Lowassa, Magufuli nunueni Kamera muwafunge wafuasi wenu

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Juzi, Agosti 10, nilijumuika na wanamabadiliko wenzangu kumsindikiza The Don a.k.a Matumaini, Edward Ngoyai Lowassa kwenda ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuchukua fomu ya kugombea Urais. Mimi naye kwa kupapatikia siasa sijambo, saa 12 asubuhi tayari nilikuwa Buguruni.

Utaniambia nini? Matumaini yetu yanaendelea. Niliimba: "CCM wana Magufuli, Ukawa tuna funguo… Magufuli toroka uje, Lowassa anazo funguo."

Mishale ya saa 4 asubuhi msafara wa kutoka Buguruni zilipo ofisi za Cuf kwenda Nec ulipoanza, nikamuona mwanamke mmoja amejichora usoni mseto wa rangi za Cuf, Chadema na NCCR-Mageuzi, nikamkumbuka. Nilimuona pia katika ule msafara ulioanzia Lumumba kumsindikiza John Pombe Magufuli kwenda kuchukua fomu.

Na siku hiyo alikuwa amekoga kijani tupu. Na nilimshuhudia akiimba: "Hatujinyongi, hatunywi sumu, CCM mbele kwa mbele. Tunaipenda wenyewe, chaguo letu milele, na wavimbe wapasuke, watajijua wenyewe, acha waisome namba eeeh, CCM mbele kwa mbele."

Nikajisogeza jirani yake na kumuuliza hili na lile angalau nipate gia ya kuanzia, akaniambia anaitwa Mama Chaupele. Baada ya hapo nikamhoji inakuwaje anakuwa shabiki wa CCM na vyama vya upinzani kwa wakati mmoja?

Mama Chaupele: "Kaka wewe umefuata maandamano au umekuja kufuatilia mambo ya watu? Mbona mimi sijakuufuatilia?"
Alikaribia kunikata maini lakini nikagoma kushindwa. Nikamwambia nataka kumpa ‘dili' la kujitia wazimu kwenye kampeni apate pesa nzuri, kwa hiyo nilichohitaji ni yeye kuniambia yupo chama gani.

"Ooh kumbe, basi mwenzio sina hata chama. Hiki ni kipindi cha mavuno naangalia wapi kwenye ulaji naingia. Siku ile nilijichanganya CCM, leo nipo huku kwa Lowassa," alinijibu Mama Chaupele.

Akakoleza: "Halafu kama kweli unataka kuniunganishia dili liwe zuri, usinipe dili la mchuzi mbuzi, sikawii kubadilika."
Nikamuuliza mpango wake ni kumpigia kura nani? Akajibu: "Kama uchaguzi ungefanyika leo nikiwa katika haya maandamano ya Lowassa ningempigia kura Lowassa. Na siku ile ya Magufuli alipokwenda kuchukua fomu, ningempigia Magufuli. Sijui kesho nitakuwa na mawazo gani.

"Oktoba 25 ni mbali sana, itategemea na mazingira nitakayokutana nayo mbele ya safari. Kadi yangu ya kupigia kura ni mtaji, akitokea mnunuzi mzuri nauza."

Majibu ya Mama Chaupele yalinipa wazo la kuzama katikati zaidi kuzungumza na mmoja baada ya mwingine, niliona kuna majibu tofautitofauti. Nilishaona dalili kuwa tupo kwenye msafara wa Matumaini lakini kila mmoja anaweza kuwa na shabaha yake.

Nilipiga hatua kadhaa kuachana na Mama Chaupele, akanivuta fulana, akasema: "Hilo dili vipi? Chukua namba yangu ya simu ili baadaye unipigie." Nikanakili nambari yake ya simu kisha akaongeza: "Mimi ndiye Mama Chaupele, ukinikuna nakunika, kazi kwako na hilo dili lako."

Nikakutana na dada mwingine aliniambia anaitwa Moza, nikamuuliza yeye ni chama gani, akanijibu: "Mimi ni CCM damu na Rais wangu ni Magufuli."

Nikashtuka, CCM damu mwenye mapenzi na Magufuli anakuwaje tena katikati ya maandamano ya Lowassa na Ukawa? Moza akafunguka: "Mume wangu ni Chadema, si unajua siku hizi Chadema kuna zile timu wafia chama na timu ufisadi na Slaa? Kuna Chadema Mpya ya Lowassa na Chadema Asili ya Babu Slaa. Basi mume wangu ni timu Slaa.

"Kama wewe ni mjanja utakuwa unajua kuwa timu Slaa wamechukia Lowassa kuingia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea Urais. Sasa usiku mimi na mume wangu tuligombana, nilifumania SMS ya mapenzi kwenye simu yake. Kwa hasira nimekuja kwenye maandamano haya ya Lowassa ili nimkere. Hapa kila hatua najipiga picha za ma-selfie na kuweka Facebook na Instagram mpaka akome."

Nilishangaa kwa muda, staili ya Moza ni ya aina yake, akafanya kuniibia siri: "Sikiliza brother, ndani ya ndoa kuna maudhi mengi, kwa hiyo mumeo au mkeo akikutibua, usigombane naye, fanya kile ambacho hakipendi atanyooka tu. Mfano, yeye hapendi ndoa ya Lowassa na Chadema, mimi nimekuja kumsindikiza kuchukua fomu, hapa kila muda ananitumia SMS nirudi nyumbani, ananibembeleza."

Nilipoachana na Moza nikamsogelea kijana mmoja aliyechokachoka, nilipomuuliza kilichompeleka kwenye msafara, aling'aka: "Mimi hata sijaja kumuibia mtu, mimi siyo kibaka wala nini."

Nilimwambia kwa msisitizo yeye ni kibaka kwa sababu haiwezekani ajishtukie, akasema: "Bro unaona huu umati ulivyo mkubwa, ukisema kwa sauti nitauawa, naomba nikuahidi sitamuibia mtu, nitunzie roho yangu."

Kabla sijamalizana na huyo kijana ‘kibaka', nikasikia mbele yangu vijana wawili wananong'onezana: "Huko Nec tunakokwenda si ndiyo kule kwa CCM walikomkata Lowassa mara ya kwanza?" Mwenzake akaitikia: "Ndiyo kwenyewe, hapa tunaandamana kwenda kuwashinikiza CCM wamrudishe Lowassa agombee Urais."

Kuna mtu wa tatu alisikia mazungumzo yao ikabidi aingilie kati kusaidia: "Hii Nec tunayokwenda leo siyo ile Halmashauri Kuu ya CCM, hii ya leo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tunakwenda kuchukua fomu ya kugombea Urais."

Mmoja kati ya wale wawili wa mwanzo akauliza: "Kwani huyo Lowassa anachukua fomu mara ngapi yeye peke yake? Alichukua fomu ya CCM, akachukua ya Chadema kisha Ukawa, leo tena Nec, yeye fomu zote hizo anazitaka za kazi gani? Na zitamsaidia nini?"

Kabla hajajibiwa, mwenzake akadakia: "Kweli mwana, huyu Lowassa anapenda sana kuchukua fomu, bora nyingine angekuwa anawagawia, mimi nitamuomba moja."

Nikajua hawa watu ni kenge kwenye msafara wa mamba, yaani hawajui chochote. Nilitaka kuwaelimisha lakini kwa kelele zile za maandamano nikajua hawatanielewa, na zaidi nitatumia nguvu kubwa kupayuka. Nikaangalia upande mwingine.

Kulikuwa na jamaa mtanashati sana, wazoefu wa mjini wangemwita brother-man. Alivaa jeans mpya, t-shirt nadhifu na kofia aina ya kapelo kichwani. Mkononi alikuwa ameshikilia leso tatu, kila baada ya muda alijifuta vumbi na jasho. Jinsi alivyokuwa anatembea, ni wazi hakutuka kuguswa na watu hovyohovyo.

Nilihamasika kumsogelea, nikamuomba nipige naye picha, akaniuliza ya nini? Nikamjibu: "Si unajua mambo ya instagram na facebook?" Alikataa katakata na hakutaka kabisa kusikia habari hizo, akaema: "Unataka kuniletea matatizo nini? Unajua mimi ni mfuasi wa Chama cha ACT-Wazalendo, najulikana kwa viongozi wote wa kitaifa, hata Zitto Kabwe mwenyewe ananijua."

Mfuasi wa ACT anayejulikana kitaifa mpaka Zitto (Kiongozi wa Chama) anamjua, sasa kilichompeleka kwenye maandamano ya Lowassa kwenda kuchukua fomu ya kugombea Urais Chadema na Ukawa ni nini?

Yule jamaa mtanashati alinijibu: "Ila usimwambie mtu, unajua kote huko mitaani inajulikana kwamba warembo wakali, yaani wale wenye mvuto hasa ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wanamshabikia Lowassa. Na leo ni siku muhimu sana kwa Lowassa, kwa hiyo nilijua lazima watoto wazuri waje kwa wingi kumsindikiza."

Sasa hao warembo wanaomshabikia Lowassa yeye wanamhusu nini? Nilimuuliza na akanijibu: "Kaka acha ushamba, unauliza kalamu ya kukata majina ya wagombea wa CCM kwa Phillip Mangula? Kiingereza hakiulizwi kwa Muingereza, hapa nimekuja kufanya yangu, nachangamkia fursa."

Fursa gani anayoichangamkia? Bado niliona utata wa majibu yake, ikabidi afunguke: "Hapa nimefuata totoz, nipo na wenzangu kama 10, tumekuja kuwinda warembo. Kwetu huu msafara tumeuchukulia kama jukwaa rahisi la kukutana na warembo wakali mjini."

Huyu jamaa kwa kweli alinishinda tabia. Nilimuweka kando na kusogea upande mwingine. Kupenya katikati ya watu ilikuwa kazi sana kutokana na umati mkubwa uliokuwepo, nikampita jamaa mmoja hivi, akaniambia anaitwa Sauli. Alinishika mkono, akanipa namba 13 za pikipiki, kwamba nikiiona yoyote kati ya hizo nimjulishe, akanipa namba yake ya simu.

Hizo pikipiki alizihitaji za nini? Akanijibu: "Bosi wangu kanipa kazi ya kufuatilia pikipiki zake. Ana pikipiki 34, nimeshaziona 21, bado hizo 13. Nipo na wenzangu saba, kazi yetu ni kufuatilia kujua hizo pikipiki kama zote zipo ili tuhesabu pesa ya bosi leo ni shilingi ngapi.

"Madereva wa bodaboda wana kawaida ya kuwapunja hesabu mabosi. Sasa leo ni neema, tumesikia kila bodaboda inajazwa full tank na shilingi 20,000. Pikipiki 21 tumeziona na kuhakikisha zipo kwenye msafara, bado 13 hatujaziona."

Nikamuuliza: "Kumbe wewe siyo mwana maandamano ni mfuatilia pikipiki za bosi wako?" Kwa kauli iliyonyooka akanijibu: "Kwani kila unayemuona hapa unadhani amefuata maandamano? Wengine tumefuata yetu. Hapa kuna vibaka, wauza ice cream, wamachinga wameleta biashara zao. Kuna wanaume wamekuja kuwachunga wake zao wasije kuporwa."

NASHAURI WAGOMBEA WAWAFUNGE KAMERA WAFUASI WAO
Uchaguzi Mkuu 2005, Mwenyekiti wa Tanzania Labor Party (TLP), Augustino Lyatonga Mrema, alipigwa butwaa baada ya kukuta kituoni amepata kura moja tu. Akawa mbogo, akalalamika: "Ina maana hata mke wangu hakunipigia?"

Wingi wa wafuasi siyo idadi ya kura. Huu ni ujumbe kwa Lowassa na Magufuli. Binadamu wanabadilika sana. Utakuwa naye kwenye maandamano kumbe ni kimwili tu, kiroho yupo mbali. Na wengine wanafuata maslahi yao.

Zimekuwa zikiibuka hoja nyingi kuhusu wizi wa kura. Na nyingine zinatia shaka ya usalama wa baadaye katika nchi. Nashauri wagombea wasidanganyike na umati wa pamoja. Watu walioandamana kumsindikiza Lowassa kuchukua fomu, hawafiki hata moja ya nane ya wapigakura wa Jiji la Dar es Salaam. Hapo tunazo taarifa za uwepo wa watu waliosafarishwa kuja Dar kumsindikiza kwenda tume.

Ni tabia ileile ambayo Lowassa alitia nayo fora wakati akisaka wadhamini nchi nzima. Kila mkoa alisafiri na mabasi, ndege na helikopta. Tutambue kuwa mapambio ya kujaza watu ni kazi bure kama hayataendana na matokeo ya jumla.

Labda Magufuli na Lowassa wanunue kamera maalum, wawafunge wapigakura wao ndipo wataweza kujihakikishia idadi. Maana hoja za kuibiwa kura zinaonesha hata mawakala ambao husimamishwa vituoni na vyama bado hawaaminiki.

Tukumbuke, wanawake walivua kanga na kumtandikia Mrema atembee juu yake ili asikanyage vumbi. Gari la Mrema halikuwa na haja ya kupelekwa kituo cha mafuta, wafuasi wake walilisukuma. Swali ni je, wote wanaoandama wanayo shabaha moja ya maandamano? Au wengi wao ni bendera inayofuata upepo? Na je, wote watapiga kura? Oktoba 25, 2015 ndiyo mwamuzi!

By Luqman Maloto
 
Ni kweli baadhi ya watu kwenye ule msafara walikuwa na ishu zingine..

Mfano mtoa mada nadhani lengo kubwa ulikuwa unatafuta madem...
Ndo maana ulikuwa unajishughulisha nao tu...
 
yani mtoa mada unatuona humu jf ni watoto mno! mpaka utupikie haka ka hadidhi kauongo? pelekea kahadidh kako watoto wa chekechea. wanaweza wakajua nikweli.
 
Mtatafuta sababu sisizo na vichwa wala miguu kuaminisha watu eti ule umati walikua hawajui kinachoendelea lakini mtagonga mwamba.Katika umati ule eti ukamfahamu mtu ambaye kwa magufuri alikuwa kwenye full kijani alafu huku akiwa amejichora rangi za vyama vya ukawa inawezekanaje?Hili linawezekana tu ikiwa huyo mtu ulikiwa unamfahamu kabla ya matukio haya mawili so ulipomuona kwa magufuri ukamtambia alafu ukabahatika kuwa karibu naye kwa lowasa ukamfahamu kwa kuwa mnafahamiana.
Nikukumbushe kuwa walioenda kwa magifuli ni wajumbe na wanachama ndakindaki wa ccm waliochukuliwa mpaka mkiranga kwa UDA,lakini kwa Lowasa ni watu kwa nauli na jasho lao waliwiwa kwenda.
MWAKA HUU MMESHIKA PAMOTO WAKUU
 
Chai hiii ww mtoa mada na ww nichaji ya Kobe unachaji kila betri ulienda kuchunguza nn kwenye maandamano?
 
Kinachonishangaza kwenye huu utafiti wake ni kwamba hakupata hata moja aliyekwenda kwenye maandamano hayo kwa sababu anampenda Lowassa. Ina maana sampling yake ilikuwa biased?
 
Mtoa mada muongo sana andika vitabu vya hadidhi za watt ndio watakuckiliza na kufurahia uzi mrefu kutuchosha tu lkn hakuna cha maana.
 
ungetuambia kwanza kule ulikumuona mama chaupele kwa mara ya kwanza ulienda kufanya nini alafu ndio uedit story yako maana inakumbusha hadithi za bibi ambazo hazikuwa za kweli lakini zilitaka kutoa funzo kwa mjukuu
 
We mburura wote ulikuwa unawauliza wewe walifuata yao , mbona kwa magufuli hukuulizaa au wewe ulifwata nini, mafuliko yakifika hayachagui woteeeeeeeeeeee yanasomba tu.
 
Back
Top Bottom