M/kiti CCM Taifa, Rais Dr. Magufuli ambakiza Kinana

DOFFA

JF-Expert Member
Jul 31, 2016
425
233
images

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amembakiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika wadhifa huo wakati akijaza nafasi zilizokuwa wazi katika Sekretarieti ya chama hicho.


Aidha, ameendelea kuwaamini wanajeshi katika uongozi wake baada ya kumteua Kanali Ngemela Lubinga kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, huku kada mwingine maarufu, Humphrey Polepole akiula.


Katika mabadiliko ya kujaza nafasi zilizo wazi katika Sekretarieti yaliyotangazwa jana baada ya kikao cha kwanza cha NEC kuongozwa na mwenyekiti huyo mpya aliyechaguliwa Julai mwaka huu, Polepole ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi huku Rodrick Mpogolo akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.


Katibu wa Itikadi na Uenezi ambaye sasa anaondoka kumpisha Polepole, Nape Nnauye ambaye pia ndiye Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, alitangaza uteuzi huo uliobarikiwa na NEC katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.


Aliwaambia wanahabari katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba, kwamba mabadiliko hayo hayakumgusa Kinana, Katibu wa NEC wa Oganaizesheni Dk Muhammed Seif Khatib, Katibu wa NC wa Uchumi na Fedha, Zakia Meghji na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Zanzibar, Vuai Ali Vuai.


“Wajumbe wengine ambao sikuwataja hapa watabaki katika nafasi zao. Hao ni Mheshimiwa Kinana, Mama Meghji, Seif Khatib na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai,” Nape aliwaambia wanahabari jana jioni saa chache baada ya NEC kukamilisha kikao chake cha siku moja chini ya Dk Magufuli.


Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Mwenyekiti wa CCM hupendekeza majina ambayo hupelekwa kwa NEC kwa ajili ya kuridhiwa au kukataliwa, na kwa mujibu wa Nape, majina hayo matatu yalipitishwa kwa kauli moja.


Wakati Polepole aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, na kada maarufu wa CCM aliyekuwamo katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, anamrithi Nape, Kanali Lubinga anajaza nafasi ya Dk Asha-Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Februari mwaka huu.


Kanali Lubinga alikuwa jeshini kabla ya kupelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kisha kurejeshwa jeshini, ambako amekuwa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na sasa anapelekwa CCM.


Kwa upande wake, Mpogolo ambaye naye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoani Geita na kisha Msaidizi wa Rais Magufuli wa Masuala ya Siasa, anachukua nafasi ya Rajab Luhwavi aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Balozi.


Mapema wiki hii baada ya kutangazwa kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kulikuwa na hisia za kuwapo kwa mabadiliko makubwa katika Sekretarieti ya chama hicho tawala baada ya kuondoka kwa viongozi wengi.


Hao ni kina Luhwavi, Dk Migiro, Dk Pindi Chana aliyekuwa akikaimu nafasi ya Dk Migiro, pia Nape kushikilia wadhifa wa uwaziri na uteuzi wa mwishoni mwa wiki wa Msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.


Hata hivyo, dalili za kubaki kwa Kinana katika wadhifa wake zilionekana tangu asubuhi wakati wa ufunguzi wa kikao cha NEC licha ya mwenyewe kujichomekea kuwa amewekwa kiporo baada ya uteuzi wa mabalozi.


Katika utambulisho wa mabalozi hao wateule pamoja na Mkuu mpya wa Mkoa wa Njombe, Sendeka, Katibu Mkuu Kinana alieleza kuwa amefahamishwa kuwa duniani kote ni watu wawili tu wanaotajwa kwa cheo cha Mtukufu, nao ni Rais na Balozi.


“Jana kuna mtu alinifahamisha kwamba duniani ni watu wawili tu wanaofahamika kwa cheo cha His Excellence (Mtukufu), akaniambia ni Rais na Balozi. Akaniuliza sasa wewe ulikosaje kosaje (kicheko kwa wajumbe). Nikamwambia kuwa Mwenyekiti ameniweka kiporo, atanipa zaidi ya hayo,” alisema Kinana na kusababisha kicheko kikubwa ndani ya ukumbi wa Ikulu. Alipotoa shukrani kwa watu mbalimbali, Mwenyekiti wa CCM Taifa, alimuelezea mbunge huyo wa zamani wa Arusha na Kanali mstaafu wa Jeshi nchini kuwa “nguzo na hazina muhimu katika chama chetu.”
 
Kanali Lubinga alikuwa jeshini kabla ya kupelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kisha kurejeshwa jeshini, ambako amekuwa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), na sasa anapelekwa CCM.

Nimeipenda hii.CCM kweli kiboko.
 
Hugo Mwanajeshi kakata kadi ya Ccm Jana tuu baada ya kuteuliwa au alikuwa na kadi siku nyingi?
Kwa hiyo ni ruksa vyama kutafuta na kuwa na wanachama katika majeshi yetu?
Na itikadi ya vyama vya upinzani ikiingia jeshini tutaweza kuhimili mihemko yake au tunajifanyia tuu mambo bila kujali athari zake?
 
Huyu jamaa huwezi kumfananisha na makatibu was vyama via ngine vya siasa kwa mikakati ya ushindi
 
4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom