa na ndiyo maana kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kiingereza zilizokuwa zikifuatwa na Zanzibar na Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti katika kifungu cha (viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza lake la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.

Hoja ya kwanza inayojitokeza hapa na ambayo imeshindwa kupatiwa majibu hadi leo ni kushindwa kupatikana kwa nakala halisi ya Mkataba huo ikiwa na saini za Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Hoja hii imeibuliwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar ambako Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi kufanya hivyo.

Nusura pekee iliyobaki ni kutegemea nakala halisi (iwapo ipo) inayoelezwa kwamba ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za Umoja huo kujiridhisha kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Kuonekanwa kwa nakala halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa kile kilichokubaliwa baina ya nchi zetu mbili.

Hoja ya pili ni ile inayohusu utekelezwaji wa matakwa ya uthibitishaji (the want of ratification) wa Mkataba huo kwa upande wa Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge la Tanganyika lilikutana na kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili, 1964. Kwa upande mwengine, hakuna ushahidi wowote kwamba Baraza la Mapinduzi likishirikiana na Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikaa kuuridhia Mkataba huo kwa kupitisha Sheria ya Kuthibitisha (Ratification Decree) kama ilivyotakiwa na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi ulioibuliwa na Prof. Issa Shivji katika kitabu chake cha karibuni kabisa, Pan-Africanism or Pragmatism? Lesssons of Tanganyika-Zanzibar Union umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba Mkataba huo haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo.

Ukiachilia mbali hoja hizo, na kwa msingi wa hoja tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali, bado ukitazama kwa jicho la sheria, utaona kiini cha matatizo ya Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964.

Mfumo uliopo sasa ambao ulianza kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti; madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.

UVUNJWAJI WA MKATABA WA MUUNGANO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Mbali na suala la muundo wa Muungano, maeneo mengine mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa Muungano yaliendelea kuvunjwa na Tanganyika ikivaa joho la Serikali ya Muungano.

Kifungu cha (iv) cha Mkataba wa Muungano kiliorodhesha mambo 11 tu ambayo ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kuwa mambo ya Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 49 ya Muungano kimeshuhudia mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia chombo kisicho na mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa kufikia 22 lakini ukiyanyumbua yanafikia 37.

Mfano unakuta kifungu kimoja cha 11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, anasema ni makontena 22 yenye mambo 37 ya Muungano. Ikumbukwe kwamba kila hatua ya kuongeza mambo ya Muungano maana yake ni kuchukua mamlaka ya Zanzibar na kuyahaulisha kwa Serikali ya Muungano ambayo kama tulivyokwisha onyesha kwa hakika hasa ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika joho la Muungano.

Mambo hayo yaliyoongezwa juu ya Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na moja (11) ni haya, kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano:-

1. 1.Mambo yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
2. Leseni za Viwanda na Takwimu.
3. Elimu ya Juu.
4. Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi asilia.
5. Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
6. Usafiri na Usafirishaji wa Anga.
7. Utafiti.
8. Utabiri wa Hali ya Hewa.
9. Takwimu.
10. Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
11. Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo.
Ukiondoa mambo hayo, yapo pia mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano kwa Bunge tu kutunga sheria na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar.

Mfano wa masuala kama hayo ni Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na Haki za Bianadamu. Yapo baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo Zanzibar ilikataa kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge na hatimaye ikatunga sheria yake yenyewe kuhusiana na suala hilo.

Aidha, kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa CCM huku chama hicho kipya kikijipa madaraka juu ya vyombo vyengine vyote vya maamuzi katika nchi ikiwemo Serikali na Bunge na Baraza la Wawakilishi ilikuwa ni mtihani mkubwa na ukiukwaji wa mkataba wa Muungano. Dhana hiyo ya Chama kushika hatamu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, lengo lake lilikuwa ni kujilimbikizia madaraka yeye na Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi.

Chini ya mfumo huo, CCM iliweza kutoa maagizo na maamuru mazito bila ya kujali madaraka ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa kupitia Mkataba wa Muungano na hivyo kujinyakulia uwezo wote wa kuitawala Zanzibar ipendavyo huku viongozi wa Zanzibar wanaohoji wakituhumiwa kwamba wanapinga nidhamu ya Chama.

