Lupaso, Mtwara: Rais Mstaafu, Hayati Benjamin William Mkapa azikwa kwa Heshima

Roving Journalist

JF-Expert Member
Apr 18, 2017
590
1,000
1595597598012.png


Historia ya Benjamin Mkapa

MFULULIZO WA MATUKIO MBALIMBALI YALIYOTOKEA WAKATI WA MSIBA NA MAZISHI YA HAYATI MZEE BENJAMINI WILLIAM MKAPA

WANANCHI WASIMAMA BARABARANI KUAGA MWILI WA RAIS MKAPA
Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wameonekana wakisimama barabara kuonyesha heshima kwa mwili wa Rais Mkapa unaopelekwa katika Uwanja wa Uhuru kuagwa rasmi

Wananchi wa imani tofauti tofauti wamekuwa kando ya barabara wakipunga mikono na wengine wakimwaga maua ya kwa heri kwa Rais aliyetangulia mbele za haki

MWILI WA RAIS MSTAAFU MKAPA KUAGWA UWANJA WA TAIFA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa msibani nyumbani kwa marehemu, Masaki-Dar amesema Mwili wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, utaagwa kwenye uwanja wa Taifa Dar

Hata hivyo, amesema siku ya kuaga mwili huo itatangazwa baada ya taratibu zote kukamilika na taarifa kamili itatolewa baadaye


SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA KWA VIONGOZI WA NCHI NA MATAIFA MBALIMBALI
RAIS KIKWETE: NILIMJULIA HALI RAIS MKAPA JANA NA HALI YAKE HAIKUWA YA KUTIA SHAKA

Rais wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema hali ya kiafya ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa haikuwa mbaya alipoenda kumuona jana jioni hospitali

Amesema, “Jana jioni nilikwenda kumuona hospitali. Tulizungumza sana kwa karibu saa moja. Alikuwa na maumivu ila si yale maumivu ya kutoka kumuona mgonjwa na kumwambia mwenzako nimemuona mgonjwa ila eenhe!”

Ameongeza, “Nilipopata taarifa usiku wa manane kwamba Mzee amefariki niliuliza kumetokea nini tena kwasababu hakuwa mgonjwa wa kutia shaka na niliondoka nikamuaga kwamba nitakuja kukuona kesho ila siombei uendelee kukaa nyumbani, tuonane nyumbani”

Amemalizia “Kifo ni siri ya Mwenyezi Mkungu. Ila kubwa ni kwamba tumepoteza moja ya viongozi mashuhuri, Mkuu wa nchi yetu aliyetumikia taifa letu vizuri kwa uadilifu mkubwa na moyo wa upendo. Nawaomba Watanzani kuwa na moyo wa ustahimilivu na uvumilivu”

1595598580579.png

Rais Kikwete akisaini kitabu cha rambirambi msibani

UPDATES
TAARIFA ZAIDI KUHUSU MSIBA WA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa pole kwa Watanzania kwa kuondokewa na Rais Mstaafu wa awamu ya 3. Ameungana na Rais Magufuli kuomboleza na kama ambavyo amewasihi Watanzania kuendelea kuwa watulivu

Nimewaita kwa lengo la kuwapa ratiba nzima ya tukio hili hadi siku ya mazishi. Rais wetu pamoja na Kamati ya mazishi ya Kitaifa imeandaa utaratibu mzima wa tukio hilo ambapo Marehemu atazikwa Kijijini kwake Lupaso, Masasi Mkoani Mtwara

Lupaso ni Kijiji kilichopo pembezoni mwa Mji wa Masasi, si mbali sana. Mazishi haya yatafanyika Julai 29, 2020 siku ya Jumatano ya wiki ijayo - Kuanzia sasa tunaendelea kupokea waombolezaji pale nyumbani kwa marehemu

Tutatoa fursa kwa Watanzania wote Jumapili kwa shughuli za kuaga zitakazofanyika uwanja wa Taifa yaani Uwanja wa Uhuru, Dar. Shughuli za kuaga zitafanyika kwa siku 3 mfululizo, kuanzia Julai 26 hadi Julai 28 (Jumapili hadi Jumanne)

Jumapili kuanzia saa 4, dhehebu la Roman Catholic litaongoza Misa ambapo Watanzania watapata fursa ya kuanza kuaga mwili baada ya misa. Zoezi la kuaga litaendelea siku nzima hata kama ni usiku bado kutakuwa na fursa ya kuendelea kuaga mwili

Niwakaribishe pia watu wote hata Watumishi kwasababu shughuli hiyo tutaenda nayo hadi saa 6 mchana na baadaye Watumishi watarudi maeneo ya kazi. Shughuli za kuaga zitaendelea hadi saa 8 mchana. Baada ya hapo mwili utapelekwa Lupaso, Mtwara

Jumatano WanaLupaso, WanaMasasi, ndugu na jamaa na wote watakaofika kuanzia asubuhi watapata fursa ya kuaga mwili hadi saa 6 mchana. Saa 8 mchana, siku hiyo mazishi yatafanyika. Ni saa 8 ili wale wanaoguswa na kutamani kushiriki wasafiri

