Lowassa vs Magufuli:Yupi ni ‘shetani nafuu’ tumpe kura? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Lowassa vs Magufuli:Yupi ni ‘shetani nafuu’ tumpe kura?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by singidadodoma, Sep 3, 2015.

 1. s

  singidadodoma JF-Expert Member

  #1
  Sep 3, 2015
  Joined: Nov 11, 2013
  Messages: 4,398
  Likes Received: 545
  Trophy Points: 280
  Lowassa vs Magufuli:Yupi ni ‘shetani nafuu' tumpe kura?

  Mwandishi Wetu

  PAPA Francis – Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani aliwahi kusema hivi: "This is me, a sinner on whom the Lord has turned his gaze. Iam a sinner, but I trust in the infinite mercy and patience of our Lord Jesus Christ". Tafsiri isiyo rasmi ya maneno hayo yaweza kuwa hivi: "Mimi ni mwenye dhambi ambaye Mungu amemwangazia. Mimi ni mwenye dhambi, lakini naamini katika msamaha na uvumilivu wa Bwana wetu Yesu Kristo."

  Kabla sijaainisha kauli hiyo ya Papa Francis na ujumbe wangu wa leo, napenda kuwafahamisha wasomaji wangu wote ya kwamba nimepokea sms na emails za baadhi yenu zinazonilalamikia kuwa nimewachanganya kuhusu mgombea urais yupi kati ya Edward Lowassa (Chadema) na John Magufuli wanapaswa kumpigia kura Oktoba 25.

  Wasomaji hao wamelalamika kwamba nimewaacha njia panda kwa sababu katika maandishi yangu ya hivi karibuni nimewakosoa wote – Magufuli na Lowassa (japo kwa viwango tofauti) kwamba hawana sifa za kutosheleza kushika wadhifa huo mkubwa kabisa nchini.

  Wasomaji hao wamerejea makala niliyoiandika katika toleo Na.415 la Julai 22-28 yenye kichwa kinachosomeka: "Kama akiwa Rais, nani atamfunga ‘gavana' Magufuli?". Wamerejea pia makala kadhaa nilizoandika kuhusu nakisi ya uadilifu ya mgombea urais wa Chadema – Lowassa.

  Ni kweli kwamba katika toleo hilo Na.415 nilieleza kwa kirefu kutosisimshwa na uteuzi wa CCM uliomfanya Magufuli awe mgombea urais wake. Nilitoa mifano ya mapungufu yake machache kuanzia kwenye maamuzi yake ya jazba hadi kwenye kauli zake za hovyo. Kitu ambacho pengine sikukieleza katika makala hiyo ni kwamba (kama ilivyo kwa Lowassa) Magufuli naye amepata kuandamwa na kashfa ya ufisadi. Kwa hiyo, si kweli kwamba yeye ni mwadilifu kwa asilimia 100!

  Labda nitoe mfano mmoja tu ninaoukumbuka kwa haraka unaohusu namna alivyosimamia kifisadi zoezi lile la uuzwaji wa nyumba za serikali lililoasisiwa na utawala wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Mwaka 2006 gazeti la Rai liliwahi kuandika habari kadhaa za uchunguzi kuhusu namna Magufuli alivyomuuzia ndugu yake na ‘kidosho' wake mmoja nyumba mbili za NHC zilizokuwepo Ubungo ilhali wawili hao hawakuwa wafanyakazi wa serikali au NHC. Tena waliuziwa kwa bei poa.

  Nakumbuka ya kwamba baada ya habari ya kwanza kuchapishwa, Magufuli alisihi tusiendelee kuandika habari hiyo, lakini ushawishi wake uliposhindikana alifanya jambo la kipuuzi ambalo mpaka leo tunalikumbuka sisi tuliokuwa Habari Corporation na sasa Raia Mwema. Jambo lenyewe la kipuuzi ni kwamba Magufuli aliamua kwenda kituo kidogo cha Polisi cha Mabatini kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam na kufungua madai ya uongo kwamba eti alikuwa anatishiwa kuuawa na wahariri wa gazeti la Rai.

  Kwa sababu ya madai hayo ya uongo, aliyekuwa Mhariri Mtendaji, John Bwire na mhariri wa gazeti hilo ambaye ndiye aliyekuwa akiandikia habari hizo za uchunguzi, Muhingo Rweyemamu, wakafikishwa katika kituo hicho cha polisi kwa tuhuma nzito za kutaka kumuua Magufuli!

  Nakumbuka ya kwamba siku hiyo ilikuwa ni Ijumaa (mchana) na ilikuwa ni mpango wa Magufuli kuwakomoa wawekwe ndani wikiendi nzima hadi Jumatatu! Hata hivyo, polisi wa kile kituo walipofahamu kwamba chanzo ni skandali hiyo ya Magufuli iliyokuwa ikiandikwa na gazeti la Rai, wakayapuuza madai hayo ya Magufuli, na hivyo kuwaruhusu wahariri hao kujidhamini wenyewe.

  Madai hayo ya hatari yalikuja kufa baadaye kifo cha asili baada ya Magufuli mwenyewe kutolifuatilia tena suala hilo kwenye kituo hicho cha Polisi. Mpaka leo tukilikumbuka tukio hilo huwa tunacheka; maana kote duniani ni waandishi wa habari ndio wanaotolewa roho na wanasiasa na watawala, na wala si watawala ndiyo wanaotolewa roho na waandishi!

  Kwa hiyo, hata Magufuli si msafi kihivyo. Tukio hilo la mwaka 2006 ninalolizungumzia si la uzushi au kutunga. Bahati nzuri nakala za magazeti hayo ya Rai yaliyoandika kuhusu ufisadi wake huo bado zipo kule New Habari Corporation.

  Na bahati nzuri pia ni kwamba wahariri hao wawili bado wapo hai – waulizwe kama mimi ninayeandika haya ninadanganya. Kwa sasa, John Bwire ni mkurugenzi mwenzangu katika gazeti hili la Raia Mwema na Muhingo Rweyemamu ni Mkuu wa Wilaya ya Makete – waulizwe. Sasa, huyo ndiye John Pombe Magufuli wetu ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa rais wetu mpya. Hebu jiulizeni: Kama aliweza kuwatungia wahariri uongo huo mkubwa na wa hatari, na kuwafikisha polisi akiwa ni waziri wa kawaida tu, vipi atakapokuwa rais?

  Nilimsikiliza hivi karibuni wakati akihutubia pale Jangwani kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM. Miongoni mwa mambo mengi aliahidi kuwa ataheshimu na kulinda uhuru wa vyombo vya habari. Mimi kwa kulikumbuka tukio hilo la mwaka 2006, natia shaka kuhusu kauli yake hiyo. Ndugu zangu, nimelizungumzia tukio hilo la mwaka 2006 kuongezea tu katika yale niliyokwisha kuandika kuhusu ugombea urais wa Magufuli katika ile makala yangu kwenye toleo Na. 415. Kwa ufupi, uteuzi wa Magufuli kuwania urais mimi binafsi haujanisisimua na haukupata kunisisimua.

  Nikirejea kwenye mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, huyo ndiye hanisisimui kabisa. Sina haja ya kurudia hapa niliyokwishaeleza kuhusu tuhuma za ufisadi ambazo zimemwandama kwa takriban miaka 20.

  Labda tu kwa kuwa nimemzungumzia Magufuli katika muktadha wa suala zima la uhuru wa vyombo vya habari, nimzungumzie pia kidogo Lowassa kwa muktadha huo huo wa uhuru wa vyombo vya habari; hasa kwa kuwa hivi sasa amewavuta upande wake wahariri wengi wa habari nchini.

  Na hapa nalikumbuka tukio la mwaka 2010. Tukio hilo linahusu baadhi ya wanafamilia yake na maswahiba wake kujaribu kutushawishi tusichapishe katika gazeti hili habari za mwanawe Fred Lowassa kuchunguzwa na polisi wa Uingereza baada ya kuhamishia huko kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununulia nyumba jijini London!

  Katika toleo lake Na. 161 la Novemba 2010 Raia Mwema liliandika habari kubwa ukurasa wa mbele iliyokuwa na kichwa kinachosomeka hivi: Familia ya Lowassa yapelelezwa London.

  Mazingira ya kuingizwa fedha hizo kwenye akaunti ya kampuni ya uwakala inayoitwa Mishcon ndiyo yaliyoifanya Taasisi ya SCD 6 Economics and Specialist Crime Proceeds of Corruption Unit ya Uingereza kuanzisha uchunguzi huo ikitilia shaka uhalali wa fedha hizo. Kutokana na mazingira hayo, SCD 6 Economic and Specialist Crime Proceeds of Corruption Unit yenye ofisi zake Victoria Block, New Scotland Yard, London ililazimika kuwasiliana na Kitengo cha Ufuatiliaji wa Fedha Haramu cha hapa nchini ikitaka maelezo ya awali kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi kuhusu fedha hizo.

  Wakati huo Raia Mwema liliwasiliana na Fred ambaye alikana kununua nyumba Uingereza lakini alikiri kuwahi kutuma fedha hizo huko! Hata hivyo, kwa upande mwingine, gazeti hili lilibaini kuwa, maelezo ya awali ambayo yalitakiwa kutoka Tanzania na makachero hao wa Uingereza, ilikuwa ni pamoja na kutaka kufahamu kama kweli Fred ni mbia katika kampuni za Alphatel Partnership (Tanzania), Barare Ltd na Intergrated Tanzania Limited - kampuni ambazo zimefahamika kumilikiwa na familia ya Lowassa.

  Nakumbuka ya kwamba baada ya familia ya Lowassa na maswahiba wake kufahamu kuwa tulikuwa na habari hiyo ya uchunguzi, walijaribu kutushawishi tusiichapishe na hata kwenda kiwandani kumtisha kumshitaki mwenye kiwanda kama atachapa toleo hilo. Hata hivyo, pamoja na juhudi zote za kutuzuia, tulifanikiwa kuichapa habari hiyo, lakini kesho gazeti lilipoingia mitaani kukawa pia na gazeti moja la kila siku lililokuwa na habari inayokanusha habari hiyo ya gazeti letu.

  Hiyo nayo ilikuwa ni kituko kama kile cha Magufuli. Yaani gazeti moja siku hiyo lina habari inayohusu kuchunguzwa kwa Fred Lowassa na polisi wa Uingereza lakini siku hiyo hiyo kuna gazeti jingine linaloikanusha habari hiyo aya kwa aya, na yote mawili yaliingia mitaani asubuhi hiyo moja! Hilo si jambo la kawaida kwa magazeti duniani. Na maana yake ni kwamba kuna ‘faulo' ilichezwa na wahusika kupata nakala ya gazeti hilo usiku huo huo kabla halijaingizwa mitaani, na ndiyo maana walipata fursa hiyo ya kukanusha habari hiyo yenye ukweli katika ‘gazeti lao rafiki' usiku huo huo. Ni mbinu za kimafia hizo!

  Vyovyote vile, nimetoa mfano huo wa mwaka 2010 si tu kuthibitisha kwamba mgombea huyo wa Chadema (Lowassa) ‘ana makandokando mengi' (nikitumia maneno ya Kikwete pale Jangwani) yanayotia shaka kuhusu uadilifu wake, lakini pia kwamba naye nitamtilia shaka akiahidi kuwa ataulinda uhuru wa vyombo vya habari akiwa rais.

  Kwa hiyo, ninaposema ya kwamba si Magufuli wala Lowassa ambao ugombea urais wao unanisisimua, maana yangu ndiyo hiyo. Ndugu zangu, kazi ya urais ni kazi nyeti mno na nashangaa baadhi ya Watanzania, kwa uzuzu wao, wameligeuza suala la urais kuwa la ushabiki wa mithili ya Yanga na Simba!

  Kazi ya urais ni kazi nyeti mno na ya kitakatifu. Katika nchi yoyote ile rais ni baada ya Mungu. Akisema uuwawe, unauawa (kama ilivyotokea kwa Robert Ouko). Akisema uteswe, utateswa (kama Dk. Ulimboka). Kama umefungwa gerezani na akasema uachiwe huru, utaachiwa huru hata kama wewe ni jambazi au mbakaji! Akisema nchi iingie vitani, itaingia vitani!

  Ndiyo maana Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alisema Ikulu ni mahali patakatifu. Marais waadilifu tu ndo wanaostahili kuingia hapo. Rais si uchapakazi tu, ni zaidi ya uchapakazi. Rais lazima awe mvumilivu, asimamie haki za binadamu na awe na busara na hekima zinazokaribia kidogo alizokuwanazo Mfalme Suleiman!

  Je, Lowassa na Magufuli wana sifa hizo? Mimi naamini hawana sifa hizo, na pengine ndiyo sababu kuna Watanzania ambao mpaka sasa wako njia panda – hawajui wampigie kura mgombea urais yupi; maana wote wana mapungufu makubwa.

  Je, hao wasusie uchaguzi kwa sababu tu wameletewa wagombea urais wawili wasiofaa? Jibu langu ni "hapana". Kama alivyopata kusema msomaji wangu Condrad Mariki: No matter what, the future is ahead of us. Bado tuna wajibu wa kumchagua rais mpya hata kama tulioletewa kuwapigia kura ni ‘shetani' wawili wanaofanana – Magufuli na Lowassa.

  Na hapa niirejee ile nukuu ya Papa Francis. Hawa wawili – Magufuli na Lowassa si wasafi sana, lakini ndo ambao tumepewa tumchague mmoja wao. Tayari tumeshaanza kusikia ya kuwa mmojawao eti ni mpango wa Mungu! Mwingine naye itakuja kusemwa hivyo hivyo.

  Kama kweli ujio wao ni mipango ya Mungu, basi angalau wafanye kile ambacho Papa Francis alifanya wakati alipoulizwa iwapo yupo tayari kuwa papa. Yaani wagombea wetu hao wa urais nao wakiri kuwa ni wenye dhambi (nakisi za uadilifu) lakini wanaotegemea msamaha na uvumilivu wa Yesu Kristo! Nasema hivyo maana, kama nilivyoeleza mwanzo, uadilifu wao unatia shaka.

  Nikirejea kwa wale wasomaji wangu ambao wamelalamika kuwa nimewachanganya na kuwaacha njia panda baada ya kuwakosoa wagombea wote hao wawili, jibu langu ni hili: Lowassa na Magufuli ni ‘shetani' wawili wanaofanana. Wanafanana hata kwa maamuzi ya jazba na ufokeaji hadharani watendaji. Lakini chagueni ‘shetani' mmoja mwenye nafuu kidogo - Waingereza wanasema a lesser devil (shetani mwenye nafuu).

  Hata hivyo, wakati mtakapokwenda kumpigia kura huyo lesser devil wenu, Oktoba 25, msimpigie pia mgombea ubunge wake. Kwa mfano, kama kura yako ni kwa Lowassa, basi kura ya mbunge mpe mgombea wa ACT Wazalendo au CCM, na kama a lesser devil wako ni Magufuli - basi mpe mgombea wa Chadema au ACT Wazalendo kura ya ubunge.

  Hiyo inaweza kutusaidia kidogo kujiaminisha kwamba lesser devil wetu tutakayemwingiza Ikulu hatakuwa na wingi mkubwa wa wabunge wa chama chake bungeni. Na hiyo maana yake ni kwamba Bunge linaweza kumdhibiti hapo atakapoanza kuleta ‘ushetani' wake serikalini!

  Ndugu zangu, nihitimishe kwa kusema ya kwamba mimi tayari ninamjua a lesser devil wangu (‘shetani poa') nitakayempigia kura yangu ya urais Oktoba 25. Usiniulize ni nani ‘shetani poa' kati ya Magufuli wa CCM na Lowassa wa Chadema. Mwenye macho haambiwi tazama, mwenye bongo haambiwi fikiri, na mwenye masikio haambiwi sikia.

  Nisisitize ya kwamba yeyote kati ya hao wawili atakayefanikiwa kuingia Ikulu tutamkubali – maana chaguo la wengi ni chaguo la Mungu. Huyo ndiye tuliyempata, na huyo ndiye atakuwa hatima yetu, na itakuwa hivyo kwa miaka mitano ijayo.

  Hata hivyo, matumaini yangu ni kwamba rais wetu mpya tutakayempata Oktoba atayakumbuka yale maneno ya mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki, Socrates – He who does not remember the past is condemned to repeat it. Rais wetu mpya akikumbuka kuwa huko nyuma alitenda dhambi (ufisadi), atajitahidi asizirudie tena dhambi hizo akiwa Ikulu – mahali patakatifu! Tafakari.

  Raia Mwema
   
 2. The Boss

  The Boss JF-Expert Member

  #2
  Sep 3, 2015
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 37,852
  Likes Received: 22,947
  Trophy Points: 280
  Mbwambo.....the best writer alive....
   
 3. Kaunga

  Kaunga JF-Expert Member

  #3
  Sep 3, 2015
  Joined: Nov 28, 2010
  Messages: 12,586
  Likes Received: 823
  Trophy Points: 280
  Nice balanced article.
  Nami nimeshamchagua lesser devil. Ni yule ambaye nyuma yake kuna fewer or no miniature devils. Na pia ni kule ambako sijawahi kuwapima kama wanatekeleza ilani zao na ahadi; maana huku kungine najua how unreliable they are.
   
 4. Kaunga

  Kaunga JF-Expert Member

  #4
  Sep 3, 2015
  Joined: Nov 28, 2010
  Messages: 12,586
  Likes Received: 823
  Trophy Points: 280
  Sio kama Mzee Mwanakijiji eeh. Hata mie nimempenda
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 5. The Boss

  The Boss JF-Expert Member

  #5
  Sep 3, 2015
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 37,852
  Likes Received: 22,947
  Trophy Points: 280
  Haahaa we umempenda kwa article hii tu
  zingine utamlaani
  mi namsoma kila jumatano gazeti la RaiaMwema..namuelewa sana
  most important napenda honesty yake
  anakiri alimpigia Mrema kura mwaka 1995 ingawa leo anaona alikosea
   
 6. The Boss

  The Boss JF-Expert Member

  #6
  Sep 3, 2015
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 37,852
  Likes Received: 22,947
  Trophy Points: 280
 7. Shoo Gap

  Shoo Gap JF-Expert Member

  #7
  Sep 3, 2017
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 236
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Du!
   
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
Loading...