MATATIZO YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kiini cha tatizo la msingi la Muungano ambalo kwa mtazamo wangu ni muundo wake unaotokana na tafsiri potofu ya Mkataba wa Muungano ndicho kimepelekea kujitokeza kwa matatizo mengine katika miaka 49 hii na ambayo yanaongezeka kila uchao.

Mtu anapoangalia matatizo au hizi zinazoitwa kero, atagundua kuwa karibu yote yanatokana ama na mshirika mmoja (mara nyingi Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia shaka upande mwengine, au mshirika wa pili (mara nyingi Tanganyika ikivaa joho la Muungano), huku ikiamini kwamba ina haki ya moja kwa moja kuamua na kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata ridhaa ya upande wa pili ambao inahisi kama imeubeba tu. Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa tatizo linarudi kwenye muundo.

Zanzibar haifahamu mamlaka ya Muungano katika Serikali ya Muungano yanaishia wapi ambapo mamlaka kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika yanaanza.

Tanganyika nayo kwa kuwemo kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya ishindwe kufahamu ni vipi na wapi Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya Muungano hata kama hayakuwemo katika Mkataba wa asili wa Muungano. Hali hii inaonekana katika kila kile kinachoitwa "kero"za Muungano.

Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote, lakini kwa madhumuni ya mkutano huu na waandishi wa habari tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo yanayozusha malalamiko nayo ni:
1. Umilikaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
3. Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.

NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MUUNGANO


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa kuendelea, ni vyema sasa tuangalie nafasi ya Zanzibar katika Muungano huu, hasa kufuatia kauli za kuidhalilisha Zanzibar zilizotolewa na wanasiasa wa Tanganyika hivi karibuni wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.

Kutokana na kule kule kujaribu kujisahaulisha kuwepo kwa Mkataba wa Muungano ambao ndio sheria kuu (grundnorm) ya Muungano na kuifanya Katiba inayoitwa ya Jamhuri ya Muungano ionekane kuwa ndiyo Katiba mama na hivyo kuikweza kwamba eti iko juu ya Katiba ya Zanzibar, zimetolewa kauli kwamba kufuatia hatua ya kuungana na Tanganyika, Zanzibar imepoteza hadhi na sifa ya kuwa nchi.

Waliosema hivi wanasahau kwamba Zanzibar ina Katiba yake ambayo ina hadhi sawa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kwamba zote mbili zinapaswa kutafsiri kisawa sawa Makubaliano ya Muungano.

Katiba ya Zanzibar inatamka wazi wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Utangulizi wa Katiba hiyo ambao unaeleza dhamira ya Wazanzibari wakiwa ndiyo wenye Katiba hiyo unabainisha wazi wazi dhamira ya Wazanzibari kulinda na kudumisha nchi yao na yale yote yanayoitambulisha Zanzibar kama nchi.

Huko nyuma kabla ya Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyopitishwa mwaka 2010, ni bahati mbaya kwamba baadhi ya watu walikuwa wakinukuu vibaya kifungu cha (1) cha Katiba ya Zanzibar kilichokuwa kikisomeka kwamba, "Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" kumaanisha kwamba kwa kuwa kwake sehemu ya Jamhuri ya Muungano kunaiondolea na kuipotezea Zanzibar hadhi yake ya kubakia kuwa nchi.

Tafsiri hiyo haikuwa sahihi kama ilivyofafanuliwa na Jaji Abdullahi D. Zuru kutoka Nigeria, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kupitia Sheria (Law Review Commission) Zanzibar.

Jaji Zuru katika maelezo yake alisema kuwa anaamini kwamba waanzilishi wa hatua ya kuzileta pamoja Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja, hawajakusudia kuwa hatua hiyo ipoteze (erode) uhuru wa nchi yoyote kati ya nchi mbili kamili zilizohusika.

Kinyume na hayo, maoni yake ni kwamba nia ilikuwa kuimarisha uhuru wa kila moja ya nchi hizo mbili sambamba na ule wa Muungano utakaozaliwa. Mtaalamu huyo anafahamisha kwamba kisheria, "Haki mbili zikikutana ndani ya mtu mmoja, ni sawa na kusema kwamba ziko ndani ya watu wawili."

