Lulu kutumikia kifungo cha miezi 5 gerezani kabla ya mchakato wa rufaa kuanza

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
MSANII wa fi lamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ atapaswa kutumikia theluthi ya kifungo chake ambacho ni miezi mitano gerezani kabla ya mchakato wa rufaa dhidi ya kifungo chake.


Lulu alianza kutumikia kifungo cha miaka miwili juzi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumtia hatiani kwa kumuua bila ya kukusudia msanii Steven Kanumba. Akitoa ufafanuzi wa kisheria katika mtandao wa kijamii wa Instagram, Wakili wa Lulu, Peter Kibatala alieleza hakuna cha kufanya kwa Lulu kabla ya kutumikia theluthi ya kifungo chake.


Alisema kisheria katika miezi hiyo mitano ya kutumikia kifungo, wanaweza kuomba dhamana wakati wakisubiria rufaa na kama Lulu atakuwa na bahati anaweza kupata wakati wowote.


Kibatala alisema wanakata rufaa kwa kuwa hawawezi kumuacha kijana wa miaka 22 mwenye malengo mengi ya baadaye kuyaharibu kutokana na hukumu za makosa ya jinai. ‘’Dhamana wakati wa kusubiri rufaa isikilizwe pamoja na kifungo cha nje vinaweza kufanyika wakati mmoja,’’ alisema Wakili Kibatala.


Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole alisema sheria ya makosa ya jinai inasema adhabu ya juu kwa mashitaka ya kuua bila kukusudia ni kifungo cha maisha lakini hakuna ukomo wa adhabu ya chini.


Kambole alisema mahakama inaweza kutoa adhabu ndogo kutokana na kigezo cha umri, muda wa kukaa gerezani kwa mshitakiwa na kama ni mkosaji wa kwanza na kajutia kosa.


‘’Mahakama ndiyo inayoamua kutoa adhabu kwa kuwa sheria inaonesha adhabu ya juu ni kifungo cha maisha lakini hakuna ukomo wa adhabu ya chini hivyo inaweza kumhukumu kifungo cha nje, kifungo cha miaka miwili au mmoja kulingana na sababu hizo,’’ alisema Kambole.


Pia alisema mfano mzuri ni kesi ya mauaji ya bila kukusudia iliyokuwa ikimkabili askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), namba G 58 Pacificius Simon (27) kwa kosa la kumuua bila kukusudia mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi mwaka 2012 kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa Alisema katika hukumu hiyo, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 15 jela, hivyo inategemeana na utashi wa jaji, ushahidi na vigezo hivyo.


Mwananchi Tumsifu Mwamini aliwataka wanaotaka kumsaidia Lulu watumie njia ya sheria kwa kuwa ina msamaha na huruma ndani yake na ni mfumo ulioruhusiwa na Mungu.


Chanzo: Habari Leo
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom