Dodoma: Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge la 10, Nov 2010

Kagemro

JF-Expert Member
Jan 11, 2010
1,433
633
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE UZINDUZI RASMI WA BUNGE LA KUMI LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 18 NOVEMBA, 2010

FINAL VERSION


Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo ada niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kushiriki na kushuhudia uzinduzi wa Bunge la Kumi tangu kuundwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni siku adhimu katika historia ya nchi yetu na Bunge letu ambapo sote hatuna budi kujipongeza.

Mheshimiwa Spika;

Niruhusu nikupongeze kwa kuchaguliwa kwako kwa kishindo kuwa Spika wa Bunge letu. Ni ushindi ulioustahili kufuatia historia yako iliyotukuka ya miaka 35 ya kuwa Mbunge na miaka kadhaa ya utumishi wa umma nchini. Umefungua ukurasa mpya katika maisha yako binafsi, Bunge letu na nchi yetu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hii. Ni heshima kwako na ni fahari kwa nchi yetu kwamba hatuna ajizi katika kuwapa fursa wanawake. Bila ya shaka umefungua milango kwa wanawake kuweza kuaminiwa kushika nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa nchi yetu, Inshaalah. Nakuahidi ushirikiano wangu na ule wa wenzangu wote Serikalini katika kufanikisha majukumu yako na ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika;

Napenda kuchukua fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Samuel Sitta kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuliongoza Bunge la Tisa. Atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri aliyoyafanya katika kipindi chake. Tunamtakia kila la heri katika kuwahudumia wananchi wa Urambo Mashariki na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge, kwa kuaminiwa na wananchi na kuchaguliwa kuwa wawakilishi wao katika Bunge hili. Hiyo ni heshima kubwa mliyopewa. Nawatakieni kila la heri hasa wakati huu mnapojiandaa kuonyesha kuwa kweli mmestahili heshima hiyo. Napenda kuwakumbusha kuwa msijisahau kuwatembelea wapiga kura wenu kwa maelezo kuwa mna shughuli nyingi za Bunge na Kamati zake. Wananchi hukasirishwa sana wasipowaona wawakilishi wao wakiwatembelea na kuzungumza nao. Aghalabu hasira zao wanazionyesha kwenye uchaguzi. Mkumbuke miaka mitano si mingi.



Shukrani kwa Wananchi Kuchagua CCM


Mheshimiwa Spika,
Narudia tena kutoa shukrani zangu kwa wananchi kwa kunichagua mimi, Dkt Mohamed Gharib Bilal na Chama Cha Mapinduzi kuongoza nchi yetu kwa miaka mitano ijayo. Ushindi wetu ni ushahidi tosha kwamba Watanzania wanatambua na kuthamini kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Chama chetu katika miaka mitano iliyopita. Aidha, kwamba wamekubaliana na hoja tulizozitoa kuhusu mikakati yetu ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu na kusukuma gurudumu la maendeleo.

Nawashukuru wana-CCM wenzangu wote, kuanzia viongozi wa kitaifa hadi kwenye mashina pamoja na wapenzi na washabiki wa CCM kote nchini kwa kuutafuta ushindi na kuupata. Kazi iliyo mbele yetu sasa ni kutimiza ahadi zetu kwa Watanzania. Napenda kuwahakikishia kuwa chini ya uongozi wangu kazi hiyo ipo katika mikono salama.



Shukrani kwa Waziri Mkuu


Mheshimiwa Spika,
Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kukubali uteuzi wangu wa Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. Wengi wenu mnamjua vizuri. Mmekuwa nae kwa kipindi kilichopita na ndiyo maana hapakuwa na taabu kumthibitisha. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge mumpe ushirikiano kama mlivyofanya kipindi kilichopita.



Majukumu ya Msingi


Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,
Nilipozindua Bunge la Tisa, Desemba 30, 2005, nilifafanua majukumu yetu ya msingi, yaani kwangu, Serikali yetu, Wabunge na wananchi wote kwa jumla. Niliainisha mambo makuu matatu: Kwanza, kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini, maeneo watokayo na ufuasi wa vyama vya siasa. Aidha, nilisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuwa nchi yenye usalama, amani na utulivu. Pili, kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa nchi yetu na watu wake. Na, tatu, kuhakikisha kuwa demokrasia yetu inazidi kustawi na Serikali inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na maovu katika jamii.

Mheshimiwa Spika;

Leo miaka mitano baadaye, tunapozindua Bunge la 10 bado naamini kuwa mambo haya matatu yanastahili kuendelea kuwa ndiyo majukumu yetu ya msingi. Yanafaa kuendelea kuwa mwongozo kwetu katika kupanga vipaumbele vyetu, kubuni sera na kutengeneza mipango ya maendeleo. Safari ile nilisema tutatekeleza majukumu yetu kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya, safari hii nasema tutafanya hivyo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.



Vipaumbele 13


Mheshimiwa Spika,

Kwa ajili ya hiyo basi, Serikali nitakayoiunda siku chache zijazo itakuwa na vipaumbele 13 vifuatavyo:

1. Kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kudumu na kuimarika;

2. Kuendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini kwa kuchukua hatua thabiti za kuharakisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda. Aidha, tuboreshe mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ili tuvutie wawekezaji wengi wa ndani na nje kuwekeza katika sekta mbalimbali;

3. Kuongeza jitihada za kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi wetu unaokua. Tuboreshe mipango iliyopo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wote wanaotaka kujiajiri. Aidha, tuweke mipango thabiti ya kuwatambua na kuwawezesha wajasiriamali wa tabaka la kati ili wastawi na waweze kushiriki katika uwekezaji mkubwa ndani na hata nje ya nchi yetu;

4. Kuendelea kujenga na kuimarisha sekta binafsi nchini na kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya ushirikiano na sekta ya umma. Aidha, tuimarishe uwezo wa Serikali kupanga mipango ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wake bila kuingilia isivyostahili shughuli za sekta binafsi;

5. Kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Kwa ajili hiyo hatuna budi kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na teknohama. Aidha, tuongeze ufanisi katika utendaji na utoaji wa huduma wa miundombinu hiyo;

6. Kuongeza jitihada za kuhakikisha Taifa letu linanufaika zaidi na maliasili zake zilizopo juu na chini ya ardhi. Tutahakikisha kuwa tunazo sera na sheria za uvunaji na matumizi ya rasilimali hizo zinazonufaisha taifa letu sawia;

7. Kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma;

8. Kuendeleza juhudi za kupanua fursa za elimu kwa vijana wetu tangu elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Aidha, tutoe msukumo na kipaumbele maalum kwa masomo ya sayansi katika ngazi zote. Pia, tuweke mkazo maalum wa kuboresha elimu ya msingi na sekondari ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi;

9. Kuongeza jitihada za kupanua na kuboresha huduma muhimu za kiuchumi na kijamii hususan afya, maji, umeme, barabara, reli, bandari, anga, simu, teknohama na huduma za fedha;

10. Kuimarisha utawala bora, demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali ya umma. Kwa ajili hiyo tutaendelea kuvijenga na kuviwezesha kirasilimali, kimuundo na kisheria vyombo vinavyoongoza mapambano hayo na vile vya kutoa na kusimamia haki nchini;

11. Kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri uliyopo baina ya nchi yetu na majirani zetu pamoja na mataifa mengine duniani na mashirika ya kimataifa. Aidha, tutaendelea kutafuta marafiki wapya na kuboresha diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya nchi yetu;

12. Kuongeza maradufu juhudi za kuhifadhi mazingira hasa wakati huu ambapo makali ya athari za mabadiliko ya tabia nchi yanazidi kutuumiza sote; na

13. Kulinda mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pamoja na yale ya tangu uhuru mpaka sasa. Aidha, tukamilishe yale tuliyoyaahidi mwaka 2005 ambayo hatukuweza kuyakamilisha.



Tudumishe Umoja wa Nchi yetu


Mheshimiwa Spika,
Nguvu ya mnyonge na maskini ni umoja. Hivyo basi, na sisi hatuna budi kudumisha umoja wa nchi yetu kwa gharama yoyote ile. Umoja wa nchi yetu una sura tatu kuu. Kwanza ni mipaka inayotambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa salama. Nafurahi kusema kuwa mipaka ya nchi yetu iko salama na wala hakuna tishio lolote la kutoka ndani au nje ya nchi yetu dhidi ya mipaka yetu.

Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Maafisa na askari wote wa JWTZ kwa kazi nzuri waifanyayo ya kulinda mipaka ya nchi yetu. Nawaomba waendelee na moyo wao huo wa uzalendo. Napenda kuwahakikishia kuwa kazi tuliyoianza ya kuliimarisha Jeshi letu kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa vya utendaji kivita tutaiendeleza bila ajizi. Aidha, tutaendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi wetu pamoja na mazingira yao ya kuishi na kufanyia kazi.



Muungano


Mheshimiwa Spika;
Sura ya pili ya umoja wa nchi yetu ni Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika uliozaa nchi moja mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa Muungano wetu unadumu na unazidi kuimarika. Nafurahi kusema kuwa Muungano wetu ni imara licha ya changamoto za hapa na pale. Na, kinachonipa faraja zaidi ni ule ukweli kwamba pande zetu zote mbili za Muungano zinayo dhamira ya dhati ya kutatua kero zilizopo kwa lengo la kuuimarisha.

Mheshimiwa Spika;

Nafurahi kwamba dhamira yangu ya kuimarisha kamati ya pamoja ya Serikali zetu mbili kuhusu masuala ya Muungano imefanikiwa. Kamati hiyo imefanya kazi nzuri sana na mambo mengi yaliyokuwa yanaleta usumbufu na misuguano yamezungumzwa kwa uwazi na kupatiwa majawabu. Yale machache yaliyosalia tutaendelea kuyapatia ufumbuzi ulio muafaka kwetu sote.

Mheshimiwa Spika;

Niruhusu nimshukuru na kumpongeza kwa dhati aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mzuri. Aidha, nawapongeza kwa namna ya kipekee Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na Mheshimiwa Edward Lowassa kabla yake, kwa upande wa Serikali ya Muungano na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nawapongeza kwa umakini wao, moyo wao wa uzalendo na kwa juhudi zao zilizozaa matunda mema.



Umoja wa Watu


Mheshimiwa Spika;
Sura ya tatu ya umoja wa nchi yetu ni ile ya wananchi wetu kuwa wamoja, wanaopendana, kushirikiana na kushikamana. Pamoja na changamoto za hapa na pale, Watanzania wameendelea kuwa watu wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini, maeneo wanayotoka na ufuasi wa vyama vya siasa. Kubaguana na kuchukiana kwa sababu za tofauti zao hizo ni mambo mageni kabisa kwao. Nafurahi kwamba hata pale waliposhawishiwa wengi wao walikataa na waliunga mkono kwa wingi sana juhudi za kutafuta suluhu.

Mheshimiwa Spika;

Bila ya shaka sote tunaikumbuka hali tete ya kisiasa na kiusalama iliyokuwepo Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni. Katika hotuba yangu ya Desemba 30, 2005, nilielezea kusononeshwa na hali hiyo na kuahidi kushirikiana na viongozi wa kisiasa wa pande zote kulitafutia ufumbuzi. Nafurahi kwamba ahadi hiyo imetimia. Zanzibar sasa ni shwari na watu wanaishi kindugu. Serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa na hasama zimeisha.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Mheshimiwa Seif Shariff Hamad ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wao thabiti uliowezesha kupatikana maridhiano ya kisiasa yaliyomaliza mzozo Visiwani humo. Nawapongeza wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuwaunga mkono viongozi wao. Zanzibar sasa ni nzuri kwa kila mtu kuishi.

Mheshimiwa Spika;

Kwa mara nyingine nampongeza Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nampongeza Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Tunawatakia heri katika kazi yao ya kujenga Zanzibar mpya. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana nao kwa lolote watakaloona naweza kuwa wa manufaa. Ahadi yangu hiyo ni ahadi ya Serikali ya Muungano pia.


Mheshimiwa Spika;

Kwa upande wa Tanzania Bara uchaguzi wa mwaka huu umeacha nyufa za mgawanyiko hatari wa kidini ambao hatuna budi tuchukue hatua haraka kuziziba. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana na wanasiasa wenzangu, viongozi wa dini na wa kijamii kulitafutia ufumbuzi suala hili. Si vyema na siyo busara kuliacha likaota mizizi na kulimongonyoa taifa letu. Naomba wenzangu mkubali tuinusuru nchi yetu.


Usalama wa Raia


Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuimarisha usalama wa raia. Kama mjuavyo, tulianza kazi wakati nchini kuna wimbi kubwa la ujambazi ulioonekana kama vile umeshindikana. Nashukuru kwamba Jeshi letu la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya usalama limefanikiwa kudhibiti ujambazi. Uhalifu huo bado upo, lakini upo kwa kiwango cha kudhibitika. Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza maradufu juhudi za kupambana na uhalifu huu na wa aina zote nchini.

Mheshimiwa Spika;

Niruhusu pia nitoe pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi chini ya uongozi wa Inspekta Jenerali Saidi Mwema kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kufanya. Wananchi wanajisikia kuwa salama. Tutaendelea kuliimarisha Jeshi letu hili kwa kuwapatia zana na vifaa vya kisasa vya kazi pamoja na kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya Maafisa na Askari.



Kukuza Uchumi


Mheshimiwa Spika;
Miaka mitano iliyopita ilikuwa migumu sana kwa kazi ya kujenga uchumi wa nchi yetu na kupunguza umaskini. Uchumi wetu ulipata misukosuko mikubwa ikiwemo ukame mkubwa wa mwaka 2005 2006 uliokausha mazao mashambani na kusababisha njaa kubwa iliyoifanya Serikali kulisha watu zaidi ya 3,776,000. Ukame huo pia ulikausha maji katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme na kusababisha upungufu mkubwa sana wa umeme. Kwa ajili hiyo uzalishaji viwandani na utoaji wa huduma muhimu kwa maisha ya Watanzania uliathirika sana.