Aidha, alisema ni imani ya Tume yake kabisa kuwa ulipoundwa Muungano, Zanzibar ilikusudia na ilisisitiza juu ya kuendeleza mamlaka yake ndani ya utaratibu wa Muungano. Na hapa namnukuu: "Kutokana na haya, tunaamini kwamba hadhi ya Zanzibar kama inavyoelezwa katika kifungu cha (1) imepotoshwa kwa sababu (kifungu) hakielezi nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution) na madaraka yaliyotolewa na watu wa Zanzibar…"

VIPI TUTOKE HAPA TULIPO?


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Inakaribia miaka 49 sasa tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikuwa na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro zilizopo. Hilo halikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kuwatia shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama alivyotaka yeye hata baada ya "kuondoka madarakani".

Si jambo la kuficha kwamba wananchi wa pande zote mbili za Muungano wamechoshwa na unafiki uliopo na wanadai mfumo na muundo mpya wa Muungano utakaoweka misingi mipya ya ushirikiano.

Katika mijadala mbali mbali inayoendelea katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi, vyama vya siasa na taasisi nyengine za kijamii kumetolewa hoja kwamba suluhisho la matatizo niliyoyafafanua hapo juu na mengine mengi yanayoukabili Muungano huu, kumejitokeza mapendekezo yanayoelekeza kwamba ufumbuzi wake ni muundo wa Serikali Moja, Serikali Mbili zilizopo sasa pamoja na marekebisho kadhaa au Serikali Tatu.

Kwa upande wa Zanzibar, wananchi walio wengi wamependekeza kuwepo kwa Muungano wa Mkataba (Treaty based Union) kama njia bora ya kudumisha mahusiano makongwe kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Kwa upande wangu, siamini kama Serikali Moja, Mbili au Tatu zitaweza kumaliza matatizo yaliyopo ya Muungano na hasa kule kutokuaminiana kukubwa kulikojengeka kutokana na matatizo hayo kuachwa muda mrefu bila ya kushughulikiwa au kushughulikiwa kwa njia za hotuba za kisiasa zaidi zisizofuatiwa na utekelezaji wowote. Sababu zangu za kutoiona mifumo hiyo kama njia sahihi ya ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili ni hizi zifuatazo.

Serikali Moja:

Mfumo wa Serikali moja umekuwa ukitajwa kuwa utaondoa manung'uniko na kelele zote kuhusu matatizo ya Muungano lakini bado unaonekana kuwa na matatizo yafuatayo:
1. Mfumo huu utazifuta kabisa nchi za Tanganyika na Zanzibar na kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja inayosimamiwa na Serikali moja.
2. Ingawa mfumo huu unaweza kuungwa mkono na Watanganyika walio wengi, Wazanzibari hawawezi kuukubali kabisa mfumo huu kwa sababu utafuta utambulisho wao na historia yao.
3. Katika mfumo huu wa kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja, Zanzibar itachukuliwa kama eneo jengine lolote la Tanzania na hivyo kutokuwa na uwezo wa kujiletea maendeleo yake na badala yake itategemea maendeleo yatakayopangwa na Serikali kuu kulingana na rasilimali zitakazotengwa kwa ajili ya eneo la Zanzibar kama inavyopangwa kwa maeneo mengine.

Serikali Mbili:

Mfumo wa serikali mbili uliopo hivi sasa una mkanganyiko wa mambo kadhaa kwa mfano:
1. Kutokuwepo kwa mshirika mmoja wa asili wa Muungano yaani Tanganyika. Hivyo linapotokea tatizo la Muungano badala ya kukutana pande mbili za Muungano na kujadiliana kwa misingi ya usawa sasa majadiliano yanakuwa baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Majadiliano ya namna hii yanakosa misingi ya haki na usawa.
2. Mabadiliko ya Katiba yaliyomuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalikwenda kinyume kabisa na makubaliano ya awali ya Muungano. Mabadiliko haya yanamuondoa mmoja wa washirika wakuu katika Serikali ya Muungano ambaye ni Rais wa Zanzibar.
3. Kumekuwa na mkanganyiko vile vile kwa mambo ya Zanzibar ambayo siyo ya Muungano lakini mambo hayo yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano katika ngazi zote za kimataifa. Kwa mfumo huu, Tanganyika inatumia jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujifaidisha kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano katika nyanja za kimataifa. Kama vile elimu, afya, kilimo, mazingira, michezo, utamaduni, mawasiliano, miundombinu, usafiri baharini na angani.
4. Aidha, mfumo uliopo wa Serikali mbili hautoi fursa ya wazi kwa upande mmoja wa Muungano (Tanganyika) kutetea maslahi yake ndani ya Muungano.
5. Wabunge wa Zanzibar wanashiriki katika Bunge la Muungano kujadili mambo ambayo siyo ya Muungano.
6. Mfumo uliopo unaochanganya mamlaka mbili (ile ya Serikali ya Muungano kwa mambo yote ya Muungano na ile ya Tanganyika kwa mambo yake yasiyokuwa ya Muungano) unaleta mkanganyiko mkubwa katika suala la kujua mipaka ya gharama za uendeshaji wa Muungano na mapato yanayotokana na taasisi za Muungano.
Ushahidi mwengine wa wazi wa kwamba mfumo uliopo umeshindwa kufanya kazi na wala hauwezi kurekebishika ni kwamba katika miaka 20 iliopita kumeundwa Tume na Kamati 8 kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Tume na Kamati 13 kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mbali na kuwepo kwa Kamati ya Kudumu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwajumuisha Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais (zamani Waziri Kiongozi) wa SMZ lakini zote zimeshindwa kutatua matatizo ya Muungano na badala yake yamekuwa yakizidi kila uchao.

Serikali Tatu:

Baadhi ya vyama vya siasa na hata wasomi wa sheria wamekuwa wakipendekeza mfumo wa Serikali tatu (Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar) kama suluhisho la matatizo ya Muungano. Hata hivyo, mfumo huu nao kwa sasa unaonekana bado hautaondoa manung'uniko kwa upande wa Zanzibar kwa sababu:
1. Mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu utatoa mamlaka ya ndani kwa nchi mbili zinazounda Muungano huu na kuwa na Serikali zake za kusimamia mamlaka hayo lakini bado mamlaka ya kidola yatabaki katika Serikali ya Muungano.
1. Madai makubwa yanayotolewa na Zanzibar hivi sasa yanahusu kurejesha ‘sovereignty' ili kuifanya Zanzibar, serikali yake na viongozi wake wawe na hadhi ya kutambuliwa kitaifa na kimataifa. Hilo halitapatikana katika mfumo wa Serikali tatu kwa sababu:
2. Mamlaka yanayoshikiliwa na Serikali ya Muungano ambayo ndiyo itakayoziwakilisha nchi mbili kimataifa bado ina nafasi kubwa ya kuweza kutumika kumfaidisha mshirika mkubwa zaidi katika Muungano huo (Tanganyika) kuliko kwa mshirika mdogo (Zanzibar) kwa kule tu kujiona kwake ni mkubwa (big brother attitude).
3. Upo uwezekano wa kuendelea kuwepo kwa kutoaminiana kutokana na kila nchi kuwa na Serikali yake na hivyo kuwa na chombo cha kupanga mambo yake, hali inayoweza kuifanya Serikali ya Muungano ijikute haina uwezo wa kuzisimamia Serikali hizo za mamlaka ya ndani na hivyo kupoteza uhalali wake wa kisiasa.
4. Iwapo mambo ya Muungano yatabaki kama yalivyo au yatarekebishwa kwa uchache, kuwepo kwa mfumo wa Serikali tatu hakutorudisha mamlaka ya Zanzibar kupanga na kusimamia uchumi wake.

MFUMO MPYA WA MUUNGANO WA MKATABA:


Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama nilivyotangulia kueleza, tumedumu na Muungano wa Katiba kwa miaka 49 ambao pamoja na mafanikio ya kuziweka nchi zetu mbili pamoja katika kipindi chote hicho, bado umeshindwa kutujengea kuaminiana kwa dhati na zaidi umeshindwa kuyatatua matatizo ya msingi yanayotokana na maumbile ya mfumo huo.

Ulimwengu wa sasa umeshuhudia aina mpya ya mahusiano kati ya nchi huru ambao hutoa nafasi ya mashirikiano kwa maeneo yanakayokubaliwa na nchi husika huku kila nchi ikibaki na mamlaka yake kama nchi kamili. Mfumo huu kisheria unaitwa‘CONFEDERATION' ambao kimsingi ni Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).

Katika mfumo huu, yale maeneo ya ushirikiano huwekwa katika mkataba au mikataba baina ya nchi zilizoamua kushirikiana na hutoa fursa ya kurekebishwa kila mahitaji yanapojitokeza kwa kadiri na kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye mkataba au mikataba hiyo.

Umoja wa Ulaya (European Union – EU) ni mfano mzuri wa muungano wa aina hii ambapo nchi wanachama zinashirikiana katika maeneo mengi yaliyomo katika Mikataba tofauti lakini kila nchi mwanachama imebaki kuwa na hadhi yake kama nchi na kubaki na uanachama wake katika Umoja wa Mataifa (UN) na hata katika mashirika mengine ya kimataifa.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa kumalizia, nasema kuwa kutokana na hoja nilizozieleza hapo juu, mimi nimependekeza katika maoni yangu kwa Tume ya Maoni ya Katiba kuwa, baada ya uzoefu wa miaka 49 wa Muungano wa Katiba (Constitutional Union) kati ya Zanzibar na Tanganyika ambao baadhi ya matatizo yake ya kimaumbile nimeyaeleza na kuyafanua hapo juu, sasa Zanzibar na Tanganyika ziingie katika mfumo wa
"CONFEDERATION"kupitia Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).

Chini ya mfumo huo wa Muungano wa Mkataba, kuwe na Serikali mbili ambapo Jamhuri ya Tanganyika itakuwa na Serikali yake na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakuwa na Serikali yake, zote mbili zikiwa na mamlaka kamili Kitaifa na Kimataifa. Kisha Serikali hizo mbili zitafunga mkataba wa mashirikiano baina yao ambao unaweza ukapewa jina la ‘Tanzanian Union Treaty'. Yale maeneo yatakayokubaliwa kuwa chini ya ushirikiano wa nchi mbili huru yatasimamiwa na Kamisheni ya Muungano (Tanzanian Commission), kama ilivyo kwa Kamisheni ya Ulaya (European Commission) au jina jengine lolote litakalokubaliwa na nchi mbili hizo.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
________________________________________
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, uchumi wa nchi hiyo utaendelea kukua maradufu kutokana na mifumo bora ya uwekezaji iliyopo, hali itakayosaidia pia kushindana katika soko la Afrika Mashariki. Mizengo Pinda amesema, fursa muhimu ndizo zinazovutia wawekezaji kwenda nchini humo na pato la nchi kuendelea kukua maradufu. Pinda amesema hayo wakati wa uzinduzi wa duka la kusambaza bidhaa za Beko kutoka Uturuki, zikiwemo televisheni, friji na majiko ya umeme. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesisitiza kuwa, serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba, mwenendo wa ukuaji uchumi unaendelea. Ameongeza kuwa, mara zote Tanzania imekuwa katika kutafuta masoko na wawekezaji, hivyo kuzinduliwa kwa duka hilo ni ishara kuwa nchi imepiga hatua kwenye maendeleo. Licha ya Mizengo Pinda kuelezea mwenendo wa ukuaji uchumi nchini Tanzania, lakini kupanda kwa gharama za maisha kunaendelea kuripotiwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kuyafanya maisha ya Mtanzania wa kawaida kuwa magumu.

Jeshi la Nigeria limemtia mbaroni Muhammad Zangina mmoja wa viongozi wa kundi la Boko Haram. Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema, Zangina ametiwa mbaroni karibu na mji wa Maiduguri. Jeshi la Nigeria limesema kuwa, Zangina anatuhumiwa kuhusika ana mashambulio kadhaa ya kigaidi dhidi ya raia na vikosi vya polisi katika mji wa Maiduguri na kwamba, ametiwa mbaroni masaa machache kabla ya kutekeleza mpango wa mashambulio mengine katika mji huo. itakumbukwa kuwa, serikali ya Nigeria ilikuwa imetenga kitita cha dola laki moja na sitini elfu kama zawadi kwa atakayetoa taarifa za uhakika za kutiwa mbaroni Muhammad Zangina. Kundi la Boko Haram linatuhumiwa kuhusika na mauaji mengi yaliyofanyika nchini Nigeria, na wanachama wake wamekuwa wakisakwa kwa udi na uvumba na jeshi la nchi hiyo. Hadi sasa mamia ya watu wameshapoteza maisha yao na majengo kadhaa ya serikali na makanisa kuchomwa moto kutokana na mashambulio yanayofanywa na kundi hilo kaskazini mwa Nigeria.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa, takwa la waasi wa Syria la kutaka kuachia ngazi Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo kama sharti la kufanya mazungumzo, halitekelezeki. Sergey Lavrov amesema kuwa, sharti hilo la waasi la kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa halitekelezeki. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amewataka waasi hao kutoa mapendekezo yenye lengo la kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Syria. Wakati huo huo, kwa mara nyingine tena Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetoa taarifa na kusisitiza kwamba, kuna udharura wa mgogoro wa Syria kutatuliwa kwa njia za amani na kwamba, njia za kijeshi hazipaswi kutumika. Hayo yanaripotiwa huku, Qatar, Saudia, Uturuki zikishirikiana na Marekani zimeendelea kuchochea machafuko nchini Syria na hivyo kukwamisha jitihada za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za amani.


 

SEIF kwanini HAKUONGELEA ni VIJE Mzee ABEID KARUME alikuwa Rais wa Zanzibar? Anaongelea KARUME kuwa RAIS tayari hakuongelea JINSI GANI ZANZIBAR ilikuwa inatawaliwaje; MATABAKA yaliyokuwepo na JINSI Mwananchi HALALI wa Zanzibar alivyokuwa ananyimwa HAKI... Kwahiyo MAPINDUZI na KARUME kuwa RAIS kuliondoa MATATIZO ambayo ILIKUWA inaikabila ZANZIBAR na sasa hivi HAYO HAYO ndio YAMEANZA KUTOKEA na kuonyesha JINSI sehemu fulani ya Wana_Zanzibari kuwa bora karibu na WaaRABU na kuwa ni nchi ya KIARABU; wakati huohuo SALIM AHMED SALIM wa PEMBA hawapendi awe RAIS wa ZANZIBAR sababu anaUARABU...

Maalim SEIF ni MJANJA haswa... Yeye hapo ameongelea MADUKUDUKU na UCHOYO wa MADARAKA wa NYERERE wakati RAIS MWINYI alipochukua MADARAKA hakuna CHOCHOTE kilibadilishwa... kwahiyo Alikuwa na NGUVU zile zile Ambazo Mwl NYERERE alikuwa nazo... Sasa akaja na MAAZIMIO yake kama AZIMIO la ZANZIBAR; SIONI MAALIM SEIF akiliongelea...

Maongezi yake always ni BIAS... SIJUI kwanini MUUNGANO USIVUNJIKE...
 
Sijui kama kuna mchoyo wa madaraka Tanzania kama Seif na Mrema. Hoja alizoongelea hazina jipya bali kutaka kujionyesha kuwa anaijua historia ya muungano. Kimsingi, Zanzibar kwa walioko madarakani hakuna mwenye ubavu wa kusema tuvunje muungano vinginevyo watajjkuta ukimbizini.

SEIF kwanini HAKUONGELEA ni VIJE Mzee ABEID KARUME alikuwa Rais wa Zanzibar? Anaongelea KARUME kuwa RAIS tayari hakuongelea JINSI GANI ZANZIBAR ilikuwa inatawaliwaje; MATABAKA yaliyokuwepo na JINSI Mwananchi HALALI wa Zanzibar alivyokuwa ananyimwa HAKI... Kwahiyo MAPINDUZI na KARUME kuwa RAIS kuliondoa MATATIZO ambayo ILIKUWA inaikabila ZANZIBAR na sasa hivi HAYO HAYO ndio YAMEANZA KUTOKEA na kuonyesha JINSI sehemu fulani ya Wana_Zanzibari kuwa bora karibu na WaaRABU na kuwa ni nchi ya KIARABU; wakati huohuo SALIM AHMED SALIM wa PEMBA hawapendi awe RAIS wa ZANZIBAR sababu anaUARABU...

Maalim SEIF ni MJANJA haswa... Yeye hapo ameongelea MADUKUDUKU na UCHOYO wa MADARAKA wa NYERERE wakati RAIS MWINYI alipochukua MADARAKA hakuna CHOCHOTE kilibadilishwa... kwahiyo Alikuwa na NGUVU zile zile Ambazo Mwl NYERERE alikuwa nazo... Sasa akaja na MAAZIMIO yake kama AZIMIO la ZANZIBAR; SIONI MAALIM SEIF akiliongelea...

Maongezi yake always ni BIAS... SIJUI kwanini MUUNGANO USIVUNJIKE...
 
"Dhana hiyo ya Chama kushika hatamu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, lengo lake lilikuwa ni kujilimbikizia madaraka yeye na Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi"

Hii kauli ya maalim kwa mwenye heri inatafsiri zaidi ya moja
 
Mkongwe Maalim Seif yeye maoni yake juu ya katiba mpya ni kuhusu muungano tu, period!!!!
 
nngu007,

..kuna sehemu umeiacha.

..tuletee taarifa nzima ya maelezo ya Maalim.
 
Last edited by a moderator:
itachukua another 100 years watakanyika kuelewa seif anaongelea nn.
 
kwanini huu muungano usife.hauna maana yyte,wazanzibari na watanganyika wote hawataki muungano
 
"Dhana hiyo ya Chama kushika hatamu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, lengo lake lilikuwa ni kujilimbikizia madaraka yeye na Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi"

Hii kauli ya maalim kwa mwenye heri inatafsiri zaidi ya moja

Lakini tulikuwa SALAMA... Hakujilimbikizia MALI na kuongeza GAP kati ya WALIOKUWA nacho na Wasio nacho kuwa kubwa Hakufunga na KUUZA viwanda vilivyokuwa vinawapatia WANANCHI AJIRA...

TULIKUWA HATUTUKANANI; UDINI na UKABILA... Sasa kila HOTUBA ya Rais KIKWETE anasema karibia kungekuwa na KUMWAGIKA DAMU mwaka 2012... Hana LINGINE zaidi ya kuweka pesa USWISI yeye na VIBARAKA wake...

AHERI ya NYERERE... hata huko Zanzibar kulikuwa hakuna MATABAKA kama Sasa HIVI
 
Naona mleta habari kaileta kwa nusu nusu, au haijakubali kukaa yote! By the way hoja zipo mezani Watanganyika kama kawaida yenu jipakeni KINYESI, maana nyinyi hamuna uwezo kuchangia hoja mzito kama hizi! Hapa kikubwa mutaishia matusi, kejeli, vijembe na au kujadili mtu/watu binafsi lakini abadan hamutojikita katika kuchangia hoja kwa kutumia hoja!
 
itachukua another 100 years watakanyika kuelewa seif anaongelea nn.

NI kwasababu wana akili ila hawatumii kufikiria na wanamacho ila hawaoni!

Basu subirini mujemujute na kuomba msamaha vizazi vyenu baada ya miaka 100.
 
mpemba mbishi,

..mimi ni Mtanganyika na nakubaliana na 99% ya mapendekezo ya Maalim Seif.

..1% yangu ni kwamba kusiwe na bilateral treaty baina ya Tanganyika na Zanzibar.

..badala yake tuwe na multilateral treaty chini ya mwamvuli wa East African community.

..kama alivyoeleza Maalim matatizo yetu yameacha kushughulikiwa kwa miaka 45++. hali hiyo imejenga mazingira ya kulaumiana na kutoaminiana.

..tukiwa ndani ya EAC hali ya kushutumiana, kulaumiana, na kutoaminiana, baina ya Tanganyika na Zanzibar itapungua, kama siyo kutoweka kabisa.

cc: Nguruvi3, Barubaru, takashi
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom