Lucas Mhomba aeleza jinsi alivyopata ulemavu mpaka kukimbiwa na mke wake

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
704
1,457
Lucas Mhomba ambaye amekatwa miguu na viganga vyote viwili (kushoto) na kulia ni awali akiwa na viungo vyote.

Oktoba 14, 2023 haitasahaulika katika maisha ya Lucas Mhomba, mkazi wa Dumila wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.

Alivamiwa na watu wasiojulikana akajikuta akipoteza miguu yote miwili na mikono yote.
Mhomba (24), akizungumza na Mwananchi anasema alikuwa dereva bodaboda alipofikwa na kadhia hiyo.

“Nilikuwa nafanya shughuli zangu hapa Dumila, Oktoba 14 niliamka asubuhi kuendelea na shughuli zangu. Nilifanya kazi kama siku zote, mara nyingi huwa nakesha,” anasema.

Anaeleza ilipofika saa sita usiku alitokea kijana anayelingana naye umri aliyemtaka ampeleke katika moja ya maeneo yaliyopo Dumila.

Anasema walikubaliana bei akawasha pikipiki wakaanza safari.

“Wakati naendelea na safari ghafla abiria akanigeuka akaanza kunishambulia. Nilijikuta nikiishiwa nguvu, nikaachia pikipiki wote tukaanguka. Nikaanza kujitetea lakini kwa kuwa alishanipiga nikashindwa, wakajitokeza wenzake watatu wakaungana wakawa wanne,” anasema.

“Kwa hiyo wakanishughulikia kwa kunitesa kwa muda kidogo,” anasimulia.

Anasema walimfunga kwa kamba miguu na mikono, kumziba mdomo kwa kitambaa kisha wakamweka kwenye jumba jirani na eneo walikomtesa wakamwacha hapo.

Anasema alikaa kwenye jumba hilo kwa siku tatu, ya nne mwenye eneo hilo alipokuwa amekwenda saa saba mchana alimkuta akamfungua akatoa taarifa Polisi waliofika kumchukua.

“Nilipelekwa hospitali ya St Joseph hapa Dumila kupatiwa huduma ya kwanza, walivyoona hali yangu nikapewa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, nako walinipa huduma lakini wakanipa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili,” anasema.

Anasema madaktari bingwa wa Muhimbili walimweleza mikono na miguu imeshaathirika baada ya kufungwa kamba na kukaa siku tatu bila damu kupita, hivyo wakamshauri viungo hivyo vikatwe.

Uamuzi kukatwa viungo
Anasema haikuwa rahisi kwake kuruhusu viungo vyake vikatwe kwa kuwa hakuamini kama anakwenda kuwa mlemavu wa kudumu.

“Madaktari waliponiambia kwamba wanahitaji kunikata miguu na mikono kwa kuwa haikuwa ikifanya kazi tena baada ya mishipa ya damu kutofanya kazi kwa siku tatu kwenye viungo hivyo, haikuwa rahisi hata kidogo,” anasema.

Anaeleza baada ya kutafakari na kushauriana na ndugu zake akaamua kuruhusu vikatwe.

Ulemavu wamkimbiza mke
Baada ya kupata ulemavu huo anasema mke wake waliyekuwa wamezaa mtoto mmoja alimkimbia.
“Nilitoka Muhimbili Machi 2024, baada ya kufika nyumbani mke wangu akaniona, akaniambia kwa hali niliyonayo anaamini hatapata tena mahitaji yake kutoka kwangu, hivyo akaamua kuniaga na kuondoka,” anasema.

Anasema kabla hajaondoka alitafakari akaona kweli hataweza kumhudumia.
“Sikumzuia, nikamuacha aondoke lakini tunawasiliana mara chache kwa kuwa aliondoka na mtoto wangu,” anasema.

Maombi kwa Watanzania
Kutokana na ulemavu alionao, amewaomba Watanzania wamsaidie kupata bajaji imwezeshe kutafuta mahitaji yake ili maisha yaendelee.

“Serikali ya Wilaya ya Kilosa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya, Shaka Hamdu Shaka ameahidi kuninunulia miguu na mikono bandia. Bado nina mahitaji mengi, ikiwamo mahitaji yangu binafsi na ya kumlea mwanangu, naamini kama nikipata vifaa bandia na bajaji nitafanya kazi na baadaye nitamrejesha mke wangu tuendeleze familia yetu,” anasema.

Shaka amesema ofisi yake itahakikisha anapata viungo bandia.

“Tutamsaidia kijana huyu kupata viungo bandia kwa ajili ya kumsaidia kujiwezesha mwenyewe kwenye baadhi ya shughuli, tumefuatilia gharama za viungo ni Sh15 milioni. Tutapata mikono yote miwili, miguu yote miwili, na gharama za kwenda kwenye matibabu. Tutahakikisha anapatiwa vifaa hivyo ili arudi kwa kiasi fulani kwenye maisha ya kawaida,” alisema Shaka.

Anayemsaidia
Baada ya kutoka hospitali kwa sasa anaishi kwa Adam Athuman Khalifa ambaye ni binamu yake.
Anasema kutokana na hali aliyonayo Lucas anaomba Watanzania wamsaidie.

“Tangu atoke hospitali ninaishi naye kwangu najaribu kumsaidia lakini ana mahitaji mengi kwa kuwa hana mikono wala miguu. Kuna wakati anakata tamaa kutokana na hali aliyonayo lakini ninamuweka sawa kisaikolojia aikubali hali yake, hivyo naomba Watanzania wamsaidie,” anasema.

Nelson Swai dereva bodaboda Dumila aliyekuwa akifanya kazi na Lucas anasema siku alipotekwa hawakugundua.

“Tulikuwa tunapaki eneo moja, lakini ghafla tulishangaa kuona siku tatu hayupo hapa kijiweni, baadaye ndipo tukapata taarifa kwamba mwenzetu alitekwa na kuporwa pikipiki kwa kuwa matendo ya utekaji hapa Dumila yamekuwa yakitokea na kutoweka,” anasema.

Ameliomba Jeshi la Polisi kuongeza ulinzi ili watu wasiojulikana wasiendelee kuleta madhara kwao.

CREDIT: MWANANCHI
 
Back
Top Bottom