Ukitoka Dar unaweza kufika Mtwara kabla ya saa 8, ukazika na kuwahi kurudi - Wakaosafiri kwa ndege, tutatumia viwanja vya Mtwara na Nachingwea. Mwili utatua Nachingwea. Nachingwea na Masasi ni Km 35 ni jirani kuliko uliko Uwanja wa Mtwara

UPDATES
KUFUATIA KIFO CHA MKAPA: BENDERA ZA KENYA KUPEPEA NUSU MLINGOTI

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametangaza siku 3 za maombolezo ya Kitaifa nchini humo na bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia Julai 27 - Julai 29 kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Amesema, "Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bendera ya Kenya zitapepea nusu mlingoti. Bendera ya Kenya itafanya hivyo kwenye majengo yote ya Serikali pamoja na Balozi zake"

Ameongeza kuwa hiyo ni ishara ya heshima na shukrani kwa jukumu kubwa ambalo Mkapa alichukua katika kukuza mshikamano ndani ya Taifa lao, na kwa kuzingatia heshima kubwa aliyonayo katika Taifa la Kenya

Amesema, "Kenya tutashukuru milele kwa jukumu muhimu lililochezwa na Marehemu Rais Mkapa katika mchakato wa upatanishi uliomaliza vurugu za baada ya Uchaguzi na machafuko ya kisiasa 2007/08"

Amesisitiza, "Amani ya Taifa letu, maridhiano na umoja mkubwa unaweza kuhusishwa moja kwa moja na vitendo, hekima, upatanishi na kujitolea kwa Rais na Marehemu Mkapa na wenzake"

Soma: President Uhuru Kenyatta has declared three days of national mourning with flags set to fly at half-mast in honour of late President Mkapa


UPDATES
KIFO CHA RAIS MKAPA: ACT WAZALENDO YAAHIRISHA SHUGHULI ZA KISIASA LEO

Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe amesema wameahirisha shughuli ya Wananchi wa Lindi kumkaribisha Bernard Membe ili kupisha maombolezo ya kifo cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Taarifa ya Kiongozi huyo imetoa pole ikisema "Tunaendelea kuwapa pole Watanzania na Famiia ya Rais Mkapa kwa msiba mzito huu. Maisha ya Mkapa kiuongozi ni Mafunzo"

Jana, Zitto alifanya ziara ya kimkakati katika Jimbo la Nachingwea Mkoani Lindi ya ukaguzi wa uhai wa chama na kuwataka Viongozi na Wanachama waendelee kujiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao


JULAI 25, 2020 UPDATES:
KIFO CHA MKAPA: RAIS MUSEVENI ATUMA SALAMU ZA POLE. BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI SIKU 3

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametuma salamu za pole kwa Mama Anna Mkapa na Watanzania wote. Amesema Bendera za nchi yao zitapepea nusu mlingoti kwa siku 3 kuanzia leo

Amesema, "Nimepata taarifa ya kifo cha Kaka yetu, Benjamin Mkapa kwa masikitiko makubwa. Nilianza kufanya kazi na Mkapa mwaka 1967 tulipokuwa Chuo na alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti"

Ameongeza "Wakati wa mzozo wa mwaka 1979, Mkapa alipewa jukumu la kushughulikia Mkutano wa Moshi uliovileta pamoja vikundi vya Waganda waliozuiwa kuingia nchini kikiwemo FRONASA. Alikuwa Waziri wa Mambo ya nje wakati huo"

Rais Museveni amesema kuwa Mkapa alipokuwa Rais walifanya kazi pamoja kuunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa kifo chake ni pigo kubwa kwa Afrika

Soma: Museveni mourns Tanzania’s Mkapa


JULAI 26, 2020 - UPDATES
WAZIRI MKUU AKAGUA SEHEMU UTAKAPOWEKWA MWILI WA RAIS MKAPA ILI KUAGWA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua Kibanda Maalum kilichopo katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar ambapo mwili wa Marehemu Mzee Benjamin Mkapa utawekwa kwa ajili ya kuagwa

Watanzania wote watapewa fursa ya kuaga mwili wa marehemu kwa siku 3 kuanzia leo, Julai 26 hadiJulai 28, 2020 kabla ya mwili huo kupelekwa Lupaso, Mtwara kwa ajili ya mazishi

Zoezi la kuaga litaanza mara baada ya kumalizika kwa misa itakayofanywa na Kanisa Katoliki itakayoanza saa nne asubuhi hii

A2ECAFE8-356D-4644-9E09-F10956D034B5.png


5B001043-9780-4B45-BB7C-109F0FAA614E.png

UPDATES:
Shuhudia Msafara wa Kuuleta mwili wa Rais Mkapa Uwanja wa Uhuru.

Mwili wa Rais Mkapa unatarajiwa kuaga katika kiwanja hicho kuanzia leo. Watanzania wote watapewa fursa ya kuaga mwili wa marehemu kwa siku 3 kuanzia leo, Julai 26 hadiJulai 28, 2020 kabla ya mwili huo kupelekwa Lupaso, Mtwara kwa ajili ya mazishi

UPDATES:
Mwili wa Rais Mkapa umeshafika Uwanja wa Uhuru na sasa ni Ibada ya Misa takatifu ya kumuaga Marehemu. Baada ya Misa kila Mtanzania atapata fursa ya kuuaga mwili wa Marehemu.


JULAI 27, 2020 -UPDATES

KIFO CHA MKAPA: RWANDA YATANGAZA SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ametangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo hadi Julai 29 kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Benjamin William Mkapa (81)

Rais Kagame ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amemzungumzia Rais Mstaafu Mkapa kama kiongozi ambaye mchango wake ulienda nje ya mipaka ya Tanzania

Rwanda inaungana na Watanzania kuomboleza kifo hicho na bendera za nchi hiyo pamoja na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitapepea nusu mlingoti


KIFO CHA MKAPA: BURUNDI YATANGAZA SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO
Serikali ya Burundi imetangaza siku 3 za maombolezo kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambapo kwa siku zote 3 Bendera zitapepea nusu mlingoti nchini humo na kwenye Balozi zake zote kuanzia leo, Jumatatu

Waziri Mkuu wa Burundi, Alain Guillaume Bunyoni aliwasili jana na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, CP Thobias Andengenye katika mpaka wa Manyovu ambapo ataiwakilisha Burundi kwenye Msiba wa Rais huyo wa awamu ya 3

Soma - kifo cha Rais Mkapa: Burundi yatangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo. Waziri Mkuu wake afika kuhudhuria msiba


UPDATES JULAI 27, 2020

RATIBA YA MAZISHI YABADILIKA, MWILI WA RAIS MKAPA KUTOSHUSHWA LINDI


Mwili wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa utawasili moja kwa moja kijijini Lupaso, mkoani Mtwara kesho jioni kutoka jijini Dar es Salaam tayari kwa maziko yatakayofanyika Julai 29.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa wakati akieleza kuhusu maandalizi ya maziko ambayo amesema hadi sasa yamefikia asilimia 80.

Byakanwa amesema kuwa ratiba imebadilika ambapo awali mwili ulikuwa ushushwe Uwanja wa Ndege wa Nachingwea mkoani Lindi na kisha upelekwa kijijini kwao, lakini sasa utatolewa Dar es Salaam hadi Lupaso.

Amesema taratibu za kuhakikisha kunapatikana malazi na usafiri kwa wageni wote watakaofika bado zinaendelea.

JULAI 27, 2020 UPDATES

SERIKALI YATOA MWONGOZO WA RATIBA YA MAZISHI YA MKAPA KESHO

Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema kesho ni siku ya maziko ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa awamu ya 3, Benjamin William Mkapa na misa itafanyika Kanisa la Immaculata, Dar kuanzia saa 1 asubuhi.

Kutakuwa na utaratibu tofauti kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi, Mabalozi, Wabunge na Wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa ambao wametakiwa kuacha magari yao ukumbi wa Karimjee na watapelekwa uwanjani kwa magari maalum.

Shughuli zitaanza rasmi muda wowote baada ya mwili wa Mzee Mkapa kuwasili uwanjani kutokea Kanisani na kutakuwa na hotuba za viongozi na baadaye mwili utasafirishwa kwenda Masasi.

Mwili utakapowasili Masasi, kutakuwa na misa ya mazishi Julai 29 na shughuli za maziko zitaendelea kuanzia saa nne asubuhi.

Julai 28, 2020 UPDATES

SIKU YA KUAGA MWILI WA HYATI BENJAMIN WILLIAM MKAPA KITAIFA= > Ibada ya kuagwa kwa mwili imefanyika katika Kanisa la Immaculata lililopo Upanga.

= > Mwili unapelekwa Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuagwa na Viongozi wa Juu wa nchi na Viongozi wa Kimataifa.

= > Mwili umeshafika Uwanja wa Uhuru baada ya hapo utaratibu wa Uagaji utaendelea.

Viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikiristo wa Tanzania wamepewa nafasi ya kufanya maombi mafupi kwa ajili ya Hayati Mzee mkapa. Wote wamemuomba Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani.

Aidha, tukio hili limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Tanzania pamoja na Viongozi wa Mataifa mengine.

Kwa upande wa Tanzania yupo Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wengine wa Kitaifa. Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa amepata nafasi ndogo ya kutoa pole kwa taifa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Prof. Kabudi.

Kwa upande wa Mataifa ya Nje, yupo Waziri Mkuu wa Burundi pamoja na Mabalozi wa nchi mbalimbali. Waziri wa Burundi amepata nafasi ya kutoa neno kwa Ufupi huku Balozi wa Commoro ambaye ni Hamidi wa Mabalozi akiongea kwa niaba ya Mabalozi wengine.

Waziri wa Mambo ya Nje Prof. Kabudi asoma Wasifu wa Hayati Benjamin William Mkapa

WASIFU WA HAYATI MZEE MKAPA:
Rais Mkapa alizaliwa Wilayani Masasi, Mtwara mwaka 1938.

Alianza elimu ktk shule ya Wamishionari na kisha kupata cheti kutoka Chuo cha Mtakatifu Francis mwaka 1956, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, ambako alisomea shahada ya Sanaa.

Rais Benjamin William Mkapa aliongoza awamu ya tatu ya Urais wa Tanzania kutoka Oktoba 1995 hadi Novemba 2005.

Alikuwa Rais wa kwanza aliyechaguliwa katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992.

Alipata elimu ya msingi na sekondari kati ya mwaka 1945 – 1956.

Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Kimataifa ktk Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani mwaka 1963.

Aliajiriwa kama Afisa Tawala na Afisa Mambo ya Nje. Kati ya 1966 na 1976 alifanya kazi ktk Taasisi mbalimbali za Umma

Amefariki Julai 23, 2020.

PIA SOMA: Je, Benjamin William Mkapa ni nani hasa?

Hotuba ya Rais Magufuli Uwanja wa Uhuru

Julai 23, 2020 Taifa letu lilipata pigo la kuondokewa na Rais Benjamin Mkapa. Kifo chake sio pigo tu kwa familia bali kwa Taifa zima, Afrika Mashariki, Afrika na Duniani. Nawahakikishia wanafamilia kwamba tupo nanyi na msiba huu sio wa kwenu peke yenu.

Tangu msiba huu umetokea, watu wengi wamemuelezea Rais wetu kwa vile walivyomfahamu. Amefariki ikiwa ni miezi michache tangu alipotoa kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ ambapo ameelezea mambo mengi ikiwemo maisha yake na Uongozi tangu akiwa Lupaso.

Naomba nielezee baadhi ya mambo kwa namna nilivyomfahamu Mzee Mkapa. Nitajikita sana kuelezea mchango au mafanikio ya Mzee Mkapa akiwa Rais na baada ya kutoka madarakani. Ni ukweli kuwa nchi yetu, bara la Afrika na dunia imepoteza hazina kubwa

Alikuwa jasiri, shupavu, mzalendo, mcha Mungu, mwenye msimamo usiyoyumbishwa na mpenda amani. Mzee Mkapa ni Baba wa Demokrasia. Utaratibu wa kutoa ruzuku kwa Vyama vya siasa yeye ndiye aliuanzisha. Alisimamia utawala bora na kuanzisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa.

Aidha, wakati wa uongozi wake aliweka mkazo mkubwa sana katika Utawala Bora. Yeye ndiye alikuwa wa kwanza kuanzisha Wizara Maalum ya kushughulikia masuala ya Utawala Bora. Alipoingia madarakani aliahidi Serikali yake ingejengwa katika misingi ya ukweli na uwazi.

Mwanzoni mwa utawala wake aliunda Tume ya Warioba ili kukusanya maoni kuhusu hali ya rushwa nchini. Pia, alinzisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa-TAKURU ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa-TAKUKURU. Tunamkumbuka kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Wakati akiingia madarakani nchi yetu ilikuwa kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na kuwepo kwa madeni makubwa > Hii ilifanya Taasisi nyingi za fedha za Kimataifa na nchi nyingi Wahisani kusitisha kutoa mikopo na misaada kwa nchi yetu.

Mzee Mkapa aliikuta nchi ikiwa na madeni, akapambana na nchi ikasamehewa deni la USD Bilioni 3 kati ya USD Bilioni 7 katika mpango ambao ulisimamiwa na Benki ya Dunia na IMF. Pia, aliamini kuwa Nchi inapaswa kujitegemea licha ya kusamehewa deni.

Mzee Mkapa aliikuta nchi ikiwa na madeni, Aliweza kuzishawishi taasisi za kifedha za kimataifa pamoja na nchi wahisani na kufuta madeni yake na kurejesha uhusiano na nchi yetu, jitihada hizo zilizaa matunda ambapo tuliweza kusamehewa deni la Dola za Marekani milioni tatu kati ya USD Bilioni 7 katika mpango ambao ulisimamiwa na Benki ya Dunia na IMF. Pia, aliamini kuwa Nchi inapaswa kujitegemea licha ya kusamehewa deni/

Mzee Mkapa aliwapenda Watanzania hususan Wanyonge ndiyo maana alifuta kodi ya kichwa, kodi ya mifugo na kodi ya baiskeli. Alianzisha MKURABITA na TASAF kusaidia kaya masikini. Alianzisha Mfuko wa Bima ya Afya 2001 ili wananchi wapate huduma za afya kwa urahisi.

Alianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES). Pia, alianzisha Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, NECTA, TCU na kuifanya VETA kuwa Taasisi inayojitegemea.

Mzee Mkapa alikuwa na vipaji vya kulea na kukuza, yeye ndiye aliniibua mimi. Alimteua Mzee Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 baadaye akawa mrithi wake. Ni kama alikuwa anamuandaa kuwa Rais, alimuibua Rais Shein kwa kumpa Umakamu wa Rais.

Bila Mzee Mkapa nisingekuwa hapa nilipo, itoshe tu kusema Mzee Mkapa ni shujaa wangu na ni mtu muhimu katika historia ya maisha yangu. Alinilea kama Baba na hakuniacha hata pale nilipopata matatizo.

Nilipopata shida au changamoto alinisaidia. Alikuwa ananionesha upendo. Kuondoka kwake ni pigo kwangu > Nimepoteza mtu muhimu sana ktk maisha yangu, nilikuwa nimemzoea sana Mzee Mkapa. Kifo cha Mzee Mkapa ni ukumbusho wetu hapa dunia kuacha alama.

Mzee Mkapa niliongea nae akiwa Hospitalini kwa simu akaniambia John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri. Sikujua kuwa maneno yake yalikuwa ni ya kuniaga. Namshukuru Mungu kazi ameikamilisha. Mkapa, Mwinyi, Kikwete mara nyingi tulikuwa nao pamoja leo Mkapa hayupo

Rais Magufuli asema Uwanja wa Taifa utaitwa 'Mkapa Stadium'
Katika kuenzi mambo mazuri yaliyofanya na Hayati Mzee Mkapa Rais Magufuli aamua kuubadilisha jina uwanja wa Taifa wa Mpira wa Miguu na Kuupa jina la Mzee Mkapa (Mkapa Stadium).

Katika hili Raisi Magufuli amesema "Mzee Mkapa aliujenga uwanja mkubwa wa michezo. Wengi wanataka uitwe Mkapa Stadium. Alikuwa hapendi vitu viitwe kwa jina lake, lakini hawezi kuniadhibu amelala. Natamka rasmi uitwe Mkapa Stadium"

ZOEZI LA UAGAJI NA UTOAJI WA HESHIMA ZA MWISHO
= >
Baada ya Rais Magufuli kutoa hotuba zoezi lililofuata ni Familia ya Mzee Mkapa pamoja na Viongozi wa Kitaifa Wakiongozwa na Rais Magufuli kutoa heshima za Mwisho kwenye Mwili wa Mzee Mkapa.

= > Zoezi la Uagaji na utoaji wa heshima Kitaifa limekamilika, kwa sasa Mwili wa Hayati Mzee Mkapa unaelekea Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Mtwara kwa ajili ya Maziko hapo kesho.

= > Mwili umefika Uwanja wa ndege na sasa umewekwa kwenye ndege ya Kijeshi ili kuusafirisha.

= > Mwili wa Rais Mstaafu Mkapa umewasili Mkoani Mtwara kwa Helkopta ya Jeshi ukitokea Dar - Unashushwa kwenye ndege hiyo na kupakizwa kwenye gari tayari kwa safari ya kuelekea Lupaso.

1.jpg

Mwili wa Mzee Mkapa ukishushwa kwenye ndege ya jeshi Mkoani Mtwara

2.jpg

Msafara uliobeba mwili wa Mzee Mkapa ukielekea Kijijini Lupaso

3.jpg

Mwili wa Mzee Mkapa ukiwa umewekwa kwenye nyumba yake kijijini Lupaso

JULAI 29, 2020 UPDATES

SIKU YA MAZISHI YA HAYATI MZEE MKAPA JULAI 29, 2020

RAIS MAGUFULI AMEONGOZA MAZISHI YA HAYATI MZEE BENJAMINI WILLIAM MKAPA KIJIJINI LUPASO MKOANI MTWARA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29-07-2020 anatarajia kuliongoza taifa katika mazishi ya rais wa awamu ya tatu Hayati Mzee Mkapa katika kijiji cha Lupaso Mkoani Mtwara.

= > Mwili wa Mzee Mkapa umeshafikishwa katika viwanja hivi vya Lupaso

= > Tayari ratiba iliyopangwa imeanza kutekelezwa kwa sasa ni Ibada ya Misa takatifu imeanza kufanyika katika viwanja vilivyoandaliwa.

= > Viongozi mbalimbali wa kitaifa wameshafika katika Uwanja huu, Wamo Rais wa Zanzibar Ally Mohamed Shein, Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wengine wengi.

= > Wanachi wamepewa fursa ya kutoa heshima ya mwisho na kuaga mwili wa Mzee Mkapa.

= > Rais Magufuli amewasili katika Kiwanja cha Lupaso tayari kwa ajili ya kuongoza zoezi la mazishi.

Kwa sasa Viongozi mbalimbali wamepewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi.

Salamu za Rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali
-
Balozi wa Nchi ya Msumbiji Mh. Monica Patric amepewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya nchi yake na Rais wa Msumbiji.

Salamu kutoka kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ally Mohamed Shein
"Leo tumekusanyika hapa kumuaga kwa madhumuni ya kumsindikisha katika safari yake ya mwisho, safari muhimu katika maisha ya kila mwanadamu"

Kwa majonzi makubwa Wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Takribani siku sita zilizopita tulikuwa na majonzi makubwa lakini sio kwa kusikitika maana ndio uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Ni jukumu letu kumuombea Mzee wetu, kumuomba Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na amjaalie alale mahali pema. Na sisi tuliobaki Mwenyezi Mungu atupe hatma njema za maisha yetu hapa duniani.

Nataka nimalizie kwa kusema Hayati Mzee Mkapa aliyahifadhi na kuyatunza mapinduzi ya Zanzibar kwa vitendo, aliuhifadhi na kuutunza muungano wa Tanzania kwa vitendo tunamuheshimu kwa hali yake hiyo na uzalendo wake huo alionao.

Salamu kutoka kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete
Ni ngumu kupata maneno ya kumuelezea Mzee Mkapa, nimemfahamu miaka mingi lakini nimemfahamu zaidi nilipokuwa Katibu CCM-Masasi na yeye alikuwa Mbunge Nanyumbu. Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ila pamoja na u-busy aliwatumikia Wananchi.

Wilaya hii ya Masasi ilikuwa na tatizo la njaa wakati ule > Nikiwa Katibu CCM na DC tukabuni mradi wa kilimo cha muhogo, hakikupendeza sana sababu Wamakuwa hawapendi sana kula ugali wa mihogo kama Mashemeji zangu Wamakonde, ila Mzee Mkapa alisimama nasi.

Wakati tunaanza mchakato wa Urais mwaka 1995 nilimueleza Mzee Mkapa kuwa anafaa kuwa Rais ila baadaye nikasukumwa na mimi kugombea, akanishinda. Aliposhinda ingawa kura zetu zilikaribiana akaniteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje bila hiyana.

Mzee Mkapa alikuwa anawasikiliza sana wananchi wake na anarudi kuwaambia jinsi ambavyo ameshughulikia matatizo yao. Mzee Mwinyi aliponiteua maarifa ya Mzee Mkapa nilikaa nayo kichwani, sina hakika kama nilifaulu kama yeye ila nadhani nilifaulu kidogo

Nilipokuwa Rais Mzee Mkapa amenisaidia sana. Kuna wakati nikiwa Rais nilipitia changamoto kadhaa, mambo yalikuwa magumu kweli lakini Mzee Mkapa alisimama na mimi. Alikuwa kiongozi thabiti, hakujali kusifiwa maana unaweza kusifiwa ili uharibu.

Mzee Mwinyi amepokea Tanzania uchumi wa Nchi ukiwa katika mazingira magumu, amefanya jitihada kuuinua. Mzee Mkapa akaipokea Nchi uchumi ukiwa bado, akapigana sana na kipindi chake cha miaka 5 ya mwisho uchumi wa Tanzania ukawa unakua kwa 7%.
Salamu kutoka kwa Rais Mstaafu awamu ya pili Mzee Ally Hassan Mwinyi
Katika hafla kama hii mwanadamu yanamwishia ya kusema hata kama akiwa na mengi. Lakini Sisi Waislamu tunahusiwa kuwa binadamu kwa umbo lake ni mkosaji. Mzee Mkapa ni mwanadamu kama wanadamu wengine. Huenda katika umri wake amewahi kufanya makosa. Jambo la kwanza la kufanya pindi ndugu yetu anapoondoka ni kumuombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu.

Leo nasimama hapa kwanza kutoa rambirambi vilevile kwa Mama mkapa, ndugu zake na Mkapa na watu wote kwa kuondokewa na Mpendwa wetu. Mkapa alikuwa mtu mzuri sana, mwema sana, mkarimu sana lakini mfanya kazi kwelikweli.

Leo nimeona jambo dogo wakati wa kuaga lakini limeniathiri sana. Nimeona vijana wengi wamevaa viatu, wakati wangu mimi tumekwenda shule, madrasa na sehemu mbalimbali tukiwa miguu chini. Mimi nimevaa viatu mara mbili. Mara ya kwanza nilipokwenda jandoni na mara ya pili nilipokuwa na miaka 13 nilichuma karafuu nikanunua viatu.

Tuendelee kumuombea asamehewe kama ana makosa yoyote. inawezekana wakati mwingine aliteleza teleza Mwenyezi mungu amsitiri na ailaze roho yake mahali pema peponi.

HOTUBA YA RAIS MAGUFULI LUPASO
Ndugu zangu waombolezaji niliona walau tusikilize neno kutoka kwa mzee kikwete na Mzee Mwinyi. Ingawaje Mzee mwinyi hakusema hivyo viatu alivitundika kwa muda gani.

Waheshimiwa waombolezaji, tumekuja hapa kwa kazi moja ya kumuaga Mzee wetu Benjamini William Mkapa ambaye ametimiza kazi yake kwa miaka 82. Nipende kwa mara nyingine tena kuwashukuru Watanzania wote mahali pote walipo. Lakini kuwashukuru viongozi wa dini ambao wameshiriki kikamilifu kumuombea Mzee wetu apumzike kwa amani.

Ndugu zangu waomboleza nataka niseme kitu kimoja, kuna wakati serikali ilipanga mahali pa maziko pa viongozi. Tulianzisha utaratibu wa Marais kuzikwa Makao Makuu Dodoma. Siku 1 Mzee Mkapa akaniuliza, ‘Mlipanga maziko yawe Dodoma? Mimi mnizike Lupaso’. Mzee Kikwete akasema Msoga, nikaogopa kumuuliza Mzee Mwinyi kutokana na umri. Mimi nilijisema nitazikwa Chato.

Kwasababu hakuna anayetaka kuzikwa Dodoma lile eneo nikaamua kuwapa wananchi na tayari walishaanza kujenga. Mkapa alipenda kwao. Angeweza kuzikwa Dar es Salaam au Lushoto lakini alipenda sana nyumbani, akataka azikiwe kwao.

