• Mpendwa mteja, tunakusihi jitahidi kuosha mikono kwa maji safi na sabuni mara kwa mara na kwa siku chache hizi jaribu kutulia nyumbani kuepusha maambukizi ya #CORONAVIRUS

Ludovick Utouh aeleza siri iliyomfanya aandike kitabu.

N

nyumbamungu

JF-Expert Member
Joined
Mar 3, 2017
Messages
562
Points
500
N

nyumbamungu

JF-Expert Member
Joined Mar 3, 2017
562 500
Dar es salaam; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amesema kukatishwa tamaa alikokutana nako wakati wa uongozi wake kulimfanya ajione ameachwa peke yake na taasisi hiyo.

Hilo lilitokana na namna suala la uwajibikaji lilivyoachiwa taasisi hiyo pekee, ilhali jamii nzima inapaswa kuhakikisha dhana hiyo inatekelezeka.

Ni sababu hiyo ndiyo imemsukuma Utouh kuandika kitabu kiitwacho " Uwajibikaji ndani ya kalamu isiyokuwa na wino" Pia ukurasa wa 129 wa kitabu hicho,mkaguzi huyo mkuu mstaafu wa hesabu za Serikali ametoa mapendekezo ya uimarishaji wa uwajibikaji nchini.

"Kwa kipindi chote cha miaka minane cha mimi kuwa CAG, nimekuwa nikishauri Serikali, Bunge na Mahakama kuhusu namna ya kuboresha na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, na njia bora ya matumizi yake" alisema jana wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.

Alisema mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi ni pamoja na uimarishaji wa mifumo ya uwajibikaji na utawala bora.

Alisema inafaa kuimarisha mifumo ya ndani ya utendaji kazi na ulipwaji wa mishahara inayokidhi mahitaji muhimu ya mfanyakazi.

Vilevile lipo suala la malipo ya mishahara hewa na uimarishaji wa miundombinu nchini.

Ndani ya kitabu hicho ambacho dibaji imeandikwa na katibu mkuu kiongozi mstaafu, Ombeni Sefue na chenye kurasa 153, Utouh ameeleza mambo aliyokutana nayo katika kipindi cha miaka minane.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, alisema miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikimuumiza ni kutofuatwa kwa mapendekezo aliyokuwa akiyatoa kwa ajili ya kuleta maboresho.

Utouh ambaye kwasasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, alisema pamoja na kumuumiza jambo hilo lilisababisha ajione mpweke.

Alisema "Wakati mwingine kama CAG nilikuwa najiona niko mwenyewe kwasababu unakuja na pendekezo ambalo unaamini ndani ya moyo wako kuwa likitekelezwa litaisaidia Serikali, halafu halitekelezwi."

"Ni sababu hiyo ikanifanya niandike hiki kitabu ili kuelimisha kuhusu dhana ya uwajibikaji na kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hili suala ni letu sote. Najua fedha na nguvu niliyotumia kuandika kitabu hiki haitarudi kwasababu Watanzania hawana utamaduni wa kusoma , ila binafsi nimesukumwa niandike kutoa elimu"

Utouh alisema mambo kadhaa alikuwa akishauri, lakini hayakufanyiwa kazi hadi Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuyaangalia kwa jicho la tatu.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na sakata la watumishi hewa, Escrow, kutambulika kwa makao makuu ya Serikali na mgogoro wa kimaslahi unaotokana na Wabunge kuingia kwenye bodi za mashirika ya umma.

Kuhusu suala la watumishi hewa, alisema kwa muda mrefu alikuwa akilitolea ushauri, lakini haukuzingatiwa ila sasa baada ya hatua kuchukuliwa manufaa yameonekana kutokana na fedha nyingi kuokolewa.

Kwa upande wake, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), John Cheyo alisema Utouh alichangia kwa kiasi kikubwa kuifanya ofisi ya CAG kuwa taasisi imara na yenye heshima kubwa hapa nchini.

Cheto alisisitiza kuwa uwajibikaji katika mali za Serikali ni jambo muhimu linalopaswa kuzingatiwa na taasisi na watumishi wote wa umma.

Alisema iliyokuwa kamati yake ilifanya kazi kwa karibu na Utouh kuifanya ofisi ya CAG kuwa chombo kinachojitegemea na kusimama imara kwa ajili ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kama zilivyopitishwa na Bunge.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Asasi za Kiraia, Francis Kiwanga alisema kipindi ambacho Utouh alikuwa akiongoza ofisi hiyo kulikuwa na changamoto kubwa katika suala la uwajibikaji Serikalini.


Chanzo: Mwananchi, Julai 28,2018.


Sent using Jamii Forums mobile app
 

Forum statistics

Threads 1,406,594
Members 532,389
Posts 34,520,444
Top