Maadhimisho ya kwanza ya siku ya Kiswahili Duniani 07/07/2022: Mustakabali wa Tanzania na Kiswahili ni upi?

Tanzania Nchi Yetu Sote

JF-Expert Member
Mar 12, 2017
505
854
MAADHIMISHO YA KWANZA YA SIKU YA KISWAHILI DUNIANI 07/07/2022: MUSTAKABALI WA TANZANIA NA KISWAHILI NI UPI?

(Muhtasari wa masuala muhimu niliyohojiwa katika kipindi cha Stimela cha TBC FM tarehe 07/07/2022 saa 10:00 -11:00 jioni)

1.0 UTANGULIZI
Tarehe 23/11/2021 ndio siku ambayo Shirikika la Kimataifa la Elimu, Sayansi an Utamaduni (UNESCO) katika mkutano wake wa 41, mjini Paris, Ufaransa lilibariki/lilipitisha maazimio ya Kiswahili kupewa siku ya kuadhimishwa kila mwaka (7/7). Mwaka 2022 kwa mara ya kwanza tarehe 07/07 tunaadhimisha siku hii kubwa. Hii ni hatua nyingine kubwa sana kwa lugha ya Kiswahili. Ifahamike kwamba Kiswahili ni lugha iliyopitishwa kutumiwa na Umoja wa Jumuiya ya Maenedeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika. Kiswahili ni lugha rasmi ya Taifa katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya. Kiswahili kinatumiwa na idhaa za redio na runinga zaidi ya 300. Kiswahili kinafundishwa katika vyuo zaidi ya 150 duniani kote. Lugha hii kwa sasa inakadiriwa kuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200.

Ifahamike kwamba Kiswahili ni lugha ya nane duniani na lugha ya kwanza Afrika kupewa siku maalumu ya kuadhimishwa duniani na UNESCO. Lugha nyingine zilizopewa siku maalumu ya kuadhimishwa ni:

i. Kiarabu - tarehe 18 Disemba;

ii. Kichina- tarehe 20 Aprili;

iii. Kiingereza- tarehe 23 Aprili;

iv. Kifaransa - tarehe 20 Machi;

v. Kirusi – tarehe 6 Juni;

vi. Kihispaniola- tarehe 23 Aprili;

vii. Kireno – tarehe 5 Mei.

WEWE NA MIMI TUKIWA WATANZANIA TUNAWAZA MUSTAKABALI GANI KUHUSU LUGHA YETU YA KISWAHILI HAPA NCHINI KWETU?

2.0 HALI YA KISWAHILI NCHINI TANZANIA

2.1 Mtazamo wa Watanzania kwa Lugha Kiswahili

Tanzania ndio nchi inayotajwa kuwa chemichemi ya Kiswahili. Nchi nyingine za Kiafrika huitazama Tanzania kama nchi yenye utajiri mkubwa sana wa lugha hii ya Kiswahili, na wakati mwingine Watanzania tunaonewa fahari. Haya yalithibitiswa pia na mwananchi mmoja (sikuweza kulipata jina lake) kutoka nchi ya Ghana aliyehudhuria Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Dunia (MASIKIDU) tarehe 06/07/2022 katika ukumbi wa Mw. Nyerere Conventional Centre uliopo jijini Dar es salaam. Aidha, siku hiyohiyo, mtu mwingine kutoka Kenya aitwaye Walah Bin Walah alitanabaisha kwamba Watanzania wanajivunia Kiswahili bila kuvuna matunda yanayotokana na Kiswahili. Aliendelea kusema kwamba Watanzania wengi hawakithamini na kukihangaikia Kiswahili kama wanavyofanya Wakenya. Alitoa mfano akisema kwamba kamusi nzuri zinazoandaliwa na mamlaka au/na taasisi mbalimbali za Tanzania zinanunuliwa na kuuzwa zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania.

Kwa hiyo, kwa ujumla, Watanzania si watu ambao wanakitazama Kiswahili kwa jicho la thamani. Kwa lugha ya mtaani, tungeweza kusema: Watanzania wanakichukulia poa Kiswahili lakini mataifa mengine yanaupiga mwingi sana na Kiswahili!

WEWE NA MIMI TUKIWA WATANZANIA TUNAWAZA MUSTAKABALI GANI KUHUSU LUGHA YETU YA KISWAHILI HAPA NCHINI KWETU?