Nawapongeza sana wananchi wa kijiji cha Lupaso kwa sababu katika kijiji hichi amezaliwa mtu aliyekuwa na uzalendo Mkubwa. Tuendelee kumuombea Mama Mkapa pamoja na familia wakaendelee kuishi kwa upendo na kumtangiuliza Mungu kwa sababu tumaini lao kubwa ni Mungu.

= > Baada ya salamu kutoka kwa Viongozi sasa ni sala ya buriani.

= > Taratibu za mazishi zimeanza kufanyika kwa sasa inasomwa ratiba na taratibu za vitendo vya kijeshi zinavyofanyika wakati wa mazishi hayo.

= > Tayari mwili wa Hayati Mzee Mkapa umebebwa na Wanajeshi kwa ajili ya kufanya taratibu za maziko.

= > Mwili wa Hayati Mzee Mkapa kwa sasa unashushwa kaburini

= > Baadhi ya Viongozi wamepewa nafasi ya kuweka mchanga ndani ya kaburi.

Anna Mkapa.jpg

Mama Anna Mkapa akiweka mchanga kwenye kaburi la mumewe

magufuli.jpg

Rais Magufuli akiweka mchanga kwenye kaburi la Mzee Mkapa

= > Zoezi lililopo sasa ni kufunika kaburi la Hayati Mzee Mkapa.

= > Zoezi la ufunikaji wa kaburi limekamilika.

= > Zoezi la uwekaji msalaba kwenye kaburi linafanywa na kukamilika.

= > Kwa sasa ni zoezi la uwekaji wa mashada ya maua kwenye kaburi la Hayati Mzee Mkapa. Imenza familia ya Marehemu kisha Marais wote wa Tanzania wakiongozwa na Rais Magufuli.

Marais.jpg

Rais Magufuli na Marais Wastaafu (Mzee Mwinyi na Kikwete) wakiweka mashada ya maua

= > Tukio la uwekaji mashada wa maua limekamilika kwa sasa unafata utaratibu wa kijeshi ikiwamo upigaji wa Mizinga 21.

= > Zoezi la upigaji mizinga 21 linafanyika na kukamilika.

= > Zoezi la Mazishi ya Hayati Benjamini William Mkapa limekamilika.

= > Kwa sasa unasomwa wasifu wa Hayati Benjamini William Mkapa

MWISHO

== PUMZIKA KWA AMANI HAYATI MZEE BENJAMINI WILLIAM MKAPA ==
 

Roving Journalist

JF-Expert Member
Apr 18, 2017
590
1,000
Salaam Wakuu,

Leo ni siku ya Kwanza kati ya Tatu ya kuuaga Mwili wa Aliyekuwa rais wa Tanzania Benjamin Wiliam Mkapa katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar Es Salaam.

Tutaendelea kujuzana kile Kinachojiri.

Stay tuned.


=====

UPDATES:

======
IMG_20200726_091903_224.jpg
IMG_20200726_091909_111.jpg

0910hrs: Mwili wa Marehemu upo Njiani kutoka Hospitali ya Jeshi Lugalo kuelekea Uwanja wa Uhuru Temeke. Ambapo kazi hii inaongozwa na Jeshi la Ulinzi (JWTZ).

Mwili ukifika Uwanja wa Taifa, kutakuwepo na Misa itakayoongozwa na Askofu Tercius Ngalekumtwa.

0935hrs: Msafara wa Mwili wa rais Mstaafu Mkapa, bado upo njiani kutokea Jeshini Lugalo Kawe Dar Es Salaam kupitia barabara ya Hassan Mwinyi, Katikati ya Mji hadi Temeke.
IMG_20200726_093243_419.jpg

Kila Sehemu Msafara unapopita, Wananchi wamejipanga barabarani kuaga na kutoa heshima zao za mwisho.

0945hrs: Mwili Wa Marehemu Mkapa ndo unaingia Viwanja vya Uhuru Temeke
20200726_105509.jpg

20200726_100036.jpg

Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa, akiwa tayari kwenye Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kushiriki Misa na kuuaga mwili wa Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa
20200726_100043.jpg

Rais Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu wakiwa tayari wamewasili katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki Misa na kuaga mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
IMG_20200726_100748_108.jpg

1000hrs: Mwili wa Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa ukishushwa kutoka katika Gari maalum ndani ya Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuanza kwa misa ya kumuaga.

WAKATI HUO HUO;
20200726_101331.jpg

Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakiendelea na shughuli ya ujenzi wa kaburi atakwamozikwa Rais Mstaafu, Marehemu Benjamin Mkapa.

Kiongozi huyo atazikwa kijijini kwao Lupaso, mkoani Mtwara, Julai 29 mwaka huu.

Shughuli za kuuaga mwili wake zinaendelea Dar es Salaam.

1140HRS: Ibada ya kuaga Mwili wa rais Mstaafu Benjamin Mkapa inaelendelea Uwanja wa Uhuru.

MSEMAJI WA FAMILIA: RAIS MKAPA ALIKUTWA NA MALARIA

William Erio, Msemaji wa familia amesema Rais Mstaafu Benjamini Mkapa alipatwa na Malaria Jumatano na akalazwa na kuanza matibabu

Siku ya alhamisi alikuwa anaendelea vizuri, na akaendelea kufuatilia uchaguzi wa kura za maoni uliokuwa unaonyesha mubashara

Baada ya muda, aliinuka alitaka kutoka, alivyoinuka akarudi kukaa na akainamisha kichwa, na akathibitika amefariki kwa mshituko wa moyo, ‘Cardiac arrest’

Msemaji wa familia amewataka watu kuheshimu ukweli huo, na sio kuzusha mambo yasiyo na ukweli kwenye mitandao.

KASEMA;

"Nitoe shukrani kwa Serikali kwa ambavyo wamekuwa pamoja nasi na kushughulikia msiba huu na wanavyoendelea kushughulikia, tunawashukuru kwa uamuzi wa kuanza shughuli ya kuaga kwa Misa Takatifu, tunawashukuru Maaskofu kwa kukubali kuendesha Misa”- William Urio,

“Mzee Mkapa alikuwa hajisikii vizuri akaenda Hospitali akaonekana alikuwa na Malaria akaanza matibabu akalazwa Jumatano,Alhamisi mchana aliendelea vizuri nilikuwa nae hadi saa mbili alikuwa anaangalia Live ya chaguzi za wagombea Ubunge Viti Maalum CCM”-

“Mzee Mkapa Alhamisi usiku baada ya kutazama LIVE ya chaguzi Viti Maalum akasikiliza taarifa ya habari, baadaye aliinuka akitaka kutoka akakaa akainamisha kichwa, walipokuja kumpima wakathibitisha kuwa amefariki, sababu ya kifo cha Mzee Mkapa ni mshtuko wa moyo”-

“Chanzo cha kifo cha Mkapa alipata mshtuko wa moyo, tumeona ni vizuri tuliseme hili kwasababu kumeanza kuwa na manenomaneno kila Mtu akijifanya Nabii katika mitandao ya kijamii na kwingine, tumuenzi Mzee wetu aliyetangulia mbele za haki kwa kuukubali ukweli huo"

20200726_181154.jpg
20200726_181206.jpg

PICHA: Kutoka Uwanja wa Uhuru DSM ambako imefanyika Misa Takatifu ya kuuaga mwili wa Marehemu Mzee Mkapa kisha Watanzania mbalimbali kupata nafasi ya kupita karibu na Jeneza na kutoa heshima zao za mwisho, haya ndio matukio mbalimbali ya picha uwanjani.
 

kamili

JF-Expert Member
Feb 10, 2011
1,055
2,000
Tangu asubuhi nimekuwa nikifuatilia coverage ya kuifiwa na kiongozi wetu mstaafa mh. Benjamin William Mkapa kupitia ITV.

Ilipofika takriban saa saba na dakika kumi na tatu, ITV ilikuwa ikimhoji mh. Msekwa kufuatana na kifo hicho. Cha kushangaza mheshimiwa huyo alianza kuongelea maandamano baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 katika mwelekeo ambao ungefufua vidonda vilivyopona. Hongera sana sana ITV kwa kukatisha maongezi hayo.

Marehemu alikuwa jasiri sana hadi akasema mauaji yale yalimsononesha sana. Naamini hata familia zilizoathirika zimesamehe na sasa tu wamoja. kuongelea maandamano yale kwa jinsi alivyoanza mh. Msekwa ilikuwa ni hatari.
 

kigogo warioba

JF-Expert Member
Jul 11, 2015
5,596
2,000
Tangu asubuhi nimekuwa nikifuatilia coverage ya kuifiwa na kiongozi wetu mstaafa mh. Benjamin William Mkapa kupitia ITV.

Ilipofika takriban saa saba na dakika kumi na tatu, ITV ilikuwa ikimhoji mh. Msekwa kufuatana na kifo hicho. Cha kushangaza mheshimiwa huyo alianza kuongelea maandamano baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 katika mwelekeo ambao ungefufua vidonda vilivyopona..
Kwa nini iwe ni hatari? mi naona waendesha kipindi hawajamtendea haki Mzee msekwa, yaani ndio alikua anaeelekea vizuri, hayo ndio mambo tunayoyataka kuyasikia!
 

tindo

JF-Expert Member
Sep 28, 2011
33,607
2,000
Tangu asubuhi nimekuwa nikifuatilia coverage ya kuifiwa na kiongozi wetu mstaafa mh. Benjamin William Mkapa kupitia ITV.

Ilipofika takriban saa saba na dakika kumi na tatu, ITV ilikuwa ikimhoji mh. Msekwa kufuatana na kifo hicho. Cha kushangaza mheshimiwa huyo alianza kuongelea maandamano baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 katika mwelekeo ambao ungefufua vidonda vilivyopona..
Mkuu una mpango wa kunajisi box la kura nini hiyo October, ndio maana umeshukuru hayo mahojiano yamekatishwa, kwani umejua mkiiba safari hii watu wataandamana tena nini?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom