Image caption Jaji Lubuva alikutana na Rais Magufuli baada ya kutoka kikao cha EAC Kampala kilichojadili uchaguzi mkuu wa Uganda
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania Jaji Damian Lubuva amesema Rais John Magufuli hafai kuingilia kwenye mzozo wa uchaguzi unaoendelea visiwani Zanzibar.
Akizungumza alipokutana na Dkt Magufuli katika ikulu, Dar es Salaam Jumatatu, Jaji Lubuva amesema tume za uchaguzi zinafaa kuwa huru na hazifai kuingiliwa kimaamuzi na Rais wala kiongozi yeyote.
Amesema wanaosema Rais anapaswa kuingilia kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani Rais hana mamlaka hayo.
“Unaposikia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama kujikanganya, huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa halafu huku unasema aingilie kati maamuzi ya tume,” amesema Jaji Lubuva, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kutoka ikulu na kaimu mkurugenzi ya mawasiliano ya ikulu, Bw Gerson Msigwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika visiwani humo tarehe 25 Oktoba mwaka uliopita akisema kulikuwa na kasoro nyingi.
Wiki iliyopita, Bw Jecha, kupitia tararifa, alitangaza kwamba uchaguzi utarudiwa Machi 20.
Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kimekuwa kikisisitiza kwamba mshindi wa uchaguzi wa mwaka jana anafaa kutangazwa, kimesema hakitashiriki marudio hayo ya uchaguzi.