2.2 Kiswahili na Lugha ya Kufundishia Sekondarini na Vyuoni

Nchini Tanzania kumekuwa na mjaala mkubwa sana kuhusu ulazima wa Kiswahili sasa kutumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi ya shule za sekondari na vyuo (vikuu). Ukipima mjadala kati ya wanaotaka Kiingereza kiendelee kutumika kama lugha ya kufundishia ngazi tajwa na wale wanaopendekeza mabadiliko, kitumike Kiswahili; upande wa wanaopendekeza mabadiliko wana hoja thabiti na zenye mantiki zaidi kuliko upande mwingine. Licha ya jambo hili kufahamika kwa uwazi mkubwa, bado mabadilko hayo hayajafanyika.

Kwa nini Watanzania tumekuwa wagumu wa kufanya maamuzi ya kutumia Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia? Au tunataka hadi nchi jirani waanze kisha na sisi tuige au tufuate? Kuweka kumbukumbu sawa, nchini Tanzania, hata masomo ya Shahada ya Umahiri na Uzamivu, miaka ya 2000 kurudi nyuma yalikuwa yanafundishwa kwa Kiingereza yaani unasoma Shahada ya Umahiri na Uzamivu ya Kiswahili kwa Kiingereza. Naam! Usishangae, na ukaona ni maajabu! Hivi ndivyo ilivyokuwa. Baada ya kuona Kenya wameanza kutoa shahada hizo kwa Kiswahili ndipo na sisi nchini Tanzania tukaanza kutoa shahada hizo za Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili.

Jitihada kubwa sana zimefanywa na wasomi/wanazuoni wa Kiswahili kuhamasisha na kuonesha umuhimu wa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi zote. Mathalani, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, iliwahi kutekeleza mradi wa uandishi wa vitabu vya sekondari kwa lugha ya Kiswahili kama njia ya kuonesha kwamba mambo haya yanawezekana. Lakini jitihada hizi hadi leo zimegonga mwamba.

WEWE NA MIMI TUKIWA WATANZANIA TUNAWAZA MUSTAKABALI GANI KUHUSU LUGHA YETU YA KISWAHILI HAPA NCHINI KWETU?

2.3. Matumizi ya Kiswahili Miongoni mwa Wasomi/Wanazuoni na Wanahabari

Tunapozungumzia matumizi ya lugha fulani katika jamii, tunafahamu kwamba yapo matumizi ya lugha katika muktadha rasmi na matumizi ya lugha katika muktadha ambao si rasmi. Hatuna shida kabisa na ubanangaji wa lugha katika miktadha ambayo si rasmi. Shida yetu ni pale tunaposhuhudia lugha ikibanangwa katika miktadha rasmi tena na wasomi/wanazuoni au/na wanahabari.



Hali ya matumizi ya Kiswahili nchini Tanzania katika miktadha rasmi si mazuri hata kidogo miongoni mwa wanazuoni/wasomi na wanahabari. Kuna baadhi ya makosa ni kama vile yamehalalishwa. Kinachosikitisha ni kwamba hata wanazuoni ambao ni wataalamu wa Kiswahili bado hawapo makini wanapoitumia lugha ya Kiswahili na kujikuta wakikosea mara kwa mara. Makosa haya yanaanza na utamkaji wa jina la lugha yenywewe; ukiwasikiliza watu wengi wakiwemo baadhi ya wataalamu wa Kiswahili wanatamka “Kiswaili” badala ya "Kiswahili" Wanazuoni na wasomi wengi hususani wa Tanzania Bara hatuwi makini kutamka kwa usahihi maneno yenye silabi zifuatazo:

i. gha, ghe, ghi, gho, ghu,

ii. dha, dhe, dhi, dho, dhu;

badala yake, tunatamka hivi:

i. ga, ge, gi, go, gu,

ii. za, ze, zi, zo, zu;

mtawalia.

Makosa mengine yanayoongoza katika matamshi na maandishi ni haya:

I. “ambae” badala ya “ambaye”

II. “hatimae” badala ya “hatimaye”

III. "baadae” badala ya “baadaye”

IV. "dhalura au dharula” badala ya “dharura”

Watu pia wanashindwa kutofautisha matumizi ya maneno “kua” na “kuwa”; wamekuwa wakiyatumia kimakosa ambapo sehemu ya kutumia “kuwa” wanatumia “kuwa”.

Kutazama makosa zaidi yanayofanywa mara kwa mara na Watanzania wakiwemo baadhi ya wanazuoni/wasomi na wanahabari, soma moja ya makala zangu kupitia kiungo hiki https://www.ajol.info/index.php/jclfkt/article/view/214096/201916

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba hakuna watu wengi wanaonyooshea kidole hali hiyo ya watu kufanya makosa; lakini endapo mtu maarufu au kiongozi akikosea lugha ya Kiingereza, watu watamwandama sana katika mitandao; ujumbe ambao ameukosea utasambazwa wiki moja mitandaoni huku wakimcheka na kumdhihaki. Hili halifanyiki hata kidogo endapo mtu akikosea Kiswahili. Huenda tunaandamwa sana na ubeberu wa kiisimu kwa maana ya kuona lugha ya Kiingereza ni lugha yenye hadhi ya juu na ndio lugha inayotakiwa kutokosewa huku tukikibeza Kiswahili chetu kwa kuona ni lugha ambayo hata ukikosea si vibaya.

Kuna baadhi ya vyombo vya habari ni kama vile vimehalalisha baadhi ya makosa katika matumizi ya Kiswahili sanifu. Ninasema hivyo kwa kuwa baadhi ya vyombo hivyo vimekuwa vikikosea kwa namna fulani moja katika mfululizo wa habari zake. Mathalani, viko vyombo vya habari vyenye leseni (vilivyosajiliwa), vimekuwa vikiandika hivi: “kwakuwa”, “nakadhalika” na “ kwasababu” katika habari zao nyingi wakiamini kwamba maneno haya yanatakiwa kuunganishwa wakati maneno hayo yanatakiwa kutenganishwa katika namna hii: “kwa kuwa”, “na kadhalika” na “kwa sababu” mtawalia.

WEWE NA MIMI TUKIWA WATANZANIA TUNAWAZA MUSTAKABALI GANI KUHUSU LUGHA YETU YA KISWAHILI HAPA NCHINI KWETU?

3.0 HITIMISHO

Huu ni wakati wa Watanzania kuamka na kuthamini lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Maadhimisho haya ya kwanza yawe chachu kwetu kujiriekebisha kimtazamo, kifikra na kivitendo kuhusu lugha ya Kiswahili. Vyombo vya habari, makampuni, na taasisi mbalimbali viajiri wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili waweze kuhariri nyaraka na/au habari kabla hazijasambazwa kwa umma. Hatari iliyopo ni kwamba kwa kuwa vyombo vya habari vinaamiwa sana, watu pia watakuwa wanaambukizwa makosa yaliyofanywa na wanahabari na kuvuruga matumizi ya lugha hii adhimu ya Kiswahili. Vyombo vyenye mamlaka/dhamana ya kusimamia Kiswahili nchini vinaweza kuandaa mkakati wa kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa habari zilizoandikwa kwa Kiswahili fasaha na/au sanifu kwa kuwa wao hawana kisingizo cha kuwa katika muktadha usio rasmi.

Aidha, ni vema viongozi wetu waendelee kutafakari umuhimu wa kutekeleza mapendekezo ya wanazuoni kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili kufundishia ngazi zote za elimu huku somo la Kiingereza likibaki kufundishwa vema kwa ubunifu wa hali ya juu na walimu wa Kiingereza tu.

Endapo ushauri huu wa kutumia Kiswahili kufundishia ngazi zote za elimu utaendelea kutotekelezwa, ni vema lugha inayotumika kufundishia ngazi ya sekondari na vyuo itumike hiyohiyo kufundishia ngazi ya shule ya awali na msingi. Sababu ya msingi ni kwamba, kuwa na lugha tofauti kati ya ngazi ya shule ya msingi na sekondari (kisha chuo) kunaondoa muumano mzuri kati ya mfumo wa ujifunzaji wa ngazi moja na ile inayofuata.

Hili ndilo jibu sahihi na muafaka wa swali hili: WEWE NA MIMI TUKIWA WATANZANIA TUNAWAZA MUSTAKABALI GANI KUHUSU LUGHA YETU YA KISWAHILI HAPA NCHINI KWETU?

Dkt. Issaya Lupogo

Mwalimu wa Kiswahili – Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania

Mawasiliano:

WhatsApp +255712143909

Baruapepe _lupogoissaya1@gmail.com

07/07/2022

 
Back
Top Bottom