mkiluvya
JF-Expert Member
- May 23, 2019
- 802
- 725
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wamiliki wa ardhi ambao hati zao za ardhi zinaishia miaka 33 kwenda ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni kuzihuisha ili kupatiwa za miaka 99.
Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Mara wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Mara ambayo ni ofisi ya kumi na mbili kuzinduliwa ikiwa ni mfululizo wa kuzindua ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Alisema, kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi kwenye mikoa mbalimbali ambao viwanja vyao vimepimwa na michoro kuidhinishwa lakini hati zao ni za miaka 33 na wamiliki hao watakapoenda kuzichukua wanatakiwa kuziangalia ili zibadilishwe na kupatiwa hati za miaka 99.
‘’ Hati nyingi za wale wamiliki ambao hawajazichukua zimekwisha muda wake, muende kwenye ofisi za ardhi za mikoa, huko mtaelekezwa na Wasajili Wasaidzi wa ardhi katika ofisi hizo namna ya kuzibadilisha ili mpatiwe za miaka 99’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, zaidi ya wamiliki wa ardhi 50,000 kwenye mkoa Mara hawajachukua hati za ardhi wengi muda wa hati zao unaishia miaka 33 na kutaka kufika ofisi za ardhi mkoa wa Mara kurekebishiwa na kupatiwa za miaka 99 ili iwe rahisi kupata mikopo mikubwa . Akizungumzia uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Mara, Lukuvi alisema mkoa huo umekuwa na migogoro mingi ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo utawawezesha wananchi wa Mara kumaliza migogoro kupitia ofisi hiyo badala ya kuipeleka migogoro kwake.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa, pamoja na Wizara yake hapo awali kushughulikia kero na migogoro ya ardhi lakini tatizo la kimfumo lilikuwa kubwa na kuweka wazi kuwa uzinduzi wa ofisi za mikoa unakomesha kero ambapo sasa hakutakiwa na gharama yoyote kwa mmiliki wa ardhi zaidi ya ile atakayolipia wakati wa kuomba hati.
‘’Mgogoro wa kimfumo ulikuwa mkubwa zaidi na leo hii tumekomesha kero na hakuna gharama yoyote mmiliki wa ardhi ataingia kufuatilia hati zaidi ya ile aliyolipa wakati wa kuomba hati, serikali ya awamu ya tano imeondoa kero zote kwa wananchi kwenye utawala wa ardhi’’ alisema Lukuvi.