Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,315
- 33,111
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza maelezo ya awali ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumshi wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba, kufuatia mshitakiwa huyo kutokuwepo mahakamani kwa sababu anaumwa.
Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimwongo aliyesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwinga, alisema anakubaliana na ombi la mawakili wa pande zote la kutaka kesi hiyo iahirishwe kwa sababu ya mshitakiwa huyo ni mgonjwa na kuongeza kuwa anaahirisha kesi hiyo hadi Septemba 21, ambapo itakuja kwa ajili ya kutajwa na Septemba 25, kesi hiyo itakuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali na kutoa amri kwamba mshitakiwa aletwe mahakamani kwa mujibu wa tarehe hizo.
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Justus Mulokozi, aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya wao kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali, na upande wa serikali ulikuwa tayari kufanya hivyo, lakini taarifa alizozipata toka uongozi wa Jeshi la Magereza muda mfupi baada ya kuingia mahakamani hapo, ni kwamba askari wa jeshi hilo wameshindwa kumfikisha mahakamani mshitakiwa kutoka gereza la Keko kwa sababu anaumwa.
Kwa upande wake, Wakili wa utetezi Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, walisema hawana pingamizi na hoja ya upande wa serikali.
Mei 28, mwaka huu, Mulokozi alidai mahakamani hapo kuwa, Liyumba anakabiliwa na makosa mawili ya jinai katika kesi hiyo Na. 105/2009 kwa matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006 akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.
Aidha, anadaiwa kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha kosa linaloangukia kwenye shitaka la kwanza.
Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Mei 27, mwaka huu, Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina dosari za kisheria.
Wakati huo huo, Hakimu Mkazi Benedict Mhingwa na Catherine Revocate, waliahirisha kusikiliza kesi ya wizi wa sh bilioni 2.2 inayomkabili kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein kwa sababu mwanajopo mmoja, Fatma Masengi ameteuliwa kuwa jaji na kwa sasa yupo likizo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 21.
Chanzo: Tanzania Daima