Mwaka 2007 tukakumbwa na tatizo la kupanda sana kwa bei za mafuta na bei za vyakula duniani. Kana kwamba hiyo haitoshi mwaka 2008 2009 kukaja tatizo la kuyumba kwa masoko ya fedha ya kimataifa na kudorora kwa uchumi wa dunia kulikoathiri nyanja zote za uchumi wetu.

Matokeo ya misukusuko yote hiyo ni kudumaa kwa uwekezaji, kudorora kwa shughuli za uzalishaji, biashara na utalii, kupanda sana kwa mfumuko wa bei, kupungua kwa mauzo nje, kushuka kwa mapato ya fedha za kigeni na mapato ya Serikali pamoja na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi. Kwa sababu hiyo pia kasi ya kupunguza umaskini nayo ilikuwa chini ya lengo tulilojiwekea katika MKUKUTA I.

Mheshimiwa Spika;

Tulilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia uchumi wetu usiporomoke na nafurahi kwamba juhudi zetu zilifanikiwa. Hivi sasa uchumi wetu umekuwa tulivu tena. Kasi ya ukuaji ni nzuri (asilimia 7.1), mfumuko wa bei umeshuka sana kutoka wastani wa asilimia 12.1 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 4.2 hivi sasa. Watalii wameongezeka, shughuli za viwanda na biashara zinarejea katika hali ya zamani. Tunategemea mambo kuwa mazuri zaidi katika miaka mitano ijayo, labda kama kutatokea misukosuko mingine ambayo hatuwezi kuitabiri sasa. Tutaendeleza juhudi hizo za kukuza uchumi ili uchumi wetu uzidi kutengemaa.



Kuendeleza Sekta za Uzalishaji Mali


Mheshimiwa Spika,
Pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwepo juhudi kubwa ilielekezwa katika kuendeleza sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda na madini. Mafanikio ya kutia moyo yalipatikana na dhamira yetu ni kuyadumisha na kupata ufanisi zaidi miaka mitano ijayo.



Kilimo na Mifugo


Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa kilimo na ufugaji, mwaka 2006 tulianzisha programu kubwa ya kuendeleza sekta hizo. Baadaye mwaka 2009 kwa kushirikiana na sekta binafsi tukatengeneza mkakati wa Kilimo Kwanza kuongeza kasi na ufanisi wa utekelezaji wa malengo ya kuleta mapinduzi katika kilimo chetu na ufugaji wetu.

Mheshimiwa Spika;

Matunda ya juhudi zetu hizo yameanza kuonekana. Mavuno kwa mazao ya chakula na biashara yameendelea kuongezeka na mwaka huu tunacho chakula cha kutosha nchini. Tutaendeleza juhudi hizo maradufu katika miaka mitano ijayo. Kwa ajili hiyo vipaumbele vyetu vitakuwa vifuatavyo:
1. Kuendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya sekta ya kilimo na kufikia asilimia 10 ya bajeti ya Serikali;

2. Kuharakisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo ili wakulima, wafugaji na wavuvi wapate mikopo itakayowawezesha kukuza na kuboresha shughuli zao, hivyo kuongeza tija na mapato yao;

3. Kutengeneza na kutekeleza programu maalumu ya kuendeleza ufugaji itakayojumuisha pia uendelezaji wa malisho na kukabiliana na athari za ukame;

4. Kuendeleza utafiti wa kilimo na mifugo;

5. Kuendelea kuhimiza kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya kanuni bora za kilimo, mbolea, mbegu bora, zana za kisasa za kilimo, uboreshaji wa masoko na miundombinu;

6. Kupanua mafunzo ya wataalamu wa kilimo na mifugo wa ngazi mbalimbali ili kupata maafisa ugani wa kutosha wa kuelimisha wakulima na wafugaji; na

7. Kuendeleza mikakati ya kuanzisha kanda za kilimo na kuhamasisha kilimo cha mkataba katika kanda hizo na kwingineko itakapowezekana.



Uvuvi


Mheshimiwa Spika,
Kuhusu uvuvi, tutaendeleza kazi nzuri tuliyoifanya katika miaka mitano iliyopita ya kuendeleza shughuli za uvuvi na kuwaendeleza wavuvi wa baharini na katika maziwa na mito. Tutaendelea na jitihada za kulinda hazina yetu ya samaki dhidi ya uvuvi haramu. Ni makusudio yetu kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010-2015 ya kutengeneza programu kabambe ya kuendeleza sekta ya uvuvi nchini kama tulivyofanya kwa kilimo.



Kuleta Mapinduzi ya Viwanda

Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumeanzisha mkakati wa dhati wa kuendeleza viwanda nchini. Tumeunganisha mamlaka mbili za uendelezaji wa maeneo maalum ya uchumi, yaani Special Economic Zones (SEZ) na Export Processing Zones (EPZ) kuwa chini ya Wizara moja na chini ya uongozi mmoja. Kufanya hivyo kumeimarisha upangaji na utekelezaji wa mipango ya kuendeleza viwanda nchini. Mikoa yote na Wilaya nyingi nchini zimetenga maeneo ya kujenga viwanda yatakayosimamiwa na mamlaka ya Export Processing Zones Authority (EPZA).

Mheshimiwa Spika;

Kwa jumla juhudi zetu za kuendeleza viwanda nchini zina muelekeo mzuri. Sekta ya viwanda inakua kwa kasi nzuri ya karibu asilimia tisa, na inatoa mchango wa zaidi ya asilimia nane katika pato la taifa. Katika miaka mitano ijayo tutaongeza maradufu juhudi za kukuza na kuendeleza viwanda nchini. Tutaongeza uhamasishaji wa uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vipya na kufufua vilivyopo. Aidha, tutaboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo pia kuboresha upatikanaji wa umeme na maji pamoja na kurahisisha taratibu za utoaji wa leseni za biashara na upatikanaji wa malighafi na ardhi.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kuimarisha Benki ya Rasilimali ili iwe chachu ya kukuza viwanda nchini kwa kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa wawekezaji, hasa wazawa. Pia, tutachukua hatua za makusudi za kuliimarisha Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili liweze kuwafikia na kuwawezesha watu wengi zaidi. Tutaitazama na kuiboresha ipasavyo Sheria iliyoanzisha SIDO.



Madini


Mheshimiwa Spika;
Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili nyingi yakiwemo madini ya aina mbalimbali. Katika miaka mitano iliyopita tulielekeza nguvu zetu kwenye kurekebisha mapungufu yaliyokuwemo kwenye mikataba ya madini, sheria na kanuni mbalimbali ili taifa linufaike inavyostahili. Tumefanikiwa kurekebisha mikataba hiyo na makampuni yenye migodi mikubwa yamenza kulipa kodi. Tumetunga Sera Mpya ya Madini (2009) na Sheria Mpya ya Madini (2010). Pia tumeunda kitengo cha Ukaguzi wa Madini. Viwango vya mrabaha vimerekebishwa, ushiriki wa wazawa na Serikali umeainishwa vizuri. Maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo yameanza kutengwa na leseni zinatolewa. Kutokana na hatua hizo mwelekeo wetu sasa ni mzuri na tunahakika taifa litanufaika inavyostahili kwa madini yake. Katika miaka mitano iliyopita madini yameliingizia taifa dola za Kimarekani milioni 4,725.4 na kushika nafasi ya pili nyuma ya utalii kwa tofauti ndogo sana.

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano ijayo, tutaendelea kutatua changamoto ambazo bado hazijapata ufumbuzi. Aidha, tutaliimarisha Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) ili kwa niaba ya Serikali liweze kushiriki katika umiliki wa migodi mikubwa na ya kati na hivyo taifa kunufaika zaidi. Tutaendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika utafutaji na uchimbaji wa madini, gesi asilia, mafuta ya petroli pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali hizo.



Utalii


Mheshimiwa Spika;
Utalii ni sekta inayoongoza katika kuliingizia taifa letu fedha za kigeni. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2005-2009) sekta hii iliingiza jumla ya dola za Kimarekani 4,987.5 milioni. Mafanikio haya yametokana na juhudi kubwa ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ndani na nje ya nchi. Katika miaka mitano ijayo tutaendelea na juhudi hizo kwa kuongeza rasilimali na kupanua wigo wa aina za utalii kuhusisha utamaduni, mazingira, historia/makumbusho na michezo. Pia tutaboresha miundombinu na mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji kwenye mahoteli ya hadhi ya nyota 3 hadi 5.



Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi


Mheshimiwa Spika;
Katika kujenga uchumi wa nchi yetu, hatutafanikiwa bila ya kuwawezesha wananchi na sekta binafsi ya ndani kushiriki na kunufaika. Katika miaka mitano iliyopita tulifanya jitihada kubwa ya uwezeshaji wa wananchi kwa kuanzisha mifuko, taasisi na programu mpya na kuziboresha zilizokuwepo ikiwa ni pamoja na TASAF na MKURABITA. Aidha, tuliwahimiza wananchi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili iwe rahisi kukopesheka. Wamefanya hivyo na wengi wamenufaika sana kupitia SACCOS na VICOBA.

Mheshimiwa Spika;


Ahadi yetu ya kuanzisha Benki ya Wanawake imetimia. Benki hiyo imeanza kazi na tayari inatoa huduma. Katika miaka mitano ijayo, tutaendelea kuijengea uwezo zaidi Benki ya Wanawake, pamoja na kuongeza fedha katika mifuko iliyopo, kuimarisha Benki ya Rasilimali na kuanzisha Benki ya Kilimo. Lengo letu ni kuongeza na kuwawezesha watu wengi kupata mikopo ili waendeleze shughuli zao za ujasiriamali. Pia tumedhamiria, kama nilivyosema awali, kutengeneza mkakati maalum wa kuwawezesha wafanyabiashara wa kati washiriki katika uwekezaji mkubwa.



Kukuza Ajira


Mheshimiwa Spika;
Tutaongeza jitihada za kuwajali vijana wetu wanaoongezeka kila mwaka mijini na vijijini kutafuta ajira na riziki. Tutaboresha mikakati ya kukuza ajira nchini ili watu wengi zaidi hususan vijana waajiriwe na kujiajiri. Tutaongeza kasi ya kujenga majengo ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) kama tulivyofanya pale Ilala, Dar es Salaam ili wawe na mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao. Tutaendelea kujenga majengo ya namna hiyo Dar es Salaam, Mwanza na baadaye katika miji mingine mikuu ya Mikoa hatua kwa hatua. Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wajasiriamali wadogo kujiunga kwenye vikundi ili waweze kutambuliwa na kukopeshwa kwa urahisi.



Tanzania Kuwa Lango Kuu la Biashara


Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu imejaaliwa kuwa mahali ambapo jiografia yake ni rasilimali ya kiuchumi. Tanzania inapakana na nchi za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda ambazo zinategemea bandari, reli, barabara na anga yetu kusafirisha bidhaa zao ziendazo na zitokazo nje.

Bado hatujaitumia kwa ukamilifu rasilimali hii ingawaje biashara ya usafirishaji (transit trade) inazidi kukua na inatuingizia fedha nyingi zaidi za kigeni kuliko kilimo. Tunataka tuikuze zaidi biashara hii ili tunufaike zaidi. Kwa ajili hiyo tutaendeleza, kwa kasi zaidi kazi ya kuimarisha miundombinu ya bandari, reli, barabara, viwanja vya ndege na teknohama katika miaka mitano ijayo.



Bandari na Reli


Mheshimiwa Spika;
Tunao mpango wa kupanua na kuimarisha bandari ya Dar es Salaam ili iweze kupitisha bidhaa nyingi zaidi na kwa ufanisi zaidi. Tutafanya hivyo hivyo kwa bandari za Mtwara, Tanga, Kigoma na Mwanza. Vile vile tutaimarisha bandari za Kasanga, Mbamba Bay, Lindi, Musoma na Bukoba. Pamoja na mchango wa Serikali, tunakusudia kushirikisha sekta binafsi katika juhudi hizi.

Mheshimiwa Spika;

Tutaongeza kasi ya kutatua matatizo yanayozikabili reli zetu mbili yaani TRL na TAZARA. Kwa upande wa reli ya kati tunategemea kuanza ujenzi wa reli mpya ya upana wa kimataifa kutoka Isaka kwenda Rwanda na Burundi na kuboresha reli yetu kutoka Isaka hadi Dar es Salaam iwe ya kiwango hicho. Aidha, tutaanza mchakato wa kuboresha reli kutoka Isaka kwenda Mwanza na kutoka Tabora kwenda Kigoma ili iwe ya kimataifa. Ni matumaini yangu pia katika kipindi hiki tutafanikiwa kupata wabia wa kushirikiana nasi kwa ujenzi wa reli ya Tanga hadi Musoma.



Barabara


Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumejitahidi sana kuimarisha miundombinu ya barabara. Tumejenga barabara za lami, za changarawe na za udongo kote nchini na kuwezesha maeneo mengi hata ya vijijini kufikika. Ni makusudio yetu kuendeleza juhudi hizo maradufu katika miaka mitano ijayo. Tutakamilisha ujenzi wa barabara unaoendelea hivi sasa na kuanza ujenzi wa barabara nyingine zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka huu. Kwa ajili hiyo tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa bajeti ya sekta ya miundombinu kama tulivyofanya katika miaka mitano iliyopita.



Kuboresha Huduma za Kijamii na Kiuchumi



Elimu


Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumefanikiwa kupanua fursa za watoto na vijana wetu wengi sana kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Katika miaka mitano ijayo tutaendelea na upanuzi wa fursa za kupata elimu lakini mkazo mkubwa tutauelekeza katika kuboresha elimu inayotolewa.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa bajeti ya elimu ili tufundishe na kuajiri walimu wengi zaidi, tupate vitabu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Tutaongeza matumizi ya teknohama katika utoaji wa mafunzo pamoja na kujenga uwezo wa wanafunzi na waalimu kiteknolojia ili kwenda sambamba na karne hii ya utandawazi. Aidha, tutajenga maabara za sayansi katika sekondari zetu zote.

Katika kipindi hiki pia tutachukua hatua thabiti za kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi ya walimu na watumishi wa sekta ya elimu. Kwa ajili hiyo, tutakamilisha na kuanza kutekeleza mpango kabambe wa kujenga nyumba za walimu kote nchini. Tutahakikisha kuwa mpango huo unatengewa pesa ya kutosha.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya kwa ajili ya kuandaa vijana wetu kwa stadi mbalimbali za kazi. Kwa upande wa elimu ya juu, katika miaka mitano ijayo tutatekeleza Mpango wetu mpya wa Maendeleo ya Elimu ya Juu ambao malengo yake makuu ni kupanua fursa za elimu ya juu na kuongeza ubora wa elimu ili ikidhi viwango na utashi wa soko la ajira nchini na kimataifa. Tutaimarisha na kupanua vyuo vilivyopo na kujenga vipya.

Mheshimiwa Spika:

Katika miaka mitano ijayo, tutakamilisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na kuanza mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere huko Butiama, Musoma. Katika kipindi hicho pia, tutajenga makazi mapya kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Udaktari cha Muhimbili yatakayokuwa Mloganzila. Tutaendeleza mchakato wa kuipandisha hadhi Taasisi ya Teknolojia ya Mbeya kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia. Ni dhamira yetu pia kutengeneza mpango wa muda wa kati na muda mrefu wa ujenzi wa vyuo vikuu nchini. Kwa maoni yangu Serikali iwe na Chuo Kikuu katika kila kanda hapa nchini.



Afya


Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2007 tulitunga Sera Mpya ya Afya na kutengeneza Mpango wa miaka 10 wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa kutekeleza sera hiyo. Shabaha yetu ni kufanya mambo manne: Kwanza, kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu. Lengo letu hasa ni kuona Watanzania hawatembei zaidi ya kilometa tano kufuata huduma ya zahanati. Aidha, kuwa na vituo vya afya katika kila kata na kuboresha huduma katika hospitali za Wilaya, Mikoa na Kanda ili matatizo mengi yamalizwe huko. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iimarishwe ili iweze kushughulikia matatizo makubwa zaidi yanayohitaji taaluma za kibingwa na vifaa bora zaidi.

Pili,
kujenga uwezo wetu wa ndani wa kutibu maradhi ili tupunguze watu wanaopelekwa nje kwa matibabu. Tatu, kuongeza uwezo wetu wa kupambana na maradhi hasa yale yanayoathiri na kuua watu wengi. Na, nne kuongeza ajira ya madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya ili kupunguza tatizo la uhaba mkubwa wa watumishi wa afya.

Mheshimiwa Spika;

Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wa shabaha zote za MMAM umeanza na unaendelea vizuri. Huu ni mwaka wa pili tu wa utekelezaji na mwelekeo wake ni mzuri. Sina shaka kabisa kuwa tutafanikiwa kutekeleza malengo yetu katika muda wa miaka 10 ya mpango huu.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti ya sekta ya afya kama tulivyofanya katika miaka mitano iliyopita tulipoiongeza kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 1,205.9 mwaka huu. Aidha, tutaendeleza ushirikiano na mashirika ya dini katika utoaji wa huduma ya afya. Vile vile, tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri na kushawishi wenzetu wa sekta binafsi wenye uwezo na wale wenye hospitali kubwa huko nje wajenge hospitali za aina hiyo hapa nchini.



Maji na Mazingira


Mheshimiwa Spika,
Pamoja na juhudi kubwa tulizozifanya katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji nchini, uhaba wa maji bado ni tatizo kubwa katika maeneo mengi. Tumedhamiria kulitatua tatizo hili kwa kuongeza mgao wa fedha za bajeti ya Serikali kwa ajili ya huduma ya maji. Nilishaagiza kwamba tufanye kila tuwezalo ili bajeti ya sekta ya maji iongezwe kwa kiasi kikubwa kuanzia mwaka ujao wa fedha.
Tutaendelea kuwaomba wabia wetu wa maendeleo waongeze mchango wao katika kuendeleza huduma ya maji nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani maalum kwa Benki ya Dunia na wahisani wengine kwa msaada wao mkubwa wanaoutoa kwa sekta ya maji. Ni matumaini yangu kuwa mchango wao na wadau wengine utaongezeka katika miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika;

Lipo tatizo kubwa la kuendelea kupotea kwa vyanzo vya maji hapa nchini. Matendo yetu wenyewe ya uharibifu wa mazingira ndicho chanzo kikubwa kilichotufikisha hapa. Sasa wakati umefika wa kutolifumbia macho jambo hili. Tutachukua hatua thabiti za kuhakikisha kuwa miongozo mbalimbali iliyokwishakutolewa kuhusu hifadhi ya mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji inatekelezwa.

Lazima mamlaka husika katika Mikoa, Halmashauri za Wilaya na Mabonde ya Mito zitimize ipasavyo wajibu wao kuhusu suala hili muhimu. Wahenga wamesema ajizi nyumba ya njaa. Tukifanya ajizi na kuacha kuchukua hatua muafaka katika miaka si mingi ijayo kutakuwa na uhaba mkubwa wa maji unaoweza hata kuhatarisha amani. Tuchukue hatua sasa kuepuka janga hili.



Nishati


Mheshimiwa Spika;
Bila ya shaka sote tunakumbuka kuwa nilianza uongozi wa nchi yetu kukiwa na tatizo kubwa la upungufu wa umeme kutokana na ukame mkubwa ulioikumba nchi yetu wakati ule. Tulilazimika kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na tatizo hilo ambazo zilitusaidia kupunguza ukali wa tatizo. Matatizo yale yalitufundisha kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji na kuongeza mchango wa vyanzo vingine vilivyopo kama vile gesi asilia na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika;

Tumefanya hivyo na tayari tumeongeza megawati 145 za umeme kwa kutumia gesi asilia. Mipango ya kuongeza megawati 100 za umeme unaotokana na gesi asilia imekamilika, imebaki kazi ya utekelezaji kuanza. Katika miaka mitano ijayo tunategemea kuongeza megawati 640 za umeme unaotokana na gesi asilia, maji na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika;

Tumepata mafanikio ya kuridhisha katika usambazaji wa umeme nchini. Kazi ya kuyapatia umeme makao makuu ya Wilaya imeendelea vizuri. Tulikuwa tumebakiza Wilaya ya Namtumbo pekee ambayo nayo mchakato wake umekwishaanza. Hivi sasa tunajipanga kutengeneza mipango ya kuzipatia umeme Wilaya mpya zilizoundwa ambazo hazitakuwa na umeme.

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza jitihada za kuiunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa. Aidha, tutaongeza kasi ya kusambaza umeme mijini na vijijini kwa lengo la kuwafikia asilimia 30 ya Watanzania ukilinganisha na asilimia 14 wa sasa au asilimia 10 wa mwaka 2005. Naamini jitihada tunazozifanya za kuimarisha TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na dhamira yetu ya kuongeza bajeti ya sekta ya nishati vitatuwezesha kutimiza malengo yetu ya kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini.



Kuimarisha Demokrasia

Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeshuhudia kukua na kustawi kwa demokrasia nchini. Vyama vya siasa vimeongezeka kwa idadi na kuimarika katika kufanya kazi za siasa. Asasi za kidemokrasia kama vile Bunge na Mabaraza ya Madiwani zimeendelea kutimiza kwa ufanisi zaidi wajibu wao wa kuwa vyombo vya uwakilishi wa wananchi vya kutumainiwa. Hali kadhalika sauti ya asasi za kiraia imeendelea kusikika kutoa maoni juu ya masuala muhimu kwa taifa letu na watu wake. Vyombo vya habari navyo vimeendelea kufanya kazi zake kwa uhuru.

Mheshimiwa Spika;

Ni makusudio yangu na yetu Serikalini kuona kuwa demokrasia inazidi kustawi na raia wanapata fursa ya kutoa maoni kwa uhuru na uhuru wa vyombo vya habari unaheshimiwa. Tutaendelea kusaidia na kuliwezesha Bunge na Mabaraza ya Halmashauri kutimiza wajibu wao ipasavyo. Tumefanya hivyo miaka mitano iliyopita, naahidi kuwa tutajitahidi kufanya vizuri zaidi katika miaka mitano ijayo.



Utawala Bora

Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba, 2005, niliahidi kuwa Serikali nitakayoiunda itahakikisha kuwa demokrasia inastawi, itazingatia utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Pia niliahidi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa na maovu katika jamii. Nafurahi kwamba katika miaka mitano iliyopita tumetimiza ahadi zetu kwa kiasi kikubwa. Natambua wajibu wa kuimarisha mafanikio tuliyoyapata na kuongeza juhudi pale ambapo hatuna budi kufanya vizuri zaidi. Natambua, pia, haja ya kuboresha utendaji kazi na uwajibikaji Serikalini: katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali na, katika Halmashauri za Wilaya na Miji.

Tumejitahidi sana katika miaka mitano iliyopita kutoa mafunzo na kusisitiza nidhamu, uwajibikaji na ufanisi zaidi. Lakini bado hatujafika pale tunapopataka. Naahidi kuwa tutajipanga vizuri zaidi na kusukuma kwa nguvu zaidi nidhamu na uwajibikaji katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Naahidi pia kwamba tutaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa maana ya mishahara, marupurupu, malipo ya uzeeni na mazingira ya kazi.



Mapambano Dhidi ya Rushwa


Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa mapambano dhidi ya rushwa katika miaka mitano iliyopita tumechukua hatua muafaka za kujenga uwezo wa kisheria, kimfumo na kitaasisi wa kupambana na rushwa nchini. Tumetunga sheria mpya kali zaidi na yenye upeo mpana zaidi wa kukabili tatizo hili. Pia tumetunga Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi. Tumeunda chombo kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU, chenye mamlaka zaidi kisheria na chenye uwezo mkubwa zaidi wa rasilimali watu na vifaa wa kutekelezea majukumu yake.

Mheshimiwa Spika;

Ni ukweli ulio wazi kuwa katika kipindi hiki tuhuma nyingi zimeibuliwa, kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani. Watuhumiwa wengi zaidi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa. Rushwa kubwa zimeshughulikiwa na vigogo wamewajibishwa bila kuonewa muhali. Pamoja na hayo bado ipo haja ya kufanya zaidi kwani tatizo la rushwa bado ni kubwa.

Nimesikia, tumesikia na wamesikia kilio cha wananchi cha kutaka tufanye vizuri zaidi. Tutaongeza bidii katika mapambano haya. Naomba wananchi waendelee kutuunga mkono na kututia moyo na hasa TAKUKURU. Kauli za pongezi pale wanapofanya vizuri zinawaongezea ari vijana wetu ya kufanya vizuri zaidi. Lakini, tabia za kubeza hata pale walipofanya vizuri zinawavunja moyo, kuwakatisha tamaa na kushuhsa morali wao wa kazi. Tuwapongeze wanapofanya vizuri, tuwakosoe wanapokosea na lililo muhimu zaidi tuwape ushauri juu ya njia bora ya kupata ufanisi. Tukifanya hivyo tunajenga, kinyume chake tunabomoa.



Utawala wa Sheria


Mheshimiwa Spika;
Tutaendelea kuimarisha na kuboresha mfumo wetu wa utoaji haki nchini. Serikali itashirikiana na Mahakama kupanga na kutekeleza mipango ya kuongeza uwezo wa vyombo vya kutoa haki ili vitimize ipasavyo wajibu wao. Tutaendelea kuongeza bajeti ya Mahakama nchini. Tutakamilisha mchakato wa kuanzisha mfuko wa Mahakama ambao utaongeza uhuru na uwezo kwa masuala ya fedha na rasilimali. Tutaendelea kuongeza Majaji, Mahakimu na Mawakili wa Serikali. Aidha, tutahakikisha kuwa mchakato wa kuboresha mfumo wa utawala katika Mahakama nchini unakamilishwa.

Mheshimiwa Spika;

Katika miaka mitano hii tutalivalia njuga na kulipatia ufumbuzi muafaka tatizo kubwa la mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani. Mapema iwezekanavyo nakusudia kukutana na wahusika katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Idara ya Magereza kuelewana juu ya hatua za kuchukua .



Wanawake Katika Nafasi za Maamuzi


Mheshimiwa Spika;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge lililopita na hata kabla, nilitoa ahadi ya kuchukua hatua za makusudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwa kiasi gani tumetimiza ahadi hiyo katika Baraza la Mawaziri, utumishi wa umma na kwingineko. Aidha, tuliahidi kufikia asilimia 50 kwa 50 katika Bunge hili. Bado hatujafikia lengo hilo, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba Bunge hili ndilo la kwanza tangu Uhuru, Mapinduzi na Muungano kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake. Tutaendelea kutafakari namna bora ya kufikia lengo letu hilo adhimu.



Tume ya Mipango

Mheshimiwa Spika;
Mwaka 2008 niliunda upya Tume ya Mipango na kuipa muundo wake wa sasa ili kuirejesha nchi kwenye utaratibu mzuri wa kupanga maendeleo yake ya muda mrefu, wa kati na mfupi. Tume itapanga mipango, kisha itaratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango hiyo na kuishauri Serikali ipasavyo. Nilipoteua watendaji wa Tume niliwataka watazame upya shabaha na malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025 ili wahuishe panapostahili. Kisha watengeneze mkakati wa kutekeleza Dira hiyo kwa miaka 15 iliyosalia. Niliwataka wagawe utekelezaji wa mkakati huo katika vipindi vitatu vya miaka mitano mitano na kila kipindi kiwe na mpango wake wa maendeleo.

Mheshimiwa Spika;

Kwa sababu hiyo mwaka ujao tutazindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Miaka Mitano, kati ya hiyo mitatu ya kutekeleza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Naiona njia hii kuwa ni ya uhakika zaidi ya kutekeleza Dira hiyo badala ya kuacha kila Wizara, Idara au Taasisi kufanya inavyofikiria yenyewe inafaa. Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wetu kote nchini ataipa Tume ya Mipango ushirikiano na msaada unaostahili ili waweze kutekeleza kwa ufanisi jukumu lao hilo muhimu na la kihistoria.



Michezo na Utamaduni


Katika miaka mitano iliyopita tumeanza safari ya kuboresha michezo nchini ili tuwape fursa vijana wetu kuendeleza vipaji vyao na Tanzania isikike katika medani za michezo duniani. Nilitimiza ahadi yangu ya kugharamia makocha wa michezo mbalimbali watakaochaguliwa na vyama vya michezo husika. Hivi sasa tunao makocha wa mpira wa miguu, ndondi, riadha na netiboli. Bado hatujapata mafanikio ya juu, lakini mwanga wa matumaini unaonekana. Kinachotakiwa sasa ni kuimarisha uongozi na utendaji wa vyama na vilabu vya michezo husika ili muda mwingi utumike kuendeleza vipaji vya wana-michezo wetu badala ya hali ilivyo sasa ambapo muda mwingi hutumika kugombania uongozi na maslahi binafsi.

Mheshimiwa Spika;

Katika kipindi hiki pia tumerejesha michezo mashuleni, lakini lazima tujipange vizuri zaidi kufanikisha michezo mashuleni. Tufundishe walimu wa michezo na tuhakikishe viwanja na vifaa vya michezo vinapatikana mashuleni. Sasa wakati umefika kwa vyama au vilabu vya michezo kuanzisha shule za michezo yao ili kukuza vipaji vya vijana mapema.

Katika kipindi hiki pia tumeshuhudia maendeleo makubwa ya sanaa za maonyesho yaani muziki na filamu. Wameibuka wanamuziki wengi wazuri wa muziki wa kizazi kipya, taarabu na rumba. Pia kuna maendeleo makubwa ya filamu na uigizaji. Kuna haja ya kujipanga vizuri kusaidia kuendeleza sanaa hizo na wasanii wake. Mimi binafsi nimeanza kuchukua hatua za hapa na pale za kujaribu kutatua baadhi ya matatizo yanayowakabili. Sasa wakati umefika wa kuwa na mipango thabiti ya kuendeleza fani hizi na kuwawezesha wasanii kuendeleza vipaji vyao na kunufaika na kazi zao.



Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa


Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika miaka mitano iliyopita. Jina la Tanzania linangara katika medani za kimataifa. Tunaheshimika na kushirikishwa katika mambo mengi ya kikanda na kimataifa. Tumetembelewa na wageni wengi mashuhuri na tumepata misaada mingi ya maendeleo na kufutiwa baadhi ya madeni yetu.

Tumeitangaza vyema nchi yetu na mafanikio yake yanaonekana. Mauzo yetu ya nje yanazidi kuongezeka, uwekezaji unakua na watalii wanaongezeka. Tumekuwa wenyeji wa mikutano mikubwa ya kimataifa. Yote hayo yamekuwa chachu kwa uchumi wetu kukua na kustawi. Katika miaka mitano ijayo tutaendeleza diplomasia yetu na ushirikiano wa kimataifa kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.

Mheshimiwa Spika;

Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wabia wetu wa maendeleo, yaani nchi na mashirika ya kimataifa kwa misaada yao ambayo imesaidia sana kuifikisha Tanzania hapa ilipo. Kwa vile bado tunahitaji na tunastahili kusaidiwa, naomba wasituchoke, waendelee kutusaidia. Naamini miaka si mingi kutoka sasa hawatakuwa na ulazima wa kufanya hivyo. Hata sasa wanauona ushahidi kwa kiasi gani mwaka hadi mwaka tunaongeza uwezo wetu wa kujitegemea. Hiyo ndiyo dhamira yetu na mwelekeo wetu wa siku za usoni.




Mapato na Matumizi

Mheshimiwa Spika;
Katika miaka mitano iliyopita tumeongeza mapato yetu kutoka wastani wa shilingi 177.1 bilioni kwa mwezi mwaka 2005 hadi shilingi 453 bilioni kwa mwezi hivi sasa. Tumepunguza kutegemea misaada kutoka asilimia 44 mwaka 2005 hadi asilimia 28 mwaka huu. Tutaongeza maradufu jitihada zetu za kukusanya mapato na kuimarisha nidhamu ya matumizi. Tutaboresha mfumo wa ukusanyaji mapato ya Serikali na kupanua wigo wa walipa kodi. Tutakuwa wakali kuhakikisha mianya inayovujisha mapato inazibwa na pesa za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Uzembe, wizi na ubadhirifu havitavumiliwa. Tutaendelea kuzipa uzito unaostahili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua zipasazo kasoro zinapobainika.



Ushirikiano wa Kanda

Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na Umoja wa Afrika (AU). Katika miaka mitano iliyopita tumeshiriki kwa ukamilifu katika asasi hizo za kikanda na nchi yetu imenufaika kisiasa, kiuchumi na kiusalama. Mauzo yetu katika nchi za EAC na SADC, ambayo yameongezeka sana, yamekuwa nguzo yetu kuu ya biashara ya nje ya nchi yetu. Tumenufaika sana na ushirikiano huu wa kanda. Katika miaka mitano ijayo tutazidi kuimarisha ushiriki wetu kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yanayotokea katika Jumuiya hizo na hasa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambapo kasi ya utangamano ni kubwa. Kama mjuavyo tarehe 1 Julai, 2010 Soko la Pamoja limeanza baada ya kukamilika kwa mafanikio, ujenzi wa Umoja wa Forodha. Hivi sasa mchakato wa kuanzisha Umoja wa Sarafu unaendelea kwa kasi na unategemewa kukamilika mwaka 2012. Lazima tuhakikishe kuwa tunashiriki kwa ukamilifu katika vikao vyote vinavyozungumzia masuala ya utangamano wa Afrika Mashariki ili kutetea na kulinda maslahi yetu.

Mheshimiwa Spika;

Hatuna budi kuchangamka na kujipanga vizuri kwani muda si mrefu kutoka sasa mjadala kuhusu kukamilisha hatua ya mwisho ya utangamano yaani Shirikisho la Kisiasa utaanza. Kwa nijuavyo mimi, kwa jinsi shauku ya kuwa na shirikisho ilivyo, mjadala huo huenda ukaendeshwa kwa ari na kasi kubwa. Si vyema kwa Tanzania kubaki nyuma kwa jambo lenye maslahi kwetu sote. Lazima tushiriki vizuri ili kuhakikisha kuwa maslahi yetu yanazingatiwa ipasavyo mchakato huo utakapokamilika.

Mheshimiwa Spika;

Tutaendelea kudumisha urafiki na ujirani mwema na mataifa yote yanayotuzunguka. Ni jambo lenye maslahi kwa uchumi na usalama wa nchi yetu. Tutaendelea kutoa mchango wetu katika masuala ya amani na maendeleo kwenye ukanda wetu, barani Afrika na duniani kwa kiwango tutakachoweza. Tutaendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki ipasavyo katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na ushirikiano wa Kanda.

Hitimisho


Mheshimiwa Spika
,

Nimesema mengi, lakini pia kuna mengi sikuyasema. Ni vigumu, katika muda tulionao nikasema yote. Naomba mridhike niishie hapa kwa leo. Nimetoa kwa muhtasari sana mwelekeo na baadhi ya vipaumbele vitakavyoongoza Serikali nitakayoiunda.

Katika siku chache zijazo nitaunda Baraza la Mawaziri. Dhamira yangu ni kwamba tupate Serikali makini, yenye watu waadilifu na wachapakazi hodari. Watu ambao wataongoza nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango ya Serikali kwa umahiri mkubwa. Watu ambao wataondoa urasimu katika Serikali, watakuwa karibu na watu na watashirikiana vizuri na Waheshimiwa Wabunge bila kujali vyama vya siasa wanavyotoka.

Mheshimiwa Spika;

Narudia kuwaomba muwape ushirikiano ili sote kwa pamoja tutimize wajibu wetu kwa wananchi waliotuchagua. Wabaneni kisawasawa panapostahili, wasahihisheni wanapoteleza, lakini pia msiwe wachoyo wa kuwapa sifa wanapofanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge,

Naomba nimalize kwa kuwahimiza Watanzania wenzangu kwamba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu, tuamue kwa dhati kukusanya nguvu zetu, akili zetu na maarifa yetu yote, kama ndugu wa Taifa moja, kuifanya Tanzania kuwa nchi bora ya kuishi. Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge



Asanteni sana kwa kunisikiliza.



Mungu Ibariki Afrika.



Mungu Ibariki Tanzania.



YA KWANZA ILIKUWA NI DRADT... angalia attachment



tujadili hii hotuba.
 

Attachments

  • Hotuba2010.doc
    90 KB · Views: 214
Hii hotuba imepatikanaje kabla hata hajahutubia?
Hebu nielewesheni mwenzenu.
 
Source plziiiii, isije ikawa umepest ya 2005 ukaweka hapa tukatumia nguvu na akili kuchambua past paper ambayo haitoki kwenye mtihani...
 
Labda ungesema tujadili ubunifu au ubashiri wako, maana hotuba ya mtu haijadiliwi kabla haijatolewa!
 
Source plziiiii, isije ikawa umepest ya 2005 ukaweka hapa tukatumia nguvu na akili kuchambua past paper ambayo haitoki kwenye mtihani...

Labda kama ametunga lakini haiwezi kuwa ya mwaka jana, inaweza kuwa ilikua ni draft ya kwanza na ndio maana hata jina la Waziri Mkuu halipo ila kuna hii inayonyesha Spika Mwanamke;

"Nafarijika sana kwamba sisi katika Chama cha Mapinduzi tumeijengea heshima na kuitengenezea historia nchi yetu kwa kuiwezesha kuwa na Spika mwanamke wa kwanza tangu...."
 
Unajua siku hizi TEKE LINALOTUIJIA yaani kwa lugha ya malkia "TECHNOLOGY" ni "CUT AND PASTE" THEN EDIT! Sasa kasheshe huwa pale unaposahau kuedit ndipo unapokamatwa kilainiiiiiiiiiiii kama mwana tetere aliyenyeshewa mvua. Njia ya mwongo ni fupi na siku zote mwongo huwa hawezi kumbuka uongo aliousema siku za nyuma. Tumeyaona haya hata kwa yule mama " WATOTO WA NDEGE" alivyojikanyaga kuhusu mafisadi akasahau ile kauli yake ya miaka ya nyuma aliyowahi kuitoa.
 
Labda ungesema tujadili ubunifu au ubashiri wako, maana hotuba ya mtu haijadiliwi kabla haijatolewa!

tANZANIA YA LEO SIO TZ YA YA JANA,TATIZO SIO HOTUBA KPATIANA KABLA HAIJATOLEWA, SASAHIVI KILA KITU HAPA BONGO UKITAA UNALETEWA HATA MUHURI WA IKULU.
 
source plziiiii, isije ikawa umepest ya 2005 ukaweka hapa tukatumia nguvu na akili kuchambua past paper ambayo haitoki kwenye mtihani...

wakati unajiandaa na mtihani huwezi jua nini kitatoka ktk mtihani,bali unajiandaa na kila kitu, sasa hivi kila kitu kinawezekana ,maana hata huko ccm kuna watu wameichoka ccm wengi tu,kwahiyo swala la hotuba kuwa nje kabla ya wakati hilo ni jambo la kawaida sana kwa tz ya leo,maana ukitaka hata muhuri wa ikulu utapewa.
 
Sisi wakulima tuliopo nje ya system ni vigumu kuamini kuwa unaweza ukasoma hotuba ya kiongozi kabla ya tukio. Labda hiyo haikuwezekana enzi za Mkapa lakini kwa jk ni zoezi rahisi kabisa. Kuna wazalendo wapo kwenye system wameudhwi sana na namna nchi inavyoendeshwa kisanii na hao ndiyo wanaosaidia upatikanaji wa taarifa hizo muhimu.

Tunaposema nchi yetu inahitaji mabadiliko ya uongozi mojawapo ya sababu ndiyo hiyo. Haiwezekani nchi ikawa salama wakati siri hata za ikulu zinasambaa mitaani tu.
 
Wana jamii mwenzenu nipo mbali na Runinga na kwa kazi ya leo sitakuwa na uwezo wa kucheck hata TV (Vijijini) Naombeni updates za huko Dom Bungeni.. Nasikia Prime Minister ameapishwa, vipi msimamo wa Chadema, walihudhuria, au kuna lipi jipya.
 
Jamani mtupe habari zenye uhakika...si mwingine anasema kaapishwa asubuhi mwingine anasema amesikia anaapishwa jioni???!!!!!!!!!!!
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom