Maalim na Dkt. Muhammed Seif Khatib katika siasa za visiwani

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,908
30,249
VIFO VYA MABINGWA WA SIASA ZA ZANZIBAR VILIVYOPISHANA MUDA MFUPI: DKT. MUHAMMED SEIF KHATIB NA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD

Nikiwa bado katika maombolezo nimeingia Maktaba kuangalia picha na makala nilizoandika kuhusu Maalim.

Nimeikuta makala hii niliyoandika 1st April 2016, Siku ya Wajinga Duniani.

Makala hii nilikuwa nazungumza na Dkt. Muhammed Seif Khatib.

Hii makala imenikumbusha mengi sana katika siasa za Zanzibar ambazo naamini zimefika mwisho na sasa Visiwa vinaingia katika muhula mpya wa udugu utangamano na maendeleo.

Ni kwa ajili hii nimeona niweke hii makala hapa kama tabaruku ya kuwakumbuka mabingwa hawa wawili wa siasa za Zanzibar kama zilivyokuwa:

"Dkt. Muhammed Seif Khatib,

Kuna makala uliandika na ukaiweka hapa JF lakini kwa haraka sana ikaondolewa lakini nilikuwa nimeisoma na nishatoa jibu.

Anaependa kufuatilia mjadala huo nilioutaja hapo juu na aingie hapa:

''Dkt Muhammed Seif Khatib na Mohamed Said wazungumzia siasa za Zanzibar.''

Safari hii umerudi na mengine kuhusu ''makosa'' ya Maalim Seif Sharif Hamad.

Umesema mengi na naamini kwa hadhi ya Maalim Seif Sharif itakuwa vigumu kwake kukujibu kwa sababu zilizo wazi kabisa.

Kwa ajili hii basi hatutoweza hapa kupata ukweli wa nini kilipitika kati ya Maalim Seif na Mzee Abdul Wakil ingawa yoyote ajuaye siasa za Zanzibar hatopata tabu kuhisi nini lilikuwa tatizo.

Dkt. si kweli kuwa mpasuko kati ya Pemba na Zanzibar chanzo chake ni Maalim Seif kama ulivyosema.

Sote tunaijua historia ya Zanzibar na Dkt. ukipenda ingia hapa uone sababu ya mpasuko huo:

Mohamed Said: "PEMBA: THE FIRE NEXT TIME."

Kwa kuwa wewe ni mtu wa fasihi naamini umemsoma James Baldwin: "The Fire Next Time," kwa hiyo utaelewa kilio cha jamii inayodhulumiwa.

Sote tunaijua historia ya Zanzibar.

Kuna mengi umesema lakini sioni sababu ya kujibu yote khasa kwa kuwa baada ya uchaguzi wa marejeo ukweli sasa uko wazi.

Wazanzibar walikataa kupiga kura na kama ulivyogusia walimsikiliza kiongozi wao na wakabaki majumbani mwao kwa amani na salama.

Itoshe tu kwa msomaji anetaka kujua nguvu ya Maalim Seif, kuingia hapa na kujisomea mwenyewe kujionea kuwa CCM Zanzibar haiwezi kupambana na Maalim Seif katika uchaguzi wowote Zanzibar kwani atawashinda hata iweje:

Mohamed Said: "TAKWIMU ZA USHINDI WA DK. SHEIN NI ''FAIRY TALE'' HADITHI ZA KUWALAZA WATOTO USINGIZI" - MOHAMED GHASSANY

Mohamed Said: "UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR - ALICE IN WONDERLAND"

Mwisho ningependa kusema kuwa Maalim Seif ni kiongozi hodari ambae juu ya vigingi vyote alivyowekewa ameweza kuijenga CUF kuwa chama makini chenye nidhamu ya juu na kuweza kuwapata vijana ambao ndiyo wapiga kura walio wengi kukipenda chama na kuleta ndani ya chama elimu zao na ujuzi wao ambao umekuwa msaada mkubwa kwa CUF na Zanzibar.

Kuwa Maalim Seif alijitangaza mshindi wala si hoja ya maana.

Ukweli ushajulikana.

Sina haja ya kusema kuwa Maalim Seif ameshinda kila chaguzi iliyofanyika Zanzibar toka 1995 na hii si siri.

Haikutushangaza wengi kuwa katika uchaguzi wa 2015 Maalim Seif alimshinda Dkt. Shein.

Dkt. analifahamu hili kama mimi na wengi tunavyolifahamu.

Sina sababu ya kueleza barua ya Ali Ameir ya 1995 iliyokataa ushindi wa Maalim Seif wala sina haja ya kukumbusha uchaguzi wa 2010 na juhudi za Mzee Hassan Nassor Moyo.

Dkt. nina hakika unafahamu kuwa kama si busara ya Maalim Seif usiku ile Bwawani wazazi Zanzibar wangezika vijana wao wengi.

Zanzibar ingepata si yale ya Pemba 2001 bali bali ingepata Amritsar (1919) na Sharpville yake (1960).

Naamini Dkt. uliona vipi siku ile jinsi hali ya Bwawani, Amritsar na Sharpville ilivyoshabihiana.

Nataka nikufahamishe kitu.

Siku mbili baada ya Bwawani na Dr. Shein kuapishwa Rais wa Zanzibar nilikuwa mgeni wa mmoja wa viongozi wakubwa Zanzibar.

Alinambia maneno haya, ''Sisi tunamshukuru Maalim Seif kama si yeye wewe leo usingekuja Zanzibar ingawa serikali ingekuwa mikononi mwetu.''

Atakae hukumiwa na historia hakika si Maalim Seif...

Wenyewe wanajijua na tayari wameshasimamishwa kizimbani na dunia.

Dkt. asipoteze muda wake kwa kukimbilia chombo kinachozama.

Nyakati zimebadilika sana na hawatoweza kuwategemea Ton Ton Macoute kwa
muda mrefu.

Wakati umefika kwake na kwa wahafidhina wenzake wakajiuliza nini kinasababisha wao kukataliwa na Wazanzibari katika kila uchaguzi kitu kinachowafanya kuchukua serikali kwa kutumia mtutu wa bunduki?

Picha: Ton Ton Macoute wa Haiti.
Screenshot_20210219-150405~3.jpg
 
Back
Top Bottom